Jumatano, 13 Aprili 2022
ASILIMIA 26 YA WATU WAZIMA WANASHINIKIZO LA JUU LA DAMU.
Jumatano, 6 Aprili 2022
PROF. MAKUBI ATOA WITO KWA WANANCHI KUWAHI KUFANYA UCHUNGUZI WA SARATANI.
Na Rayson Mwaisemba WAF - DSM.
KATIBU MKUU Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi ametoa wito kwa Watanzania kujenga tabia ya kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kuweza kujua hali zao mapema na kuepuka dhidi ya magonjwa ikiwemo Saratani inayo pelekea kifo pindi mgonjwa anapochelewa kuanza matibabu.
Prof. Makubi ametoa wito huo leo wakati akiongea na Waandishi wa Habari baada ya ufunguzi wa Kongamano la 8 la Kisayansi la masuala ya tafiti na mafunzo lililofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Sayansi Shirikishi Muhimbili, Jijini DaresSalaam. Kauli mbiu ikiwa "utafiti na mafunzo ni daraja la kuelekea huduma bora kwa wagonjwa wa saratani ya damu."
"Nitoe wito kwa Wananchi kuwahi kufanya uchunguzi ili kujua hali ya magonjwa hasa ugonjwa wa Saratani katika miili, dalili za ugonjwa wa Saratani tunazijua, zipo nyingi, inawezakuwa kupungukiwa damu, inaweza kuwa kujisikia homa, inawezakuwa kupungua uzito au kukohoa damu kwa wagonjwa wenye kansa za Kifua, au hata kushindwa kula chakula." Amesema.
Aliendelea kusema kuwa, endapo mtu amepata dalili zozote kati ya hizi ni vizuri kwenda mapema katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kufanya uchunguzi kujua hali ya afya na kuanza matibabu, kwani yaweza kuwa ni ugonjwa wa Saratani au ugonjwa mwingine, amesisitiza Prof. Makubi.
Sambamba na hilo, Prof. Makubi amesisitiza kuwa, ni vizuri kila baada ya miezi sita mpaka mwaka mmoja kujenga tabia ya kwenda kufanya uchunguzi (check up) ili kujua hali ya afya ya mwili, ikiwamo kuangalia magonjwa yasiyoambukiza kama vile ugonjwa wa Saratani.
Aidha, Prof Makubi amesema kuwa, takribani watu 40,000 wanagundulika kuwa na saratani kila mwaka hapa Tanzania, huku akisisitiza kuwa asilimia 80% ya wagonjwa hawa hupoteza maisha kwasababu ya kuchelewa kufanya uchunguzi ili kuanza matibabu ya ugonjwa wa Saratani.
"Takribani watu elfu 40 wanagundulika kuwa na saratani kila mwaka hapa Tanzania, na 80% ya wagonjwa hawa hupoteza maisha."amesema Prof Makubi.
Hata hivyo, Prof Makubi ameushukuru uongozi wa Chuo cha Muhimbili kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele kwa kutoa elimu kwa wananchi jinsi ya kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo ugonjwa wa Saratani.
Vile vile, Prof. Makubi amewashukuru Wataalamu mbalimbali waliotoa mchango mkubwa katika kusaidia tiba ya magonjwa ya Saratani ya damu, Wataalamu hao ni pamoja na Prof. Magesa (Daktari wa Haematology, Chuo cha Muhimbili), Dkt. Maunda (Taasisi ya Saratani Ocean Road), Dkt. Trish (Daktari wa Watoto).
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Sayansi
Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Prof. Andrea Pembe amewashukuru Wataalamu na
wanafunzi waliojitokeza kushiriki Kongamano hili la Kisayansi lenye kujadili
Saratani ya Damu lenye lengo la kutafuta matibabu ili kuwasaidia wananchi
wanaopoteza maisha kwasababu ya ugonjwa wa Saratani, hasa Saratani ya damu.
MWISHO.
Ijumaa, 4 Februari 2022
"ONGEZEKO KUBWA LA SARATANI LINACHANGIWA NA MTINDO WA MAISHA" - WAZIRI UMMY MWALIMU
Katika
kipindi cha miaka kumi nchi imeshuhudia ongezeko kubwa la wagonjwa wa
saratani unaochangangiwa na mtindo wa Maisha usiozingatia lishe Bora ikiwa ni
Pamoja na kutokufanya mazoezi.
Kauli hiyo imebainishwa na Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu leo jijini Dodoma wakati akitoa tamko la siku ya saratani duniani ambapo amesema sababu nyingine kuwa ni unene ulikithiri,matumizi ya tumbaku na bidhaa zake,matumizi ya pombe kupita kiasi na ulaji usiofaa kama kutokula mbogamboga na matunda,matumizi ya chumvi na sukari kwa wingi.
"Ongezeko la wagonjwa wa saratani pamoja na magonjwa mengine yasiyoambukiza, linachangiwa zaidi na mtindo wa maisha usiozingatia afya bora kama kutokufanya mazoezi (Tabia Bwete), unene uliokithiri, matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, matumizi ya pombe kupita kiasi na ulaji usiofaa kama kutokula mbogamboga na matunda, matumizi ya chumvi na sukari kwa wingi”, amesisitiza Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema kutokana na changamoto hiyo Serikali imeimarisha huduma za kibingwa katika hospitali 6 za Rufaa za Kanda na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya Uchunguzi na Tiba kwa kuongeza wataalam, miundombinu pamoja na Vifaa Tiba.
Waziri Ummy amesema takwimu za Shirika
la Umoja wa Mataifa la Tafiti za Saratani (IARC) za 2018, zikionyesha kuwepo
kwa wagonjwa wapya 42,060 kwa mwaka na takribani wagonjwa 28,610 sawa na
asilimia 68 hufariki kutokana na ugonjwa huo.
Hata hivyo Waziri Ummy amesema kuwa katika kila watu 100,000, watu 76 hugundulika kuwa na ugonjwa wa Saratani.
Katika taarifa za mwaka 2021 kutoka kanzi data ya wagonjwa iliopo Taasisi ya Saratani ya Ocean Road inaonesha kuwa Saratani zinazoathiri wanaume zaidi ni pamoja na saratani ya tezi dume (21%), Saratani ya Koo (11.8%), Saratani ya utumbo mkubwa na mdogo (9%) na Saratani ya mdomo na kinywa (7.3%) na kwa upande wa wanawake saratani zinazowaathiri zaidi ni pamoja na Saratani ya Mlango ya Kizazi (43%), Saratani ya Matiti (14.2%) na Saratani ya koo (3.8%).
Waziri Ummy ameweka wazi kuwa saratani ni ugonjwa ambao unaathiri watu wa rika na jinsia zote watoto, watu wazima, wanawake na wanaume ambapo takwimu za Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani (IARC) na Shirika la Afya Duniani (WHO), 2018 zinaeleza kwamba kila mwaka duniani kote kunatokea wagonjwa wapya wanaokadiriwa kufikia milioni 18.1, na kati ya hao, zaidi ya wagonjwa milioni 9.6 hufariki kutokana na ugonjwa wa saratani kila mwaka ambao ni sawa na takribani asilimia 50.
Aidha, zaidi ya watu ya millioni 43.8 wanaishi na saratani duniani. "Kama hatua madhubuti za kinga, uchunguzi wa mapema na tiba stahiki hazitachukuliwa haraka, tatizo la saratani linakadiriwa kuongezeka na idadi ya wagonjwa wapya kufikia milioni 24 ifikapo mwaka 2035, huku ongezeko kubwa likiwa katika ukanda wa nchi zinazoendelea kama Tanzania".
Vile vile ameeleza kuwa takwimu kutoka kwenye kanzi data zilizo anzishwa kwa Kanda , zinaonesha kwamba wagonjwa wapya 14,136 walifikiwa na huduma ambayo ni sawa na asilimia 33 ya makadirio ya wagonjwa wapya wote kwa mwaka 2021 ikiwa ni ongzeko la asilimia tano ukilinganisha na takwimu za Mwaka 2020 ambapo jumla ya wagonjwa wapya 12,096 (28%) walionwa.
Waziri Ummy amesema katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, Tanzania imeshuhudia
ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani zinazochangiwa na mtindo wa maisha
ikilinganishwa na ilivyokuwa awali ambapo wagonjwa wengi walikuwa ni wale wenye
saratani zinazotokana na maambukizi ya virusi.
"Ni vyema kila mmoja akapima afya yake mara kwa mara ili kutambua hali yake ya kiafya. Endapo utatambuliwa kuwa una ugonjwa wa Saratani tumia huduma za afya kulingana na ushauri utakaopewa na wataalam wa afya".
"Kwa wale ambao wameshajitambua kuwa na matatizo ya Saratani lakini hawatumii huduma za afya ipasavyo, nawaasa watumie huduma za afya zilizopo kwa manufaa ya afya zao na kuepusha athari zinazotokana na ugonjwa wa Saratani na kwa wale ambao hawajapata ugonjwa huu waendelee kuchukua tahadhari kwa kuzingatia kanuni za Mtindo bora wa maisha,"ameongeza Waziri Ummy.
Hata hivyo amesema kuwa Tanzania imetunga Sheria mbalimbali , miongozo na mikakati ya udhibiti wa vihatarishi ili kuweza kudhibiti ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza ambapo karibu theluthi moja ya Saratani zinaweza kutibika endapo mgonjwa atabainika mapema.
Waziri Ummy Mwalimu amesema Serikali ya awamu ya sita imehakikisha huduma za kinga na matibabu ya saratani zinapatikana nchini ambapo vituo vya uchunguzi na matibabu ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi zaidi ya 800 vimefunguliwa nchi nzima kuanzia kwenye ngazi ya Zahanati hadi kwenye ngazi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa na Kanda.
"Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 51.5 ikilinganishwa na vituo 350 vilivyokuwepo kwa mwaka 2015. Mafanikio haya yamepelekea serikali kuweza kutoa huduma za uchunguzi za saratani ya mlango wa kizazi kwa Jumla ya wanawake 513,375 sawa na ongezeko mara nne idadi ya wanawake 127, 188 waliopatiwa huduma hizo mwaka 2015" amefafanua Waziri Ummy Mwalimu.QU
MWISHO
Jumapili, 30 Januari 2022
TUONGEZE KASI YA MAPAMBANO ILI TUTOKOMEZE UGONJWA WA UKOMA IFIKAPO 2030 – DKT. MOLLEL
Na Englibert Kayombo WAF – Singida
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewataka wataalam wa afya nchini kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukoma ili ifikapo Mwaka 2030 ugonjwa huo uwe umetokomea nchini.
Dkt. Mollel amesema hayo leo kwenye Siku ya Kitaifa ya kuadhimisha Siku ya Ukoma Duniani iliyofanyika katika eneo la Sukamahela katika Wilaya ya Manyoni Mkoa wa Singida.
“Niwapongeze wataalam wamefanya kazi nzuri sana ya kuwatambua wenye Ukoma lakini bado tuna kazi kubwa mbele yetu kwasababu tunataka miaka 9 ijayo kabla ya mwaka 2030 Ukoma uwe historia ndani ya Tanzania. amesema Dkt. Mollel.
Amesema wataalam wa afya pamoja na wadau wakiunganisha nguvu za pamoja na kushirikishana mikakati na afua mbalimbali za mapambano, Ugonjwa huo unaweza kuwa umetokomea hata kabla ya kufikia mwaka 2030.
“Ni lazima tushikamane, tusiishie kwenye kutunza utu wa watu wenye Ukoma tuu lakini tuhakikishe hakuna mwingine anayekwenda kupata ukoma, na hata kama yupo basi tuhakikishe tunamtambua mapema ili tumsaidie asiweze kupata ulemavu” amesisitiza Dkt. Mollel.
“Ni lazima tuutokomeze Ukoma; dawa za kuponyesha Ukoma tunazo na zinatolewa bila malipo, kiwango cha maambukizi mapya kimeshuka na kufikia chini ya asilimia 5, na pia asilimia 90 ya wagonjwa wote wapya tunawaowaibua ni wagonjwa walioambukizwa miaka mingi iliyopita” amefafanua Dkt. Mollel
Dkt. Mollel ameagiza fedha zinazotengwa na Serikali pamoja na kutolewa na wadau wa maendeleo ziwe zinaenda kushughulikia mapambano ya kutokomeza Ukoma.
“Fedha nyingi sana zinaweza kuwa zinatumika kujadili kuhusu Ukoma, kufanya Semina za Ukoma na kumjadili mgonjwa wa Ukoma kuliko hata fedha zinazokwenda kumsaidia mgonjwa mwenyewe” ameendelea kusema Dkt. Mollel.
Amewataka wataalam wa afya kubadilisha mikakati ya mapambano dhidi ya Ukoma kwa kuwafikia wagonjwa walipo pamoja na kutoa elimu zaidi kwa wananchi dhidi ya Ugonjwa wa Ukoma.
Jumanne, 28 Septemba 2021
TAHADHARI YATOLEWA KWA WANANCHI DHIDI YA UGONJWA WA KICHAA CHA MBWA
Na Englibert Kayombo
Katika kuadhimisha Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani kila mwaka ifikapo tarehe 28 ya kila mwezi Septemba, Wizara ya Afya imewatahadharisha wananchi kujikinga na ugonjwa huo hatari ambao unaweza kusababisha vifo.
Ijumaa, 24 Septemba 2021

WAZIRI MKUU AMUAGIZA WAZIRI AFYA KUPELEKA JOKOFU, DAKTARI KITUO CHA AFYA NDUNGU.
Na WAMJW -KILIMANJARO
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Afya Mhe. Dkt Dorothy Gwajima kununua na kipeleka Jokofu la kuhifadhi pamoja na kuongeza Daktari mmoja katika kituo cha afya Ndungu Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro wakati serikali ikijipanga kukamilisha ajira za watumishi sekta ya afya kwa lengo la kuboresha utoaji huduma kwa wagonjwa.
Agizo hilo amelitoa wakati akikagua ukarabati wa kituo cha afya ndungu wilaya ya same mkoa wa kilimanjaro na kisha akazungumza na wabanchi katika eneo hilo.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa, serikali imejipanga kujenga vituo vya afya viwili na hospitali mbili katika jimbo la Same Magharibi na Same Mashariki kwa lengo la kusogeza huduma za afya kwa hamii.
Aidha waziri mkuu Kassim Majaliwa amewapongeza madaktari wa kituo cha afya Ndungu kwa jitihada zao za kuwahudumia wananchi wanaokabiliwa na Magonjwa katika eneo hilo.
Kwa Upande wake Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii,jinsia wazee na watoto Dkt Dorothy Gwajima ametoa maelekezo kwa Katibu wa Wizara ya Afya Dkt Makubi kutekeleza agizo hilo kwakupeleka Daktari mmoja kwa ajili ya kusaidiana na Dkt aliyepo kwenye kituo cha afya Ndungu ambacho kimeonesha kuzidiqa na wagonjwa ambapo kwa mwaka hufanya upasuaji unaofikia wagonjwa 305.
Katika hatua nyingine Dkt Gwajima amesema kuwa, ili Tanzania iwe salama wananchi wanatakiwa kushikamana kwa umoja wao kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya huku akitilia mkazo kwa wananchi kujitokeza kwa ajili ya kupata chanjo kwa kuwa ugonjwa wa uviko 19 unahatalisha maisha ya watu.
Katika Hafla hiyo Waziri Gwajima amesema kuwa, serikali imefanya ukarabati wa kituo cha afya Ndungu Same kitengo cha maabara, chumba cha wazazi na chumba cha kuhifadhi maiti na tayari wizara imetenga shilingi milioni 35 kwa ajili ya kununua jokofu la vyumba sita ambapo ameagiza MSD ihakikishe inapeleka jokofu katika kituo cha afya ndungu Same
Akizungumzia mikakati ya kuboresha huduma za afya mkoa wa Kilimanjaro,
Waziri Dkt Gwajima Amesema serikali ya awamu ya Sita umetenga kiasi cha sh bi 12 kwa ajili ya ujenzi wa jengo ka mama na Mtoto katika hospitali ya mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi ambapo ujenzi umefikia asilimia 70
Awali mbunge wa jimbo la Same magharibi Anne Kilango Malecela ameiomba serikali kujenga hospitali mbili kwa kuwa wilaya ya same ina majimbo mawili yenye watu wengi kiasi kwamba wanasabanisha msongamano mkubwa kwenye zahanati, na Vituo vya Afya.
MWISHO.
Jumapili, 27 Juni 2021
TAALUMA YA FAMASI NI MUHIMU KATIKA VITA YA NCD: Dkt. GWAJIMA
Katika vita dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza Taaluma ya Famasi ni muhimu katika kuwezesha upatikananji wa bidhaa za dawa kwa wale watakaoshindwa kuzuia kupata magonjwa yasiayoambukiza na ikawalazimu wafike vituoni kupata tiba.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa Kongamano la 12 la kisayansi la Chama cha Wanafunzi wa Taaluma ya Famasi (TAPSA) lililofanyika jijini Mwanza.
Dkt. Gwajima amebainisha kwamba bidhaa hizo za dawa kwa ajili ya kundi hilo ni ghali na bahati mbaya nchini Tanzania hakuna kiwanda cha kutengeneza na badala yake wanaagiza toka nje ya nchi.“Tunapaswa kutafakari iwapo kasi ya kukua kwa maradhi haya ni inaongezeka je tunazijazititi vipi kwenye kasi ya kinga kwani bado kasi hiyo ni ndogo”.Aliongeza Dkt. Gwajima.
Alisema kuwa, katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza Serikali imeendelea kuboresha upatikanaji wa huduma bora karibu zaidi na wananchi kwa kujenga miundombinu , kuajiri watumishi na kuweka vifaa tiba na dawa. Maboresho haya yameendelea kufanyika katika vituo vya huduma za afya ngazi zote.
Hata hivyo amesema kumekuwa na changamoto mbalimbali ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi ikiwemo changamoto ya upatikanaji wa bidhaa za dawa na vifaa tiba kwa ajili ya huduma mbalimbali zikiwemo na huduma kwa ajili ya wanaougua magonjwa hayo yasiyoambukizwa.
Aidha, Dkt. Gwajima amesema wapo baadhi ya wanataaluma wachache wasio waadilifu na wasio wazalendo ambao ni doa kubwa kwenye taaluma hiyo adimu ambayo inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa kwenye ajenda ya afya. Hivyo iwapo itasimama kwa nafasi yake basi wanataaluma hao wanaweza kufanya mapinduzi makubwa ya afya na kiuchumi.
“Hii itawezekana kwa kujikita kwenye ajenda ya jinsi gani viwanda vya ndani viweze kuzalisha bidhaa mbalimbali na kuhakikisha matumizi yasiyotia shaka ya bidhaa za afya zinazopokelewa kwenye vituo vya huduma na kuepuka upotevu na matumizi yasiyofuata miongozo na kusababisha usugu wa baadhi ya dawa na pia baadhi kuleta madhara kwa wateja kama ilivyokusudiwa”.
Dkt. Gwajima alitoa rai kwa jamii ya kitanzania kuzingatia ulaji unaofaa ambapo kila mlo uwe na makundi yote matano ya vyakula halisi, kutotumia mafuta mengi,chumvi nyingi,kufanya mazoezi ,kupata usingizi wa kutosha,kuepuka matumizi ya tumbaku na madawa ya kulevya na pia kuchunguza afya angalau mara moja kwa mwaka.
Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 75 ya vifo vyote duniani vinavyohusu watu wenye miaka 30 hadi 70 husababishwa na magonjwa hayo.Hapa nchini inakadiriwa kuwa magonjwa yasiyoambikiza husababisha asilimia 27 ya vifo vyote.Kauli mbiu ya Kongamano hilo mwaka huu ni “Wataalamu wa Famasi: kuongeza wigo katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza”.
Awali akiongea wakati wa kongamano hilo Mfamasia Mkuu wa Serikali Bw. Daudi Msasi aliwataka wafamasia na wataalum wengine wa afya nchini kuhakikisha wanatumia fomu za dawa( prescription form) kama nyenzo muhimu za kuondoa changamoto za dawa kwani dawa ni fedha za haraka hivyo wahakikishe kabla hawajatoka lazima wahakikishe dawa zinatoka kwa kujaza fomu hizo.
Aliongeza kuwa kwenye kutenda kazi za umma lazima wafuate miongozo ikiwemo muongozo wa matibabu nchini (STG) wanapokuwa sehemu za kazi hivyo ni wakati wao sasa wa kupitia na kuelewa nini wanapaswa kutekeleza kwenye kazi zao.
Hata hivyo Bw. Msasi aliwataka chama hicho kuanziasha klabu za mazoezi kwenye vyuo vyao ili kuweza kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kwa vitendo na hiyo itasaidia jamii kuelewa umuhimu wa kufanya mazoezi.
Naye Mlezi wa wanafunzi wa Famasi na Masajili wa Baraza la Famasi nchini Bi. Elizabeth shekalaghe aliwataka wanafunzi hao kufanya kazi kwa kujitoa, kuwajibika na kuipenda taaluma yao ili kuweza kuitumikia vyema taaluma yao.
Bi. Shekalaghe alisema kama Baraza wataendelea kusimamia na kuhakikisha wanaendeleza taaluma kwa kutoa elimu ya maadili kwenye vyuo vya famasi nchini ili wanapokua chuoni wazitambua na kuzijua angali wanafunzi.
Naye Rais wa Chama cha Wafamasia Wanafunzi Tanzania(TAPSA) Bw. Hamis Msagama ameipongeza Serikali kwa uboreshaji wa dawa na vifaa tiba ambapo kazi kubwa inafanywa na wafamasia na kuonesha jinsi gani inawajali watanzania.
Pia Bw.Msagama ameipongeza Wizara ya
Afya kwa kuanzisha kitengo cha Magonjwa Yasiyoambukiza (NCD) hivyo wao
kama chama waliona ni vyema kongamaono lao mwaka huu kujadili kwa kina
namna ya kupambana na magonjwa hayo ambayo yanaathiri watu wengi nchini na
duniani.
Jumatatu, 21 Juni 2021

Mganga Mkuu wa Serikali afanya ziara Hospitali ya Rufaa ya Amana
Na.WAMJW - DSM
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifelo Sichalwe amefanya ziara fupi katika hospitali ya rufaa ya Mkoa Amana Jijini Dar es Salaam yenye lengo la kukagua Utekelezaji wa maagizo ya Viongozi wa Wizara waliyoyatoa kwa nyakati tofauti kuhusu maandalizi na utayari wa Watumishi wa afya katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa covid 19.
Akiwa hospitalini hapo Dkt. Sichalwe amezungumza na uongozi wa hospitali hiyo ambapo amewataka viongozi hao wa wafanyakazi kujitayarisha kwa vifaa na matibabu kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
Amesema Kama watumishi wa Afya, ni vyema kuwa tayari wakati wowote hususan katika kipindi hiki ambacho nchi jirani wamekumbwa na wimbi la tatu la ugonjwa wa Corona kwa kuwa raia wa nchi hizi wana muingiliano mkubwa wa shughuli za kiuchumi na biashara, hivyo kama nchi hatuna budi kujipanga.
Sambamba na kikao hicho Dkt.Sichalwe amekagua miundombinu ya hospitali na utekelezaji wa afua za kuzuia maambukizi mahali pa kazi (Infection, prevention and control). Ameupongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa juhudi na jitihada kubwa wanayofanya hospitalini hapo kwa lengo la kuzuia ueneaji wa maambukizi kwani watumishi wote walikutwa wamevaa barakoa na sehemu za kunawia zenye sabuni na maji zikiwepo kila wodi, sehemu ya mapumziko na getini.
“Nimeona mmevaa barakoa, mnatoa elimu kwa wananchi pia. Haya mnayotekeleza hapa ni kama darasa kwa wananchi wote wanaokuja kupata huduma hapa nao watakuwa mabalozi kwa wenzao kwenye jamii. Nina imani utekelezaji huu mnaendeleza hata baada ya kazi”.
Aidha, Dkt.Sichalwe amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa nchini kusimamia utekelezaji wa afua hii, kwani unatukinga siyo tu na ugonjwa wa covid 19 bali na Magonjwa mengine mengi yanayosababishwa na kula vitu kwa mikono isiyo safi na kuvuta hewa yenye vimelea vya maambukizi.
Vilevile Dkt.Sichalwe ametembelea mtambo maalumu wa kuzalisha hewa ya Oksijeni hospitalini hapo ambapo ameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza zaidi ya Milioni 600 ili kuhakikisha wanaokoa Maisha ya watanzania wanaohitaji huduma hiyo.Mtambo huo wenye matoleo Zaidi ya 89, unauwezo wa kuzalisha mitungi 200 ya hewa ya Oksjeni kwa masaa 24 na hospitali ina uwezo wa kuhudumia watonjwa wenye uhitaji 150 kwa wakati mmoja.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume amesema kuwa juhudi hizo zinaendelea kufanywa na hospitali zote ndani ya Dar es Salaam ili kuhakikisha wanalidhibiti ipasavyo wimbi hili la tatu.
Jumatano, 26 Mei 2021

WIZARA YA AFYA KUJA NA MFUMO WA UFUAUTILIAJI WA WAJAWAZITO NCHI NZIMA
Na Englibert Kayombo – WAMJW, Dodoma
Wizara ya Afya inatarajia kuja na mfumo wa ufuatiliaji wa taarifa za wajawazito wote toka wanapofika kliniki kwa mara ya kwanza hadi baada ya siku 42 za kujifungua.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima leo alipokutana na wataalam wa afya katika kikaokazi cha maandalizi ya utengenezaji wa mfumo huo.
“Nataka muwe mnafuatilia taarifa za wajawazito na kujua maendeleo yao toka wanapofika kituoni siku ya kwanza mpaka baada ya kujifungua kwa data za kila siku na kujua kwa namna gani wajawazito au mama baada ya kujifungua ameweza kupata huduma zetu na muweze kuchukua hatua pale mnapoona changamoto” amesema Dkt. Dorothy Gwajima.
Waziri Gwajima amesema kuwa ili kuweza kuwa na mfumo wenye ufanisi ni lazima tusisitize matumizi sahihi ya takwimu na kuwataka wataalam wa afya katika kazi zao kuhakikisha wanachukua takwimu zote zinazohitajika kwa ajili ya matuzimu katika mfumo huo.
Waziri Dorothy Gwajima amesema kuwa Serikali katika kupambana na vifo vya wajawazito imefanya mambo mengi ikiwemo kuanzisha Kampeni maalum ya Jiongenze Tuwavushe Salama iliyoanzishwa na aliyekuwa Makamu wa Rais na sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan yenye lengo la kupunguza na kudhibiti vifo vitokanavyo na uzazi.
“Serikali imejenga vituo vingi vya huduma ngazi zote na mwamko wa wajawazito wanaojitokeza kuhudhuria kliniki umekuwa mkubwa” amesema Dkt. Dorothy Gwajima na kuongezea kuwa bado elimu inahitajika kutolewa kwa ili wajawazito wafike katika vituo vya kutolea huduma za afya na kuanza kliniki mapema.
“Sasa hivi mwitikio umeongezeka, wajawazito wanajitokeza na kujifungua katika vituo vya kutolea huduma kati yao wengine wanafariki, lakini tukijadili kujua kwanini amefariki na tukifuatilia wakati alipokuwa kliniki tunagundua hatukumfuatilia vizuri, hiki ndio kitu tunachoimarisha ili ufuatiliaji uwe imara” amefafanua Dkt. Dorothy Gwajima.
Waziri Gwajima amesema kuwa katika kuimarisha mfumo wa usimamizi na ufuatiliaji wa taarifa za wajawazito, wanatarajia kuimarisha ufuatiliaji wa mteja mmoja mmoja toka anapopata ujauzito, muda wa kuanza kliniki, kujifungua mpaka baada ya siku 42.
Naye Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichwale amesema kuwa kwa kupitia kanzidata wanazochukua kutoka kwenye taarifa za wajawazito zinawasadia kujua bidhaa gani za dawa zinazihitajika kumhudumia mjamzito, miundombinu ipi wanahitaji, inaonyesha uwajibikaji wa watumishi wa afya kwa ujumla wao na mmoja mmoja, pamoja na kutuonyesha kama miongozi iliyopo inatija katika kusaidia kutoa huduma bora kwa wajawazito.
