TAMKO KUHUSU UGONJWA WA EBOLA ULIOTOKEA KATIKA NCHI JIRANI YA JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO
Utangulizi
Ndugu wanahabari,
Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea kutoa
taarifa kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika nchi jirani ya Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Nchi hiyo ya DRC imetangaza tena kuwa
na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola mnamo tarehe 1 mwezi Agosti, 2018, ambapo
jumla ya wagonjwa 26 na vifo 10 vilitolewa taarifa na wagonjwa 4 kati
yao walithibitishwa kimaabara kuwa na ugonjwa wa Ebola. Wagonjwa hawa
wametokea katika vijiji/Maeneo ya Mangina ikiwa ni kama km 30 tu
magharibi mwa mji wa Beni kwenye jimbo la Kivu Kaskazini linalopakana na
nchi ya Uganda ikiwa ni kama km 100 tu, na pia likiwa karibu sana na
nchi ya Rwanda.
Huu ni mlipuko wa 10 wa ugonjwa wa
Ebola kutokea nchini DRC, na umetokea wiki moja baada ya nchi hiyo
kutangaza kuisha kwa mlipuko mwingine uliotokea mwezi Mei mwaka huu
ambao ulikuwa katika jimbo la Equator, Magharibi mwa DRC, umbali wa
zaidi ya km 2,000 kutoka eneo la huu mlipuko mpya uliotokea.
Ndugu wanahabari,
HADI
SASA HAPA NCHINI TANZANIA HAKUNA MGONJWA YOYOTE ALIYEHISIWA AU
KUTHIBITISHWA KUWA NA VIRUSI VYA EBOLA. Hata hivyo, kugunduliwa kwa
ugonjwa huu kwenye jimbo la Kivu Kaskazini linalopakana na nchi za
Uganda na Rwanda ni jambo la kutuweka kwenye wasi wasi kwani eneo hili
liko karibu sana na nchi yetu kuliko eneo lingine lolote ambako ugonjwa
huu umeshawahi kutokea kwenye nchi ya DRC. Hivyo nchi yetu ipo hatarini
kuambukizwa ugonjwa huu kutokana na ukaribu na muingiliano wa watu, hasa
kuhusiana na wasafiri wanaotoka na kuingia hapa nchini.
Kwa
sababu hizi, watanzania hatuna budi kuchukua tahadhari ya hali ya juu
ili kujikinga na kudhibiti na ugonjwa wa Ebola. Hivyo Wizara inapenda
kutoa tahadhari ya ugonjwa huu kwa wananchi wote katika Mikoa yote ya
Tanzania, lakini hasa ile inayopakana na nchi jirani za DRC, Uganda na
Rwanda. Mikoa hiyo ni pamoja na Mwanza, Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa na
Songwe. Aidha tahadhari na hatua stahiki zichukuliwe katika maeneo yote
ya mipakani ambapo abiria wanaingia nchini kutoka nchi jirani.
Ugonjwa wa Ebola
Ugonjwa wa Ebola husababishwa na virusi vya Ebola ambavyo huambukiza kwa njia zifuatazo;
Kugusa Damu au majimaji kutoka kwa mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo,
Kugusa maiti ya mtu aliyekufa kwa ugonjwa huo,
Kugusa wanyama (Mizoga na wanyama wazima) walioambukizwa kama vile Sokwe na Swala wa msituni.
Dalili za Ugonjwa
Dalili
za Ugonjwa huanza kuonekana kwa mtu aliyeambukizwa baada ya siku 2 hadi
21 tangu kupata maambukizi. Dalili hizo ni pamoja na;
Homa kali ya ghafla,
Kulegea kwa mwili,
Maumivu ya misuli,
Kuumwa kichwa na vidonda kooni.
Mara nyingi dalili hizo hufuatiwa na kutapika, kuharisha, vipele vya ngozi na pia figo na Ini kushindwa kufanya kazi.
Kwa baadhi ya wagonjwa kutokwa na damu ndani na nje ya mwili.
Namna ya Kujikinga na ugonjwa wa Ebola:
Ugonjwa wa Ebola unaweza kuzuilika. Njia kuu za kujikinga na ugonjwa huu ni:-
Kuepuka
kugusa au kuingiwa na mate, damu, mkojo, jasho, kinyesi, machozi na
majimaji mengine yanayotoka mwilini mwa mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa
wa Ebola
Kuepuka kushughulikia maiti ya mtu
aliyefariki akiwa na dalili za Ebola; badala yake watoe taarifa kwa
uongozi wa kituo cha huduma za Afya kwa ushauri.
Kuepuka kula nyama za Wanyama wa porini kama sokwe, swala na popo na pia kugusa mizoga ya Wanyama hao
Kuepuke mila na desturi zinazoweza kuchelewesha kupata huduma muhimu na kuzidi kueneza ugonjwa wa Ebola.
Kuzingatia usafi wa mwili
Kutoa
taarifa mapema kwa viongozi wa Serikali na wa huduma za Afya katika
ngazi zote pale anapotokea mtu mwenye dalili za Ebola.
Kuwahi katika vituo vya huduma za Afya pale mtu anapoona dalili za ugonjwa huu.
Hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara kufuatia kupatikana kwa taarifa ya Ugonjwa huu huko DRC
Kufuatia
kuwepo kwa taarifa hizi tangu mwezi Mei 2018, hatua zifuatazo
zinaendelea/zimechukuliwa na Wizara ili kujiandaa kukabiliana na mlipuko
huo:
Kufanya tathmini ya utayari wa kukabiliana na
ugonjwa wa Ebola nchini (Operational readiness assessment) kwa nchi
nzima kwa kushirikiana na WHO na kuainisha mapungufu ambayo yanapaswa
kufanyiwa kazi. Mapungufu hayo yanaendelea kuyafanyiwa kazi ili kujenga
uwezo na utayari katika nchi yetu.
Tumetengeneza
mpango mkakati wa kujiandaa na kupambana na mlipuko wa Ebola endapo
utatokea nchini (Costed Ebola Contingency Plan). Mpango huu umeandaliwa
kwa kushirikiana na WHO. Mpango umeainisha maeneo ya kujenga uwezo kwa
wakati huu wa kujiandaa, pamoja na hatua za kuchukua endapo ugonjwa
utaingia ikiwa ni pamoja na gharama zake.
Tumefanya
mafunzo ya Timu za dharura (Rapid Response Teams) ngazi ya Taifa na
katika Mikoa ya Dar es Salaam, Songwe, Rukwa, Katavi, Kigoma na Kagera
Tumeimarisha
ufuatiliaji wa wasafiri mipakani (travellers entry screening) kwa
kutumia vifaa vya kupima joto la mwili (thermo scanners) na fomu maalum
za wasafiri
Wizara imepokea vifaa vya kukabiliana
na Ebola kutoka WHO vikiwemo; Thermo scanners, Vifaa Kinga, au PPE, kama
vile gloves, body bags, vifaa vya ufungashaji wa sampuli nk. Vifaa
hivyo vimeanza kusambazwa mikoani kupitia MSD
Uelimishaji
wa umma umefanyika na unaendelea kufanyika kwa kupitia vyombo vya
habari vya kitaifa na kijamii, na mitandao ya kijamii. Vile vile
vipeperushi na mabango vinaendelea kuandaliwa
Vikao
vya uratibu vimefanyika katika ngazi ya taifa na mikoa ambayo ipo
katika hatari zaidi. Pia ufuatiliaji wa karibu unaendelea kupitia Kituo
cha ufuatiliaji wa magonjwa ya dharura cha Wizara (Public Health
Emergency Operation Centre is on High Alert)
Wataalam
kutoka ngazi ya Taifa kwa sasa wako katika mikoa ya Kigoma Katavi Rukwa
Kagera Kilimanjaro Mwanza Songwe na Mbeya kufanya tathmini ya utayari
katika ngazi ya mikoa na Wilaya (Readiness Assessment)
Maandalizi yanaendelea kwa ajili ya kutekeleza kazi nyingine kama ifuatavyo:
Kufanya
mafunzo katika mikoa iliyo salia ikiwemo Mwanza, Kilimanjaro na Mbeya
ambayo imesalia katika ile mikoa nane iliyo katika hatari zaidi
Mafunzo ya waandishi wa habari 30 (media orientation)
Zoezi la udhibiti wa matukio ya dharura (simulation exercise) katika ngazi ya Taifa
Mafunzo kwa wasfirishaji wa sampuli kwenda katika maabara
Hitimisho
Nawaomba
Wakuu wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri wote nchini
kuchukua Tahadhari na kuendelea kuelimisha wananchi wote juu ya ugonjwa
huu na kuwataka kutokuwa na hofu ila kuendelea kuchukua tahadhari za
kujikinga na ugonjwa huu kwani mpaka sasa hakuna mtu aliyethibitishwa
kuugua ugonjwa huu hapa nchini.
Aidha
Wizara itaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali katika kuimarisha
ufuatiliaji na kuendelea kutekeleza mikakati ya kudhibiti ili ugonjwa
huu usiingie nchini. Vilevile Wizara itaendelea kutoa taarifa pamoja na
Elimu kwa Jamii kadri itakavyohitajika.
Imetolewa na
Ummy A. Mwalimu (Mb)
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto
10/08/2018
0 on: "TAMKO KUHUSU UGONJWA WA EBOLA ULIOTOKEA KATIKA NCHI JIRANI YA JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO"