Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu akiongozana na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel pamoja na Mhandisi kutoka TBA Glady Jefta, wakiwa katika ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita.
Baadhi ya Majengo ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita
Na.Rayson Mwaisemba, WAMJW- GEITA
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 1.9 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la huduma za mama wajawazito na Watoto Mkoani Geita.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya Mh. Ummy Mwalimu wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita ambayo imefika zaidi ya asilimia 80 ya ujenzi
"Habari njema kwa Wananchi, Serikali kupitia Wizara ya Afya tuna Bilioni 1.9 kwa ajili ya kujenga jengo la akina mama wajawazito pamoja na Watoto wachanga, tunakamilisha taratibu tayari kuanza ujenzi huo" alisema Waziri Ummy.
Waziri Ummy aliendelea kusema, Hospitali hiyo inajengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la upasuaji (thieta), jengo la mionzi (radiolojia), huku akisisitiza kuwa majengo hayo ya wodi yaliyokamilika yataanza kutoa huduma ili kuendelea kuwasaidia wananchi.
Waziri Ummy amesema, Serikali tayari imepeleka Milioni 400 kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa kituo cha Afya vya Katoro, ikiwa ni azma ya Serikali ya kuboresha huduma za Afya katika ngazi ya chini, ili kuzipunguzia mzigo Hospitali za Rufaa za Wilaya na Mikoa.
"Tulianza kujenga vituo vya Afya zaidi ya 352 katika Halmashauri mbali mbali, muelekeo tunazungumzia huduma za Afya kwa wote, kupitia kuwekeza katika vituo vya Afya na Zahanati, ndio maana wiki iliyopita tulileta Milioni 800 kwa ajili ya kuongeza majengo katika kituo cha Afya Katoro na Buseresere" amesema Waziri Ummy
Licha ya kuridhishwa na ujenzi huo, Waziri Ummy amemuagiza Mkandarasi kutoka TBA kuhakikisha unamaliza unakamilisha ujenzi wa Hospitali hiyo mapema, huku akisisitiza ifikapo mwaka kesho Mwezi Machi 31, Hospitali hiyo ianze kutoa huduma za Afya kwa Wananchi.
"Mipango ya Serikali, tunategemea ifikapo tarehe 31 Machi, nikija hapa anikabidhi Hospitali, sitokuja kukagua Hospitali, mimi nitatimiza wajibu wangu wa kutafuta fedha, nataka ifikapo tarehe hiyo tuanze kutoa huduma kwa Wananchi " amesema.
Aidha, Waziri Ummy, amewatoa hofu wananchi wa Mkoa wa Geita kuwa ,Serikali imejipanga kuhusu Watumishi wataohudumu katika Hospitali hiyo, huku akiwatoa wasi wasi kuhusu upatikanaji wa vifaa vya kutolea huduma katika Hospitali hiyo.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli kupitia Wizara ya Afya kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya uboreshaji wa huduma za Afya katika Mkoa wa Geita.
"Naomba niendelee kumshukuru Mh.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli kwa kuendelea kutenga fedha katika Mkoa wetu kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wanyonge, huu ni Mkoa mpya una watu wengi, na una changamoto nyingi, lakini changamoto zote Wizara imezichukua na kutekeleza" alisema
MWISHO.
0 on: "BILIONI 1.9 KUJENGA JENGO LA MAMA WAJAWAZITO NA WATOTO GEITA"