Na. WAMJW-Kahama
Serikali imeweka mikakati ya kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria na kitaaluma kikundi cha watu wachache ambao wamekuwa na tabia ya kuiba dawa za Serikali kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa kutoa salamu za wizara yake kwa wakazi wa wilaya ya Kahama kwenye ziara ya kikazi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.
Dkt. Gwajima alisema kuwa kumekuwa na kikundi cha watu wachache kwenye eneo la kutumia ambalo limeshindwa kubadilika kutokana na watumishi hao kukosa uzalendo wa mali za nchi yao.
“Kikundi hicho tutakibaini na kuwachukulia hatua za kisheria kwani wamekuwa wakikwaza wanachi ambao wanaenda kupata huduma na kusababisha kukosa dawa kwa kudokoa dawa na hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya Serikali”.
Aidha, alisema Serikali kupitia Mabaraza ya kitaaluma na utumishi wa umma watapambana kwa pamoja na kikundi hicho ili dhana ya kutunza rasiliamali ya nchi itimie,“mbali na hatua za mahakamani watumishi wasio waadilifu watawajibika kwenye hatua za mwajiri na mabaraza yao ya kitaaluma”.Alisisitiza Dkt. Gwajima.
Alisema Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye eneo la dawa ila bado kumekuwa na changamoto kwa upande wa matumizi hali hiyo imetokana na baadhi ya watumishi wa sekta hiyo kushindwa kubadilika na kusababisha ukosefu wa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Kwa upande wa Mabaraza ya Kitaaluma Dkt. Gwajima alisema watayahoji Mabaraza ya kitaaluma kama kuna sababu ya kuendelea na ajira kwani kama mtaaluma amekosa maadili na hivyo kurudisha nyuma sekta ya afya nchini na utumishi wa umma kwa ujumla
Hata hivyo Dkt. Gwajima aliwashukuru wananchi kwa kuendelea kutuma maoni, taarifa na ushahidi kwa namba ya simu aliyoitoa mwishoni mwa mwaka hivyo kumuhakikishia Mhe. Rais kwamba wizara yake itapambana kikundi hicho na kuwataka wananchi waendelee kumtumia maoni ili kuweza kuwabaini wale wote ambao wamekosa uzalendo kwenye utendaji kazi wa utumishi wa umma hapa nchini.