Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (kulia ) akiangalia baadhi ya vitabu vinvyotuika kutoa elimu kwa wananchi wakati alipotembelea banda la maonesho la Shirika lisio la kiserikali la AGPAHI, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani ambayo yamefanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (kulia ) akipokea maelezo kutoka kwa mmoja wa wakunga ya namna wanavyowahudumia wakina mama wajawazito na watoto wakati alipotembelea Banda la Chama cha Wakunga Tanzania(TAMA), katika Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani ambayo yamefanyika Kitaifa katika Uwanja wa Bariadi Mkoani Simiyu.
Baadhi ya
wakunga wakiwa katika maandamano wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wakunga
Duniani ambayo yamefanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri
ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.
Naibu Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Faustine
Ndugulile akimkabidhi mmoja wa kunga wa moa wa Simiyu cheti kama zawadi ya
kufanyakazi nzuri, katika Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani ambayo
yamefanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa
Bariadi Mkoani Simiyu.
Na WAMJW - Simiyu
Naibu Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile
ametoa rai kwa viongozi wa Kisiasa hapa nchini kuacha kuingilia kazi za
Kitaaluma katika sekta ya Afya na kuwaomba wawaache wataalam wafanye kazi zao
kwa misingi na miiko ya Kitaaluma inayowaongoza.
Dkt. Ndugulile
ameyasema hayo katika Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani
yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, chini ya
Kauli Mbiu “Wakunga Watetezi wa Haki za Wanawake”, ambapo alikuwa akimwakilisha
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Amesema hivi
karibuni kumekuwa na matamko yanayotolewa na baadhi ya viongozi wa kisiasa
yanayowakatisha tamaa watumishi wa sekta ya afya na baadhi ya viongozi wameanza
kuingilia masuala ya kitaalum, hivyo akawaomba ikiwa viongozi hao watakutana na changamoto za watendaji wa afya
waishirikishe wizara ya afya ili wachukuliwe
hatua kwa mujibu wa taaluma zao.
“Niwaombe sana
viongozi wa Serikali na Viongozi wa vyama, masuala ya kitaaluma yanashughulikiwa
kitaaluma kama kuna changamoto na wanataaluma ndiyo maana tuna mabaraza ya
taaluma na ndiyo maana sisi wizara tupo mtushirikishe, nimelisema hili kwa
sababu nimeona sekta imeanza kuingiliwa” alisema Dkt. Ndugulile.
Aidha, Dkt.
Faustine Ndugulile amewataka wakunga hapa nchini kuendelea kuzingatia miiko na
misingi ya taaluma yao katika huduma wanazotoa kwa jamii na kuahidi kuwa
Serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote watakaokiuka misingi hiyo kwa
kuwa jamii inahitaji heshimu, utu, upendo na kutiwa moyo
Katika hatua
nyingine Dkt. Ndugulile ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa maendeleo na jamii kwa
ujumla kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za afya ili
changamoto ya vifo vitokanavyo na uzazi vibaki kuwa historia ambapo amesema kwa
sasa wanawake 11,000 wanakufa kila mwaka kutokana na uzazi.
Rais wa Chama cha
Wakunga Tanzania, Bibi. Feddy Mwanga ameiomba Serikali kuongeza idadi ya
wakunga ili mkunga aweze kutoa huduma kwa kiwango kinachokubalika Kitaifa na
kimataifa huku akisisitiza Serikali kuona haja ya kujenga nyumba za wakunga
katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya vinavyoboreshwa na vinavyojengwa.
Naye Mkuu wa
Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Mhe. Anthoy Mtaka amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa shilingi bilioni saba fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa na shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali tatu za
Wilaya Bariadi, Busega na Itilima ambazo ujenzi wake unaendelea vizuri.
Aidha, Kiswaga
ameshukuru Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu
Duniani(UNPFA) kwa namna linavyoshirikiana na Serikali mkoani Smiyu kwa
kukarabati baadhi ya vituo, kununuaa vifaa mbalimmbali, kutoa mafunzo kwa
wakunga jitihada ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo
vitokanavyo na uzazi.
Akitoa taarifa ya
Mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amesema
Idadi ya wakunga
katika vituo vya kutolea huduma za afya Simiyu imeongezeka hali iliyofanya
wajawazito wengi kujifungulia katika vituo vya afya kutoka asilimia 62 mpaka
asilimia 68, hivyo vifo vya mama wajawazito vimepungua kutoka vifo 48 mwaka
2017 mpaka vifo 40 mwaka 2018.
Naye Makamu Mwakilishi Mkaazi wa UNFPA hapa nchini, Dkt.Hashina Begum
amesema kwa kushirikiana na Chama cha Wakunga nchini (TAMA) limetoa mafunzo kwa
wakunga 90 kutoka katika vituo vilivyoboreshwa ili kuwasaidia wakina mama
wajawazito na watoto kupata huduma za dharura na kupunguza vifo kwa mama na
mtoto vitokanavyo na uzazi.
Grace Magengeni
Mkunga kutoka Jijini Dodoma amesema” siku yetu imefana tunashukuru hotuba ya
Naibu Waziri imetutia moyo katika kuwahudumia wanawake na watoto, nawashauri wenzangu
tusimamie taaluma zetu tufanye kazi kwa bidii naamini hao wanaotuingilia majukumu
yetu wataachaa maana ni kweli, tunashukuru
Naibu Waziri kulisemea hili suala”
Mwisho