Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumanne, 19 Mei 2020

LICHA YA JANGA LA CORONA, HUDUMA ZA CHANJO NA UFUATILIAJI WA MAGONJWA YANAYOZUILIKA KWA CHANJO ZAENDELEA KWA UANGALIFU MKUBWA TANGA

- Hakuna maoni
Ofisa Mradi wa Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Chanjo, Richard Magodi (katikati) akikagua namna ya uingizaji wa data za chanjo pamoja na muongozo wa kujikinga na janga la COVID 19 katika Hospitali ya Wilaya ya Pangani, Mkoani Tanga

Ofisa Mradi wa Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Chanjo, Richard Magodi akipitia data za chanjo kwenye mfumo maalumu wa kieletroniki wakati wa ziara maalum ya muongozo wa kujikinga na COVID19 kwa watoa huduma za chanjo katika kituo cha Chanjo Zabanati ya Bushiri, Pangani Mkoani Tanga.


Na Mwandishi Maalum –Pangani,Tanga.

LICHA ya janga la Virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa homa kali ya Mapafu (COVID19), Watoa huduma za chanjo na ufuatiliaji wa magonjwa yanayozuilika kwa Chanjo hizo Wilayani Pangani Mkoani Tanga zinaendelea kama kawaida huku wahudumu wakichukua tahadhari kubwa kwa kuzingatia muongozo wa kujikinga na janga hilo.

Hayo yameelezwa na  Mratibu wa Huduma za Chanjo Mkoa wa Tanga,  Seif Shaib wakati wa ziara maalum ya usimamizi elekezi na uhamasishaji wa muongozo wa kujikinga na COVID 19 kwa watoa huduma hizo iliyofanywa na Ofisa Mradi wa Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Chanjo, Richard Magodi.

Mratibu huyo wa Chanjo mkoa, Seif Shaib alisema chanjo zipo na huduma vituoni zinaendelea kwa kuzingatia muongozo.

Kwa upande wake, Ofisa Mradi wa Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Chanjo, Richard Magodi ameweza kushuhudia uwepo wa chanjo hizo kwenye vituo sambamba na watoa huduma wakifuata miongozo ikiwemo kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu kwa kuacha nafasi, uwapo wa maji safi na tiririka ya kunawa mikono na uvaaji barakoa.

"Watoa huduma za chanjo na wafuatiliaji wa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo kwa watoto wanatakiwa waendelee  kulingana na ratiba za chanjo zao lakini kwa kuzingitia muongozo wa kujikinga dhidi ya COVID 19." Alisema Richard Magodi

Akielezea upande wa chanjo ya kukinga ugonjwa wa Saratani ya mlango wa kizazi (HPV) inayotolewa kwa wasichana  wa umri wa miaka 14 ipo na inatolewa kwa walengwa hao.

"Chanjo hii ya HPV bado ipo lakini tunacho sisitiza kwa watoto ambao ratiba zao zinafikia hivi sasa wanaweza kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Kamati za afya za kituo  na Uongozi  wa vijiji ama mtaa wahusishwe kuhamasisha wananchi kuwapeleka watoto wa kike wenye miaka 14 kupatiwa chanjo hiyo." Alisema Magodi.

Sambamba na hilo, watoa huduma hao wametakiwa kufuatiliaji pia magonjwa yanayozuilika kwa chanjo hususani ugonjwa wa Surua, Polio na Pepopunda kwa watoto kwa kipindi hiki cha COVID19.

"Tuongeze jitihada za chanjo. Kwani tusipofanya hivyo watu wengi wanaweza kufariki na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.

"Mfano tukiangalia takwimu za mwaka jana nchini Congo (DRC), ugonjwa wa Ebola uliua watu wachache kuliko Surua hii ni kutokana na kuipa kipaumbele Ebola na kuacha magonjwa yanayozuilika kwa chanjo nchini humo..Hivyo sisi Tanzania tunaendelea na huduma kwa kufuata muongo na tahadhari kubwa ikiwemo kuhimiza suala hilo la chanjo." Alisema Magodi.

