Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo UMMY MWALIMU. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo UMMY MWALIMU. Onyesha machapisho yote

Jumatatu, 20 Juni 2022

WADAU WA MAENDELEO KUCHAGIA BILIONI 98.1 KUPITIA MFUKO WA AFYA WA PAMOJA

Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu akisema jambo kwenye Mkutano na Wadau wa Maendeleo wanaochangia kwenye Mfuko wa Afya wa pamoja (hawapo pichani) uliofanyika Jijini Dar Es Salaam.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange akisema jambo kwenye Mkutano na Wadau wa Maendeleo wanaochangia kwenye Mfuko wa Afya wa pamoja (hawapo pichani) uliofanyika Jijini Dar Es Salaam.





Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu (wa kushoto) akisema jambo na wadau wa maendeleo wanaochangia fedha kwenye Mfuko wa Afya wa pamoja (Health Basket Fund)


Na Englibert Kayombo - Dar es Salaama

Wadau wa Mfuko wa Afya wa pamoja nchini (Health Basket Fund) wamepanga kuchangia kiasi cha shilingi Bilioni 98.1 kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini kwa mwaka 2022/2023.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa kikao cha kujadili uboreshaji wa mfuko huo kupitia ushirikiano wa pamoja  kati ya Serikali na wadau Jijini Dar Es Salaam.

“Kwa niaba ya Serikali tunawashukuru wadau wetu wanaochangia kwa pamoja kwenye Mfuko wa Afya na tunatarajia kwa Mwaka wa fedha ujao wa 2022/23 wadau wetu kwa pamoja kuchangia Shilingi Bilioni 98.1 na fedha hizo zitaingizwa moja kwa moja kwenye akaunti za Vituo vya kutolea huduma za Afya nchini” amesema Waziri Ummy Mwalimu

Waziri Ummy amesema katika mwaka wa fedha uliopita wadau kupitia Mfuko walichangia kiasi cha shilingi bilioni 74.3 ambapo asilimia 90 ya fedha zimekwenda kwenye Halmashauri na zimeingizwa moja kwa moja kwenye Zahanati, Vituo vya Afya pamoja na Hospitali za Wilaya nchini.

Aidha Waziri Ummy Mwalimu amesema upo umuhimu kwa wadau wa maendeleo kuchanga fedha kwa pamoja na kuweka kwenye Mfuko wa Afya wa pamoja na kusema kuwa kufanya hivyo ni kuzingatia Mifumo na taratibu za Serikali za kutoa fedha kwa ajili ya Huduma za Afya nchini pamoja na kuwekeza fedha kwenye maeneo ya vipaumbele vya Serikali.

“Fedha zinazoingizwa nchini kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali za afya tunapenda ziingizwe kwenye Mfuko wa Afya wa pamoja ili tuweke kushirikiana kufanya kazi pamoja na kupata matokea ya haraka kwa pamoja.

mapendekezo yetu wadau wengine wachangia kupitia mfuko huo kwani tumeona mafanikio makubwa" amefafanua Waziri Ummy Mwalimu.

Kwa upande wake Naibu Waziri kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange ameshukuru wadau hao kwa kuendela kutoa ushirikiano na Serikali na kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Mhe. Dugange amepongeza wadau hao kwa kuongeza kiwango cha fedha kutoka Shilingi Bilioni 74.3 mwaka wa fedha 2021/22 hadi Bilioni 98.1 kwa mwaka wa fedha 2022/23 na kusema kuwa kupitia mchango huo pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanyika, Serikali kufanya mapinduzi makubwa kwenye ubora wa huduma za afya kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Mhe. Dkt. Dugange amesema kuwa asilimia 33.3 ya fedha hizo hutumika kwenda kununua dawa, vifaatiba na ‘reagents’ kwa ajili ya vipimo vya maabara ikiwa na pamoja kuboresha huduma za mama na mtoto katika vituo vya kutolea huduma za afya.

