Baadhi ya Maafisa wa Wizara ya Afya na Taasisi zake wakiwa pamoja na Waandishi wa Habari walipotembelea Maabara ya NIMR Mkoani Mbeya.
Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu kanda ya nyanda
za juu kusini (NIMR) imepiga hatua kubwa katika shughuli za utafiti inazofanya
ikiwa ni pamoja na kuwa na vifaa vya kisasa vya maabara pamoja na watalaamu
waliobobea.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa NIMR wa kanda hiyo Dkt. Nyanda
Ntinginya wakati akiongea na maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Wizara
ya Afya na Taasisi zake ambao wametembelea nyanda za juu kusini katika
kutekeleza kampeni ya “Tumeboresha Sekta
ya Afya” ili kuona mafanikio ya sekta ya afya katika kipindi cha miaka mitano
ya Rais John Magufuli akiwa madarakani.
Dkt. Nyanda amesema moja ya mafanikio makubwa ya NIMR ya
kanda hiyo ni Utafiti wa vipimo vya awali vya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa
watoto wachanga waliozaliwa na akina mama wenye maambukizi.
Utafiti huo ujulikanao kwa jina la 'BABY' uliofanywa na
Taasisi hiyo unatumia kipimo cha “Early Infant Diagnosis (EID)” ambacho
ufanyika kwa kutumia mashine za Gene Xpert.
Kwa mujibu wa Dkt. Nyanda amesema awali, upimaji wa kawaida
ulikuwa unafanywa kwa watoto wachanga wenye wiki 4 hadi 6 na majibu yake
yalikuwa yakichukua wiki mbili.
Dkt. Nyanda amesema utafiti huo uliofanyika Julai 2015
hadi Novemba 2016 kituo cha NIMR Mbeya kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha
Munich cha nchini Ujerumani ulilenga kutathimini vipimo vya awali vya VVU kwa
watoto wachanga ambao wazazi wao wameathirika.
"Huu utafiti ulilenga kufanya tathmini ya vipimo vya
awali vya VVU katika kituo cha kutolea huduma na vipimo vilifanywa na wauguzi
tofauti na upimaji wa sasa ambao huhitaji wataalamu wa maabara na hivyo
kuhitaji usafirishaji wa sampuli za damu kwenda maabara ya kanda au ya mkoa”. Amesema
Dkt. Nyanda.
Matokeo ya utafiti yameonesha vipimo hivyo vilifanya vizuri
kwa asilimia 100 na vinatoa majibu ndani ya masaa mawili tu na hivyo mgonjwa
kupewa majibu yake siku hiyo hiyo ukilinganisha na upimaji wa kawaida ambapo
huchukua wiki mbili au zaidi kupata majibu.
“Upimaji wa VVU wa awali kwa watoto wachanga umejumuishwa
katika muongozo wa sasa wa utoaji wa huduma za VVU nchini,”alisema.
Hata hivyo, matokeo ya utafiti huo uliofanywa nchini
Tanzania, Afrika ya kusini na Msumbiji yamepelekwa Shirika la Afya Duniani(WHO)
kutoa miongozo ya upimaji wa VVU kwa watoto hao katika muongozo wa utoaji wa
huduma za VVU wa mwaka 2016.
Maabara ya Taasisi ya Taifa ya utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ya Mkoani Mbeya imepata ithibati ya ubora wa kimataifa Maabara za utafiti ya nchini Marekani "College of American Pathologists" (CAP) kutokana na ubora wake wa kufanya tafiti ambapo ithibati hiyo imetolewa kwa nchi mbili tu katika ukanda wa Afrika Mashariki ikiwa ni Tanzania na Uganda.
|
0 on: "NIMR MKOANI MBEYA YAFANIKIWA KUTAFITI KIPIMO CHA VVU KWA WATOTO WACHANGA"