SERIKALI kupitia Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesisitiza jamii ya Tanzania juu
ya utumiaji wa maji safi na salama ili kuweza kupambana na ugonjwa wa
kipindupindu kwa urahisi.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara ya Afya) Dkt. Mpoki Ulisubisya wakati wa ufunguzi wa kikao
cha siku tatu cha kujadili mikakati ya kukabiliana na ugonjwa kipindupindu
nchini kinachoendelea jijini Dodoma.
"Ili kupambana na ugonjwa huu
Watanzania wanatakiwa kutunza mazingira
hasa kutumia vyoo bora pamoja na kutumia maji safi na salama katika jamii
inayotuzunguka" alisema Dkt. Ulisubisya.
Aidha Dkt. Ulisubisya amesema kuwa hadi
sasa kwa takwimu iliyopo inaonesha kuwa watu elfu 32 wameugua na watu 600
wamepoteza maisha kutokana na kipindupindu hapa nchini.
Dkt. Ulisubisya amesema kuwa ili kuweza
kutokomeza ugonjwa huo mpaka kufikia 2030 wadau mbalimbali ikiwemo Wizara ya
maji, TAMISEMI, na wadau wengine wa afya
wanatakiwa kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na Shirika la Afya Duniani
(WHO) katika kuweka mikakati ya kupambana na ugonjwa wa kipindupindu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya
Waziri Mkuu Prof. Faustine Kamuzora amesema kuwa Serikali itaendelea kuwaweka
pamoja wataalam mbalimbali kwa ajili ya kuzuia ugonjwa wa kipindupindu nchini
Tanzania.
Aidha Prof. Kamuzora amesema kuwa tayari
wameshaandaa madawati mbalimbali ya wataalamu katika ofisi yake ili kuwexa
kuweka mifumo ya kushughulikia kwa
uharaka magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu.
Naye Afisa wa kudhibiti na kukinga
Magonjwa kutoka Shirika la Afya Duniani hapa
nchini Dkt. Grace Saguti amesema kuwa kutokana na ushirikiano wa wadau
mbalimbali Serikali ya Tanzania imeweza kufanikiwa kutokomeza ugonjwa wa Kipindupindu kwa sehemu
kubwa ya Tanzania.
"Mpaka hivi sasa mikoa inayokabiliwa na
ugonjwa wa kipindupindu katika maeneo
yake ni Rukwa, Songwe na Arusha lakini maeneo yote yaliyobaki tumefanikiwa
kutokomeza ugonjwa huo" alisema Dkt. Saguti.
0 on: "JAMII YA TANZANIA INATAKIWA KUTUMIA MAJI SAFI NA SALAMA ILI KUEPUKA KIPINDUPINDU. "