Na Englibert Kayombo
Katika kuadhimisha Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani kila mwaka ifikapo tarehe 28 ya kila mwezi Septemba, Wizara ya Afya imewatahadharisha wananchi kujikinga na ugonjwa huo hatari ambao unaweza kusababisha vifo.
Katika kuadhimisha Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani kila mwaka ifikapo tarehe 28 ya kila mwezi Septemba, Wizara ya Afya imewatahadharisha wananchi kujikinga na ugonjwa huo hatari ambao unaweza kusababisha vifo.

Na WAMJW -KILIMANJARO
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Afya Mhe. Dkt Dorothy Gwajima kununua na kipeleka Jokofu la kuhifadhi pamoja na kuongeza Daktari mmoja katika kituo cha afya Ndungu Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro wakati serikali ikijipanga kukamilisha ajira za watumishi sekta ya afya kwa lengo la kuboresha utoaji huduma kwa wagonjwa.
Agizo hilo amelitoa wakati akikagua ukarabati wa kituo cha afya ndungu wilaya ya same mkoa wa kilimanjaro na kisha akazungumza na wabanchi katika eneo hilo.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa, serikali imejipanga kujenga vituo vya afya viwili na hospitali mbili katika jimbo la Same Magharibi na Same Mashariki kwa lengo la kusogeza huduma za afya kwa hamii.
Aidha waziri mkuu Kassim Majaliwa amewapongeza madaktari wa kituo cha afya Ndungu kwa jitihada zao za kuwahudumia wananchi wanaokabiliwa na Magonjwa katika eneo hilo.
Kwa Upande wake Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii,jinsia wazee na watoto Dkt Dorothy Gwajima ametoa maelekezo kwa Katibu wa Wizara ya Afya Dkt Makubi kutekeleza agizo hilo kwakupeleka Daktari mmoja kwa ajili ya kusaidiana na Dkt aliyepo kwenye kituo cha afya Ndungu ambacho kimeonesha kuzidiqa na wagonjwa ambapo kwa mwaka hufanya upasuaji unaofikia wagonjwa 305.
Katika hatua nyingine Dkt Gwajima amesema kuwa, ili Tanzania iwe salama wananchi wanatakiwa kushikamana kwa umoja wao kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya huku akitilia mkazo kwa wananchi kujitokeza kwa ajili ya kupata chanjo kwa kuwa ugonjwa wa uviko 19 unahatalisha maisha ya watu.
Katika Hafla hiyo Waziri Gwajima amesema kuwa, serikali imefanya ukarabati wa kituo cha afya Ndungu Same kitengo cha maabara, chumba cha wazazi na chumba cha kuhifadhi maiti na tayari wizara imetenga shilingi milioni 35 kwa ajili ya kununua jokofu la vyumba sita ambapo ameagiza MSD ihakikishe inapeleka jokofu katika kituo cha afya ndungu Same
Akizungumzia mikakati ya kuboresha huduma za afya mkoa wa Kilimanjaro,
Waziri Dkt Gwajima Amesema serikali ya awamu ya Sita umetenga kiasi cha sh bi 12 kwa ajili ya ujenzi wa jengo ka mama na Mtoto katika hospitali ya mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi ambapo ujenzi umefikia asilimia 70
Awali mbunge wa jimbo la Same magharibi Anne Kilango Malecela ameiomba serikali kujenga hospitali mbili kwa kuwa wilaya ya same ina majimbo mawili yenye watu wengi kiasi kwamba wanasabanisha msongamano mkubwa kwenye zahanati, na Vituo vya Afya.
MWISHO.
Katika vita dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza Taaluma ya Famasi ni muhimu katika kuwezesha upatikananji wa bidhaa za dawa kwa wale watakaoshindwa kuzuia kupata magonjwa yasiayoambukiza na ikawalazimu wafike vituoni kupata tiba.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa Kongamano la 12 la kisayansi la Chama cha Wanafunzi wa Taaluma ya Famasi (TAPSA) lililofanyika jijini Mwanza.
Dkt. Gwajima amebainisha kwamba bidhaa hizo za dawa kwa ajili ya kundi hilo ni ghali na bahati mbaya nchini Tanzania hakuna kiwanda cha kutengeneza na badala yake wanaagiza toka nje ya nchi.“Tunapaswa kutafakari iwapo kasi ya kukua kwa maradhi haya ni inaongezeka je tunazijazititi vipi kwenye kasi ya kinga kwani bado kasi hiyo ni ndogo”.Aliongeza Dkt. Gwajima.
Alisema kuwa, katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza Serikali imeendelea kuboresha upatikanaji wa huduma bora karibu zaidi na wananchi kwa kujenga miundombinu , kuajiri watumishi na kuweka vifaa tiba na dawa. Maboresho haya yameendelea kufanyika katika vituo vya huduma za afya ngazi zote.
Hata hivyo amesema kumekuwa na changamoto mbalimbali ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi ikiwemo changamoto ya upatikanaji wa bidhaa za dawa na vifaa tiba kwa ajili ya huduma mbalimbali zikiwemo na huduma kwa ajili ya wanaougua magonjwa hayo yasiyoambukizwa.
Aidha, Dkt. Gwajima amesema wapo baadhi ya wanataaluma wachache wasio waadilifu na wasio wazalendo ambao ni doa kubwa kwenye taaluma hiyo adimu ambayo inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa kwenye ajenda ya afya. Hivyo iwapo itasimama kwa nafasi yake basi wanataaluma hao wanaweza kufanya mapinduzi makubwa ya afya na kiuchumi.
“Hii itawezekana kwa kujikita kwenye ajenda ya jinsi gani viwanda vya ndani viweze kuzalisha bidhaa mbalimbali na kuhakikisha matumizi yasiyotia shaka ya bidhaa za afya zinazopokelewa kwenye vituo vya huduma na kuepuka upotevu na matumizi yasiyofuata miongozo na kusababisha usugu wa baadhi ya dawa na pia baadhi kuleta madhara kwa wateja kama ilivyokusudiwa”.
Dkt. Gwajima alitoa rai kwa jamii ya kitanzania kuzingatia ulaji unaofaa ambapo kila mlo uwe na makundi yote matano ya vyakula halisi, kutotumia mafuta mengi,chumvi nyingi,kufanya mazoezi ,kupata usingizi wa kutosha,kuepuka matumizi ya tumbaku na madawa ya kulevya na pia kuchunguza afya angalau mara moja kwa mwaka.
Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 75 ya vifo vyote duniani vinavyohusu watu wenye miaka 30 hadi 70 husababishwa na magonjwa hayo.Hapa nchini inakadiriwa kuwa magonjwa yasiyoambikiza husababisha asilimia 27 ya vifo vyote.Kauli mbiu ya Kongamano hilo mwaka huu ni “Wataalamu wa Famasi: kuongeza wigo katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza”.
Awali akiongea wakati wa kongamano hilo Mfamasia Mkuu wa Serikali Bw. Daudi Msasi aliwataka wafamasia na wataalum wengine wa afya nchini kuhakikisha wanatumia fomu za dawa( prescription form) kama nyenzo muhimu za kuondoa changamoto za dawa kwani dawa ni fedha za haraka hivyo wahakikishe kabla hawajatoka lazima wahakikishe dawa zinatoka kwa kujaza fomu hizo.
Aliongeza kuwa kwenye kutenda kazi za umma lazima wafuate miongozo ikiwemo muongozo wa matibabu nchini (STG) wanapokuwa sehemu za kazi hivyo ni wakati wao sasa wa kupitia na kuelewa nini wanapaswa kutekeleza kwenye kazi zao.
Hata hivyo Bw. Msasi aliwataka chama hicho kuanziasha klabu za mazoezi kwenye vyuo vyao ili kuweza kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kwa vitendo na hiyo itasaidia jamii kuelewa umuhimu wa kufanya mazoezi.