Aidha aliwataka watoa huduma hao kuzingatia  matumizi sahihi  ya mfumo wa kieletroniki ngazi ya kituo (Tanzania Immunizations Registry -TImR) ili kuwa na takwimu sahihi na zitakazosaidia kufanya maamuzi bora kwa  wakati kwenye ngazi ya kituo hadi ngazi ya Taifa.

"Katika vituo ambavyo tumetembelea Watumishi wameendelea kutumia mfumo huu kwa kuchanja na kuomba dawa, vifaa vya chanjo na kupata taarifa mbalimbali  wanazozihitaji kwa wakati kupitia  Vishishwambi (tablets) na wamefundishwa namna ya kutumia mfumo huo ambao umekuwa ukisaidia sana" alisema.

Awali Magodi aliweza kutembelea vituo vya chanjo hizo katika Hospitali ya Wilaya ya Pangani, kituo cha chanjo Zahanati ya Bushiri, kituo chanjo Zahanati ya Madanga na kituo cha Chanjo Zahanati ya Kimang'a.

Nae Muuguzi mkunga wa Kituo cha Chanjo Zahanati ya Madanga alisema tokea uwepo  wa COVID 19, wamechukua hatua mbalimbali na kutoa elimu kwa wananchi wa Kijiji hicho cha Madanga.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kimang'a, Dkt. Mohammed Kombo alisema wameweza kuchukua hatua dhidi ya COVID19 ikiwemo kutoa elimu kwa wanakijiji.

"Tumechukua tahadhari ya COVID19  ikiwemo pia kutoa elimu kwa wanakijiji. Lakini wanakijiji nao wameweka utaratibu mgeni akija kijijini hapa lazima ajitenge kwa maangalizio na kuchukuliwa taarifa zake mpaka tunapojiridhisha" alisema Dkt kombo.

Ziara ya usimamizi elekezi inaendelea tena katika Wilaya mbalimbali za mkoa huo wa Tanga kwa uratibu wa Mpango wa Taifa wa Chanjo kwa kushirikiana na wadau wake.

MWISHO

Jumatano, 13 Mei 2020

WAMILIKI WA VIWANDA WATAKIWA KUZALISHA VIFAA KINGA KUKABILIANA NA CORONA

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akionesha moja ya kifaa kinga dhidi ya maambukizi ya Corona wakati akiongea na Umoja wa Wazalishaji Dawa, Vifaa na Vifaa Tiba (TPMA) nchini kwenye mkutano wa kuangalia jinsi gani wanaweza kuzalisha vifaa kinga kutoka wazalishaji wa ndani hapa nchini.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akiteta jambo na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa wakati akiongea na Umoja wa Wazalishaji Dawa, Vifaa na Vifaa Tiba (TPMA) nchini.

Baadhi ya Wazalishaji Dawa, Vifaa na Vifaa Tiba (TPMA) nchini wakitizama vazi la kujikinga dhidi ya Corona wakati wa mkutano wa kuangalia jinsi gani wanaweza kuzalisha vifaa kinga kutoka wazalishaji wa ndani hapa nchini ulioongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa.

Umoja wa Wazalishaji Dawa, Vifaa na Vifaa Tiba (TPMA) nchini wakiendelea na mkutano wa kuangalia jinsi gani wanaweza kuzalisha vifaa kinga kutoka wazalishaji wa ndani hapa nchini ulioongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa.


WAMILIKI WA VIWANDA WATAKIWA KUZALISHA VIFAA KINGA KUKABILIANA NA CORONA

Na.WAMJW- Dar es Salaam

Wamiliki wa viwanda vya Dawa, Vifaa na vifaa tiba nchini wametakiwa kuanza kuzalisha vifaa kinga kuweza kukabiliana na janga la Corona nchini ili kuondokana na changamoto ya ucheleweshaji wa kupata vifaa kinga toka nje ya nchi pamoja na kupunguza gharama.

Wito huo umetolewa leo jijini hapa  na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akiongea na Umoja wa Wazalishaji Dawa, Vifaa na Vifaa Tiba (TPMA) nchini kwenye mkutano wa kuangalia jinsi gani wanaweza kuzalisha vifaa kinga kutoka wazalishaji wa ndani hapa nchini.

