Baadhi ya chupa za maji ya tiba zinazotengenezwa na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya. |
Mtaalamu akionesha jinsi maji ya tiba yanavyotengenezwa |
Mashine ya kutengeneza maji ya tiba |
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya imetaja mafanikio iliyopata
katika kipindi cha miaka minne ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwa madarakani ikiwa ni
pamoja na kuanzishwa kwa kiwanda chenye uwezo wa kuzalisha maji tiba
lita 3,840 kwa mwezi.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo,
Dkt. Godlove Mbwanji alipokuwa akizungumza na Maafisa Habari, Mawasiliano na
Uhusiano wa Wizara ya Afya na Taasisi zake walioambatana na waandishi
mbalimbali wa habari katika kutekeleza kampeni ya “Tumeboresha Sekta Ya Afya” katika mikoa ya nyanda za juu kusini.
Dkt. Mbwanji amesema Hospitali hiyo imetekeleza kwa vitendo
sera ya Viwanda ya Awamu ya Tano pamoja maagizo ya Rais Dkt. John Magufuli kwa kuanzisha
kiwanda cha uzalishaji wa maji tiba “Drip”.
Amesema kiwanda hicho kilianzishwa Februari 2019 kwa gharama
ya TSh. Milioni 120 kwa mapato ya ndani na kinazalisha dripu hizo zenye lita
za ujazo 250 na 500 zimeanza kutumika kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wenye
uhitaji.
“Hali hii imesaidia kuondokana na adha ya kununua au kuagiza
dripu nje ya nchi na kiwanda kina uwezo wa kutengeneza maji tiba lita
3840 kwa mwezi huku uhitaji wa hospitali ni lita 5232 na hivyo kukidhi
kwa asilimia 73 ya uhitaji wa maji tiba kwa ajili ya hospitali”. Amesema
Dkt. Mbwanji.
Mkurugenzi huyo amesema wamefanikiwa kupunguza gharama za
manunuzi ya maji tiba nje nchi, wana uhakika na upatikanaji wake, wametoa
mafunzo ya utaalam wa utengenezaji wa maji tiba na kuongeza ajira kwa wataalamu
wa kutengeneza bidhaa hiyo.
Aidha Dkt. Mbwanji amesema wanatarajia kuanza kutengeneza
dawa ya macho na masikio kwenye kiwanda hicho mwaka 2020.
Hospitali hiyo inahudumia mikoa saba ya Nyanda za juu
kusini ambayo ni Iringa, Njombe, Ruvuma, Katavi Rukwa, Songwe na Mbeya na
imeendelea kuboresha huduma zake mbalimbali ili kutoa huduma bora za afya
kwa wananchi.
Mafanikio mengine yaliyotajwa ni pamoja na kuwa na ongezeko
la upatikanaji wa dawa kutoka asilimia 70 hadi 95, ongezeko la madaktari
bingwa kutoka 36 hadi 53, huduma za kibingwa za masikio, koo, pua.
Pia amesema kuanzishwa kwa chuo cha Udaktari cha Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam tawi la Mbeya kumetoa fursa kwa madaktari kuanza kufanya
tafiti mbalimbali, kuanzishwa kwa huduma ya mkalimani wa lugha ya alama, uwezo
wa kulaza wagonjwa kutoka vitanda 477 hadi 553 baada ya kukamilika jengo la
watoto.
Dkt. Mbwanji amesema Serikali ilitoa TSh. Bilioni 3 kwa ajili
ya ujenzi wa jengo la Radiolojia ambalo baada ya kukamilika limefanikisha
utoaji wa huduma za mionzi na kuanzisha huduma mpya za CT Scan, mashine
za kidigitali za X ray, Fluoroscopy, Mammography na Ultrasound.
MWISHO
0 on: "HOSPITALI YA KANDA YA RUFAA MBEYA (MZRH) YAANZISHA KIWANDA CHA UZALISHAJI MAJI TIBA (DRIP)"