Na WAMJW – Dar Es Salaam
Wauguzi na wakunga nchini wamekumbushwa kuhakikisha wanatunza vizuri taarifa za kazi kwenye
majarada ya kazini kwa kuandika yale yote ambayo wanafanya tangu wanapoingia kazini hadi kutoka.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Ziada Sellah alipokuwa akizungumza na wauguzi na wakunga katika
Hosptali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala – Dar Es Salaam.
“Kila unachofanya kazini aidha umemhudumia mgonjwa au ukiwa na majukumu mengine hakikisheni
mnatunza taarifa za kazi kwa kuandika kwenye majadara yenu ya kazi” amesema Bi. Ziada
Bi. Ziada amesema kuwa kwa kufanya hivyo itawasaidia pia madaktari, wauguzi na wakunga wengine
wanaoingia zamu tofauti kutambua kwa haraka nini ambacho kimefanyika na kuweza kuendelea na kazi
ambayo wengine wameacha.
Amesema kuwa wauguzi na wakunga wamekuwa wakilaumiwa kwa kutotunza vizuri taarifa za utendaji
kazi jambo ambali hupelekea changamtoto kwa wagonjwa kutopata huduma sahihi wakiwa hospitalini.
“Tumekuwa tukilaumiwa hatutunzi kumbukumbu zetu vizuri, andikeni kila mnachofanya, kama umemwita
daktari saa 1, hadi saa 3 hajafika andikeni, tufanye ‘documentation’ kadiri inavyowezekana” amesisitiza
Bi. Ziada.
Hata hivyo Bi. Ziada Sellah hakusita kuwakumbusha wauguzi na wakunga kufanya kazi kwa malengo ili
waweze kujipima ufanisi wa kazi zao na kujua eneo wanapofanya vizuri na kwenye changamoto.
“Tufanye kazi kwa malengo ili mwisho wa siku tuweze kujipima kwa kufanya tathimini ya malengo
tuliyojiwekea kubaini kama tumeweza kuyatimiza” amesema Bi. Ziada.
Amesema kuwa malengo yanaweza kuwa ya siku moja hadi mwaka mmoja kulingana shabaha
ulizojiwekea muuguzi au mkunga na yatawaongoza kujua ni wapi walikwama na wapi walifanikiwa.
Mwisho
Jumamosi, 17 Oktoba 2020
WAUGUZI NA WAKUNGA WATAKIWA KUTUNZA TAARIFA ZA UTENDAJI WAO WA KAZI KILA SIKU
Ijumaa, 16 Oktoba 2020
WANANCHI WAKUMBUSHWA KUCHUKUA TAHADHARI KUJIKINGA NA MAGONJWA YA MLIPUKO
Watanzania wamekumbushwa kuzingatia kanuni za afya na kuchukua tahadhari ili kuweza kujikinga na magonjwa ya mlipuko kufuatia kuanza kunyesha kwa mvua kubwa katika baadhi ya maeneo ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam na kusababisha mafuriko na uharibifu wa miundombinu.
Tahadhari hiyo imetolewa leo na Prof. Abel Makubi Mganga Mkuu wa Serikali , Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakati akiongea na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Wizara jijini Dodoma.
“Kufuatia mvua hizi, ni wazi kuwa uwezekano mkubwa wa kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa Kipindupindu, kuhara damu, na yale yanayoenezwa na mbu ikiwemo ugonjwa wa Malaria na Dengue, endapo wananchi hawatazingatia kanuni za afya na kuchukua tahadhari mapema” Alisema Prof. Makubi.
Prof. Makubi amesema kufuatia kujitokeza kwa uharibifu wa miundo mbinu ikiwemo ile ya kusafirisha na kuhifadhia maji safi na taka hali hiyo ina hatarisha afya ya jamii na hivyo kuongeza uwezekano wa kusababisha kuenea kwa urahisi kwa magonjwa ya kuambukiza na yale ya mlipuko.
Aidha, Mganga Mkuu huyo amewakumbusha wananchi kuzingatia kanuniz za afya kwa kuchemsha maji kabla ya kunywa au kutatibu kwa dawa maalumu na kuhakikisha maji ya kunywa nay ale ya matumizi ya nyumbani yanahifadhiwa katika vyombo safi.