Naye Mlezi wa wanafunzi wa Famasi na Masajili wa Baraza la Famasi nchini Bi. Elizabeth shekalaghe aliwataka wanafunzi hao kufanya kazi kwa kujitoa, kuwajibika na kuipenda taaluma yao ili kuweza kuitumikia vyema taaluma yao.
Bi. Shekalaghe alisema kama Baraza wataendelea kusimamia na kuhakikisha wanaendeleza taaluma kwa kutoa elimu ya maadili kwenye vyuo vya famasi nchini ili wanapokua chuoni wazitambua na kuzijua angali wanafunzi.
Naye Rais wa Chama cha Wafamasia Wanafunzi Tanzania(TAPSA) Bw. Hamis Msagama ameipongeza Serikali kwa uboreshaji wa dawa na vifaa tiba ambapo kazi kubwa inafanywa na wafamasia na kuonesha jinsi gani inawajali watanzania.
Pia Bw.Msagama ameipongeza Wizara ya
Afya kwa kuanzisha kitengo cha Magonjwa Yasiyoambukiza (NCD) hivyo wao
kama chama waliona ni vyema kongamaono lao mwaka huu kujadili kwa kina
namna ya kupambana na magonjwa hayo ambayo yanaathiri watu wengi nchini na
duniani.

Na.WAMJW - DSM
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifelo Sichalwe amefanya ziara fupi katika hospitali ya rufaa ya Mkoa Amana Jijini Dar es Salaam yenye lengo la kukagua Utekelezaji wa maagizo ya Viongozi wa Wizara waliyoyatoa kwa nyakati tofauti kuhusu maandalizi na utayari wa Watumishi wa afya katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa covid 19.
Akiwa hospitalini hapo Dkt. Sichalwe amezungumza na uongozi wa hospitali hiyo ambapo amewataka viongozi hao wa wafanyakazi kujitayarisha kwa vifaa na matibabu kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
Amesema Kama watumishi wa Afya, ni vyema kuwa tayari wakati wowote hususan katika kipindi hiki ambacho nchi jirani wamekumbwa na wimbi la tatu la ugonjwa wa Corona kwa kuwa raia wa nchi hizi wana muingiliano mkubwa wa shughuli za kiuchumi na biashara, hivyo kama nchi hatuna budi kujipanga.
Sambamba na kikao hicho Dkt.Sichalwe amekagua miundombinu ya hospitali na utekelezaji wa afua za kuzuia maambukizi mahali pa kazi (Infection, prevention and control). Ameupongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa juhudi na jitihada kubwa wanayofanya hospitalini hapo kwa lengo la kuzuia ueneaji wa maambukizi kwani watumishi wote walikutwa wamevaa barakoa na sehemu za kunawia zenye sabuni na maji zikiwepo kila wodi, sehemu ya mapumziko na getini.
“Nimeona mmevaa barakoa, mnatoa elimu kwa wananchi pia. Haya mnayotekeleza hapa ni kama darasa kwa wananchi wote wanaokuja kupata huduma hapa nao watakuwa mabalozi kwa wenzao kwenye jamii. Nina imani utekelezaji huu mnaendeleza hata baada ya kazi”.
Aidha, Dkt.Sichalwe amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa nchini kusimamia utekelezaji wa afua hii, kwani unatukinga siyo tu na ugonjwa wa covid 19 bali na Magonjwa mengine mengi yanayosababishwa na kula vitu kwa mikono isiyo safi na kuvuta hewa yenye vimelea vya maambukizi.
Vilevile Dkt.Sichalwe ametembelea mtambo maalumu wa kuzalisha hewa ya Oksijeni hospitalini hapo ambapo ameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza zaidi ya Milioni 600 ili kuhakikisha wanaokoa Maisha ya watanzania wanaohitaji huduma hiyo.Mtambo huo wenye matoleo Zaidi ya 89, unauwezo wa kuzalisha mitungi 200 ya hewa ya Oksjeni kwa masaa 24 na hospitali ina uwezo wa kuhudumia watonjwa wenye uhitaji 150 kwa wakati mmoja.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume amesema kuwa juhudi hizo zinaendelea kufanywa na hospitali zote ndani ya Dar es Salaam ili kuhakikisha wanalidhibiti ipasavyo wimbi hili la tatu.