“Kwa mwaka huu wa fedha 2022/23 vituo zaidi ya 175 vimepata vifaatiba kwa ajili ya huduma za upasuaji, lakini kwa mwaka ujao wa fedha, tunatarajia vituo zaidi ya 225 vitapata vifaatiba” amefafanua Mhe. Dugange

Akizungumza kwa niaba ya Wadau wanaochangia katika Mfuko wa Afya wa pamoja, akizungumza na vyombo vya Habari Dkt. Peter Nyela Meneja wa Program ya Afya kutoka Ubalozi wa ‘Ireland’ wanafanya hivyo kusaidia Serikali ili kuhakikisha Vituo vya kutolea huduma za afya nchini vinakuwa na dawa, kurahisisha huduma nyinginezo ikiwemo huduma za rufaa, pamoja na motisha kwa watoa huduma za afya nchini.

Huu ni ushirikiano mzuri sana baina ya Serikali na Wadau wa Maendeleo kuweza kufanya kazi kwa pamoja kuweza kusaidia kuboresha huduma za Afya nchini, Sisi kama Wadau kwa pamoja tutaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuboresha Sekta ya Afya nchini” amefafanua Dkt. Nyela.

Mfuko wa Afya wa Pamoja umedumu kwa miaka 23 hadi kufikia leo ambapo ni muunganiko wa pamoja baina ya Serikali na Wadau wa Maendeleo kutoka Denmark, Korea, Ireland, Switzerland, Canada, UNFPA, UNCEF na Benki ya Dunia ambao huchangia katika huduma za afya nchini kwa kutoa fedha na kuziweka kwenye akaunti moja na fedha hizo kutolewa moja kwa moja kwenye vituo vya  kutolea huduma za afya nchini.

Jumamosi, 14 Desemba 2019

KITUO CHA AFYA KOME CHAFANYA UPASUAJI WA KWANZA

Bango la Kituo cha Afya Kome, linalotoa maelekezo ya Huduma zinazotolewa katika kituo hicho.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akiongea na moja kati ya mama aliyefika kupata huduma katika kituo cha Afya Kome, Halmashauri ya Buchosa, Sengerema Mwanza.


KITUO CHA AFYA KOME CHAFANYA UPASUAJI WA KWANZA

Na.Catherine Sungura

Kituo cha afya Kome kilichopo halmashauri ya buchosa wilayani Sengerema kimefanikiwa kufanya upasuaji wa kwanza  wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni na hivyo kumuokoa mama na mtoto wake.

Akiandika kwenye mtandao wa kijamii Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema kuwa kwa mara ya kwanza kituo hicho kimeweza kufanya upasuaji huo baada ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  kujenga “theatre” na kuweka vifaa tiba kwenye kituo hicho.

Waziri Ummy ameendelea kuandika kuwa chumba hicho cha upasuaji ambacho kipo kituoni hapo kitawasaidia akina mama wajawazito wa kisiwa cha kome watakaopata uzazi pingamizi na hivyo kutokufuata huduma hizo wilayani sengerema na hivyo kutokuvuka tena maji.

“Hakika tumedhamiria kuokoa maisha  ya akina mama wajawazito na watoto wachanga,tutaendelea kuchukua hatua ili kuhakikisha huduma za uzazi  za dharura ikiwemo ya upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni(CEmONC) zinapatikana katika vituo vyote vya afya vya umma ,mama na mtoto huyo mwenye uzito wa kilo 3 na nusu wanaendelea vizuri”Amesema waziri Ummy

Naye Mganga Mkuu wa halmashauri ya buchosha Dkt. Ernest Chacha amesema walimpokea mama huyo kituoni hapo siku ya ijumaa ambaye alikua akihudhuria kliniki kwenye zahanati moja huko kisiwani hakuweza kujifungua kawaida kwani alikua akikabiliwa na uchungu pingamizi kwani nyonga zake  hazikuwa zinapanuka hivyo ili kumuokoa ilibidi afanyiwe upasuaji kuweza kumuokoa mama pamoja na mtoto .

