WATOA HUDUMA ZA TIBA ASILI WATAKIWA KUTOJIHUSISHA
NA IMANI ZA KISHIRIKINA KATIKA HUDUMA ZAO
Na
WAMJW-MWANZA
Watoa huduma
za tiba asili na tiba mbadala wametakiwa kutojihusisha na imani za kishirikina ikiwa
ni pamoja na uchawi katika kutoa huduma kwa wananchi wanaohitaji huduma hizo.
Hayo yamesemwa
na Msajili kutoka Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala Dkt. Ruth Suza wakati
akiongea na Waganga wa tiba asili na tiba mbadala wa mikoa ya Mwanza, Kagera na
Geita waliojitokeza katika kikao kazi kilichohusisha wataalam kutoka Baraza
hilo lililo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto.
Dkt. Ruth
amesema kuna baadhi ya Watoa huduma wa tiba za asili wanaojihusisha na mambo ya
kishirikina ikiwa ni pamoja na kupiga ramli chonganishi, kuhitaji viungo vya
binadamu kwa ajili ya kutengeneza dawa na kuwa na nyara za serikali ambazo
kiuhalisia hazitakiwi katika matibabu hayo.
“Ninawataka
waganga wote kutojihusisha na tiba za kishirikina zinazoenda sambamba na
uchawi, kupiga ramli chonganishi na kutumia nyara ambazo hazina vibali kama
mikia na ngozi za wanyama wa porini. Endapo mganga yeyote akikutwa na kasoro
hizi baraza halitasita kumfutia usajili mhusika na atashitakiwa kwa mujibu wa
sheria zilizowekwa na Serikali”. Amesema Dkt. Ruth.
Aidha, Dkt.
Ruth amewataka waganga hao kufuata taratibu zilizowekwa na Serikali ikiwa ni
pamoja na kupata vibali vya vitendea kazi vyao hasa nyara za Serikali
zinazotokana na wanyama, nyoka, ndege na wadudu wa porini, ambapo vibali hivyo
vinatolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Dkt. Ruth pia
amewataka waganga hao kutunza siri za wagonjwa wanaowatibu ikiwa ni haki ya msingi
ya mgonjwa kama hospitali zinavyofanya. Vile vile Dkt. Ruth amewataka waganga wa
jadi kuwapeleka Hospitalini haraka wagonjwa walioshindwa kupata ahueni kwa dawa
za jadi ili kupunguza vifo vinavyoweza kuepukika.
Kwa upande
wao Waganga wa mkoa hiyo wametoa kero zao ikiwa ni pamoja na kukamatwa mara kwa mara na vyombo vya usalama wanapokua
katika kazi zao, dawa zao kutosajiliwa kwa wakati na kupata leseni kutoka
Baraza. Hivyo kulitaka baraza hilo kuhakikisha Serikali inawatambua kwa kuwapa
vibali na kusajili dawa zao ambazo kwa kiasi kikubwa zimekua tegemeo kwa
wananchi wengi wenye matatizo mbalimbali.
Baraza la
tiba asili na tiba mbadala limeendelea kufanya zoezi la ukaguzi nchi nzima kwa
ajili ya kuangalia usajili na vibali kwa waganga wanaotoa huduma. Ambapo zoezi
hili limeanzia mkoa wa Dar Es Salaam, Kagera, Geita na Mwanza na kufuatiwa na
mikoa mingine.
0 on: "WATOA HUDUMA ZA TIBA ASILI WATAKIWA KUTOJIHUSISHA NA IMANI ZA KISHIRIKINA KATIKA HUDUMA ZAO"