Na Englibert Kayombo – WAMJW, Dodoma
Wizara ya Afya inatarajia kuja na mfumo wa ufuatiliaji wa taarifa za wajawazito wote toka wanapofika kliniki kwa mara ya kwanza hadi baada ya siku 42 za kujifungua.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima leo alipokutana na wataalam wa afya katika kikaokazi cha maandalizi ya utengenezaji wa mfumo huo.
“Nataka muwe mnafuatilia taarifa za wajawazito na kujua maendeleo yao toka wanapofika kituoni siku ya kwanza mpaka baada ya kujifungua kwa data za kila siku na kujua kwa namna gani wajawazito au mama baada ya kujifungua ameweza kupata huduma zetu na muweze kuchukua hatua pale mnapoona changamoto” amesema Dkt. Dorothy Gwajima.
Waziri Gwajima amesema kuwa ili kuweza kuwa na mfumo wenye ufanisi ni lazima tusisitize matumizi sahihi ya takwimu na kuwataka wataalam wa afya katika kazi zao kuhakikisha wanachukua takwimu zote zinazohitajika kwa ajili ya matuzimu katika mfumo huo.
Waziri Dorothy Gwajima amesema kuwa Serikali katika kupambana na vifo vya wajawazito imefanya mambo mengi ikiwemo kuanzisha Kampeni maalum ya Jiongenze Tuwavushe Salama iliyoanzishwa na aliyekuwa Makamu wa Rais na sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan yenye lengo la kupunguza na kudhibiti vifo vitokanavyo na uzazi.
“Serikali imejenga vituo vingi vya huduma ngazi zote na mwamko wa wajawazito wanaojitokeza kuhudhuria kliniki umekuwa mkubwa” amesema Dkt. Dorothy Gwajima na kuongezea kuwa bado elimu inahitajika kutolewa kwa ili wajawazito wafike katika vituo vya kutolea huduma za afya na kuanza kliniki mapema.
“Sasa hivi mwitikio umeongezeka, wajawazito wanajitokeza na kujifungua katika vituo vya kutolea huduma kati yao wengine wanafariki, lakini tukijadili kujua kwanini amefariki na tukifuatilia wakati alipokuwa kliniki tunagundua hatukumfuatilia vizuri, hiki ndio kitu tunachoimarisha ili ufuatiliaji uwe imara” amefafanua Dkt. Dorothy Gwajima.
Waziri Gwajima amesema kuwa katika kuimarisha mfumo wa usimamizi na ufuatiliaji wa taarifa za wajawazito, wanatarajia kuimarisha ufuatiliaji wa mteja mmoja mmoja toka anapopata ujauzito, muda wa kuanza kliniki, kujifungua mpaka baada ya siku 42.
Naye Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichwale amesema kuwa kwa kupitia kanzidata wanazochukua kutoka kwenye taarifa za wajawazito zinawasadia kujua bidhaa gani za dawa zinazihitajika kumhudumia mjamzito, miundombinu ipi wanahitaji, inaonyesha uwajibikaji wa watumishi wa afya kwa ujumla wao na mmoja mmoja, pamoja na kutuonyesha kama miongozi iliyopo inatija katika kusaidia kutoa huduma bora kwa wajawazito.
“Hakuna njia nyingine ambayo tutaitumia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi zaidi ya kuimarisha ufuatiliaji na usimamizi wa mama mmoja mmoja kama kanzidata hii inavyotaka” Amesema Dkt. Sichwale
-Mwisho-

Na WAMJW - Dodoma
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amesema hedhi wanayopata wanawake sio ugonjwa wala laana bali ni uumbaji wa Mungu katika kumkamilisha mwanamke.
Waziri Gwajima amesema hayo leo katika ofisi za Wizara Jijini Dodoma wakati akiongea na waandishi wa Habari kuhusu siku ya hedhi ambayo inaadhimishwa kila mwaka duniani kote kila ifikapo tarehe 28 mwezi Mei ambayo mwaka huu ina kaulimbiu inayosema “Ni wakati wa kuchukua hatua ili kuhakikisha vifaa vya kujisitiri/taulo za hedhi zinapatikana kwa urahisi na bei nafuu kwa msichana/mwanamke”.
“Siku ya hedhi duniani inaadhimishwa kila mwaka, licha ya mwaka jana kutofanyika kutokana na changamoto ya Covid 19 lakini jumuiya ya Kimataifa imeendelea kufahamishana, kuelimishana na kukumbushana juu ya jambo hili muhimu kwa njia ya mtandao. Lengo kuu ni kueleza Dunia na Umma wa Tanzania kuwa hedhi sio ugonjwa wala laana bali ni hali ya kawaida na Baraka ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu inayomtokea msichana mara baada ya kuvunja ungo kama ishara ya mabadiliko kwenye mfumo wa maumbile yake ya uzazi”. Amesema Waziri Gwajima.
Waziri huyo ameongeza kuwa tafiti zinaonesha kila siku wanawake zaidi ya milioni 12 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 wanakuwa kwenye Hedhi duniani.
Aidha, Waziri Gwajima amesisitiza Hedhi Salama akimaanisha kwamba msichana au mwanamke anapokuwa katika siku zake anatakiwa kuzingatia mazingira salama na anapata huduma zote muhimu ikiwemo miundombinu ya vyoo vyenye usiri, maji safi, taulo za kike au vifaa salama vya kujisitiri na utupaji salama wa vifaa/taulo za kike zilizotumika.
Hata hivyo, Waziri amesema kuna baadhi ya wasichana au wanawake wanakua katika mazingira ya kutokua na hedhi salama ambayo inachangiwa na miundombinu duni ya vyoo, kukosekana kwa maji safi na salama, matumizi ya vifaa vya hedhi visivyo salama na utupaji ovyo wa vifaa vilivyotumika.
“Matokeo ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) pamoja na OR -TAMISEMI kwa kushirikiana na Wadau wa Hedhi Salama mwaka 2019, yanaonesha Nchi yetu imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya ajenda ya afya ya hedhi. Hata hivyo, changamoto ni nyingi katika ngazi ya jamii hususan kuwa na uelewa mdogo wa jamii juu ya hedhi salama. Kwa mfano ni asilimia 28 tu ya wasichana ndiyo wenye uelewa thabiti juu ya hedhi salama”. Ameongeza Waziri Gwajima.
Takwimu zinaonesha kuwa maeneo mengi hapa Nchini jamii inakosa uelewa wa umuhimu wa hedhi salama. Maeneo yaliyofanyiwa utafiti na kuonesha ukosefu wa uelewa wa hedhi salama ni pamoja na Halmashauri za Namtumbo, Muleba, Mbeya, Igunga, Temeke, Karatu, Tandahimba, Rorya, Kusini Unguja na Kaskazini Pemba ambayo jamii yake ilionekana inauelewa mdogo juu ya suala la hedhi salama. Huku utafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ukionesha kuwa asilimia 60 ya wasichana walionekana kutomudu gharama za taulo za kike.
Hata hivyo, Waziri Gwajima amewashukuru wadau kupitia mtandao wa hedhi salama kuendelea kuhamasisha upatikanaji wa vifaa vya hedhi salama ndani ya nchi kwa unafuu na ubora unaotakiwa ili kila mhitaji kwa makundi yote aweze kutumia.







Na.WAMJW-Dodoma
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeanza kufanya ufuatiliaji wa maelekezo yake katika kuboresha huduma za matibabu kwa wazee kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Dkt. Dorothy Gwajima alipotembelea hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma na kujionea jinsi walivyoweza kutekeleza maagizo ya utoaji wa huduma za afya kwa wazee wanaofika kupata matibabu hospitalini hapo.
