Wauguzi na Wakunga nchini wamekumbushwa kujiendeleza kitaaluma ili kuweza kuongeza ujuzi zaidi katika utendaji kazi na kutoa huduma zilizo bora zaidi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Ziada Sellah alipokuwa akizungumza na wauguzi na wakunga wa Mkoa wa Mtwara katika kikao kazi kilichofanyika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara (Ligula)
“Tujitahidi twende na kasi wanayokwenda wauguzi na wakunga katika nchi nyingine nasi tujiendeleze kimasomo, hapo zamani tulikuwa tunaishia diploma sasa hivi tuna hadi ‘phd’ hii ina maana tunakuwa" Amesema Bi. Ziada Sellah
Amesema kuwa wauguzi na wakunga wachangamkie fursa za kujiendeleza kimasomo zinazotolewa na Wizara ya Afya pindi tu zinapotangazwa na wasiridhike ngazi za elimu walizonazo ikiwa wana nafasi ya kujiendeleza zaidi.
Bi. Ziada amesema kuwa kujiendeleza kielimu kuna faida nyingi ikiwemo, kuongeza ujuzi zaidi katika kazi, kuwa na uhakika na kile unachokifanya ukiwa kazini na kupelekea utendaji kazi mzuri pamoja na kuwa kwenye nafasi ya kupanda madaraja ya mshahara kwa haraka.
Awali akizungumza Bi. Jamila Hamudu kutoka Idara ya Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya amesema kuwa Wizara kwa kushirikiana na mamlaka husika wanapitia upya muundo wa kada hizo na endapo utakidhi vigezo husika itapindishwa na kuwa muundo rasmi wa kada za uuguzi na ukunga.
Alitumia fursa hiyo kuwahimiza wauguzi na wakunga kujiendeleza kimasomo zaidi ili kunufaika na muundo huo ambao umeongeza majumuku ya kada hizo pamoja na stahiki zao.
Kwa upande wake Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Bw. Ahmed Chibwana amesema kuwa Mkoa huo una jumla ya wauguzi 780 ambao wanatoa huduma mbali mbali katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Aidha, Bw. Chibwana amesema kuwa majumuku ya wauguzi yamekuwa yakiongezeka kuliko na ilivyokuwa awali na wamekuwa na mwamko wa kazi huku akiomba mamlaka husika kuwaangalia upya wauguzi na wakunga ili stahiki zao ziendane na kazi wanazofanya.
“Niwapongeze wauguzi hawa, kwa moyo wa kujitoa, licha ya kuongezeka kwa kazi wanazofanya lakini wamekuwa na moyo wa kujituma kuhakikisha wanatoa huduma bora, tunaziomba mamlaka husika kuwaangalia upya wauguzi hawa” amesema Bw. Chibwana.
Naye, Bi. Albertina Mlowala Afisa Muuguzi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara (Ligula) ameomba Wizara kuongeza watumishi wa kada za afya mkoani humo ili kupunguza wingi wa kazi kwa wauguzi na kuhakikisha wanatoa huduma bora zaidi.
Mwisho.
0 on: "WAUGUZI NA WAKUNGA WATAKIWA KUJIENDELEZA KITAALUMA"