Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akisema jambo kwa timu ya uongozi wa afya ya Mkoa wa Mwanza kwenye kikao kazi cha kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga kilichofanyika Wilaya ya Misungwi.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Thomas Rutachuzibwa akisema jambo kwa timu ya uongozi wa afya ya Mkoa wa Mwanza kwenye kikao kazi cha kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga kilichofanyika Wilaya ya Misungwi.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tiba anayesimamia Hospitali za Rufaa za Mikoa Dkt. Caroline Damian (kulia) pamoja na Katibu wa Mganga Mkuu wa Serikali Bi. Maurine Kunambi (kushoto) wakiwa kwenye kikao kazi cha kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga Mkoa wa Mwanza.
Timu ya uongozi wa afya ya Mkoa wa Mwanza wakiwa kwenye kikao cha kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.
Timu ya uongozi wa afya ya Mkoa wa Mwanza wakiwa kwenye kikao cha kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.
VIFO VYA MAMA WAJAWAZITO HAVIVUMILIKI TENA" – MGANGA MKUU WA SERIKALI
Na Englibert Kayombo WAMJW - MWANZA.
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi amesema kuwa Serikali haitovumia tena vifo vya akina mama wajawazito vinavyosababishwa na uzembe wa watumishi kazini.
Prof. Makubi ametoa kauli hiyo alipokuwa akifunga kikao kazi cha timu ya uongozi wa afya ya Mkoa wa Mwanza kilichofanyika Wilayani Misungwi kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.
"vifo vya akina mama wajawazito havivumiliki tena kwa sasa hivi kwenye hii dunia ambapo tumeingia uchumi wa kati, ni lazima tutafute mbinu mpya na nzuri tuweze kuziendeleza na kuhakikisha kwamba ambaye amekuja kuleta maisha asifariki” amesema Prof. Makubi.
Amesema siyo vifo vya akina mama wajawazito tuu ndio vizuiwe bali hata vya watoto wachanga wanaozaliwa pia vidhibitiwe kwa wataalam wa afya kuhakikisha watoto hao wanazaliwa salama pia.
Prof. Makubi amesema Serikali imewekeza rasilimali nyingi kwenye sekta ya afya hivyo ni vyema matunda ya uwekezaji huo yakaenda kuonekana kupitia uboreshwaji wa huduma bora za afya ikiwemo kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.
Amesema anashangazwa na vifo vingi vya akina mama wajawazito kutokea katika vituo vya kutolea huduma za afya na sio kwenye Jamii na kuwataka watumishi hao kujitafakari ni sehemu gani kuna changamoto ili zifanyiwe kazi na kudhibiti vifo hivyo.
“Nimefurahishwa kuona mmekutana hapa kutafakari, kwa hiyo mmeshaliona tatizo hamkusubiri Wizara ya Afya kuja kuwaambia mfanye nini, hilo ndio linanipa moyo mmejitambua na mmeamua kuchukua hatua wenyewe” amepongeza Prof. Makubi wa timu ya uongozi wa afya ya Mkoa wa Mwanza kwa kuanza kuchukua hatua.
Aidha,Prof. Makubi ametoa wito kwa Mikoa mingine iendeleze kile ambacho mkoa wa Mwanza imeanza kufanya kwa kufanya vikao vya tathimini na kuweka mikakati ya kudhibiti vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.
“Kabla ya mwezi wa kwanza haujaisha kila Mkoa uwe umeshakaa, ukishirikisha viongozi wote wa Mkoa, Wilaya na Halmashauri vituo vya afya mpaka zahanati wawe na wawakilishi ili mjadili mbinu ambazo zinaweza kupunguza vifo vya akina mama wajawazito kwa kiasi kikubwa zaidi”
Amesisitiza Prof. Makubi akitoa agizo hilo kwa timu za uongozi wa afya kwa mikoa yote.“Tuondoke hapa tulipo kwa sababu wananchi wanatamani twende tupige hatua moja mbele ili tukaboreshe huduma zetu, kwa mikakati mliyoweka tukiitekeleza naamini tunaweza tukatoka kwenye tatizo hili” Amesisitiza Prof. Makubi.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Thomas Rutachuzibwa amesema kuwa wameyapokea maelekezo yote aliyoyatoa Mganga Mkuu wa Serikali na watayafanyia kazi kuhakikisha vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga vinadhibitiwa mkoani humo.
“Ninakuahidi ndani ya miezi mitatu tutaanza kupata mabadiliko, tutakaa kwa muda uliobaki kuweka mpango kazi kuhakikisha tunaenda kutekeleza yale yote tuliyopanga ili kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga” amesema Dkt. Rutachuzibwa.
Dkt. Rutachuzibwa amesisitiza suala la wajibikaji kwa watumishi wa afya wakiwa kwenye maeneo yao ya kazi kwa kutambua wana wajibu upi na kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi na kupunguza changamoto zilizopo maeneo yao ya kazi.
“Kila mmoja ajitambue, tutoe huduma kwa wananchi, kuanzia leo naomba wote tuanze upya, kila mtu awajibike kwa kipande chake” amesisitiza Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Thomas Rutachuzibya.
Mwisho
0 on: ""VIFO VYA MAMA WAJAWAZITO HAVIVUMILIKI TENA" – MGANGA MKUU WA SERIKALI"