Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuendelea kuwekeza na kuboresha upatikanaji wa huduma za tiba za kibingwa nchini na kupunguza gharama za matibabu kwa watanzania waliokuwa wanapata huduma hizo nje ya nchini.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Stanslaus Nyongo kwenye kikao cha Kamati hiyo na Wataalam wa Wizara ya Afya na Tasisi zake kilichofanyika kwenye kumbi ya mikutano ya Bunge.
“Nazipongeza Taasisi zote zilizowasilisha taarifa zao, hongera kwa uzalendo wenu wa kuendelea kuokoa maisha ya Watanzania na kuipunguzia Serikali gharama za matibabu nje ya nchi” Amesema Mhe. Nyongo
Mheshimiwa Nyongo amesema kupitia kamati hiyo itaendelea kutoa ushirikiano na Wizara a Taasisi zake kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora za tiba nchini na kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wataendelea kuishauri Serikali kuwekeza zaidi kwenye huduma zia tiba za kibingwa na kuhakikisha huduma zote za tiba zinapatikana hapa nchini na kuvutia zaidi utalii wa tiba (Medical Tourusm) kwa raia wa kigeni wenye uhitaji wa tiba zinazopatikana hapa nchini.
Awali akisoma taarifa ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Julius Mwaiselage amesema kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwa kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma za kibingwa katika taasisi hiyo uliohusisha manunuzi ya mashine za kitaalam pamoja na ujenzi wa majengo umewezesha kupunguza rufaa za wagonjwa wa saratani kwenda nje ya nchi kutoka wagonjwa 164 mwaka 2014/15 hadi wagonjwa 5 mwaka 2019/20.
Dkt. Mwaiselage ameendelea kwa kusema kuwa na miundombinu hiyo hapa nchini Serikali imeweza kuokoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 10.4 kwa kutopeleka wagonjwa 208 nje ya nchi huku wagonjwa wanaotoka nchi jirani kwa ajili ya tiba imeongezeka kutoka wagonjwa 12 mwaka 2014/15 hadi kufikia wagonjwa 73 mwaka 2019/20 hivyo kuongeza mapato kwa Serikali.
“Kutokana na miundombinu tuliyonayo sasa idadi ya wagonjwa wanaotibiwa kwa siku imengezeka kutoka wagonjwa 170 hadi kufikia wagonjwa 270. Aidha tumeweza kupunguza muda wa kusubiri tiba mionzi kutoka wiki 6 mwaka 2014/15 hadi kufikia ndani ya wiki 2 mwaka 2019/20 muda ambao ndio kiwango kinachokubalika cha kusubiri tiba duniani” amefafanua Dkt. Mwaiselage.
Akiwasilisha taarifa ya Taasisi ya Mifupa (MOI) Dkt. Vivina Wananji amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne taasisi hiyo imeweza kufanya upasuaji wa kibingwa kwa wagonjwa 43,200 ambapo kwa gharama za hapa nchini upasauji huo umegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 16.5 na kama wangepelekwa nje ya nchi matibabu yangegharimu kiasi cha Shilingi Biloni 54.9 hivyo kuokoa kiasi cha Shilingi Bilioni 38.4
Dkt. Wananji amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imetoa kiasi cha Shilingi Bilioni 7.9 kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya kisasa ya upasuaji wa ubongo (Ango-Suite).
“Maabara hii itaiwezesha taasisi kufanya upasuaji wa matatizo ya mishipa ya damu kichwani pasipo kulazimika kufungua fuvu la kichwa, vilevile mashine hii itakua na uwezo wa kutibu damu iliyoganda kwenye mishipa ya damu miguuni, kwenye moyo, tumbo la uzazi, ini na figo” Amefafanua Dkt. Wananji na kuendelea kusema kuwa matibabu kwa kutumia maabara hiyo ni ya haraka hivyo wagonjwa wengi watapata huduma kwa muda mfupi huku uwepo wa Maabara hii utaifanya Tanzania kuwa moja ya Nchi chache Barani Afrika zinazotoa huduma hiyo.
Kwa upande wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohhamed Janabi amesema kuwa Taasisi hiyo yenye miaka mitano toka ianzishwe imekuwa ikihudumia wagonjwa kutoka mikoa yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wamepewa rufaa kutoka Hospitali za mikoa na za wilaya zilizoteuliwa kwa ajili ya kupata huduma ya kiwango cha juu cha tiba ya Moyo, vilevile na wagonjwa wanokuja moja kwa moja kwa matibabu kutoka nje ya nchi.
Prof. Janabi amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya ilitoa kiasi cha Shilingi Bilioni moja kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vitavyosaidia kuboresha zaidi huduma za kibingwa hapa nchini.
Amezitaja mashine hizo kuwa ni ‘Intra-Aotic balloon Pump’ inayotumika kutibu wagonjwa wenye matatizo ya kuziba mishipa ya damu, ‘Anaesthesia Machine’ inatumika kutoa dawa ya usingizi kwa ajili ya kulaza wagonjwa wanapoingia kwenye upasuaji wa moyo, ‘ICU ECHO Machine’ ambayo inatumika kwa ajili ya kuangalia uwezo wa moyo kufanya kazi, pamoja na ‘Syringe Pumps’ ambazo hutumika kupeleka vimininika (dawa) kwenye mwili wa binadamu kupitia mishipa ya damu. Vifaa tiba vyote hivi vimenunuliwa kutoka fedha za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwisho