KAULI YA SERIKALI KUHUSU MLIPUKO WA UGONJWA
WA HOMA YA DENGUE NCHINI
1.
UTANGULIZI
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa Kanuni Na. 49 Ibara ya (1), (2) na (3) ya
Kanuni za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Toleo la Mwaka
2016, naomba kutoa Kauli ya Serikali kuhusu mlipuko wa Homa ya Dengue nchini.
Mheshimiwa
Spika, ugonjwa wa Dengue sio
ugonjwa mpya. Ugonjwa huu ulianza kutolewa taarifa hapa nchini tangu mwaka
2010, na kutolewa tena mwaka 2013, 2014, 2018 na mwaka huu (2019). Kidunia
inakadiriwa watu milioni 390 huugua ugonjwa wa homa ya Dengue kila mwaka huku
vifo vitokanavyo na ugonjwa huo vikiwa 40,000 kwa mwaka ikilinganishwa na
ugonjwa wa Malaria ambapo watu 216 Million huugua ugonjwa huo kwa mwaka huku
vifo vikiwa 450,000. Kama ilivyo katika nchi
nyingi duniani zinazoathirika na mlipuko wa ugonjwa huu, mara nyingi
hutokea nyakati za mvua hasa katika maeneo ya mijini ambayo kuna mazalia mengi
ya mbu kutokana na kutuwama kwa maji. Ugonjwa huu huenezwa na mbu aina ya Aedes ambae ni mbu mweusi mwenye
madoadoa meupe ya kung’aa na ambaye hupendelea kuuma hasa wakati wa asubuhi,
mchana na jioni.
Mheshimiwa
Spika, dalili za ugonjwa huu ni pamoja na homa
ya ghafla, kuumwa na kichwa hususan sehemu za macho, maumivu ya viungo na uchovu. Dalili hizi huanza kujitokeza kati siku ya 3 hadi
14 tangu mtu alipoambukizwa virusi vya homa ya Dengue. Wakati mwingine dalili
za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za ugonjwa wa Malaria. Aidha, mara chache hutokea
mgonjwa wa homa ya Dengue, anapata vipele vidogovidogo, anavilia damu kwenye
ngozi na wengine kutokwa
na damu sehemu za fizi, mdomoni, puani, kwenye macho na pia kwenye njia ya
haja kubwa au ndogo.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka 2019, ugonjwa
huu umeanza kutolewa taarifa katika vituo vya kutolea huduma za Afya hapa
nchini kuanzia mwezi Januari hadi tarehe 19 Juni 2019 jumla ya wagonjwa 4,320 na vifo 4 vilivyotokana
na homa ya Dengue vimetolewa taarifa
huku Mkoa wa Dar es salaam ndio unaoongoza kuwa na wagonjwa wengi. Ifuatayo ni
idadi ya wagonjwa na vifo kwa mikoa: Dar es salaam 4,029 na vifo 3, Dodoma 3 na
kifo 1, Tanga 207 na vifo 0, Pwani 57 na vifo 0, Morogoro 16 na vifo 0, Arusha
3 na vifo 0, Singida 2 na vifo 0, na Kagera 2
na vifo 0. Aidha vifo vilivyotolewa taarifa ni kutoka
katika hospitali za; Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma -1, Hindu-Mandal
-1 na Hospitali ya Regency-2.
2. HATUA ZILIZOCHUKULIWA NA SERIKALI
KUDHIBITI UGONJWA HUU
Mheshimiwa
Spika, toka kuripotiwa kwa
mlipuko wa Dengue, Wizara imeendelea kuimarisha mikakati ya kudhibiti ugonjwa huu,
kwanza kwa kuandaa mpango wa dharura wa miezi sita (Mei-Oktoba, 2019) wa
kukabiliana na ugonjwa wa Denguenchini. Katika mpango huu yafuatayo
yanatekelezwa;
(i)
Kuangamiza
mazalia ya mbu wapevu (Adults mosquitoes ) na viluwiluwi nchini ambapo Wizara
imeshanunua kiasi cha lita 60,000 za Viuavidudu (biolarvicides) kutoka
kwenye kiwanda cha uzalishaji kilichopo Kibaha kwa ajili ya kuangamiza viluwiluwi
katika mazalia ya mbu. Kati ya hizi Lita 11,400 zimesambazwa kwenye Halmashauri
5 za mkoa wa Dar es Salaam. Lita 48,600 zinasambazwa kwenye Halmashauri za
Mikoa ya Geita (lita 8,092), Kagera (Lita 12,308), Kigoma (7,616), Lindi
(9,048) na Mtwara (Lita 11,536). Pia lita zingine 36,000 zimeagizwa ambapo
zitasambazwa kwenye Mikoa yenye Mlipuko wa Ugonjwa huu ikwemo Pwani, Morogoro
Tanga na Singida. Aidha Wizara imeagiza pia mashine kubwa 6 kwa ajili ya
kupulizia mbu wapevu (aina ya Fogging machine) na mashine hizi zinatarajiwa
kufika kabla ya mwisho wa mwezi Julai, 2019. Dawa za kunyunyizia nje (aina ya
Acteric) lita 2,000 kwa ajili ya kuua mbu wapevu pia zimeagizwa ambazo
zitasambazwa katika Mikoa ya Dar es salaam, Pwani na Tanga.