“Hakuna njia nyingine ambayo tutaitumia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi zaidi ya kuimarisha ufuatiliaji na usimamizi wa mama mmoja mmoja kama kanzidata hii inavyotaka” Amesema Dkt. Sichwale
-Mwisho-
Jumatatu, 24 Mei 2021

HEDHI SIO UGONJWA WALA LAANA – Waziri Gwajima
Na WAMJW - Dodoma
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amesema hedhi wanayopata wanawake sio ugonjwa wala laana bali ni uumbaji wa Mungu katika kumkamilisha mwanamke.
Waziri Gwajima amesema hayo leo katika ofisi za Wizara Jijini Dodoma wakati akiongea na waandishi wa Habari kuhusu siku ya hedhi ambayo inaadhimishwa kila mwaka duniani kote kila ifikapo tarehe 28 mwezi Mei ambayo mwaka huu ina kaulimbiu inayosema “Ni wakati wa kuchukua hatua ili kuhakikisha vifaa vya kujisitiri/taulo za hedhi zinapatikana kwa urahisi na bei nafuu kwa msichana/mwanamke”.
“Siku ya hedhi duniani inaadhimishwa kila mwaka, licha ya mwaka jana kutofanyika kutokana na changamoto ya Covid 19 lakini jumuiya ya Kimataifa imeendelea kufahamishana, kuelimishana na kukumbushana juu ya jambo hili muhimu kwa njia ya mtandao. Lengo kuu ni kueleza Dunia na Umma wa Tanzania kuwa hedhi sio ugonjwa wala laana bali ni hali ya kawaida na Baraka ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu inayomtokea msichana mara baada ya kuvunja ungo kama ishara ya mabadiliko kwenye mfumo wa maumbile yake ya uzazi”. Amesema Waziri Gwajima.
Waziri huyo ameongeza kuwa tafiti zinaonesha kila siku wanawake zaidi ya milioni 12 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 wanakuwa kwenye Hedhi duniani.
Aidha, Waziri Gwajima amesisitiza Hedhi Salama akimaanisha kwamba msichana au mwanamke anapokuwa katika siku zake anatakiwa kuzingatia mazingira salama na anapata huduma zote muhimu ikiwemo miundombinu ya vyoo vyenye usiri, maji safi, taulo za kike au vifaa salama vya kujisitiri na utupaji salama wa vifaa/taulo za kike zilizotumika.
Hata hivyo, Waziri amesema kuna baadhi ya wasichana au wanawake wanakua katika mazingira ya kutokua na hedhi salama ambayo inachangiwa na miundombinu duni ya vyoo, kukosekana kwa maji safi na salama, matumizi ya vifaa vya hedhi visivyo salama na utupaji ovyo wa vifaa vilivyotumika.
“Matokeo ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) pamoja na OR -TAMISEMI kwa kushirikiana na Wadau wa Hedhi Salama mwaka 2019, yanaonesha Nchi yetu imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya ajenda ya afya ya hedhi. Hata hivyo, changamoto ni nyingi katika ngazi ya jamii hususan kuwa na uelewa mdogo wa jamii juu ya hedhi salama. Kwa mfano ni asilimia 28 tu ya wasichana ndiyo wenye uelewa thabiti juu ya hedhi salama”. Ameongeza Waziri Gwajima.
Takwimu zinaonesha kuwa maeneo mengi hapa Nchini jamii inakosa uelewa wa umuhimu wa hedhi salama. Maeneo yaliyofanyiwa utafiti na kuonesha ukosefu wa uelewa wa hedhi salama ni pamoja na Halmashauri za Namtumbo, Muleba, Mbeya, Igunga, Temeke, Karatu, Tandahimba, Rorya, Kusini Unguja na Kaskazini Pemba ambayo jamii yake ilionekana inauelewa mdogo juu ya suala la hedhi salama. Huku utafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ukionesha kuwa asilimia 60 ya wasichana walionekana kutomudu gharama za taulo za kike.
Hata hivyo, Waziri Gwajima amewashukuru wadau kupitia mtandao wa hedhi salama kuendelea kuhamasisha upatikanaji wa vifaa vya hedhi salama ndani ya nchi kwa unafuu na ubora unaotakiwa ili kila mhitaji kwa makundi yote aweze kutumia.







