Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumapili, 27 Juni 2021

TAALUMA YA FAMASI NI MUHIMU KATIKA VITA YA NCD: Dkt. GWAJIMA








Na. Catherine Sungura,WAMJW-Mwanza

Katika vita dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza Taaluma ya Famasi ni muhimu katika kuwezesha upatikananji wa bidhaa  za dawa  kwa wale watakaoshindwa  kuzuia kupata  magonjwa yasiayoambukiza na ikawalazimu wafike vituoni  kupata tiba.

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa Kongamano la 12 la kisayansi la Chama cha Wanafunzi wa Taaluma ya Famasi (TAPSA) lililofanyika jijini Mwanza.

Dkt. Gwajima amebainisha kwamba bidhaa hizo za dawa kwa ajili ya kundi hilo  ni ghali na bahati mbaya  nchini Tanzania hakuna  kiwanda cha kutengeneza  na badala  yake wanaagiza toka nje ya nchi.“Tunapaswa kutafakari iwapo kasi ya kukua kwa maradhi haya ni inaongezeka je tunazijazititi vipi kwenye kasi ya kinga kwani bado kasi hiyo ni ndogo”.Aliongeza Dkt. Gwajima.

Alisema kuwa, katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza Serikali  imeendelea kuboresha upatikanaji wa huduma bora  karibu zaidi na wananchi kwa kujenga miundombinu , kuajiri watumishi na kuweka vifaa tiba  na dawa. Maboresho haya yameendelea kufanyika katika vituo vya huduma  za afya ngazi zote.

Hata hivyo amesema  kumekuwa na changamoto mbalimbali ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi ikiwemo changamoto ya upatikanaji  wa bidhaa  za dawa  na vifaa tiba kwa ajili  ya huduma mbalimbali zikiwemo  na huduma kwa ajili ya wanaougua magonjwa hayo yasiyoambukizwa. 

Aidha, Dkt. Gwajima amesema wapo baadhi ya wanataaluma wachache  wasio waadilifu na wasio wazalendo ambao ni doa kubwa kwenye  taaluma hiyo adimu ambayo inatarajiwa kuwa  na mchango mkubwa  kwenye ajenda ya afya. Hivyo  iwapo itasimama kwa nafasi yake basi  wanataaluma  hao wanaweza  kufanya mapinduzi  makubwa  ya afya na kiuchumi.

“Hii itawezekana kwa kujikita  kwenye ajenda  ya jinsi gani  viwanda vya ndani  viweze kuzalisha  bidhaa mbalimbali  na kuhakikisha  matumizi yasiyotia shaka  ya bidhaa za afya  zinazopokelewa kwenye  vituo vya huduma  na kuepuka upotevu na matumizi yasiyofuata  miongozo na kusababisha usugu wa baadhi ya dawa na pia  baadhi kuleta madhara kwa wateja  kama ilivyokusudiwa”.

Dkt. Gwajima alitoa rai  kwa jamii  ya kitanzania kuzingatia ulaji unaofaa   ambapo kila mlo uwe na  makundi yote matano  ya vyakula  halisi, kutotumia  mafuta mengi,chumvi nyingi,kufanya mazoezi ,kupata usingizi wa kutosha,kuepuka matumizi ya tumbaku na madawa ya kulevya  na pia kuchunguza afya angalau mara moja kwa mwaka. 

Takwimu zinaonyesha  kuwa asilimia 75 ya vifo vyote duniani vinavyohusu watu  wenye miaka 30 hadi 70 husababishwa na magonjwa hayo.Hapa nchini  inakadiriwa kuwa magonjwa yasiyoambikiza  husababisha asilimia 27 ya  vifo  vyote.Kauli mbiu ya Kongamano hilo mwaka huu  ni “Wataalamu wa Famasi: kuongeza wigo katika kupambana  na magonjwa yasiyoambukiza”.  

Awali akiongea wakati wa kongamano hilo Mfamasia Mkuu wa Serikali Bw. Daudi Msasi aliwataka wafamasia na wataalum wengine wa afya nchini kuhakikisha wanatumia fomu za dawa( prescription form) kama nyenzo muhimu za kuondoa changamoto za dawa kwani dawa ni fedha za haraka hivyo wahakikishe kabla hawajatoka lazima wahakikishe dawa zinatoka kwa kujaza fomu hizo.

Aliongeza kuwa kwenye kutenda kazi za umma lazima wafuate miongozo ikiwemo muongozo wa matibabu  nchini (STG) wanapokuwa sehemu za kazi hivyo ni wakati wao sasa wa kupitia na kuelewa nini wanapaswa kutekeleza kwenye kazi zao.

Hata hivyo Bw. Msasi aliwataka chama hicho kuanziasha klabu za mazoezi kwenye vyuo vyao ili kuweza kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kwa vitendo na hiyo itasaidia jamii kuelewa umuhimu wa kufanya mazoezi.

Naye Mlezi wa wanafunzi wa Famasi na Masajili wa Baraza la Famasi nchini Bi. Elizabeth shekalaghe aliwataka wanafunzi hao kufanya kazi kwa kujitoa, kuwajibika na kuipenda taaluma  yao ili kuweza kuitumikia vyema taaluma yao.

Bi. Shekalaghe alisema kama Baraza wataendelea kusimamia na kuhakikisha wanaendeleza taaluma  kwa kutoa elimu ya maadili kwenye vyuo vya famasi nchini ili wanapokua chuoni wazitambua na kuzijua angali wanafunzi.

Naye Rais wa Chama cha Wafamasia Wanafunzi Tanzania(TAPSA) Bw. Hamis Msagama ameipongeza Serikali kwa uboreshaji wa dawa na vifaa tiba ambapo kazi kubwa inafanywa na wafamasia  na kuonesha jinsi gani  inawajali watanzania.

Pia Bw.Msagama ameipongeza Wizara ya Afya kwa kuanzisha kitengo cha Magonjwa Yasiyoambukiza (NCD)  hivyo wao kama chama waliona ni vyema kongamaono lao  mwaka huu kujadili kwa kina namna ya kupambana na magonjwa hayo ambayo yanaathiri watu wengi nchini na duniani.

Jumatatu, 21 Juni 2021

Mganga Mkuu wa Serikali afanya ziara Hospitali ya Rufaa ya Amana






Na.WAMJW - DSM


Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifelo Sichalwe amefanya ziara fupi katika hospitali ya rufaa ya Mkoa Amana Jijini Dar es Salaam yenye lengo la kukagua Utekelezaji wa maagizo ya Viongozi wa Wizara waliyoyatoa kwa nyakati tofauti kuhusu maandalizi na utayari wa Watumishi wa afya katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa covid 19.


Akiwa hospitalini hapo Dkt. Sichalwe amezungumza na uongozi wa hospitali hiyo ambapo amewataka viongozi hao wa wafanyakazi kujitayarisha kwa vifaa na matibabu kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.


Amesema Kama watumishi wa Afya, ni vyema kuwa tayari wakati wowote hususan katika kipindi hiki ambacho nchi jirani wamekumbwa na wimbi la tatu la ugonjwa wa Corona kwa kuwa raia wa nchi hizi wana muingiliano mkubwa wa shughuli za kiuchumi na biashara, hivyo kama nchi hatuna budi kujipanga.


Sambamba na kikao hicho Dkt.Sichalwe amekagua miundombinu ya hospitali na utekelezaji wa afua za kuzuia maambukizi mahali pa kazi (Infection, prevention and control). Ameupongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa juhudi na jitihada kubwa wanayofanya hospitalini hapo kwa lengo la kuzuia ueneaji wa maambukizi kwani watumishi wote walikutwa wamevaa barakoa na sehemu za kunawia zenye sabuni na maji  zikiwepo kila wodi, sehemu ya mapumziko na getini. 


“Nimeona mmevaa barakoa, mnatoa elimu kwa wananchi pia. Haya mnayotekeleza hapa ni kama darasa kwa wananchi wote wanaokuja kupata huduma hapa nao watakuwa mabalozi kwa wenzao kwenye jamii. Nina imani utekelezaji huu mnaendeleza hata baada ya kazi”.


Aidha, Dkt.Sichalwe amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa nchini kusimamia utekelezaji wa afua hii, kwani unatukinga siyo tu na ugonjwa wa covid 19 bali na Magonjwa mengine mengi yanayosababishwa na kula vitu kwa mikono isiyo safi na kuvuta hewa yenye vimelea vya maambukizi.


Vilevile Dkt.Sichalwe ametembelea mtambo maalumu wa kuzalisha hewa ya Oksijeni hospitalini hapo ambapo ameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza zaidi ya Milioni 600 ili kuhakikisha wanaokoa Maisha ya watanzania wanaohitaji huduma hiyo.Mtambo huo wenye matoleo Zaidi ya 89, unauwezo wa kuzalisha mitungi 200 ya hewa ya Oksjeni kwa masaa 24 na hospitali ina uwezo wa kuhudumia watonjwa wenye uhitaji 150 kwa wakati mmoja.


Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume amesema kuwa juhudi hizo zinaendelea kufanywa na hospitali zote ndani ya Dar es Salaam ili kuhakikisha wanalidhibiti ipasavyo wimbi hili la tatu.