Dkt. Chacha ameishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa uboreshaji wa vituo vya afya nchini ikiwemo kituo cha afya cha kome ambacho kipo kisiwani kwa kuboresha miundombinu kwa kujengewa chumba cha upasuaji pamoja na kuwekewa vifaa tiba hivyo kusaidia kuokoa maisha ya akina mama wajawazito na watoto wachanga hususan visiwani humo.

“Wananchi walikua wanapata adha kubwa sana ya kuvuka maji kutoka kisiwani na kufuata huduma kwenye hospitali ya wilaya iliyopo sengerema,tunamshukuru Waziri Ummy Mwalimu kwa kuiagiza MSD kutufungia taa kwenye chumba cha upasuaji wakati wa ziara yake hivi karibuni visiwani hapa kwani tumeweza kuokoa maisha ya huyu mama muda mfupi baada ya taa hizo kufungwa”Amesema Dkt. chacha

Hivi karibu waziri wa afya alitembelea kisiwa hicho na kuwaahidi  kuwapatia xray mashine ya kidigitali  kwenye kituo hicho cha afya na kuwataka MSD kufunga taa kwenye chumba hicho cha upasuaji mara moja.

Kisiwa cha kome kimeongeza  idadi ya akina mama wanaojifungulia  kwenye vituo vya afya  kwa  asilimia 80  kwa mwaka ambapo wastani akina mama  50 wanajifungulia kwa mwezi

Alhamisi, 12 Desemba 2019

SERIKALI YAAGIZA HOSPITALI ZOTE NCHINI KUANZISHA MFUKO WA FEDHA ZA DAWA.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu akieleza jambo wakati wa kikao cha kuzindua Bodi ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu akiteta  jambo na Mwenyekiti mpya wa Bodi ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure  Prof. Abel Makubi wakati wa kikao cha kuzindua Bodi hiyo.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu akikata  utepe ikiwa kama ishara ya uzinduzi wa Bodi mpya ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure, Kulia kwake ni Mwenyekiti mpya wa Bodi Prof. Abel Makubi, kushoto kwake ni Kaimu RMO Mkoa Mwanza Dkt. Silas Wambura.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu na Mwenyekiti mpya wa Bodi ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure wakiwa wamebeba kitabu cha mwongozo wa Bodi ya ushauri,  wakati wa kikao cha kuzindua Bodi hiyo.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu akimkabidhi mwongozo mmoja kati  ya wajumbe wa Bodi mpya ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure, katikati ni Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Silas Wambura.

Baadhi ya Watumishi wa Hospitali  ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure waliofika kushuhudia uzinduzi wa Bodi mpya ya ushauri ya Hospitali hiyo, uliofanywa na Waziri wa Afya Mhe.@umwalimu katika ukumbi wa RMO Mkoa wa Mwanza.

Baadhi ya Watumishi wa Hospitali  ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure na Wajumbe wa Bodi ya zamani  ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure, waliofika kushuhudia uzinduzi wa Bodi mpya ya ushauri ya Hospitali hiyo, uliofanywa na Waziri wa Afya Mhe.@umwalimu katika ukumbi wa RMO Mkoa wa Mwanza.

Picha ya pamoja ikiongozwa na Waziri wa Afya Mhe.@umwalimu, akiwa na wajumbe wa Bodi mpya ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure baada ya uzinduzi wa Bodi hiyo.


SERIKALI YAAGIZA HOSPITALI ZOTE NCHINI KUANZISHA MFUKO WA FEDHA ZA DAWA.

Na Rayson Mwaisemba, WAMJW- MWANZA

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeagiza Waganga Wakuu wa Vituo vya Afya na Hospitali zote nchini kuanzisha mfuko wa fedha za Dawa kupitia makusanyo ya fedha za ndani, ili kuweza kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa dawa nchini endapo itatokea.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu katika kikao cha uzinduzi wa Bodi mpya ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza.

"Kuanzia Vituo vya Afya, Hospitali zote za Halmashauri, za Mikoa , kuanzisha mfuko wa fedha za dawa, na vyanzo vikuu vya mifuko hii ni mapato yatokanayo na mauzo ya dawa, huduma za Maabara, huduma za mionzi" alisema Waziri @umwalimu.

Amesema, Bodi hiyo ya ushauri lengo lake kubwa ni kuhakikisha inaboresha huduma za kinga na tiba katika Hospitali, huku ikihakikisha huduma hizo zinaifikia wananchi kwa ubora na gharama nafua.

Aliendelea kusema, Sera ya Afya nchini inawataka Wananchi kuchangia huduma kwa gharama nafuu isipokuwa kwa makundi yote ya msamaha, wakiwemo Wazee, Watoto walio chini ya miaka mitano na mama wajawazito, hivyo kuwataka kuweka mifumo mizuri ili kurahisisha utoaji huduma.

Mbali na hayo, Waziri Ummy ameiagiza Bodi hiyo kuhakikisha inaboresha huduma za dharura na ajali, ili kuokoa vifo vitokanavyo weza kuepukika kupitia huduma za dharura, keisha kuwashauri kujenga jengo jipya la wagonjwa wa nje (OPD) ili kuboresha huduma kwa wananchi.

"Watu wengi wanakufa wakiwa getini Mwa Hospitali, wakati utaalamu upo, kwamba mkiboresha huduma za dharura na ajari, tunaweza kuokoa maisha ya watu wengi " alisema Waziri @umwalimu.

Aidha, Waziri Ummy ameeleza majukumu ya Bodi hiyo ni kushauri, kutengeneza, kusimamia na kupitisha miongozo, malengo na mipango mikakati ya Hospitali kulingana na Sera na miongozo ya Serikali.

Nae Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sekou-Toure Dkt. Dkt. Graham Mtui ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuendelea kuboresha huduma za Afya katika Hospitali hiyo kwa kuleta mashine ya uchunguzi wa figo na ini, mashine ya kusafisha figo ambazo zinatarajia kuanza kutoa huduma Januari 2020.

Kwa upande mwingine amesema, Hospitali inatarajia kupokea mashine sita ikiwemo CT Scan, X- ray yakidigitali, vifaa vya mifupa na mashine zinazosaidia kupumulia kutoka MSD.

Hata hivyo, amesema kuwa, idadi ya Wagonjwa wanaofika kupata huduma, kutoka wastani wa wagonjwa 350 kwa siku kwa mwaka 2015 hadi kufikia wagonjwa kati ya 500 mpaka 700 kwa Mwaka huu 2019, huku akiweka wazi kupunguza Rufaa za kwenda Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Bugando kwa asilimia 50.

"Kutokana na mafanikio hayo, idadi ya wagonjwa wanaopata huduma katika Hospitali imeongezeka, kutoka wastani wa wagonjwa 350 kwa siku ambayo ilikuwa mwaka 2015, na kufikia wastani wa wagonjwa kati ya 500 hadi 700 kwa mwaka huu 2019", alisema Dkt. Graham Mtui.

Mwisho.

Jumapili, 1 Desemba 2019

MAAMBUKIZI YA VVU YASHUKA NCHINI

Logo ya Siku ya UKIMWI.

Hadi sasa Watanzania milioni.1.4 wanaoishi na VVU ambapo kiwango cha maambukizi kikiwa ni asilimia 4.7 ikilinganishwa na asilimia 7.0 ya mwaka 2014.

Hayo yamesemwa leo na Mgeni rasmi wa maadhimisho ya kitaifa ya siku ya UKIMWI duniani  na Waziri wa Sera,Bunge,Kazi,Vijana,Ajira na Walemevu Mhe. Jenista Mhagama jijini Mwanza.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu.
Waziri Mhagama amesema kuwa maambukizi mapya na vifo  vitokanavyo na UKIMWI pia vimepungua.
 "Tumeweza kupata mafanikio haya kufuatia kuboreshwa kwa huduma.za ART na afua za kinga kama vile utahiri wa kitabibu wa wanaume na kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto"Alisema Waziri Mhagama.

Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Jenister.

Aidha, amesema kiwango  cha watu wanaoishi na VVU walioko kwenye mpango wa ARV kimeongezeka kutoka asilimia 22 mwaka 2009 hadi kufikia asilimia 57 ya mwaka 2017.

Naye Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema mpaka kufikia mwezi Septemba 2019 takribani watu 1,252,205 kati ya wananchi 1,600,000 wanaokadiriwa kuishi na VVU nchini walikuwa wamepima na kufahamu hali zao za maambukizi ya VVU. 
"Hii ni sawa na asilimia 78.3 ya lengo la 90 ya kwanza.
Miongoni mwao wanaume walikuwa 413,985 sawa na asilimia 33, na wanawake walikuwa 838,220 sawa na asilimia 77".

Mhe. Jenister akiwa na Mhe. Ummy Mwalimu.
Kwa upande wa vijana Waziri Ummy amesema kuwa Vijana balehe (umri wa miaka 10 – 19) walikuwa 57,167 sawa na asilimia 4.6, na vijana (umri wa miaka 15 – 24) walikuwa 96,006 sawa na asilimia 7.7.

Aidha, amesema kati ya waliopima na kutambua afya zao watu 1,221,799 sawa na asilimia 97.6 wanatumia ARV. 

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella.

 Hata hivyo alisema Lengo la 90 ya pili ambalo ni asilimia ya kuwa watu waliopimwa na kugundulika kuwa wana maambukizi ya VVU wanatumia dawa za kupunguza makali ya VVU (yaani ARV’s), tayari tumefikia takriban asilimia 98 wanatumia zawa za kupunguza makali ya VVU yaani ARV.

"Lengo la 90 ya tatu, ambalo ni kuhakikisha kuwa asilimia 90 ya wanaotumia ARV’s wamefanikiwa kupunguza wingi wa VVU mwilini Waziri huyo alisema wamefanya vizuri sana,"ni kuwa tumekuwa tukifuatilia kwa karibu hali za watu wanaotumia dawa za kupunguza makali ya VVU".Alisema 

Mhe. Jenister Mhagama akiwa na Mhe. Ummy Mwalimu, wakipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa TACAIDS Leonard Maboko.

Waziri Ummy alitaja mafanikio mengine ya kujikinga dhidi ya maambukizi ni tohara kwa wanaume ambapo kuanzia mwaka 2009 hadi Agosti 2019 jumla ya wanaume 4,456,511 wamefanyiwa tohara kupitia njia za mkoba na huduma katika vituo vya huduma.

Takwimu zinaonesha kwamba watu 953,973 sawa na asilimia 89 ya watu 1,072,650 waliopimwa wingi wa VVU wamefanikiwa kupunguza wingi wa VVU mwilini jambo ambalo ni muhimu katika kinga dhidi ya UKIMWI.Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni "Jamii ni chachu ya mabadiliko,tuungane kupunguza maambukizi mapya ya VVU"

Wananchi waliojitokeza katika viwanja vya Rock City Mall leo, kushuhudia Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani, mgeni rasmi akiwa Waziri Jenister Mhagama, aliyemwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Kassim Majaliwa.

Picha ya Pamoja ikiongozwa na Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Jenister Mhagama, aliyemwakilisha Mgeni rasmi Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Mhe. Kassim Majaliwa.


#TunaboreshaAfya.
#WAMJW









Jumatano, 20 Novemba 2019

BILIONI 127 ZATOLEWA KUCHANGIA MFUKO WA AFYA WA PAMOJA NCHINI TANZANIA

 
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza jambo na Wadau wa Maendeleo wanaochangia Mfuko wa Pamoja wa Afya-HBF (hawapo pichani) walipotembelea Kituo cha Afya Hombolo Jijini Dodoma.

Jengo la upasuaji katika Kituo cha Afya Hombolo lililojengwa kutoka fedha za Mfuko wa Pamoja wa Afya (HBF)

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (wa tatu lutona kushoto) akimuonyesha Balozi wa Denmark nchini Tanzania Bi. Mette Spandet maboresho ya mioundombinu yaliyofanyika katika Kituo cha Afya Hombolo Jijini Dodoma.


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (wa pili upande wa kulia) akiongea jambo na Balozi wa Denmark nchini Tanzania Bi Mette Norgaard Dissing Spandet mapema leo walipotembelea Kituo cha Afya Hombolo kujionea hali ya utoaji huduma.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (kulia) akizungumza na wananchi waliokwenda kupata huduma katika Kituo cha Afya Hombolo Jijini Dodoma.

"Ukiwa mkubwa unawake kuwa nani?; Nataka kuwa kama wewe" (Utani) Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisalimiana na mtoto Agatha Daniel alipotembelea Kituo cha Afya Hombolo leo Jijini Dodoma

Na Englibert Kayombo – WAMJW, Dodoma.

Wadau wa mfuko wa Afya wa pamoja (HBF) wanaofadhili upatikanaji wa huduma za afya ngazi ya jamii wachangia Shilingi Bilioni 127 ili kuboresha huduma za afya nchini.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu alipofaya ziara na wadau wa maendeleo wanaochangia mfuko wa afya wa pamoja walipotembelea Kituo cha Afya Hombolo Jijini Dodoma.

“Tumekuja hapa na wenzetu hawa wanaochangia mfuko wa afya wa pamoja ambapo kwa mwaka huu wa fedha 2019/20 wametupatia Bilioni 127 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya” Amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy amesema kuwa kiasi cha Shilingi BIlioni 104 zitapelekwa kwenye Halmashauri za Wilaya na Sekretarieti za Mikoa kwa ajili ya kuboresha huduma za afya ngazi ya Jamii huku kiasi cha Shilingi Bilioni 23 kikitarajiwa kutumika kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za Afya zinazolenga kuboresha huduma za afya.

“Kwa hiyo tunaona hapa fedha nyingi zitakuja huku chini kwenye Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitli za Wilaya, nawashukuru sana wadau wetu wa maendeleo kwa kutupatia Bilioni 127 kwa ajili kuboresha huduma za Afya Tanzania” amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Kwa upande wake Balozi wa Denmark nchini Tanzania Bi Mette Norgaard Dissing Spandet amesema kuwa mfuko huo umekuwa ukisaidia uboreshaji wa huduma za afya ngaza ya jamii kwa miaka 20 sasa na wanajivunia kuwa na uhusiano wa karibu na kusaidia katika upatikanaji wa bora huduma za afya nchini.

“Tunafuraha kufikia miaka 20 ya kusaidia katika kuboresha huduma za afya nchini Tanzania na tutaendelea kufanya hivyo zaidi kwa miaka mingi inayokuja” amesema Balozi Mette Spandet.

Naye Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Bw. Godwin Kunambi ambaye Jiji lake ni mnufaika wa mfuko huo wa pamoja wa afya amesema kuwa walipokea fedha kiasi cha Shilingi Milioni 500 na walizitumia vizuri kwa kuboresha na kujenga miundombinu katika Kituo cha Afya hapa Hombolo.

“Kwa shilingi Milioni 500 tumeweza kujenga nyumba ya mganga, jengo la kuhifadhi maiti, jengo la upasuaji pamoja na jengo la wodi ya kina mama” anasema Mkurugenzi Kunambi.

Mkurugenzi Kunambi amesema kuwa kwa kutumia mapato ya ndani ya Jiji la Dodoma wamefanikiwa kujenga wodi ya wototo iliyogharimu kiasi cha Shilingi Milioni 63.

Mfuko wa pamoja wa afya unaoratibiwa na Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI  huku wadau wa maendeleo wakiwa ni Nchi ya Switzerland, Canada, Denmark na Korea ya Kusini, Shirika la UNFPA, UNICEF na Benki ya Dunia umekuwa ukichangia kuboresha huduma za afya nchini Tanzania kwa miaka 20 sasa toka mwaka 1999 ambapo huduma za afya ngazi ya jamii zimekuwa zikiimarika mwaka hadi mwaka.

Mwisho

Jumanne, 25 Juni 2019

WAZIRI WA AFYA ASISITIZA UBORA WA BIDHAA KATIKA KIWANDA KIPYA CHA DAWA NA VIFAATIBA SIMIYU.

