Waziri Ummy Mwalimu akisoma maandishi ya jiwe la
ufunguzi wa jengo hilo,kulia ni mwakilishi toka Global Fund Martha
Setembo.
Mkandarasi aliyejenga majengo ya Chuo cha Uuguzi Mirembe Nishit Jethwa kutoka kampuni ya V.J. Mistry Co LTD ya Mkoani Kagera.
Mshauri elekezi wa mradi huo Dkt.Moses Ockony ambae pia ni Mkurugenzi wa Mekon Arch Consult LTD.
Mwakilishi wa Wizara ya Fedha Kamishna Msaidizi Adrian Njau akitoa shukrani mara baada ya ufunguzi wa majengo hayo.
Waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiongea na Afisa wa mradi huo kutoka Wizara ya Afya Dkt.Catherine Joachim (kulia) na kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt.Mpoki Ulisubisya.
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akikata utepe
kuashiria ufunguzi wa majengo ya chuo cha Uuguzi cha Mirembe ambayo
yamegharimu shilingi Bilioni 3.1, majengo yaliyojengwa ni pamoja na bweni
moja litakalotumika na wanafunzi 256 ,nyumba mbili za watumishi,jengo
la utawala, madarasa,jiko panoja na bwalo la chakula.
Picha ya pamoja ikiongozwa na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati wa makabidhiano ya majengo hayo yaliyojengwa kwa ufadhili wa
Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI,KiFUA KIKUU na Malaria(Global
Fund), kushoto kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya.
Na WAMJW-Dodoma
Shilingi bilioni 3.1 zatumika kujenga majengo ya chuo cha Uuguzi na Ukunga
Mirembe mjini hapa ambayo yatasaidia kuongeza idadi ya wahitimu wa kada hiyo
nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto
Ummy Mwalimu wakati wa makabidhiano ya majengo hayo yaliyojengwa kwa ufadhili
wa Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI,KIFUA KIKUU na Malaria(Global
Fund).
Mhe. Ummy aliwashukuru Global fund kwa kusaidia Tanzania katika maeneo
mbalimbali nchini hasa katika mikoa kumi na saba ya Tanzania bara katika ujenzi
wa vyuo, nyumba za watumishi ,maghala ya kuhifadhia dawa pamoja na magari ya
kusafirishia dawa kupitia bohari ya dawa(MSD).
"Bila afya hakuna viwanda wala kilimo, hivyo serikali ya awamu ya tano
imejikita katika utoaji wa huduma wa afya na rasiliamali watu na hivyo
tunatarajia kuona ongezeko la wanafunzi katika vyuo vyetu"
Aidha,Ummy alisema kupitia mfuko huo umesaidia nchi katika kukabiliana na magonjwa
ya UKIMWI,Kifua Kikuu na Malaria.
Alisema Watoto 10,000 nchini Tanzania huzaliwa wakiwa na maambukizi ya
virusi vya Ukimwi kwa Mwaka huku watu zaidi ya 900,000 wakitumia dawa za
kufubaza Makali ya ugonjwa huo (ARVs).
Waziri alisema idadi hiyo ni kubwa ikilinganishwa na wajawazito wanaobainika
kuwa na VVU hivyo kunahitajika kazi ya ziada ili kukomesha kabisa tatizo hilo
na watoto wazaliwe wakiwa wazima.
Ummy alisema serikali imejipanga kuhakikisha tatizo hilo linakwisha kwani
inawezekana kabisa mtoto kuzaliwa bila ya maambukizi ya Ukimwi na hilo ndilo
lengo lake akiwa Wizara ya afya.
“Hali ya maambukizi bado iko juu, kwa sasa tumeshasajili watu laki tisa
ambao wanatumia dawa za kufubaza Makali ya Ukimwi na tatizo kubwa ni idadi ya
watoto 10,000 ambao huzaliwa wakiwa na maambukizi, nataka tutoke huko,” alisema
Mwalimu.
Waziri alisema wizara kwa sasa bajeti imeongeza kutoka asilimia 9.2 kwa
Mwaka 2016/17 hadi kufikia asilimia 10 kwa Mwaka 2017/18 na kuifanya sekta ya
afya kuwa sekta ya kipaumbele miongoni mwa sekta za kipaumbele katika mgao wa
bajeti hivyo hakuna kisingizio tena.
Kuhusu vyuo vya uuguzi alikiri Wizara kuvisahau kutokana na taarifa ya mkuu
wa chuo hicho Athanas Paul kwamba aliomba sh 300 milioni lakini kwa ajili ya
shughuli za uendeshaji lakini tangu januari serikali ilipeleka chuoni hapo Sh
150,000 tu.
Alisisitiza Wizara kutupia macho katika eneo hilo ikiwemo kufuta jina la
chuo cha Mirembe na badala yake kisomeke Dodoma Mirembe Nursing Collage kwani
Mirembe ni hospitali ambayo wengi huamini kuwa walioko huko wanamagonjwa ya
akili.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya afya Dk. Mpoki Ulisubisya alisema Chuo hicho
kinakabiliwa na uhaba mkubwa wa Watumishi bila kusahau majengo kwa ajili ya
ofisi na madarasa.
Dkt. Ulisubisya alitaja uhaba wa Watumishi lakini akasema mambo hayo
yatashughulikiwa kwa ukaribu zaidi ikiwemo Majengo yaliyojengwa na Global Fund
ambayo yanakwenda kupunguza msongamano huo.
Mwakilishi wa Global Fund Martha Setembo alisema ushirikiano wa mfuko huo na
serikali ulianza Mwaka 2003 kwa lengo la kuimarisha sekta ya afya.
Setembo alisema ziko fedha nyingi ambazo zimetengwa kwa ajili ya kusaidia
sekta hiyo katika miradi inayotekelezwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu ijayo
na akaomba Serikali kuendelea kuitumia vema miradi hiyo ikiwemo Majengo
wanayokabidhiwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Majengo ya vyuo vya
uuguzi.
0 on: "SHILINGI BILIONI 3.1 ZIMETUMIKA KUJENGA MAJENGO YA CHUO CHA UUGUZI NA UKUNGA MIREMBE"