“Tukizalisha hapa nchini tutaokoa rasiliamali fedha nyingi, muda pia tutazalisha ajira na kuwa na uhakika wa   ubora na usalama unaohitajika kupitia mamlaka zetu za ndani kwa urahisi”. Alisema Waziri Ummy.

Waziri amesema kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa vifaa kinga , hivyo wale wote wanaozalisha vifaa kinga wanatakiwa kuongeza uzalishaji ili kutosheleza mahitaji ya soko nchini na hata kuweza kuuza nchi za jirani.

Aidha, amesema  Wizara inahitaji kuipa nguvu  huduma salama kwenye vituo vya kutolea huduma za afya  vya serikali na visivyo vya Serikali kwa watumishi wa afya kuzingatia miongozo ya kukinga na kudhibiti maambukizi angalau kuvaa barakoa,glove na eproni hivyo amewasisitiza kuzalishaji vifaa vyenye  viwango vyenye  ubora ili kukidhi soko la ndani nan chi za jirani.

Naye Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa amewapongeza wamiliki wa viwanda hivyo kwa kubuni na kugundua teknolojia na uzalishaji wa  vifaa kinga kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo.

“Kuanzisha viwanda ni sehemu ya ulinzi wa nchi,hivyo kuwa na viwanda vyetu nchini hususani wakati wa shida imesaidia upatikanaji wa baadhi za vifaa kinga kwa bei nafuu”.Alisema Waziri Bashungwa.

Amesema katika kikao hicho wamekubalia kujipanga vizuri katika uzalishaji wa vifaa kinga na hivyo wamewataka Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kujikita katika kuzalisha barakoa aina ya N95 na glove kutokana na kwamba viwanda vya namna hii havipo nchini.

Pia Waziri Bashungwa ameitaka TMDA kushirikia na wizara ya viwanda kuisaidia NDC kuweza  kufanya kiwanda hicho kuanza kuzalisha kwa wakati na hivyo kusaidia watumishi wa afya walio mstari wa mbele kutoa huduma bila hofu.

Kwa upande wa MSD, Waziri Bashungwa ameitaka  kununua vifaa kinga vinavyozalishwa na viwanda vya ndani ambavyo vimekidhi viwango na vimesajiliwa na TMDA badala ya kutumia fedha iliyotengwa na Serikali kununua vifaa hivyo nje ya nchi.

Waziri Bashungwa ameahidi kukitembelea kiwanda cha Msagala Investment kilichopo Bagamoyo ambacho kinatarajia kuanza kuzalisha malighafi za utengenezaji wa barakoa kutokana na pamba zinazolimwa nchini.

 -Mwisho-

Jumanne, 12 Mei 2020

SAFISHA VITASA KATIKA MAENEO YA BIASHARA NA MAKAZI YETU

- Hakuna maoni
Mfanyabiashara wa duka la dawa baridi, eneo la Tabata Jijini Dar es Salaam akisafisha kitasa na kioo cha duka lake ikiwa ni sehemu ya maeneo hatarishi kupata virusi vya Corona kutoka na kushikwa mara kwa mara na wateja.

 Dereva boda boda eneo la Bagamoyo mjini. Bw. Octavian Leonard Nyoni akisafisha mikono yake kwa maji safi yanayotiririka na sabuni ikiwa ni sehemu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

 Timu ya uhamasishaji kutoka Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Wadau kutoka Shirika lisilo Lakiserikali la Project CLEAR wakiendelea na uhamasishaji kwa wananchi wa eneo la kituo cha mabasi cha Bagamoyo Mkoa wa Pwani, jinsi ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Sfaff sergeant (S/Sgt ) Valentine Ngowi, akitoa maelekezo namna ya kukaa mita moja au zaidi baina ya mtu mmoja na mwingine katika eneo la kituo cha mabasi ya Bagamoyo, ikiwa ni moja ya njia ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Abiria katika kituo cha mabasi cha Kisarawe Mkoa wa Pwani wakisafisha mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka na wengine kwa kutumia sanitizer kabla ya kupanda basi na kuanza safari, wamefanya hivo ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Balozi wa kampeni ya Mikoni safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba), akimkabidhi vipeperushi vya elimu juu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona kwa Afisa Afya wa Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani, Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima.

Ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani.


SAFISHA VITASA KATIKA MAENEO YA BIASHARA NA MAKAZI YETU

Na WAMJW- PWANI

Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima ametoa wito kwa Watanzania wote kujenga tabia ya kusafisha vitasa na maeneo yote yanayoshikwa mara kwa mara katika maeneo ya shughuli za kila siku na makazi yetu.

Ndg. Anyitike ameyasema hayo wakati akitoa elimu kwa wakazi wa Kisarawe na Bagamoyo Mkoa wa Pwani, kuhusu kuchukua tahadhari za kujikinga dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona katika maeneo ya biashara na makazi.

"Tuhakikishe tunasafisha maeneo yote tunayoyashika mara kwa mara kwa maji yenye sabuni, sanitizer au spirit, futa maeneo yote yanayoshikwa mara kwa mara, lakini kumbuka kufuta sehemu za vitasa vya mlango na meza " alisema

Pia, alisisitiza kuwa, ni muhimu kujenga tabia ya kufuta katika maeneo yote ambayo watu wanapendelea kukaa kama vile maeneo ya viti, meza na vioo katika maeneo ya biashara bila kusahau milango.

Aidha, Ndg. Anyitike Mwakitalima ametoa rai kwa wananchi hususan vinyozi katika maeneo ya saluni kuhakikisha wanavaa Barakoa (mask) pindi wanapokuwa katika maeneo yao ya kazi, ili kuvunja mnyororo wa maambukizi Corona kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwingine endapo utakuwepo.

"Unapoenda saluni usikubali kinyozi yoyote akunyoe nywele kama hajavaa Barakoa hali itayosaidia kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona katika maeneo ya kazi na kuvunja mnyororo wa maambukizi ya virusi hivyo" alisema.

Nae, Sfaff sergeant (S/Sgt ) Valentine Ngowi, ameendelea kuwakumbusha wazazi na walezi, kuhakikisha wanawalinda Watoto dhidi ya ugonjwa wa Corona, kwa kuwapa elimu, na kuhakikisha hawazululi hovyo mtaani, hasa katika kipindi hiki ambacho shule zimefungwa ili kuepusha misongamano inayoweza sababisha kusambaa kwa ugonjwa wa Corona.

"Tuhakikishe Watoto wanakaa nyumbani, Watoto wasiende kuzulula hovyo, ni rahisi Watoto kupata maambukizi ya Corona kwasababu ya ufahamu na uelewa wao juu ya madhara ya ugonjwa huu wa Corona " alisema.

Kwa upande wake, Balozi wa kampeni ya Mikoni safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) amewaasa wafanyabiashara wa Barakoa kutoruhusu wateja kujaribu barakoa na kuzirudisha, hali inaweka wanunuzi wengine katika hatari yakupata maambukizi ya virusi vya Corona.

" kwa wauzaji wa Barakoa, chonde chonde usiruhusu mtu ajaribu Barakoa alafu akaiacha, hii itasaidia kuvunja mnyororo wa maambukizi ya virusi vya Corona kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine endapo atatokea mtu mwenye maambukizi" alisema.

Timu ya Wizara ya Afya na Wadau kutoka Shirika lisilo Lakiserikali la Project CLEAR kupitia kampeni ya Mikono Safi, Tanzania Salama imeendelea kutoa elimu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona katika, Wilaya ya Bagamoyo, Wilaya ya Kisarawe na Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani.

Mwisho.

Ijumaa, 8 Mei 2020

SERIKALI ITAENDELEA KUTOA TAKWIMU ZA MWENENDO WA UGONJWA WA CORONA

- Hakuna maoni



Picha mbalimbali zikimuonesha Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akiangalia namna watoa huduma wanavyopokea simu kutoka kwa wananchi kwa ajili ya kupata elimu kuhusu ugonjwa wa Corona

Waziri Ummy Mwalimu akiongea na mwananchi  kupitia kituo cha afya cha huduma kwa wateja mara baada ya kukizindua
Picha ya pamoja ikionesha Waziri Mhe. Ummy Mwalimu akiwa na viongozi na wafanyakazi wa kituo cha afya cha huduma kwa wateja.

