Katika
kipindi cha miaka kumi nchi imeshuhudia ongezeko kubwa la wagonjwa wa
saratani unaochangangiwa na mtindo wa Maisha usiozingatia lishe Bora ikiwa ni
Pamoja na kutokufanya mazoezi.
Kauli hiyo imebainishwa na Waziri wa
Afya, Mhe. Ummy Mwalimu leo jijini Dodoma wakati akitoa tamko la siku ya
saratani duniani ambapo amesema sababu nyingine kuwa ni unene
ulikithiri,matumizi ya tumbaku na bidhaa zake,matumizi ya pombe kupita kiasi na
ulaji usiofaa kama kutokula mbogamboga na matunda,matumizi ya chumvi na sukari
kwa wingi.
"Ongezeko la wagonjwa wa saratani
pamoja na magonjwa mengine yasiyoambukiza, linachangiwa zaidi na mtindo wa
maisha usiozingatia afya bora kama kutokufanya mazoezi (Tabia Bwete), unene
uliokithiri, matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, matumizi ya pombe kupita kiasi
na ulaji usiofaa kama kutokula mbogamboga na matunda, matumizi ya chumvi na
sukari kwa wingi”, amesisitiza Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema kutokana na changamoto
hiyo Serikali imeimarisha huduma za kibingwa katika hospitali 6 za Rufaa za
Kanda na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya Uchunguzi na Tiba kwa
kuongeza wataalam, miundombinu pamoja na Vifaa Tiba.
Waziri Ummy amesema takwimu za Shirika
la Umoja wa Mataifa la Tafiti za Saratani (IARC) za 2018, zikionyesha kuwepo
kwa wagonjwa wapya 42,060 kwa mwaka na takribani wagonjwa 28,610 sawa na
asilimia 68 hufariki kutokana na ugonjwa huo.
Hata hivyo Waziri Ummy amesema kuwa
katika kila watu 100,000, watu 76
hugundulika kuwa na ugonjwa wa Saratani.
Katika taarifa za mwaka 2021 kutoka
kanzi data ya wagonjwa iliopo Taasisi ya Saratani ya Ocean Road inaonesha kuwa
Saratani zinazoathiri wanaume zaidi ni pamoja na saratani ya tezi dume (21%),
Saratani ya Koo (11.8%), Saratani ya utumbo mkubwa na mdogo (9%) na Saratani ya
mdomo na kinywa (7.3%) na kwa upande wa
wanawake saratani zinazowaathiri zaidi ni pamoja na Saratani ya Mlango ya
Kizazi (43%), Saratani ya Matiti
(14.2%) na Saratani ya koo (3.8%).
Waziri Ummy ameweka wazi kuwa saratani
ni ugonjwa ambao unaathiri watu wa rika na jinsia zote watoto, watu wazima,
wanawake na wanaume ambapo takwimu za Shirika la Kimataifa la Utafiti wa
Saratani (IARC) na Shirika la Afya Duniani (WHO), 2018 zinaeleza kwamba kila
mwaka duniani kote kunatokea wagonjwa wapya wanaokadiriwa kufikia milioni 18.1,
na kati ya hao, zaidi ya wagonjwa milioni 9.6 hufariki kutokana na ugonjwa wa
saratani kila mwaka ambao ni sawa na takribani asilimia 50.
Aidha, zaidi ya watu ya millioni 43.8 wanaishi na saratani
duniani. "Kama hatua madhubuti za
kinga, uchunguzi wa mapema na tiba stahiki hazitachukuliwa haraka, tatizo la
saratani linakadiriwa kuongezeka na idadi ya wagonjwa wapya kufikia milioni 24 ifikapo mwaka 2035, huku ongezeko kubwa
likiwa katika ukanda wa nchi zinazoendelea kama Tanzania".
Vile vile ameeleza kuwa
takwimu kutoka kwenye kanzi data zilizo anzishwa kwa Kanda , zinaonesha kwamba
wagonjwa wapya 14,136 walifikiwa na huduma
ambayo ni sawa na asilimia 33 ya makadirio ya wagonjwa wapya wote kwa
mwaka 2021 ikiwa ni ongzeko la asilimia tano ukilinganisha na takwimu za Mwaka
2020 ambapo jumla ya wagonjwa wapya 12,096 (28%) walionwa.
Waziri Ummy amesema katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, Tanzania imeshuhudia
ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani zinazochangiwa na mtindo wa maisha
ikilinganishwa na ilivyokuwa awali ambapo wagonjwa wengi walikuwa ni wale wenye
saratani zinazotokana na maambukizi ya virusi.
"Ni vyema kila mmoja akapima afya
yake mara kwa mara ili kutambua hali yake ya kiafya. Endapo utatambuliwa kuwa
una ugonjwa wa Saratani tumia huduma za afya kulingana na ushauri utakaopewa na
wataalam wa afya".
"Kwa wale ambao wameshajitambua kuwa na matatizo ya Saratani
lakini hawatumii huduma za afya ipasavyo, nawaasa watumie huduma za afya zilizopo
kwa manufaa ya afya zao na kuepusha athari zinazotokana na ugonjwa wa Saratani
na kwa wale ambao hawajapata ugonjwa huu waendelee kuchukua tahadhari kwa
kuzingatia kanuni za Mtindo bora wa maisha,"ameongeza Waziri Ummy.
Hata hivyo amesema kuwa Tanzania
imetunga Sheria mbalimbali , miongozo na mikakati ya udhibiti wa vihatarishi
ili kuweza kudhibiti ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza ambapo karibu theluthi
moja ya Saratani zinaweza kutibika endapo mgonjwa atabainika mapema.
Waziri Ummy Mwalimu amesema Serikali ya awamu ya sita imehakikisha huduma za kinga na matibabu ya
saratani zinapatikana nchini ambapo vituo vya uchunguzi na matibabu ya awali ya
saratani ya mlango wa kizazi zaidi ya 800 vimefunguliwa nchi nzima kuanzia
kwenye ngazi ya Zahanati hadi kwenye ngazi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa na
Kanda.
"Hii ni sawa na ongezeko la
asilimia 51.5 ikilinganishwa na vituo 350 vilivyokuwepo kwa mwaka 2015.
Mafanikio haya yamepelekea serikali kuweza kutoa huduma za uchunguzi za
saratani ya mlango wa kizazi kwa Jumla ya wanawake 513,375 sawa na ongezeko
mara nne idadi ya wanawake 127, 188 waliopatiwa huduma hizo mwaka 2015"
amefafanua Waziri Ummy Mwalimu.QU
MWISHO