Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel akisalimiana na Watumishi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pindi alipowasiri katika ofisi za Wizara ya Afya Mtumba Jijini Dodoma.
Watumishi wa Wizara ya Afya na Wakurugenzi wake, wakifuatilia kwa makini maelekezo kutoka kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika ofisi za Wizara ya Afya Mtumba Jijini Dodoma.
Picha ya pamoja ikiongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima pamoja na Naibu Waziri wake Dkt. Godwin Mollel, wakiwa na Katibu Mkuu Idara ya Afya, Prof. Mabula Mchembe (wanne kutoka kushoto) na Katibu Mkuu Idara ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu (wakwanza kushoto), pamoja na Watumishi na Wakurugenzi kutoka Idara Kuu ya Afya.
DKT. GWAJIMA AWATAKA VIONGOZI WA WIZARA YA AFYA KUSHIRIKIANA ILI KUONGEZA UFANISI KAZINI
Na WAJMW-Dodoma
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amewataka Wakurugenzi na watumishi wa Wizara ya Afya kushirikiana ili kuweza kufikia lengo la kuboresha huduma za afya nchini.
Dkt. Dorothy amesema hayo leo wakati akiongea na Wakurugenzi pamoja na viongozi mbalimbali waliompokea mara baada ya kuapishwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Waziri wa Wizara hiyo mapema katika hafla iliyofanyika Ikulu-Chamwino, Jijini Dodoma.
Dkt. Gwajima amesema ili sekta ya afya iweze kusonga mbele na kuwafikia wananchi katika kiwango cha hali ya juu inategemea na ushirikiano utakaokuwepo baina ya viongozi wa Wizara pamoja na watumishi mbalimbali wa sekta ya afya.
“Wapeni ushirikiano makatibu wakuu, mambo mengi yanafanywa na wataalam kwa kushirikiana na makatibu wakuu, tukikubaliana kufanya jambo basi wote tufunge mikanda kuhakikisha tukamalisha kwa wakati lengo likiwa kutimiza dhamira ya Mhe. Rais ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya nchini”. Amesema Dkt. Gwajima.
Aidha, Waziri Gwajima amewataka viongozi wa idara mbalimbali wanapotembelea maeneo mbalimbali ya Sekta kuja na ripoti ya ziara zao na kukabidhi kwa Katibu Mkuu ili ziweze kufanyiwa kazi na kutoa miongozo halikadhalika amewataka makatibu wakuu kutofungia ripoti hizo makabatini bali wazifanyie kazi na kutatua changamoto zinazozikabili sekta ya afya.
“Nawataka Viongozi wa Wizara mnapoenda 'Supervision' mrudi na ripoti na pia nawaomba Makatibu Wakuu msizipuuze ripoti mnazoletewa ili tuone zinaleta faida gani kwenye ofisi zetu na pia katika kuboresha huduma za afya nchini”. Ameongeza Dkt. Gwajima.
Waziri huyo amesema kwa kufanya hivyo itaongeza ufanisi kwa kila kiongozi atakayeenda ili kujua aanzie wapi na siyo kila mmoja kwenda na jambo lake huku akiendelea kusisitiza viongozi hao kushirikiana ili kutatua kero na changamoto zilizopo.
Pamoja na hayo Waziri Dorothy amezitaka Taasisi, Hospitali na vituo vya afya kutoa taarifa za mapato na matumizi na ameagiza kutengenezwa mfumo utakaosaidia kupata taarifa hizo ili ziweze kusaidia kutoa muelekeo wa uboreshaji wa huduma za afya.
Pia ametaka utengenezwe muongozo wa huduma kwa wateja ili utolewe kwa watumishi wa sekta ya afya ili wabadilike na kuwathamini wagonjwa wanaofika katika maeneo ya kazi ili kupata huduma.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Prof. Mabula Mchembe amewapongeza na kuwashukuru Waziri Dorothy pamoja na Naibu Waziri Dkt. Godwin Mollel kwa kuchaguliwa kuiongoza Wizara hiyo na kuahidi kutoa ushirikiano.
MWISHO
0 on: "DKT. GWAJIMA AWATAKA VIONGOZI WA WIZARA YA AFYA KUSHIRIKIANA ILI KUONGEZA UFANISI KAZINI"