Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Ijumaa, 29 Januari 2021

WIZARA YA AFYA KUWACHUKULIA HATUA WADOKOZI WA DAWA

- Hakuna maoni
Dkt. Dorothy Gwajima
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto 

Na. WAMJW-Kahama


Serikali imeweka mikakati ya kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria na kitaaluma  kikundi cha watu wachache ambao wamekuwa na tabia ya kuiba dawa za Serikali kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.


Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa kutoa salamu za wizara yake  kwa wakazi wa wilaya ya Kahama kwenye ziara ya kikazi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.


Dkt. Gwajima alisema kuwa kumekuwa na kikundi cha watu wachache kwenye eneo  la kutumia ambalo limeshindwa kubadilika kutokana na watumishi hao kukosa uzalendo wa mali za nchi yao.


“Kikundi hicho tutakibaini na kuwachukulia hatua za kisheria kwani wamekuwa wakikwaza wanachi ambao wanaenda kupata huduma na kusababisha kukosa dawa kwa kudokoa  dawa na hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya Serikali”.


Aidha, alisema Serikali kupitia Mabaraza ya kitaaluma na utumishi wa umma watapambana kwa pamoja na kikundi hicho ili dhana ya kutunza rasiliamali ya nchi itimie,“mbali na hatua za mahakamani watumishi wasio waadilifu watawajibika kwenye hatua za mwajiri na mabaraza yao ya kitaaluma”.Alisisitiza Dkt. Gwajima.


Alisema Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye eneo la dawa  ila  bado kumekuwa na changamoto kwa upande wa matumizi hali hiyo imetokana na baadhi ya watumishi wa sekta hiyo kushindwa kubadilika na kusababisha ukosefu wa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.


Kwa upande wa Mabaraza ya Kitaaluma Dkt. Gwajima alisema watayahoji Mabaraza ya kitaaluma kama kuna sababu ya kuendelea na ajira kwani kama mtaaluma amekosa maadili  na hivyo kurudisha nyuma sekta ya afya nchini na utumishi wa umma kwa ujumla


Hata hivyo Dkt. Gwajima aliwashukuru wananchi kwa kuendelea kutuma maoni, taarifa na ushahidi kwa namba ya simu aliyoitoa mwishoni mwa mwaka hivyo kumuhakikishia Mhe. Rais kwamba wizara yake itapambana kikundi hicho  na kuwataka wananchi waendelee kumtumia maoni ili kuweza kuwabaini wale wote ambao wamekosa uzalendo kwenye utendaji kazi wa utumishi wa umma hapa nchini.

Jumapili, 24 Januari 2021

SERIKALI YASIKITISHWA NA KITENDO CHA ASKALI KUMPIGA NDUGU WA MGONJWA.

 
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akielezea tukio la askari wa ulinzi (SUMA-JKT) aliyetuhumiwa kumpiga ndugu wa mgonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

 
 
SERIKALI YASIKITISHWA NA KITENDO CHA ASKALI KUMPIGA NDUGU WA MGONJWA. 

Na WAMJW- Dom.

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesikitishwa na kitendo askari wa ulinzi (SUMA - JKT) kumpiga ndugu wa mgonjwa aliefika kumjulia hali mama yake katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. 

Hayo yamesemwa leo na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi pindi akiongea na Maafisa habari wa Wizara ya Afya katika Ofisi za Wizara hiyo katika jengo la Bima ya Afya Jijini Dodoma. 

"Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesikitishwa na inalaani sana kitendo hicho kilichofanywa na mlinzi wa SUMA - JKT" amesema Prof. Makubi. 

Akielezea juu ya tukio hilo Prof. Makubi amesema kuwa, Mnamo Januari 22, 2021 Ijumaa jioni askari wa kujenga taifa (SUMA-JKT) alionekana akimpiga ndugu wa mgonjwa katika maeneo ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga jambo ambalo ni kinyume na maadili na taratibu za kazi.

Aidha, Prof. Makubi amesema kuwa, Wizara kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kupitia Mkuu wa Wilaya imeelekeza mlinzi huyo atolewe kwenye kituo hicho cha kazi na kurudishwa makao makuu ya kanda ya jeshi hilo kwaajili ya hatua za kinidhamu kulingana na taratibu za jeshi hilo. 

Hata hivyo, Prof. Makubi ameeleza kuwa, Katibu Mkuu (Afya) Prof. Mabula Mchembe ameelekeza kupata maelezo kutoka kwa uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga wa jinsi tukio hilo lilivotokea, mazingira yake na hatua zilizochukuliwa na uongozi wa Hospitali hiyo. 