Dkt. Gwajima amesema mahitaji ya maboresho ni mengi hivyo wizara yake imeona ianze na vitu vile vya msingi ambavyo wazee wamekuwa wakiyalalamikia kila siku wanapofika kwenye vituo vya kutoalea huduma za afya.
Ametaja malalamiko yanayokuwa yakilalamikiwa na wazee wanapofika kwenye vituo vya afya ni pamoja na mapokezi yasiyoeleweka na kutokupata huduma iliyokusudiwa na kuongeza kuwa wazee nguvu zimekwisha hivyo wanahitaji kuongozwa kwahiyo wizara yake wamefanya maboresho kwa kuwa na watu maalumu wa kuwapokea wazee hao pale wanapoifika hadi kuondoka na kuwatambulisha kwa kuvaa sare maalumu.
“Kila kituo lazima kiwe na nesi mmoja, afisa ustawi wa jamii pamoja na daktari aliyepangwa zamu na lazima wavae sare ambayo itamtambulisha na imeandikwa ‘Mzee ni Tunu, Tunakupenda, Tunakuheshimu’ pamoja na kuweka mabango yanayomuelekeza au kumuongoza mzee wapi atapata huduma anazozihitaji na ambayo yameandikwa "Mpishe Mzee apate huduma kwanza".
Dkt. Gwajima amesema maelekezo hayo wameyatoa katika hospitali na vituo vya afya vyote na kwa hatua hiyo sasa wizara inaenda kutengeneza muongozo ambao utakua wa uwiano kwa hospitali zote. Hata hivyo ameipongeza hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma kwa kuanza utekelezaji huo na kuwa itakuwa ya mfano wengine kujifunza utaratibu unaotumika na kuboresha kulingana na mazingira yao.
Aidha, Dkt. Gwajima amewataka hospitali zingine kutokusubiri miongozo katika kutekeleza maelekezo yanayolewa na kusiwe na visingizio vingi kwamba haiwezekani kwani maagizo yanayotolewa yanawezekana na utekelezaji wake ni wa mara moja hususan katika hospitali za kuanzia halmashauri hadi ngazi ya Taifa.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya Dkt. Vivian Wonanji amesema idara yake imeandaa mkakati wa huduma wa wazee wa miaka kumi na ifikapo mwezi Juni mwaka huu wataanza kuandaa mpango wa utekelezaji wake.
Dkt. Wonanji amesema mpango mkakati huo utakuwa na mambo makuu yakiwemo kuzalisha wataalam wa kutoa huduma za wazee,"kama tunavyofahamu wazee wanahitaji mambo mengi ikiwemo masuala ya lishe na utengamao hivyo mkakati huo utakua na maono muhimu ambayo yatasaidia kuboresha huduma za wazee nchini”.
Wakati huo huo Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma Dkt. Ernest Ibenzi amesema hospitali yake imejipanga kuwahudumia wazee wa rika tofauti wakiwemo wenye uoni hafifu na hivyo waratibu wa wazee huwafuata wazee mara wafikapo hospitalini hivyo wanashukuru mapokeo ya wazee pamoja na wagonjwa wanaofika kupata huduma.
Mnamo tarehe 7 Mei, mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati akiongea na wazee wa Mkoa wa Dar es salaam aliahidi kuboresha tiba kwa wazee kwani tiba ni haki yao ya msingi katika daraja lolote lile watakalokua wanaugua kuanzia vituo vya afya, zahanati hata hospitali za Taifa.
-Mwisho-

Na. Catherine Sungura, WAMJW-Dodoma
Serikali imeweza kujibu changamoto za kuwahudumia wananchi kwa kuimarisha huduma za afya ya dharura kwa kusimika mitambo ya kufua hewa tiba (Oksijeni) na hivyo kupunguza gharama za uendeshaji wa hospitali za rufaa za mikoa nchini.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati alipotembelea hospitali ya rufaa ya mkoa Dodoma kujionea jinsi walivyounganisha mitambo hiyo kwenye wodi ya wagonjwa mahututi na watoto.