Na. WAMJW,Dar es Salaam.

Serikali itaendelea kutoa takwimu za mwenendo kuhusu Ugonjwa wa Corona mara baada ya kukamilika kwa maboresho ya kiufundi ya Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akizindua kituo cha Afya cha huduma kwa wateja (Afya call center) kilichopo eneo la Chuo cha Afya ya Sayansi ya Jamii Muhimbili (MUHAS), upanga Dar es Salaam.

“Takribani siku Saba sasa hatukuweza kutoa taarifa za takwimu za maabara  kuhusu mwenendo wa Corona nchini kwa sababu sasa hivi tunafanya maboresho  ya  maabara ya taifa ya afya ya jamii,hivyo niwatoe hofu wananchi kwamba ndani ya siku chache zoezi litakamilika na tutaendelea kutoa taarifa kwa umma mara kwa mara”, alisema.

Waziri Ummy amesema kuwa Corona ipo na itaendelea kuwepo kwa  miezi kadhaa,pia kumekuwepo na vifo kutokana na ugonjwa huu, hivyo wananchi wanapaswa kujua namna ya kuishi na ugonjwa huo kwa kujikinga na maambukizi.

 “Ninawasihi wananchi muondoe hofu na muendelee kuchukua tahadhari  ya kujikinga kwani ugonjwa wa Corona bado upo Tanzania, wagonjwa wapo na vifo vinavyotakana na COVID-19  vipo, ni muhimu kutambua kuwa ugonjwa huu utaendelea kuwepo kwa miezi kadhaa hivyo lazima mchukue tahadhari ya kujikinga kama magonjwa mengine”Alisisitiza Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amewataka wananchi kuendelea na  shughuli zao za ujenzi wa Taifa za kila siku pamoja na kuchukua tahadhari kwa  kuepuka  mikusanyiko isiyo ya lazima, kunawa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka, na kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu mwingine.

Kuhusu Uvaaji wa barakoa, Waziri huyo amewataka wananchi kuendelea kuvaa   barakoa za vitambaa ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo na kuwa barakoa za viwandani ziachwe zitumike kwa ajili ya watoa huduma za afya.

Amewashauri wananchi kufua na kupiga pasi barakoa za vitambaa kabla ya kuzitumia na kusisitiza kuwa zinapaswa kuwa safi kabla ya kuvaliwa.

MWISHO

Alhamisi, 7 Mei 2020

VIFO VYA CORONA KUCHUNGUZWA

- Hakuna maoni

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akisema jambo kwa watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando (hawapo pichani)

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi (wa upande wa kulia) akipokea zawadi za kwaheri kutoka kwa watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa - Bugando alipokuw akifanya kazi awali kabla ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania  Mhe. Dkt John Pombe Magufuli kuwa Mganga Mkuu wa Serikali. 

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi (wa upande wa kushoto) akipokea zawadi za kwaheri kutoka kwa watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa - Bugando alipokuw akifanya kazi awali kabla ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania  Mhe. Dkt John Pombe Magufuli kuwa Mganga Mkuu wa Serikali. 




Na WAMJW – Mwanza
Vituo vya kutolea huduma za afya nchini vyatakiwa kufanya uchunguzi juu ya kifo chochote kitakachotokana na ugonjwa wa corona ili kubaini kama mgonjwa alihudumiwa ipasavyo kabla ya kifo kutokea.

Agizo hilo limetolewa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akiwa Jijini Mwanza mara baada ya kuagana na uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa – Bugando alipokuwa akifanya kazi awali kama Mkurugenzi Mtendaji kabla ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Mganga Mkuu wa Serikali.