(ii)
Kuunda
kikosi kazi cha watalaam cha kushughulikia udhibiti wa mbu wanaoeneza ugonjwa wa Dengue na
Malaria nchini na inategemewa kuwa kikosi kazi hiki kitaimarisha jitihada za
udhibiti mbu ndani ya Mikoa na Halmashauri
zote nchini hususan zenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya Dengue na Malaria
yaani Dar es salaam, Tanga, Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara, Kigoma, Geita na
Kagera.
(iii) Katika kuimarisha uchunguzi na matibabu ya ugonjwa wa
Homa ya Dengue, Bohari ya Dawa imeshanunua
vipimo 30,000 vya kupima Homa ya Dengue na awali Wizara ilielekeza Vituo
vya umma vya kutolea huduma kutoa huduma ya vipimo vya Dengue kwa utaratibu wa
kawaida wa uchangiaji wa gharama za matibabu.
(iv)
Kutengeneza
na Kusambaza Mwongozo wa matibabu ya ugonjwa huu kwa ajili ya watoa huduma
katika vituo vya kutolea huduma
(v)
Kuimarisha
ufuatiliaji wa magonjwa nchi nzima kwa kutumia mfumo uliopo wa ukusanyaji wa
taarifa, ambapo tunaendelea kupata taarifa za kila siku juu ya mwenendo wa
ugonjwa huu na magonjwa mengine.
(vi)
Kutoa
elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari pamoja na ujumbe kwa njia ya mitandao
ya kijamii.
Mheshimiwa Spika, kupitia hatua hizi, takwimu za hali ya maambukizi ya
ugonjwa wa Dengue zinaonyesha kuwa maambukizi mapya yameanza kupungua kutoka
wagonjwa 2494 wa mwezi Mei 2019 hadi wagonjwa 813 kufikia tarehe 19 Juni, 2019.
3.
CHANGAMOTO YA UDHIBITI WA UGONJWA WA HOMA YA DENGUE
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na changamoto mbalimbali katika kudhibiti mlipuko
wa Homa ya Dengue nchini. Changamoto hizi ni pamoja na:
1. Gharama za kupima Ugonjwa Homa ya Dengue
Ingawa Serikali
kupitia Bohari ya Dawa imenunua vipimo moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji na
hivyo kuviuza kwa bei nafuu ukilinganisha na gharama inayotozwa kutoka kwenye
baadhi ya Hospitali binafsi, bado Wananchi wanashindwa kumudu gharama za
uchangiaji matibabu ya ugonjwa wa Homa Dengue
2. Ushirikishwaji wa Jamii
Jamii bado haijaweza
kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa kampeni ya usafi wa mazingira ambayo
ni njia kuu ya kudhibiti mazalia ya mbu
3. Matibabu ya Ugonjwa huu katika vituo vya kutolea huduma
Watoa huduma za Afya
kutokufuata kikamilifu miongozo ya matibabu ya ugonjwa wa Homa ya Dengue
4.HITIMISHO
Mheshimiwa
Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa Wizara
imepitia Miongozo na Kanuni za Kimataifa, ambayo pia
ipo katika Sheria ya Afya ya Jamii namba 1. ya mwaka 2009 kuweza kupata mwongozo
wa namna bora ya utoaji wa matibabu kwa mlipuko wa ugonjwa wa Dengue ambao upo
sasa nchini. Kupitia sheria hii, vipo vipengele mbalimbali ambavyo vimeanisha jinsi
gani matibabu ya magonjwa ya milipuko mikubwa kama ya Homa ya Dengue inapaswa
kutolewa na hii ikiwemo utoaji wa matibabu bure ili kurahisisha udhibiti wa magonjwa ya
milipuko yasisambae kwa haraka katika
jamii.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia
sheria hii, Serikali ya Awamu ya tano chini ya Mhe Rais, Dkt John Pombe
Magufuli, inayojali wananchi wake, sasa imeamua kuwa vipimo kwa ajili ya Homa ya Dengue vitatolewa BURE kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya
vya umma wakati huu wa mlipuko.Aidha, Serikali itaboresha matibabu kwa
wagonjwa kwa kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa dawa za kutosha na pia
itaendelea kuwajengea uwezo wataalam wa Afya
sambamba na kuboresha mifumo ya ukusanyaji takwimu.
Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwa
tunadhibiti ugonjwa huu nchini, ninaitaka
Mikoa na Halmashauri zote nchini hasa zenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya
Dengue na Malaria kusimamia kikamilifu kampeni za usafi wa mazingira na
kuangamiza mbu kwa kunyunyizia dawa kwa ajili ya kuuwa mbu wapevu na kutokomeza
mazalia ya mbu. Aidha natoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali
katika kudhibiti ugonjwa huu kwa kuchukuwa hatua stahiki za kujikinga na
ugonjwa huu na kuimarisha usafi wa mazingira na kuangamiza mazalia ya mbu.
UMMY A. MWALIMU
WAZIRI
WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII,
JINSIA, WAZEE NA WATOTO
21/06/2019
0 on: "KAULI YA SERIKALI KUHUSU MLIPUKO WA UGONJWA WA HOMA YA DENGUE NCHIN"