Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumatano, 17 Agosti 2022

WAZIRI UMMY MWALIMU AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI KUTOKA INDIA NA FALME ZA KIARABU KUWEKEZA KWENYE SEKTA YA AFYA NCHINI

Na Englibert Kayombo WAF, Dar Es Salaam. Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu leo amekutana na kufanya mazungumzo na Wawekezaji kutoka India pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu (United Arab Emirates) kujadili na kuwakaribisha kwenye fursa za uwekezaji katika Sekta ya Afya nchini. Waziri Ummy amepongeza nchi hizo kwa kuonyesha nia ya kutaka kuwekeza kwenye Sekta ya Afya na kuongeza ushirikiano katika kusaidia maendeleo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha ubora wa huduma za afya. “Tumekuwa tukishirikiana na India kwenye mambo mengi kuhusu Sekta ya Afya, tuna madaktari wetu watanzania wanasoma masuala ya udaktari huko India, tuna wawekezaji kutoka India hapa nchini, ushirikiano huu ni mzuri na una tija kwa Serikali na Watanzania”. Amesema Waziri Ummy na kuipongeza Umoja wa Falme za Umoja wa Kiarabu kwa kuvutiwa kuwekeza kwenye Sekta ya Afya hapa nchini. Waziri Ummy amesema kuwa kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Sekta ya Afya ni ubora wa huduma, hivyo kuwakaribisha wawekezaji hao kuwekeza hapa nchini ili Watanzania na raia kutoka nchi Jirani waweze kupata huduma za kibingwa za matibabu. Aidha, Waziri Ummy ametoa wito kwa wawekezaji hao kuweka mkazo zaidi katika fursa za uwekezaji kwenye upande wa kuboresha mifumo ya TEHAMA kwenye Sekta ya Afya nchini huku akisema kuwa bado kuna changamoto nyingi kwenye mifumo ya TEHAMA ndani ya Sekta ya Afya. Bw. Lav Aggarwal ambaye ni Kiongozi wa wawekezaji kutoka India, amesema kuwa lengo kufika nchini ni kuboresha zaidi ushirikiano baina ya nchi husika na wanatarajia kuendela kushirikiana na Tanzania katika kuboresha zaidi upatikanaji wa huduma bora za matibabu hapa nchini. Naye Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu hapa nchini Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu hapa nchini Bw. Khalifa Al Marzooqi amesema ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe. Samia Suluhu Hassan katika Umoja wa Falme za Kiarabu imefungua zaidi milango ya uwekezaji kutoka Falme za Kiarabu na kufika hapa kuja kuona nini cha kuwekeza kwenye Sekta ya Afya.

Alhamisi, 4 Agosti 2022

ENDELEENI KUTOA HUDUMA BORA KWA WANANCHI-DKT. SICHALWE

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe alipotembelea Hospitali Misheni ya Haydom iliyoko Mkoani Manyara kujionea hali ya utoaji wa huduma za afya ili kuleta ufanisi mzuri katika kutoa huduma.


Na. WAF – Manyara

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe ameupongeza Uongozi wa Hopsitali ya Misheni ya Haydom iliyoko Mkoani Manyara kwa kazi nzuri wanayofanya katika kuwahudumia wanachi na kuwataka kuendelea kutoa huduma  bora za afya. 

Dkt. Sichalwe ameyasema hayo  Mkoani Manyara alipotembelea Hospitali hiyo kujionea hali ya utoaji wa huduma za afya ambapo amewataka kuwa na dawati la huduma kwa mteja ili kuleta ufanisi mzuri katika kutoa huduma.

Aliendelea kusisitiza kuwa, sababu za hospitali nyingi kushindwa kufanya  vizuri  ni pamoja na kukosekana uongozi mzuri katika utendaji, kutobadili fikra na tabia zinazodumaza maendeleo katika utoaji huduma kwa wananchi. 

“Nahitaji wataalamu wa afya mrudi katika miiko yenu na weledi wenu hii itaturudishia hadhi ya taaluma na kuleta ufanisi mzuri wakati wa kutoa huduma kwa wananchi."Amesema. 

Hata hivyo Dkt. Sichalwe amewakumbusha watumishi katika hospitali hiyo kutumia fursa iliyotolewa na Serikali ya kujiendeleza kielimu ili kuendelea kupata ujuzi zaidi katika taaluma zao.