“Kwakweli tusingependa kuona mgonjwa anafariki kwa sababu zisizo na msingi, naagiza hospitali zote zenye kamati ya uchunguzi (Clinical Audit) kufanya uchunguzi wa vifo vinavyohusiana au kutokana na corona ili kuona kama kulikuwa na tatizo lolote katika kumpokea mgonjwa au katika kumhudumia” alisema Prof. Makubi

Prof. Makubi amewataka wananchi kuelewa kuwa sio kila kifo kinachotokea hivi sasa kinasababishwa na ugonjwa wa corona kwa kuwa yapo magonjwa mengine pia ambayo yanatushamblia binadamu.

“Siyo kweli kwamba mgonjwa akiwa na presha, kisukari, figo au kansa akifariki iwe imesababishwa na corona, tuendelee kuwahudumia wananchi, kuepusha vifo vinavyoweza kuwa na uhusiano wa corona”. Alisema Prof. Makubi.

Aidha Prof. Makubi ametoa rai kwa vituo vya afya kuwapokea wagonjwa wote na kuwapatia matibabu bila kuwabagua kuwa na dalili za corona.

“Serikali inapenda kuona wagonjwa wa corona wanapokelewa nakupata matibabu, tuendelee kuwapokea na kuwahudumia huku tukichukua tahadhari ya maambukizi”. Alisema Prof. Makubi.

“Watumishi wa afya wasiwe na ubaguzi wa kuchagua wagonjwa wa kuwahudumia au mpaka apimwe kipimo cha covid-19 ndio ahudumiwe, tuwapokee wote lakini wakati huo tukichukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa”.  Alisisitiza Prof. Makubi.

Katika hatua nyingine Prof. Makubi amesema kuwa Serikali inaendelae kusambaza vifaa kinga kwa ajili ya kuwawezesha watoa huduma kujikinga na ugonjwa huo wakati wakitoa huduma.

“Serikali imeanza kugawa vifaa kinga kama vile PPE, masks pia sanitizer kwa ajili ya vituo vyote vya afya Tanzania, kwahiyo pasIwepo kisingizio chochote cha kushindwa kumhudumia mgonjwa wa corona kwa sababu ya vifaa kinga”.

Mwisho

DKT. NDUGULILE AIAGIZA NIMR KUFANYA UTAFITI KUHUSU UGONJWA WA CORONA

- Hakuna maoni

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza katika mkutano na watafiti wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR juu ya maambukizi ya ugonjwa wa Corona.
Waziri wa Afya, Dkt. Ndugulile akifafanua jambo baada ya kumalizika kwa mkutano kujadili jinsi ya kupambana na Covid-19 nchini. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Prof. Yunus Mgaya.






Dkt. Ndugulile akijadiliana jambo pamoja na watafiti wa taasisi hiyo mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo.

WAMJW- Dar es Salaam                                                                           

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeitaka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kufanya utafiti kuhusu ugonjwa wa Corona (Covid-19) kwa kuwa kuna tofauti kubwa ya dalili zilizojitokeza kwa wagonjwa hapa nchini ukilinganisha na wagonjwa waliopo nje ya  nchi.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile wakati alipokutana na watafiti wa taasisi hiyo wakati  wakijadili maambukizi ya ugonjwa wa Corona na aina ya matibabu ambayo wagonjwa wanatakiwa kupatiwa hasa baada ya kubainika kuwa dalili za ugonjwa huo zinatofautiana na dalili za wagonjwa wa mataifa mengine.

“Kuna mambo mengi ambayo tunapaswa kuyafanyia utafiti wa kisanyansi, moja ni uelewa wa jamii, tunataka kujua wagonjwa wanaougua Corona ni wagonjwa wa namna gani, wana magonjwa ya aina gani, dalili zinazowapata wagonjwa ni za aina gani.  Hapa tunataka tupate uwelewa,” amesema Dkt. Ndugulile.

Pia, amesema kupitia utafiti huo wanataka kujua aina za matibabu ambayo wagonjwa wanatakiwa kupatiwa ili kuhakikisha ugonjwa wa Covid-19 unadhibitiwa hapa nchini.

“Kutokana na muitikio mkubwa wa tiba asili na tiba mbadala, kupitia kikao hiki nawaelekeza wataalamu wetu wajipange kufanya utafiti na kutoa majibu ya tiba ya maambukizi ya virusi vya Corona,” amesema Dkt. Ndugulile.