Dkt.Gwajima amesema mitambo hiyo ambayo Serikali kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Dunia hivi sasa imefungwa kwenye hospitali za rufaa za mikoa saba ya Dodoma, Mtwara ,Manyara, Mbeya, Amana Geita na Songea na hivyo wizara yake ipo njiani kukamilisha kufungia hospitali zote za rufaa za mikoa hapa nchini.
“Mitambo hii imefungwa kwa gharama isiyopungua bilioni 1.4 kila hospitali na inalenga kuzalisha mitungi 200 ya hewa hiyo kwa masaa 24 , na kila mtambo unayo sehemu ya mabomba yenye mita 400 yanayosafirisha hewa hii pia mitungi 73 imenunuliwa pamoja na mitambo hii kwa hila hospitali haya ni mapinduzi makubwa”. Alisisitiza.
Aidha, Dkt. Gwajima amefurahishwa na uongozi wa hospitali hiyo kwa kukamilisha kufunga mitambo hiyo na kuanza kutoa huduma kwenye wodi ya wagonjwa mahututi(ICU) pamoja na wodi ya watoto na hivyo wameweza kuunganisha vitanda 78 kutoka vitanda 10 vya awali na kufanya jumla ya vitanda 88 kupatiwa huduma hiyo hospitalini hapo.
“Hatua hii itapunguza kwa kiwango kikubwa gharama za kuhudumia mgonjwa mwenye mahitaji ya hewa hii,wito wangu tuitumie vizuri na kuzingatia na kuhakikisha matengenezo kinga yanafanyika kwa ufanisi”.
Dkt. Gwajima amesema kuwa uwekezaji huo umeweza kujibu changamoto ya kipindi cha mlipuko wa Covid-19 ulioripotiwa nchin mwezi Machi mwaka 2020 na hivyo kusababisha kuongezeka kwa mahitaji ya hewa ya oksijeni na kuwa gharama zake zilipanda.
“Niwapongeze sana waganga wafawidhi wa hospitali za rufaa za mikoa kwa kuja na wazo hili la kufunga mitambo hiyo kwenye hospitali zetu na hivyo tutaweza kusaidia hospitali za wilaya na vituo vya afya na hivyo kuwapunguzia matumizi ya fedha ya kununua oksejeni ,haya ni mapinduzi makubwa kwa Serikali yetu”. Alisisitiza Dkt. Gwajima
Aliongeza kuwa Kwa upande kwa kuepuka magonjwa ya kuambukiza ambayo yameanza kuyakumba mataifa mengine, Waziri huyo aliwataka waganga wakuu wa mikoa na wafawidhi kwenye hospitali za rufaa za mikoa kuendelea kutoa elimu kwa umma kwa kutumia vyombo vya radio vilivyopo kwenye maeneo yao (Community radio) ili kuwaondolea wananchi hofu na kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza ikiwemo janga la Corona.
“Serikali kupitia sekta ya afya kwa kushirikia na wadau wake nchini iko makini kufuatilia kinachoendela duniani na kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa salama na imara katika kudhibiti milipuko ya magonjwa mbalimbali ikiwemo huu wa Covid-19”.Alisema Dkt. Gwajima.
Dkt. Gwajima aliwakumbusha wadau,wataalam pamoja na wananchi wote kuendelea kuchukua tahadhari muhimu ambazo zimekuwa zikielemishwa mara kwa mara dhidi ya kujikinga na kudhibiti magonjwa mbalimbali ikiwemo C0vid-19 kwa kuepuka hofu,kuimarisha tabia ya kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi tiririka na sabuni,kufanya mazoezi,kula lishe au vyakula vya mbogamboga kwa wingi na matunda,kutumia tiba asili, kuepuka misongamano isiyo ya lazima na mwisho kuwahi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya mara unapoona dalili za maradhi yeyote.
Naye Mganga Mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa Dodoma Dkt. Ernest Ibenzi amesema wanatarajia kufunga mitambo ya kujazia hewa tiba hiyo ili kuweza kusaidia vituo vya afya vilivyo jirani na kusambaza huduma hiyo kwenye hospitali nzima.
-Mwisho-