Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumatano, 13 Aprili 2022

ASILIMIA 26 YA WATU WAZIMA WANASHINIKIZO LA JUU LA DAMU.

- Hakuna maoni
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe akipima msukumo wa damu katika Zahanati ya Makole Jijini Dodoma, baada ya kuzindua mradi wa Healthy Heart Africa (HHA) unaoratibiwa na AstraZeneca katika Mikoa ya Dodoma na Dar es salaam.

Wananchi walioshiriki tukio la uzinduzi wa mradi wa Healthy Heart Africa (HHA) unaoratibiwa na AstraZeneca katika Mikoa ya Dodoma na Dar es salaam, wakifuatilia kwa makini neno kutoka kwa Mganga Mkuu wa Serikali aliyeongoza zoezi la uzinduzi wa mradi huo

Picha ya pamoja ikiongozwa na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe.



ASILIMIA 26 YA WATU WAZIMA WANASHINIKIZO LA JUU LA DAMU. 

Na Rayson Mwaisemba WAF- DOM.

MGANGA Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe amebainisha kuwa asilimia 26 ya watu wazima wenye umri wa miaka kati ya 25 hadi 64 wana shinikizo la juu la damu, hali inayosababishwa na mtindo wa maisha ikiwemo ulaji wa vyakula vya mafuta mengi, matumizi ya pombe kupita kiasi na kutofanya mazoezi. 

Dkt. Sichalwe amebainisha hayo leo Aprili 13, 2022 wakati akifungua Mradi wa Healthy Heart Africa tukio lililofanyika katika zahanati ya Makole Jijini Dodoma. 

"Tumefanya utafiti mwaka 2012 na kukagundua kwamba asilimia 26 ya watu wazima kati ya miaka 25 na 64 wana shinikizo la juu la damu na tatizo hili linatarajia kuongezeka kwa kiasi kikubwa endapo hatutachukua hatua." Amesema Dkt. Sichalwe. 

Aliendelea kusema kuwa, tafiti zinaonesha kuwa, zaidi ya asilimia 75% ya Wagonjwa hao wenye shinikizo la juu la damu hawatumii tiba yoyote, huku akiweka wazi kuwa zaidi ya robo tatu kati yao hawajui kama wana shinikizo la juu la damu. 

Aidha, Dkt. Sichalwe amesema kuwa, taarifa za utafiti zilizofanywa katika baadhi ya hospitali za Rufaa zimebaini kuwa, wastani wa watu 19 katika kila watu 100 wanaolazwa kwa tatizo la shinikizo la juu la damu hufariki Dunia. 

Sambamba na hilo, ameweka wazi kuwa, hali ni mbaya zaidi kwa wagonjwa wa kiharusi, ambapo katika kila watu 100 wanaolazwa, watu 39 wanafariki kwa tatizo hilo la shinikizo la juu la damu, hivyo Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea kutoa elimu na kuhamasisha jamii ili kuongeza nguvu za kupambano dhidi ya ugonjwa huo. 

Mbali na hayo Dkt. Sichalwe ameendelea kusisitiza juu ya kuzingatia utoaji huduma za afya kwa kufuata miongozo, huku akisisitiza weledi na umahiri wakati wa kutoa huduma ili kuepusha malalamiko yanayoweza kuzuilika kutoka kwa wananchi. 

Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume amewashukuru Wadau wa PATH kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo ugonjwa wa Shinikizo la juu la damu. 

Amesema, Ukuaji wa miji, Maendeleo ya Sayansi na teknolojia na mabadiliko ya mtindo wa maisha kwa kiasi kikubwa yanaendana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo ugonjwa wa shinikizo la juu la damu, hivyo kuwaomba Wadau kuendelea kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo hasa katika miji inayoendelea kwa kasi ikiwemo Dodoma, Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya. 

Mpango wa Healthy Heart Africa (HHA) ni mpango wa miaka miwili unaoratibiwa na AstraZeneca katika Mkoa wa Dodoma (HF 13) na Dar es salaam (HF 22), na unajumuisha jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 35 (zahanati 25 na hospitali 10). Mradi huu unashughulikia magonjwa ya moyo na mishipa, haswa Shinikizo la damu (HTN). 


Mwisho.

Jumatano, 6 Aprili 2022

PROF. MAKUBI ATOA WITO KWA WANANCHI KUWAHI KUFANYA UCHUNGUZI WA SARATANI.