Amesema wamekubaliana na watafiti hao kufanyia kazi maagizo hayo ndani ya muda mfupi na kutoa majibu sahihi ambayo yatasaidia katika mapambano ya ugonjwa wa Corona.

Naye Mkurugenzi Mkuu  wa NIMR, Prof. Yunus Mgaya amesema mapambano dhidi ya ugonjwa Covid-19  ni vita ambayo inapaswa kufanyiwa utafiti ambao utasaidia kupatikana kwa njia sahihi za kukabiliana na maambukizi ya ugponjwa huo.

“Tunafahamu kwamba jamii za kiafrika zina utaalamu katika miti shamba. Katika hili kuna tafiti mbalimbali zinaendelea ili kuchunguza uwezo wa miti shamba kwa lengo la kupunguza makali ya Covid-19.

Mwisho

Jumanne, 5 Mei 2020

VIFO VYA WATOTO WACHANGA VIMEPUNGUA KUTOKA 25 KWA KILA VIZAZI HAI 1000 HADI SABA KWA KILA VIZAZI HAI 1000

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akizungumza wakati akipokea msaada wa vifaa kinga,vipeperushi,mabango na vifaa vya kutoa elimu kwa umma kwa ajili ya watoa huduma za afya na waandishi wa habari nchini

Waziri Ummy Mwalimu ameishukuru UNESCO na bank ya Absa kwa msaada wao.Kutoka kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Mabula Mchembe na kulia kwa Waziri  ni Mkurugenzi wa Rasiliamali watu kutoka banki ya Absa Tanzania Ltd. Patrick Foya

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto-Idara Kuu Afya Prof.Mabula Mchembe akiongea wakati wa kupokea msaada kutoka UNESCO na Benki ya Absa Tanzania Ltd


Mwakilishi Mkazi wa UNESCO nchini Tanzania, Tirso Dos Santos akikabidhi msaada wa vifaa kinga pamoja na vifaa vya elimu kwa umma kwa ajili ya waandishi wa habari


Na WAMJW – Dar es Salaam

Vifo vya watoto wachanga wenye umri wa chini ya siku 28 vimepungua kutoka 25 kwa kila vizazi hai 1000 kwa mwaka 2015/16 na kufikia saba  kwa kila vizazi hai  1000 kwa mwezi Machi mwaka huu.

Hayo yamesemwa leo  jijini  jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akipokea msaada wa vifaa kinga, mabango,vipeperushi na vifaa vya  kutoa elimu kwa Umma kuhusu ugonjwa wa Corona kutoka kwa Benki ya Absa Tanzania Ltd na Shirika  la UNESCO.

Waziri Ummy alisema kupungua kwa vifo hivyo kumetokana na jitihada zilizofanywa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli  katika kuimarisha sekta ya afya hapa nchini hii ni pamoja na kuboresha vituo vya kutolea huduma za afya, upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba.

“Kwa namna ya kipekee niwapongeza na kuwashukuru wakunga wote hapa nchini kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya kila siku ya kuwahudumia akina mama wajawazito na watoto  wenye umri chini ya miaka mitano”,.

“Pamoja na kuwa maambukizi ya Virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona (COVID-19) yapo na watu wanaumwa ugonjwa huu, lakini tusisahau kuwa kina mama wajawazito wanajifungua kila siku na wakunga  wanaendelea kuwahudumia kinamama hawa”, alisisitiza Waziri Ummy.

Waziri huyo aliwahakikishia wananchi kuwa pamoja na kuwa ugonjwa wa Corona upo   huduma zingine zinaendelea kama kawaida  katika vituo vituo vyote vya kutolea huduma za afya zikiwemo huduma za kliniki za akina mama wajawazito na watoto, upimaji wa magonjwa mbalimbali pamoja na upasuaji.

 “Ninawashukuru wadau mliotoa vifaa hivi, ninawaomba wadau wengine waendelee kuiunga mkono Serikali katika kupambana na ugonjwa wa Corona ambao ni janga la Dunia”,.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa wizara  hiyo Prof. Mabula Mchembe alisema  vifaa hivyo vitaboresha  utoaji wa huduma za afya katika vituo vilivyopo Dar es Salaam pamoja na maeneo mengine nchini.

“Ninawahakikishia wananchi pamoja na wadau mliotoa vifaa hivi kuwa  vitatumiwa na wataalamu wetu katika kutoa huduma mbalimbali za matibabu kwa wagonjwa wanaotibiwa katika vituo vyetu vya afya”, alisema Prof. Mchembe.

Akikabidhi vifaa hivyo Mkurugenzi wa  Rasiliamali watu wa benki ya Absa Tanzania Ltd. Patrick Foya alisema vifaa kinga walivyovitoa vyenye thamani ya milioni 20 ambavyo ni glovu, barakoa na vitakasa mikono vitawasaidia watoa huduma za afya wakati wanawahudumia wagonjwa.

Mwisho

Jumatatu, 4 Mei 2020

WAFANYA KAZI WA SALUNI CHUKUENI TAHADHARI DHIDI YA MAAMBUKIZI YA CORONA.

- Hakuna maoni
Kinyozi katika eneo la Mgeninani Kijichi Jijini Dar es Salaam akiwa amevaa Barakoa kama sehemu ya kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Mkazi wa eneo la Kigamboni Jijini Dar es Salaam akisafisha mikono yake kwa sabuni na maji safi yanayotiririka ikiwa ni sehemu ya kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Mfanyabiashara katika Soko la Shangwe Kigamboni Jijini Dar es Salaam akiendelea kumhudumia mteja wake huku akiwa amevaa Barakoa ikiwa ni sehemu ya kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona

Dereva boda boda katika eneo la Geza ulole Kigamboni wakipata elimu ya maambukizi ya virusi vya Corona kutoka katika timu ya uhamasishaji Wizara ya Afya.

Eneo la Mbagala Jijini Dar es salaam ambapo timu kutoka Wizara ya Afya ilipita kutoa elimu ya kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.



WAFANYA KAZI WA SALUNI CHUKUENI TAHADHARI DHIDI YA MAAMBUKIZI YA CORONA.

Na WAMJW - DSM

Serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa wito kwa Wafanya kazi katika maeneo ya saluni kuchukua tahadhari ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona katika maeneo yao.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima wakati akitoa elimu kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuhusu kuchukua tahadhari za kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

"Kwa wale ambao wanasafisha nywele, kucha, wanafanya masaji, wanaosuka nywele, mchukue tahadhari kwasababu mpo katika hatari kubwa sana ya kuambukizwa lakini vile vile kuambukiza watu wengine maambukizi ya virusi vya Corona" alisema

Aliendelea kusema kuwa, Serikali inaendelea kuwakumbusha wafanya kazi wote katika maeneo ya saluni kuhakikisha wanaepuka msongamano pindi wanapokuwa katika majukumu yao, huku akisisitiza ni muhimu kwa kinyozi kuvaa Barakoa pindi ananyoa.

"Tunawakumbusha tena, kwa upendo kabisa, Tunawakumbusha muepuke msongamano ndani, awepo mtu anaenyoa na anaenyolewa na yule ambae ananyoa ahakikishe muda wote amevaa Barakoa, tunawaambia hivi kwasababu tunawapenda" alisema.

Kwa upande wake, Sfaff sergeant (S/Sgt ) Valentine Ngowi, amewataka madereva wote wa vyombo vya moto hususan bodaboda na bajaj kuhakikisha wanavitakasa vyombo vyao vya usafiri kwa sabuni mara kwa mara ili kuua maambukizi ya virusi vya Corona endapo vitakuwepo.

Nae, Balozi wa kampeni ya Mikoni safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) amesisitiza kuwa ili kupambana na ugonjwa huu watu wasichoke kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka ili kuepuka kupata maambukizi ya virusi vya Corona.

Uhamasishaji huu unafanywa kupitia kampeni hii ya “Mikono safi, Tanzania salama” inaratibiwa na Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Project CLEAR kwa kushirikiana na Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) kutoka Mjomba Theatre Gallery unaendelea katika Jiji la Dar es Salaam.

Mwisho