Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisema jambo wakati wa uzinduzi wa kliniki ya huduma za methadone Mkoa wa Tanga
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (katikati) akikata upete wakiati akifungua rasmi kliniki ya huduma za methadone katika Mkoa wa Tanga, kushoto ni Mkuu Wa Mkoa wa Tanga Mhe. MArtin Shigela na aliye upande wa kulia ni Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya Bw. James Kaji
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu pamoja na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya wakipongeza kwa furaha wakati Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martin Shigela akimpatia dawa ya methadone kwa mnufaika wa huduma hiyo iliyozinduliwa mkoani humo.
Kamishna Jeneral wa Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya Jamesi Kaji akisema jambo wakati wa uzinduzi wa kiliniki ya huduma za methadone Mkoani Tanga.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martin Shigela akisema jambo wakati wa uzinduzi wa kliniki ya huduma za methadone kwa Mkoa wa Tanga.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (katikati) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martin Shigela (kushoto) wakipokea maelekezo toka kwa msimamizi wa ujenzi wa jengo la huduma za tiba ya madawa ya kulevya linaloendelea kujengwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo Tanga.
Ujenzi wa jengo la kliniki ya huduma za tiba ya madawa ya kulevya katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo Tanga ukiendelea ambapo uje zi huo utagharimu kiasi cha shilingi milioni 780 za kitanzania.
Na WAMJW - Tanga
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa
maendeleo wanaendelea kuboresha huduma za afya nchini ambapo shilingi milioni
780 zimetolewa kwa ajili ya kujenga kliniki ya huduma za methadone kwa
waathirika wa madawa ya kulevya mkoani Tanga.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoo Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa kituo
cha muda cha kutoa tiba ya methadone kwa warahibu wa madawa ya kulevya
kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga - Bombo.
“Kwa kushirikiana na wadau wetu wa
maendeleo Mfuko wa Dunia (Global Fund) na Mamlaka ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya
tumepata zaidi ya milioni 780 na tumezileta kwa ajili ya kujenga jengo la
kutolea huduma ya methadone” amesema Waziri Ummy.
Hata hivyo waziri ummy mwalimu
hakusita kuupongeza uongozi wa mkoa wa tanga kwa ubunifu walioufanya kwa
kushirikiana na wadau wa maendeleo wakiwemo PEPFAR na Amref -Tanzania, kwa
kujenga kituo cha muda kwa ajili ya kutoa tiba kwa warahibu wa madawa ya
kulevya ambacho kimegharibu shilingi milioni 20 za Kitanzania.
“Tumeona tunaweza kufanya huduma hizi
kwa gharama nafuu, nnafurahi kuona kwamba zimetumika takribani shilingi milioni
20 kwa ajili ya kutengeneza kituo cha muda kwa huduma za kliniki katika Mkoa wa
Tanga” amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy Mwalimu amesema kuwa
ilikuwepo haja ya kuwa na kliniki ya methadone kwa Mkoa wa Tanga kutokana na
kuwa na waathirika wengi wanaotumia madawa ya kulevya huku mkoa huo ukishika
nafasi ya pili ya kuwa nawarahibu wengi wa madawa ya kulevya.
“Mkoa wa Tanga unashika nafasi ya
pili ya kuwa na idadi kubwa ya watumiaji wa madawa ya kulevya, takwimu za mwaka
2016 zinaonyesha Mkoa wa Tanga una watumiaji taribani 5190 wa madawa ya kulevya”
amefafanua Waziri Ummy Mwalimu
Waziri Ummy amesema kuwa hadi sasa
kuna kiliniki 8 ambazo zinatoa huduma katika maeneo mbalimbali nchini ambapo
kwa Mkoa Wa Dar Es Salaam kliniki hizo zimeanzia katika hospitali ngazi ya
mikoa na kushuka chini kwenye hospitali za ngazi ya halmashauri na kutaja
maeneo yatakayofuata kuwa na huduma hizo ni pamoja na Bagamoyo, Kigamboni,
Mbagala, Tegeta pamoja na Magereza Segerea.
Amesema kwa mujibu wa Takwimu za
Wizara ya Afya, Tanzania ina waathirika 8071 waoapatiwa huduma ya dawa za
methadone kwa ajili ya kupunguza madhara ya dwa za kulevya ambapo kati yao
wagonjwa 480 ni wanawake na 7591 ni wanaume.
Naye Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya
Kudhibiti Madawa ya Kulevya Bw. James Kaji amesema kuwa wiki hii Tanzania
inaungana na mataifa mengine kuadhimisha siku ya kupinga madawa ya kulevya
ambayo kwa mwaka huu kauli mbinu ni tujenge uelewa sahihi kwa tatizo la dawa za
kulevya ili kuimarisha mapambano dhidi ya tatizo hilo.
“Uzinduzi wa kituo hiki ni muendelezo
wa vituo vingine 8 vinavyotoa huduma nchini ambapo kwa Dar es Salaam vipo
vitatu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala
na Temeke; Mbeya – Hospitali ya Rufaa ya Nyanda za Juu Kusini; Mwanza –
Hospitlai ya Rufaa ya Sekou Toure; Bagamoyo na Dodoma – Itega” amefafanua
Kamishna Jenerali James Kaji
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga
Mhe. Martin Shigela amesema kuwa MKoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa yenye
idadi kubwa ya shughuli za usafirishaji wa madawa ya kulevya na kufanya kuwa na
idadi kubwa ya watumiaji ambao hiingia kwenye urahibu wa madawa hayo.
Aidha Mhe. Shigela ameiasa jamii
kuepukana na matumizi ya madawa ya kulevya huku akiwaomba kutoa taarifa kwa
mamlaka kwa wale wanaojihusisha na usafirishaji na biashara ya madawa ya
kulevya.
“Kwa wale ambao wameathirika na
madawa ya kulevya katika jamii zetu tuwaone ni kama sehemu ya ndugu zetu,
tusiwanyanyapae, tuwaelekeze na tuwalete kwenye matibabu na tunaamini watarudi
kwenye hali ya kawaida” amesisitiza Mhe. Shigela
Mwisho.
0 on: "MILIONI 780 KUJENGA KLINIKI YA HUDUMA ZA METHADONE MKOA WA TANGA"