Aidha amewataka kuwasimamia vizuri na kwa karibu madaktari watarajali wanaofanya mazoezi kwa vitendo (Interns), kwa kuwaelekeza miiko ya taaluma na kufanya  kazi kwa juhudi na ufanisi ili wapate ujuzi mzuri wa kulitumikia Taifa utaoleta matokeo chanya.

Mwisho


SERIKALI KUJA NA MIKATABA YA KUPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO.

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe akiongea katika kikao cha Wadau wa Sekta ya Afya kwenye eneo la mama na mtoto pamoja na Lishe kilichofanyika Mkoani Singida.


Na.Rayson Mwaisemba,WAF- SINGIDA 

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe alisema, Serikali kupitia Wizara ya Afya na OR-TAMISEMI imejipanga kupunguza vifo vya Wajawazito na watoto kupitia mikataba itakayobeba viashiria vya Wajawazito na lishe inayotarajiwa kusainiwa na Wakuu wa Mikoa. 

Dkt. Sichalwe alisema hayo katika kikao cha Wadau wa Sekta ya Afya kwenye eneo la mama na mtoto pamoja na Lishe kilichofanyika Mkoani Singida.

"Tumekubaliana kutekeleza maagizo ya Mhe. Rais aliyoyatoa ya kuja na mkataba mmoja ambao utakuwa umebeba viashiria vya utendaji vya akina mama wajawazito pamoja na masuala ya Lishe ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kupambana dhidi ya vifo vya Wajawazito na watoto wachanga".Alisema Dkt. Sichalwe 

Aliendelea kusema kuwa, pamoja na hayo Serikali kwa kushirikiana na wadau imekubaliana kuanza kutekeleza matumizi ya kanzi data, yatakayotoa fursa ya kujua viashiria vya hatari vya mjamzito endapo anavyo kutokana na maswali atayoulizwa na Mtaalamu wa afya.

Sambamba na hilo Dkt. Sichalwe alisema, kwa upande mwingine Serikali kwa kushirikiana na wadau wamekubaliana utekelezaji wa azimio la vikao vya kujadili vifo vya mama na mtoto vilivyoanzishwa na Wizara ya Afya kikanda. 

Aidha, Dkt. Sichalwe alieleza kuwa, kwa pamoja kama Wadau wa Sekta ya Afya wamekubaliana kutekeleza mfumo wa kusimamia magari ya kubebea Wajawazito (M-MAM) unaorahisisha mfumo wa rufaa nchini kama sehemu nyingine ya mkakati wa kupambana dhidi ya changamoto ya vifo vya Wajawazito na watoto. 

Mbali na hayo, Dkt. Sichalwe aliwashukuru Wadau waliojitokeza katika kikao hicho cha Kimkakati na kuweka wazi kuwa, maazimio yote ya kikao hicho yatawasilishwa kwenye uongozi wa Wizara ya Afya na TAMISEMI kwaajili ya utekelezaji na Wadau wote walioshiriki kikao hicho na wasio shiriki watakuwa katika utekelezaji. 

Hata hivyo, aliweka wazi kuwa, wamekubaliana kuleta mipango yao, namna walivyotekeleza na changamoto wanazokutana nazo wakati wa utekelezaji wa mipango hiyo na wanaishauri nini Serikali ili kwa pamoja kuona namna gani wanaweza kushirikiana kuzitatua kwa lengo la kuongeza kasi ya kupunguza vifo vya mama na mtoto katika jamii.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe alisema, katika kikao hicho wamepitia viashiria mbalimbali vinavyolenga masuala ya mama na mtoto ambavyo vitasaidia kuongeza uwajibikaji kwa viongozi mbalimbali ngazi ya Mkoa na kupima matokeo ya uwajibikaji huo kwa kupungua kwa vifo vya Wajawazito na watoto. 

Pia, Dkt. Ntuli amesema kuwa, Serikali ilifanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu ambapo vituo vya afya 650  ambavyo vinatoa huduma za upasuaji vimejengwa, huku hospitali mpya za Halmashauri 130 zikijengwa, hivyo uwekezaji huo ni lazima uende sambamba na huduma bora zitazosaidia kupungua kwa vifo vya Wajawazito na watoto. 

"Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu, katika kipindi cha miaka mitano vituo vya afya 650 vinavyotoa huduma za upasuaji, sambamba na hilo hospitali mpya za Halmashauri 130, sasa uwekezaji huo lazima uende sambamba na huduma." Alisema Dkt. Ntuli.

Mwisho.