“Tunawapongeza wananchi na ninyi wanahabari kwa kuendelea kutoa elimu katika kujikinga na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu kwa sababu wananchi wamekuwa wasikivu na kutii masharti ya usafi na jinsi ya kujikinga,ni zaidi ya mwaka na nusu sasa Tanzania tumeweza kudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu nchini”.
Aidha, amesema jitihada kubwa za maboresho ya miundombinu ikiwemo kuongezeka kwa kiwango cha upatikanaji wa maji safi na salama na ushirikiano mzuri wa wananchi na hivyo kusababisha baadhi ya magonjwa yanayotokana na uchafu yamepungua.
Hata hivyo Prof. Makubi amesisitiza kutumia ipasavyo vyoo na hasa kipindi hiki cha mvua kunawa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni mara kwa mara hasa,kabla ya kula kabla ya kula,baada ya kutoka chooni,baada ya kumnawisha mtoto aliyejisaidia na baada ya kumhudumia mgonjwa.
“Tuongeze usimamizi wa usafi wa nyumba na hasa usafi wa mikono wananchi wamekua wakihamasika usafi wa mikono katika vipindi mbalimbali,hivyo tungeomba kasi ya kunawa mikono iwe endelevu katika mikusanyiko, mashule, madukani, hospitalini,vituo vya mabasi,na taasisi pamoja na masoko,sehemu za kunawia mikono iwe ndelevu kuhakikisha wananchi wanakuwa na usafi wa kunawa mikono wa hali ya juu.
Pia,aliwata Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, wanaelekezwa kushirikiana kwa karibu na viongozi wengine wa Serikaili za mitaa, Wananchi na wadau mbali mbali ili kuhakisha kila eneo lilio chini yao, haligeuki kuwa chanzo cha magonjwa ya mlipuko kwa kutotapisha vyoo au vyovyote vinavyotoka kwenye vyoo kwenda kwenye mazingira ya wananchi.
Kwa upande wa kujikinga dhidi ya kuumwa na Mbu Prof. Makubi aliwataka wananchi kutumia ipasavyo vyandarua kabla ya kwenda kulala au wenye uwezo wa kununua dawa za kujipaka wapake ili ziwasaidie.
Prof. Makubi amewataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya hali ya hewa nchini na shime kuimarisha afya kwa kudumisha usafi wa mazingira na tabia za usafi katika familia na jamii kwa ujumla ikiwemo kudhibiti mazalia ya mbu.
-Mwisho-
Jumatatu, 12 Oktoba 2020
WAUGUZI NA WAKUNGA WATAKIWA KUJIENDELEZA KITAALUMA
Wauguzi na Wakunga nchini wamekumbushwa kujiendeleza kitaaluma ili kuweza kuongeza ujuzi zaidi katika utendaji kazi na kutoa huduma zilizo bora zaidi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Ziada Sellah alipokuwa akizungumza na wauguzi na wakunga wa Mkoa wa Mtwara katika kikao kazi kilichofanyika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara (Ligula)
“Tujitahidi twende na kasi wanayokwenda wauguzi na wakunga katika nchi nyingine nasi tujiendeleze kimasomo, hapo zamani tulikuwa tunaishia diploma sasa hivi tuna hadi ‘phd’ hii ina maana tunakuwa" Amesema Bi. Ziada Sellah
Amesema kuwa wauguzi na wakunga wachangamkie fursa za kujiendeleza kimasomo zinazotolewa na Wizara ya Afya pindi tu zinapotangazwa na wasiridhike ngazi za elimu walizonazo ikiwa wana nafasi ya kujiendeleza zaidi.
Bi. Ziada amesema kuwa kujiendeleza kielimu kuna faida nyingi ikiwemo, kuongeza ujuzi zaidi katika kazi, kuwa na uhakika na kile unachokifanya ukiwa kazini na kupelekea utendaji kazi mzuri pamoja na kuwa kwenye nafasi ya kupanda madaraja ya mshahara kwa haraka.
Awali akizungumza Bi. Jamila Hamudu kutoka Idara ya Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya amesema kuwa Wizara kwa kushirikiana na mamlaka husika wanapitia upya muundo wa kada hizo na endapo utakidhi vigezo husika itapindishwa na kuwa muundo rasmi wa kada za uuguzi na ukunga.
