Waziri wa Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Ummy Mwalimu
akisisitiza jambo wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya uendeshaji wa
hospitali za rufaa za mikoa mbele ya kamati ya kudumu ya bunge ya huduma
na maendeleo ya jamii jijini Dodoma.
Naibu waziri wa Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Dkt.
Faustine Ndugulile akiwasilisha ripoti ya uendeshaji wa Hospitali za
rufaa za mikoa mbele ya wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge huduma na
maendeleo ya jamii jijini Dodoma.
Waziri wa Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Ummy Mwalimu akiteta jambo na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Dkt.
Faustine Ndugulile wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya uendeshaji wa
hospitali za rufaa za mikoa mbele ya kamati ya kudumu ya bunge ya huduma
na maendeleo ya jamii jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya huduma na maendeleo ya jamii Mhe. Peter Selukamba akitoa neno wakati wa kuwasilisha kwa taarifa za
uendeshaji wa hospitali za rufaa za mikoa kutoka wizara ya afya,
maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto jijini Dodoma.
Wajumbe wakifuatilia mjadala uliokua unaendelea katika kikao cha
mawasilisho ya taarifa za uendeshaji wa Hospitali za rufaa za mikoa
kutoka wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto
katika kamati ya kudumu ya Huduma na maendeleo ya jamii jijini Dodoma
SERIKALI IMETENGA BILIONI 30 KUJENGA HOSPITALI ZA RUFAA ZA MIKOA
Na.WAMJW-Dodoma
Serikali
imetenga shilingi bilioni 30 kwa ajili ya kujenga na kukarabati
miundombinu ya hospitali zaRufaa za Mikoa kila mkoa ili kuweza
kuwawezesha wananchi kupata huduma za rufaa za kibingwa karibu na
wanapoishi na hivyo kupunguza adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata
huduma hizo
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa
Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Faustine Ndugulile
wakati akiwasilisha taarifa za uendeshaji wa hospitali za rufaa za Mkoa
kwa kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Jijini
Dodoma.
Dkt. Ndugulile amesema kuwa fedha hizo
zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha hospitali za Rufaa za Mikoa ya
Geita, Katavi, Simiyu, Njombe na Songwe ambapo zipo katika hatua za
ujenzi wa hospitali hizo hivyo itafanya idadi ya hospitali hizo kuwa 28
pindi zitakapokamilika.
“Serikali ilifanya
mabadiliko ya kuzihamishia hospitali za Rufaa za Mikoa Wizarani ili
kuboresha huduma za kibingwa ikiwemo kutoa fursa nzuri ya udhibiti
,usimamizi na mgawanyo wenye tija zaidi wa rasilimali chache
zilizopo”alisema Dkt.Ndugulile.
Alisema kuwa baada
ya Wizara kukabidhiwa hospitali hizo ilifanya tathimini ya awali ya
hali halisi na kubaini changamoto mbalimbali zilizoathiri utoaji wa
huduma za afya katika maeneo yote ambayo ni nguzo ya msingi katika
kuwezesha upatikanaji wa huduma bora.
“Hospitali za
Rufaa za Mikoa zinapaswa kutoa huduma za kibingwa ambazo hazitolewi
katika hospitali ngazi ya Halmashauri,Huduma za kibingwa ambazo ni
lazima kupatikana katika hospitali za Rufaa”.Alisema Naibu Waziri Dkt.
Ndugulile
Alitaja huduma za kibingwa ambazo
zinatakiwa kutolewa katika hospitali hizo za Rufaa za Mikoa ni pamoja na
upasuaji wa jumla,magonjwa ya uzazi na yanayoathiri wanawake, magonjwa
ya watoto,magonjwa ya ndani ,magonjwa ya kinywa na meno na Radilojia.
Kwa
upande wa ubora wa huduma zinazotolewa Naibu Waziri huyo alisema Wizara
ilifanya kaguzi za kuzitambua hali halisi ya ubora wa huduma za afya
zinazotolewa katika hospitali hizo na jumla ya hospitali za rufaa
ishirini na moja zilifanyiwa tathimini na kupewa nyota kutokana na
vigezo vilivyowekwa na kupewa mpango kazi wa kuboresha huduma .
“Ni
hospitali 9 zilipata nyota mbili, hospitali kumi na moja zilipata nyota
moja na hospitali moja ilipata nyota sifuri,hivyo hakuna hospitali
yeyote iliyopata nyota 3 hapa nchini.Alimalizia Dkt.Ndugulile
0 on: "SERIKALI IMETENGA BILIONI 30 KUJENGA HOSPITALI ZA RUFAA ZA MIKOA"