 

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi akifungua Kongamano la 8 Kisayansi wakijadili kuhusu mafunzo na tafiti za magonjwa ya Saratani ya damu.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi akimkabidhi tuzo ya Heshima na Prof. Magesa (Daktari wa Haematology.

Washiriki wa Kongamano la 8 la Kisayansi la masuala ya Tafiti ya magonjwa ya Kansa ya damu, lililofanyika Jijini Dar es salaam.


Picha ya Pamoja ikiongozwa na Prof. Abel Makubi, Katibu Mkuu Wizara ya Afya baada ya ufunguzi wa Kongamano la Kisayansi la masuala ya Tafiti ya magonjwa ya Kansa ya damu, lililofanyika Jijini Dar es salaam.


Na Rayson Mwaisemba WAF - DSM.

KATIBU MKUU Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi ametoa wito kwa Watanzania kujenga tabia ya kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara  ili kuweza kujua hali zao mapema na kuepuka dhidi ya magonjwa ikiwemo Saratani inayo pelekea kifo pindi mgonjwa anapochelewa kuanza matibabu.

Prof. Makubi ametoa wito huo leo wakati akiongea na Waandishi wa Habari baada ya  ufunguzi wa Kongamano la 8 la Kisayansi la masuala ya tafiti na mafunzo lililofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Sayansi Shirikishi Muhimbili, Jijini DaresSalaam. Kauli mbiu ikiwa "utafiti na mafunzo ni daraja la kuelekea huduma bora kwa wagonjwa wa saratani ya damu." 

"Nitoe wito kwa Wananchi kuwahi kufanya uchunguzi ili kujua hali ya magonjwa hasa ugonjwa wa Saratani katika miili, dalili za ugonjwa wa Saratani tunazijua, zipo nyingi,  inawezakuwa kupungukiwa damu, inaweza kuwa kujisikia homa, inawezakuwa kupungua uzito au kukohoa damu kwa wagonjwa wenye kansa za Kifua, au hata kushindwa kula chakula." Amesema.

Aliendelea kusema kuwa, endapo mtu amepata dalili zozote kati ya hizi ni vizuri kwenda mapema katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kufanya uchunguzi kujua hali ya afya na kuanza matibabu, kwani yaweza kuwa ni ugonjwa wa Saratani au ugonjwa mwingine, amesisitiza Prof. Makubi. 

Sambamba na hilo, Prof. Makubi amesisitiza kuwa, ni vizuri kila baada ya miezi sita mpaka mwaka mmoja kujenga tabia ya kwenda kufanya uchunguzi (check up) ili kujua hali ya afya ya mwili, ikiwamo kuangalia magonjwa yasiyoambukiza kama vile ugonjwa wa Saratani. 

Aidha, Prof Makubi amesema kuwa, takribani watu 40,000 wanagundulika kuwa na saratani kila mwaka hapa Tanzania, huku akisisitiza kuwa asilimia 80% ya wagonjwa hawa hupoteza maisha kwasababu ya kuchelewa kufanya uchunguzi ili kuanza matibabu ya ugonjwa wa Saratani.

"Takribani watu elfu 40 wanagundulika kuwa na saratani kila mwaka hapa Tanzania, na 80% ya wagonjwa hawa hupoteza maisha."amesema Prof Makubi.

Hata hivyo, Prof Makubi ameushukuru uongozi wa Chuo cha Muhimbili kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele kwa kutoa elimu kwa wananchi jinsi ya kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo ugonjwa wa Saratani.

Vile vile, Prof. Makubi amewashukuru Wataalamu mbalimbali waliotoa mchango mkubwa katika kusaidia tiba ya magonjwa ya Saratani ya damu, Wataalamu hao ni pamoja na Prof. Magesa (Daktari wa Haematology,  Chuo cha Muhimbili), Dkt. Maunda (Taasisi ya Saratani Ocean Road), Dkt. Trish (Daktari wa Watoto).

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Prof. Andrea Pembe amewashukuru Wataalamu na wanafunzi waliojitokeza kushiriki Kongamano hili la Kisayansi lenye kujadili Saratani ya Damu lenye lengo la kutafuta matibabu ili kuwasaidia wananchi wanaopoteza maisha kwasababu ya ugonjwa wa Saratani, hasa Saratani ya damu.

 

MWISHO.