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (kushoto) akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Dawa na Vifaatiba kwa Profesa Olipa David Ngassapa (kulia)

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisema jambo wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Dawa na Vifaatiba cha Simiyu leo Jijini Dodoma.

Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Dawa na Vifaatiba cha Simiyu wakimsikiliza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (hayupo pichani) wakati akizindua bodi hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Zainab Chaula akisema jambo wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Dawa na Vifaatiba cha Simiyu leo Jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akisema jambo wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Dawa na Vifaatiba cha Simiyu leo Jijini Dodoma.

Picha ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiwa na Watendaji Wakuu ndani ya Wizara ya Afya na Taasisi za Afya pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Dawa na Vifaatiba cha Simiyu.

Na.WAMJW.Dodoma

Bodi ya wakurugenzi wa kiwanda cha dawa na vifaa tiba cha Simiyu(SIMIYU MEDICAL PRODUCTS) wametakiwa  kuzalisha bidhaa zenye viwango na kukidhi mahitaji ya ndani nan je ya nchi.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa bodi ya wakurugenzi wa kiwanda hicho uliofanyika leo jijini hapa.

Waziri Ummy amesema kuwa bidhaa zenye viwango itasaidia kuuza nje ya nchi na watanzania kuzitumia kwani lengo la serikali ya awamu ya tano ni ya kukuza uchumi wa viwanda 

“Lakini mhakikishe maamuzi yeyote mtakayofanya mjiridhishe je ni kwa ajili ya maslahi ya Taifa na je yatatufikisha kule tunapotaka kufika,jiridhisheni katika kuhakikisha mnatumia fedha hizi chache tulizonazo katika kuleta matokeo ya haraka haya ndiyo ya kuyazingatia”.Alisisitiza Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy aliitaka bodi hiyo kuhakikisha wanaongeza thamani ya mazao ya nchi kwa kuzalisha bidhaa nchini na kuondokana na uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi,kuongeza ajira na hata kuondokana na uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Hata hivyo aliwataka wasiangalie bidhaa zinazotakana na pamba hivyo kwa baadae  ni bora wakaangalia bidhaa zingine zinazohitajika ambazo zinanunuliwa kwa haraka sana kutoka MSD kwani bohari ya Dawa hivi sasa imepata mkataba wa kununua bidhaa za hospitali kwa niaba ya nchi kumi na sita za nchi ya SADC hivyo wahakikishe bidhaa zinazozalishwa zina viwango na ubora na uzalishaji unakidhi soko la ndani nan je ya Tanzania.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy amempongeza Mtanzania Dkt. Aswar Hilonga kwa kutunukiwa tunzo na Shirika la Afya Duniani kutokana na Ubunifu wake wa kutengeneza mtambo wa kuchuja na kusafisha maji.

Mtambo huo unaotumia nanotechnology una uwezo wa kuchuja maji na kuyafanya yawe safi na salama kwa matumizi ya binadamu na kuondoa bakteria, kemikali na taka katika maji.

"Asilimia 60 ya wagonjwa wa nje wanaokwenda Hospitalini  wanatokana na kiwango duni cha hali ya usafi  ikiwenyo unywaji wa maji yasiyo safi na salama. Hivyo kupitia teknolojia hii tunaweza kuokoa fedha za Serikali kwa ajili ya kutibu wagonjwa" amesema Waziri Ummy.

Kwa upande wake Dkt. Hilonga ameiomba Serikali kuweza kuunganisha mtambo huo wa maji ambao unauzwa kwa bei nafuu katika Taasisi za Umma ambao unachuja maji kwa kuondoa batkeria na kemikali na taka katika maji ndani ya muda mfupi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (kushoto) akimpongeza Dkt. Askwar Hilonga (kulia) kwa kutunukiwa tuzo kutoka Shirika la Afya Duniani kwa  ubunifu wa mtambo wa kuchuja na kusafisha maji unaotumia nanotechnology kuondoa bakteria, kemikali na taka kwenye maji.

Mwisho.