Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisisitiza jambo mbele ya wananchi (hawapo kwenye picha) wakati wa matembezi ya hisani yanayolenga kuwezesha uwepo wa Wakunga kwa uzazi salama.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (Watatu kushoto) akiteta jambo na Waziri wa Afya wa Serikali ya Zanzibar Bw. Hamad Rashid Mohamed wakati wa matembezi ya hisani yanayolenga kuwezesha uwepo wa Wakunga kwa uzazi salama, Kulia kwa Waziri Ummy ni Mkurugenzi wa Amref Health Africa nchini Bi. Florence Temu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu pamoja na Waziri wa Afya wa Serikali ya Zanzibar Bw. Hamad Rashid Mohamed wakinyoosha viungo muda mfupi baada ya kumaliza matembezi ya hisani yanayolenga kuwezesha uwepo wa Wakunga kwa uzazi salama, yaliyofanyika katikati viwanja vya farasi Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Amref Health Africa nchini Bi. Florence Temu akiwasilisha taarifa ya mradi wa SUAM mbele ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (hayupo kwenye picha) wenye lengo la kuwezesha uwepo wa Wakunga kwa uzazi salama
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (wakatikati) pamoja na Waziri wa Afya wa Serikali ya Zanzibar Bw. Hamad Rashid Mohamed wakimkabidhi zawadi ya cheti Mkurugenzi Mtendaji wa Azania Bank, Charles Itembe kwa mchango mkubwa walioutoa kufanikisha matembezi hayo ya hisani yanayolenga kuwezesha uwepo wa wakunga kwa uzazi salama nchini.
Picha ya pamoja ikiongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Waziri wa Afya wa Serikali ya watu wa Zanzibar Bw. Hamad Rashid Mohamed wakati wa matembezi ya hisani yanayolenga kuwezesha uwepo wa Wakunga kwa uzazi salama, yaliyofanyika katikati viwanja vya farasi Jijini Dar es Salaam.
Na WAMJW- DSM
Serikali kupitia Wizara ya Afya, yaendelea kuboresha huduma za Afya za dharura nchini kwa kuviwezesha vituo vya Afya kuweza kutoa huduma za uzazi wa dharura ikiwemo upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni ili kuokoa vifo vitokanavyo na matatizo ya uzazi pingamizi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu leo wakati wa matembezi ya hisani yanayolenga kuchangia Juhudi za kupunguza na kuepusha vifo vya wajawazito na Watoto wachanga vitokanavyo na uzazi, katika viwanja vya farasi Jijini Dar es Salaam.
Waziri Ummy amesema kuwa wakati Serikali ya awamu ya tano inaingia madarakani ilikuwa vituo vya Afya takribani 109 sawa na asilimia 19 ya vituo vya Afya ambavyo vilikuwa na uwezo wa kutoa huduma za upasuaji za dharura pamoja na kumtoa mtoto tumboni, huku sasa kuongezeka hadi kufikia takribani vituo 460.
Aidha, Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa kila mwaka Wanawake 11,000 hufariki nchini, sawa na wanawake 900 kila mwezi, ikiwa ni sawa na wanawake 30 kila siku hufariki wakiwa wanatimiza wajibu wao wa msingi wakuleta kiumbe Duniani, hivyo ni lazima Juhudi za ziada ziendelee kuchukuliwa.
Kulingana na takwimu zilizofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu zinaonesha kwamba vifo katika kila vizazi hai 100,000 wanawake 556 hufariki, huku wanawake wajawazito nchini wakiwa Milioni 2 kwa mwaka
Mbali na hayo, Waziri Ummy amesema kuwa Serikali imeweza kuongeza bajeti ya dawa hadi kufikia takribani Bilioni 260, ikilinganishwa na bajeti ya Bilioni 30 iliyokuwepo kabla ya Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani, huku dawa kama ’magnesium sulfate' kwa ajili ya kifafa cha mimba zikipatikana bila malipo.
"Tumeweza kuongeza bajeti ya dawa, wakati tunaingia madarakani ilikuwa takribani Bilioni 30, sasa hivi tunazungumzia bajeti ya dawa ya Bilioni 260, huku dawa kama magnesium sulfate kwa ajili ya kifafa cha mimba zinapatikana bure bila malipo yoyote katika vituo vyetu vya kutoa huduma za Afya " alisema Waziri Ummy.
Hata hivyo, Waziri Ummy amesema kuwa licha ya maboresho makubwa yanayoendelea kufanywa bado kuna changamoto ya Watoa huduma za Afya, hivyo amelipongeza Shirika la Amref kwa jitihada za kuajiri baadhi ya Watoa huduma jambo linalosaidia kupunguza changamoto katika Sekta ya Afya.
"Tunauhitaji wa watumishi wa Afya takribani 200,008 katika vituo vya Afya vya Serikali kuanzia ngazi ya Zahanati mpaka ngazi ya Hospitali za rufaa za mikoa, huku watumishi waliopo ni takribani 98,000, hivyo pengo likiwa ni Asilimia 52, huku Zahanati zikiwa ndio waathirika wakubwa" alisema Waziri Ummy
Nae Waziri wa Afya wa Serikali ya watu wa Zanzibar Bw. Hamad Rashid Mohamed amewataka wakina mama kuwai katika vituo vya kutolea huduma za Afya pindi waonapo dalili za ujauzito, ili kuokoa vifo ambavyo vinaweza zuilika wakati wa kujifungua.
"Katika zile siku 12 za mwanzo wajitahidi kufika katika vituo vya Afya kupata uangalizi, na vifo vingi ndio huanza kutokea hapa, kwahiyo ningeomba sana wakinamama kuwahi katika vituo vya Afya, kuonana na wakunga waliopata elimu ili wapate huduma kwa wakati " alisema Hamad Rashid.
Mwisho