Alitumia fursa hiyo kuwahimiza wauguzi na wakunga kujiendeleza kimasomo zaidi ili kunufaika na muundo huo ambao umeongeza majumuku ya kada hizo pamoja na stahiki zao.
Kwa upande wake Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Bw. Ahmed Chibwana amesema kuwa Mkoa huo una jumla ya wauguzi 780 ambao wanatoa huduma mbali mbali katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Aidha, Bw. Chibwana amesema kuwa majumuku ya wauguzi yamekuwa yakiongezeka kuliko na ilivyokuwa awali na wamekuwa na mwamko wa kazi huku akiomba mamlaka husika kuwaangalia upya wauguzi na wakunga ili stahiki zao ziendane na kazi wanazofanya.
“Niwapongeze wauguzi hawa, kwa moyo wa kujitoa, licha ya kuongezeka kwa kazi wanazofanya lakini wamekuwa na moyo wa kujituma kuhakikisha wanatoa huduma bora, tunaziomba mamlaka husika kuwaangalia upya wauguzi hawa” amesema Bw. Chibwana.
Naye, Bi. Albertina Mlowala Afisa Muuguzi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara (Ligula) ameomba Wizara kuongeza watumishi wa kada za afya mkoani humo ili kupunguza wingi wa kazi kwa wauguzi na kuhakikisha wanatoa huduma bora zaidi.
Mwisho.
Jumatano, 7 Oktoba 2020
SERIKALI IMEFANIKIWA KUWEKEZA KWENYE UTOAJI HUDUMA ZA AFYA NCHINI
Na. Catherine Sungura.WAMJW-DSM
erikali kupitia Wizara ya Afya imefanikiwa kuwekeza kwenye utoaji huduma za afya kwa wananchi wote nchini kwa kuboresha majengo,dawa,vifaa na vifaa tiba.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF) Bernad Konga mwanzoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa mpango wa dunduliza utakaomuwezesha mwananchi kudunduliza fedha kidogokidogo za mchango wa bima ya afya kupitia bank ya NMB.
Konga alisema kuwa ili wananchi kuwa na uhakika wa matibabu,Serikali iliona kutafuta namna nyepesi ya mwananchi wa hali ya chini aweze kujiunga na mfuko wa bima ya afya kwa kuweka kidogo kidogo kwa muda atakaochagua na atakapokamilisha kiwango husika atapatiwa kadi ya matibabu na kuanza kunufaika na huduma za matibabu kupitia NHIF.
"Serikali imejipanga kumfikia kila mwananchi bila kujali hali yake kikazi na hata makazi,lengo ni kila mwananchi kuwa na uhakika wa matibabu katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya kwa kuwa na bima ya afya ya NHIF".Alibainisha
Hata hivyo Mkurugenzi huyo alisema Serikali inaendelea na utoaji elimu yenye lengo la kuwajengea wananchi utamaduni wa kuwa na bima kabla ya kuugua na sasa imekuja na mpango wa kujiwekea fedha kwa njia ya benki kwa ajili yake na familia yake.
"Menejimenti ya mfuko iliona uwezo wa wananchi kulipa fedha zote kwa awamu moja itakua ni changamoto,hivyo tumefungua milango wananchi wadundulize kidogo kidogo ili wawe na uhakika wa matibabu wakati wowote ".
Mwananchi anayehitaji kujiunga na huduma za NHIF ambaye atahitaji kuweka fedha kidogo kidogo kwa muda atakaochagua ni yule,anayejiunga kupitia mpango wa vifurushi ambavyo vinajulikana kwa majina ya Najali Afya,Wekeza Afya na Timiza Afya ambavyo pia vinampa fursa mwananchi anayehiraji kuchangia kuchagua huduma kulingana na mahitaji yake,umri na wanufaika anaohitaji kuwajumuisha.
Mpango huu unamwezesha mwananchi kujiwekea fedha kwa ajili yake mwenyewe ama kwa ajili yake na mwenza wake ama kwa ajili yake na mtoto ama watoto alionao.
Mfumo huo pia ni rahisi kuutumia kwa kuwa unahitaji mtumiaji kuwa na,simu ya mkononi ya aina yoyote na kuzingatia hatua zilizoweka na endapo atakwama hatua za kujisajili anaweza kupiga simu bila malipo kwa namba 0800110063 kupatiwa maelezo namna ya kufanya.
-Mwisho-