Pia, ufanyike uchaguzi kama kulikuwa na uzembe wa utekelezaji wa mfumo na mwongozo wa utoaji huduma kwa mteja (customer care)ambao ulitolewa na Wizara kwa vituo vyote vya kutolea huduma za Afya ili kuona kama kulikuwa na udhaifu mpaka tukio hili kutozuilika, huku akisisitiza baada ya uchunguzi huo hatua stahiki zitachukuliwa. 

Mbali na hayo, Prof. Makubi ametoa rai kwa wananchi kuwa watulivu wakati hatua zikiendelea kuchukuliwa, huku akiwaasa wananchi kuendelea kupata huduma za Afya bila wasiwasi kwani Serikali imejipanga kuhakikisha suala hili halijirudii tena.

"Rai ya Wizara, tunaomba wananchi wawe watulivu wakati suala hili linafanyiwa kazi, na Jamii iendelee kupata huduma katika vituo vyote vya kutolea huduma za Afya nchini bila wasiwasi wowote, kwani Serikali imejipanga kuhakikisha suala hili halijirudii" amesema Prof. Makubi. 

Wakati huo huo, Prof. Makubi ametoa wito kwa wananchi kufuata na kuzingatia taratibu zilizowekwa za muda wa kuingia na kuona wagonjwa katika vituo vyote vya kutolea huduma za Afya nchini. 

Pamoja na hilo, Prof. Makubi amewataka wananchi kutumia vizuri mifumo ya Mawasiliano ambayo imewekwa sehemu mbali mbali ikiwa ni pamoja na kupiga namba 199 bila malipo na za viongozi ili kuwasilisha malalamiko ili kufikia maamuzi sahihi ya migogoro. 

Pia, amewataka Viongozi na Watumishi wote kuendelea kusimamia vizuri huduma bora za afya kwa wananchi wanaowahudumia, kisha kuwakumbusha kusimamia vizuri miongozo ya huduma kwa wateja ambayo ilishatolewa na Wizara. 

Mwisho.


 

Ijumaa, 15 Januari 2021

DKT. MOLLEL AWAFUNDA WAFAMASIA WANAOINGIA KATIKA TAALUMA.

- Hakuna maoni

 
Naibu Waziri Dkt. Godwin Mollel akiongea wakati wa mahafali ya wahitimu wa famasia wanaoingia kwenye taaluma,mahafali hayo yamefanyika kwenye Jijini Dodoma.

 
Msajili wa Baraza la Famasi Elizabeth Shekalaghe akiongea wakatibwa mahafali hayo ambapo wahitimu 252 walikula kiapo na kuingia rasmi kwenye taaluma ya famasia.

 
Mwakilishi wa wahitimu hao Mkapa.Madebele akitoa neno wakati wa mahafali hayo.

 
Dkt. Mollel akibadilishana mawazo na  Msajili wa Baraza la Famasi kwenye mahafali ya kiapo cha wafamasia wanaoingia kwenye taaluma. 

 
Wahitimu hao wakisaini viapo mara baada ya kuapa.

 
Wafamasia hao wakila kiapo cha famasia,moja ya wajibu wao ni kuhakikisha sehemu wanayofanya kazi au kuisimamia ni halali na ina vibali.
 

 Naibu Waziri Dkt. Mollel akimpatia cheti mmoja wa wahitimu wa taaluma ya famasia kwenye mahafali hiyo


DKT. MOLLEL AWAFUNDA WAFAMASIA WANAOINGIA KATIKA TAALUMA. 

Na. Catherine Sungura, WAMJW-Dodoma

Wafamasia wote nchini wametakiwa kutoishia kutoa dawa kwa wagonjwa bali kusimamia ili kujua kama dawa zimefika kwa mgonjwa.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel wakati wa mahafali ya kiapo cha wafamasia wanaoingia katika taaluma iliyofanyika jijini hapa.

Akiongea wakati wa sherehe hizo Dkt. Mollel amesema kuwa wafamasia hao wanalo jukumu kubwa la kuokoa maisha ya wananchi hivyo kutokuhakikisha dawa walizotoa zinamfikia mgonjwa ni kupoteza maisha kwa wagonjwa wanaofika kupata huduma kwenye vituo vyao.

“Wizara inawategemea sana na kutambua kazi kubwa inayofanywa na wafamasia licha ya wachache waliopo kuiangusha taaluma hiyo,hii ni kuvunja kiapo mlichoapa leo na kituo kinapokosa dawa wapo wananchi wanaopoteza maisha na unapokuta upotevu wa dawa lazima mfamasia ahusike”.
Alisema Dkt. Mollel.

Hata hivyo Naibu Waziri huyo amewata wafamasia hao walioingia rasmi leo kwenye taaluma wasisubiri kuingiza dawa au kumpatia mgonjwa dawa bali wametakiwa kuwa wabunifu kwa kutengeneza dawa kwenye maeneo yao kazi ili kuweza kuipunguzia gharama Serikali.

“Mtakapoenda kwenye ajira nataka mjue eneo la dawa ni muhimu sana kwenye uhai wa hospitali hivyo mkiisimamia vyema serikali itakaa vizuri, muhakikishe mnasimamia vizuri eneo hilo hususani kwenye maamuzi katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini”.

Kwa upande wa matumizi ya fedha Dkt. Mollel amewataka wafamasia kuwajibika ipasavyo kwani kumekuwepo na matumizi mabaya ya fedha za dawa kwenye vituo vya umma na hivyo kusababisha kukosekana kwa dawa na vitendanishi na hivyo kusababisha wananchi kutojiunga na bima za afya ikiwemo CHF na wengine wenye uwezo kukimbilia kwenda kwenye hospitali binafsi.

Naye Msajili wa Baraza la Famasi Bi. Elizabeth Shekalaghe amesema Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye dawa hivyo wanapaswa kusimamia kikamilifu huduma zote za famasi kwa kuzingatia sheria,kanuni, taratibu ,vigezo vilivyopo ,maadili na miiko ya utendaji kazi za kila siku.

“Tumesisitiza sana suala ya uwajibikaji,tunafahamu taalama ya famasi imeanza toka mwaka 1978, lakini ukuaji wake umekua kwa taratibu sana ila hivi sasa imekua ikiongezeka kila mwaka na wastani kila mwaka wanahitimu wanafunzi wasiopungua 250 na hivyo tumeweza kusajili wafamasia 2329 hadi sasa”.Alisema.

Shekalaghe amesema Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye sekta ya afya ikijumuisha huduma zitolewazo ikiwemo huduma za dawa“Mhe Rais ametuona hivyo hatupaswi kumuangusha tuhakikishe tunasimamia kikamilifu rasiliamali hizi ambazo serikali imewekeza katika utoaji wa huduma za dawa”. Alisisitiza Shekalaghe.

Hata hivyo amesema, katika mahafali hayo wameweza kujadili namna gani wanaweza kutumia mifumo iliyopo ili kuweza kufanya huduma zinazotolewa katika mnyororo wa dawa, kusimamiwa na kuhakikisha dawa zinawafikia wagonjwa kwa kuweka kumbukumbu vizuri.

Wakati huo huo mwakilishi wa wahitimu hao Mkapa Madebele amewaasa wahitimu wenzie kufuata na kuzingatia sheria za taaluma yao kwani wanahusika kila siku kwenye famasi na kutaka kulinda weledi kwani afya za wananchi zipo juu yao.

Madebele amesema wapo tayari kutumika na kuajiriwa sehemu yoyote nchini ili kuwasaidia wananchi ambao ndio wazazi na walezi wao kwenye jamii kama wanataaluma wa dawa.

Baraza la Famasi moja la jukumu lao ni kuwasajili wanataaluma hao waliokidhi vigezo, jumla ya wahitimu 252 wamehitmu katika mahafali ya tisa yanayofanyika kila mwaka kwa awamu mbili.

-Mwisho-


Jumamosi, 9 Januari 2021

SIMAMIENI MAADILI NA WELEDI - DKT. GWAJIMA

 
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Gwajima akiongea wakati wa kikao kazi hicho ambapo aliwataka viongozi hao kutekeleza ipasavyo Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020 ya Chama cha Mapinduzi.

 
Baadhi wa watendaji wa wizara ya afya makao makuu wakifuatilia mkutano huo  ambao unajadili maadili na weledi wa wanataaluma kwenye vituo vya vya kutolea huduma nchini.
 
Washiriki wa kikao kazi hicho kwenye ukumbi wa hospitali ya Benjamin Mkapa.
 
 

SIMAMIENI MAADILI NA WELEDI - DKT. GWAJIMA

Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma

Vyama, Mabaraza pamoja na bodi za kitaaluma nchini  vimetakiwa kudhibiti maadili na weledi katika utendaji kwa  watumishi wa sekta ya afya nchini ili kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa kikao na viongozi hao kwenye ukumbi wa hospitali ya Benjamin Mkapa jijiji Dodoma.

Dkt.Gwajima amesema kuwa vyama, bodi na mabaraza ya kitaaluma ndio wasimamizi wakuu na wadhibiti wa maadili na weledi ambapo wananchi bado wanakutana na changamoto nyingi za maadili na weledi wakati wa upataji  huduma za afya.

"Kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya uchaguzi  kurasa 137 imeandikwa kushirikiana na vyama vya kitaaluma vya kada ya afya katika kusimamia uzingatiaji wa maadili na weledi katika utendaji wa watumishi hilo ndio tunalotekeleza. "Amesisitiza Dkt. Gwajima.

Amesema wanapofanya ziara kwenye mikoa mbalimbali wanakutana na kero zitokanazo na kufifia kwa maadili na weledi wa utendaji, huku akiweka  wazi kuwa, haya yote yanadhibitiwa na vyama, bodi na mabaraza ya kitaaluma.

"Ili tuweze kuhuisha hayo yote, lazima tukae pamoja na kuangalia mifumo yao ya utendaji kazi ukoje hadi unatoa mianya ya baadhi ya wanataaluma kukosa maadili na kuleta malalamiko mengi kutoka kwa wananchi?,Aliuliza Dkt. Gwajima

Aidha, Dkt. Gwajima amesema kutokana na malalamiko hayo inafanya kuonekana kukosa meno ya vyama hivyo vya kitaaluma, hivyo kikao hicho kikubwa ni kuambina ukweli na kuwakumbusha majukumu yao na wafahamu kuna tatizo kwa wanataaluma wao ndio mana hawashtuki na hata wengine kuvunja maadili bila kujali kama kuna mabaraza ya kitaaluma na kubadilika ili kuondoa kero kwa wananchi.

Kwa upande wa kuwa na mwamvuli mmoja wa mabaraza yote ni kwamba itasaidia kuwa na timu moja na matumizi ya fedha ya kuendesha mabaraza yote yatapungua na kuongeza ufanisi na tija ya wataalam wengine ili wakae kwenye maadili.

Naye Naibu Waziri Dkt. Godwin Mollel amewataka viongozi hao kuwajibika ili kuondoa matatizo ambayo ama wao kama mabaraza hawayaoni au yanaonwa na viongozi wa wilaya eneo husika.

Dkt. Mollel aliendelea  kusema kuwa, wataalamu wengi hivi sasa hawafanyi kazi kwa kuzingatia maadili na hivyo kusababisha makosa mengi ya kitaaluma yanafanyika kwenye vituo vya  kutolea huduma na wananchi wengi kupoteza maisha na wengine kupata athari kwenye jamii.

"Tunakuta makosa kwenye taaluma mfano dawa zinaibiwa lakini  wewe mwenye baraza lako na unasimamia maadili hulioni hili hivi hujioni kwamba na wewe unatakiwa kuadhibiwa? Aliuliza Dkt.Mollel.

Hatahivyo amewataka viongozi hao kujitafakari kama wanatosha kwenye mabaraza yao kama wanashindwa wao kugundua matatizo yaliyopo chini kwani wanakuwa wameshindwa kusimamia na kufanya kazi zao vizuri kwa kutoa adhabu kwa wanaofanya makosa na kusababisha matatizo kwa wananchi.

Mwisho.


 

Jumatano, 6 Januari 2021

VIONGOZI SEKTA YA AFYA TATUENI KERO ZA WANANCHI - PROF. MAKUBI

 
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akieleza jambo mara baada ya kufanya kikao na Viongozi wakuu wa sekta ya afya kwa njia ya mtandao"ZOOM" kilichowajumuisha  Waganga wakuu wa Mikoa na Wilaya,Wajumbe wa kamati ya usimamizi wa huduma za afya za mikoa(RHMT) na wilaya (CHMT) pamoja na Wakurugenzi wa hospitali za Taifa,Kanda na Maalumu.

 

VIONGOZI SEKTA YA AFYA TATUENI KERO ZA WANANCHI:PROF. MAKUBI  

Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma

Wizara ya Afya ipo tayari kupokea kero na malalamiko ya wananchi endapo itaonekana wameshindwa kusikilizwa  ama  kusaidiwa na viongozi wao wa ngazi za chini na wale wa vituo vya kutolea huduma za afya kwenye maeneo yao.

Hayo yameelezwa leo na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi mara baada ya kufanya kikao na Viongozi wakuu wa sekta ya afya kwa njia ya mtandao"ZOOM" kilichowajumuisha  Waganga wakuu wa Mikoa na Wilaya,Wajumbe wa kamati ya usimamizi wa huduma za afya za mikoa(RHMT) na wilaya (CHMT) pamoja na Wakurugenzi wa hospitali za Taifa,Kanda na Maalumu.

Prof. Makubi amesema kuwa wananchi wana matumaini na Serikali yao hivyo wanayo haki ya kusikilizwa na kutatuliwa kero zao kutoka kwa watendaji kwenye vituo vyote vya  huduma za afya nchini hivyo kamati zote zinapaswa kufanya tathimini za kero zote kwa muda wa wiki nne  na kuzitatua pia  kuwasilisha ripoti Wizarani pamoja na TAMISEMI .

“Tunaanzisha utaratibu ambao sisi viongozi wa sekta ya afya tunaenda kutafuta kero kutoka kwa wananchi na kuzitatua,Hili ni agizo na tumekubaliana wasambae kwenye ngazi zote kuanzia zahanati,vituo vya afya na kwenye hospitali,tunatakiwa kuhakikisha wananchi wapate huduma bora licha ya kuwa tumeboresha huduma kwenye vituo vyetu”.

Aidha, amesema utaratibu huu utaweza kurahisisha kutatua kero za wananchi na kuweza kupunguza kero hizo na zingine sio lazima zimfikie Mhe. Waziri hivyo kama watendaji wanatakiwa kujitafakari wanaweza kutatua vipi changamoto wazipatazo wananchi.

“tumekubalikia suala la kuimarisha suala la uongozi, uwajibikaji na usimamizi  kwani kila mmoja ameona kuna mapungufu kwenye usimamizi wa huduma za afya nchini,hivyo tumekubaliana kila kiongozi kuanzia Taifa hadi vijijini kusimamia sehemu zenye mapungufu kwani wananchi wanahitaji mazuri kutoka kwetu,hatuwezi kuwaridhisha kwa kila kitu lakini tutapunguza matatizo yao.

Upande wa kuimarisha vitengo vya huduma kwa wateja, Mganga Mkuu huyo wa Serikali amesema  kitengo hicho kinatakiwa kuboreshwa na hivyo wanapaswa kuchakata kero zote na kuzifanyia kazi na hivyo kuzibandika kwenye ubao wa matangazo wa vituo vyao pia wanapaswa kuwa hai wakati wote kwakuwa  mwananchi wanataka huduma za afya jinsi wanavyohitaji.

“Viongozi hao pia wanatakiwa kukagua ndani ya  hospitali zao kwenye maeneo ya kutolea dawa na  stoo kuona kama dawa zipo na zinawatosheleza wananchi,kama kuna wizi tuweze kuchukua hatu,waende kwenye wodi na OPD kuwasalimu wagonjwa na kama wana kero waseme ili wazitatue,pia maabara kuweza kuona kama vipimo vinafanyika”.Alisisitiza.
 
Hata hivyo wamekubaliana kuwepo na magroup ya ‘Whatsap’ ambayo watapokea na kushughulikia kero kwenye kila wilaya au mkoa husika ili kila mwananchi awezo kutoa kero zake.

 “Tumeagiza kuwe na namba ambazo zitatangazwa kwa wananchi,pia wawashirikie wananchi kupitia mikutano na kutaja namba zao ili wananchi wajue wanawasilisha vipi malalamiko yao ”.

Aliongeza kuwa wananchi wanapaswa kujenga imani na kuwaamini watendaji wote wa sekta ya afya, na kusema kuwa baada ya Mhe. Waziri kutangaza namba yake ya malalamiko kwa muda wa wiki mbili ameweza kupokea kero elfu tatu kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Kikao hicho kwa njia ya mtandao kimehudhuriwa na washiriki wapatao 220 na ajenda kubwa ilikuwa ni jinsi ya kupunguza kero za wananchi zinazousiana na huduma za afya nchini ambazo wanatuma kupitia namba ya malalamiko iliyotangazwa na Waziri wa afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima mwishoni mwa mwaka jana ambayo ni 0734124191.

-MWISHO-