Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu pamoja na viongozi wa kutoka Wizara ya Afya wakiongea na moja kati ya watu waliojitokeza kuchangia damu, katika Maadhimisho ya Siku ya Wachangia Damu Duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Mwanza, viwanja vya Furahisha.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akibadilishana mawazo na Mkurugenzi mtendaji wa EMEA Bw. Helmut Butterweck wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wachangia Damu Duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Mwanza, viwanja vya Furahisha.
Baadhi ya picha za Kikundi cha Wasanii wa filamu Tanzania wakionesha igizo kuhusu uhamasishaji kwa jamii juu ya umuhimu wa kuchangia damu, tukio limefanyika kitaifa jijini Mwanza katika viwanja vya Furahisha.
Mashine kubwa zenye gharama inayokadiriwa kuwa dola za kimarekani 600,000 (laki sita) kila moja ambayo ni sawa fedha za Kitanzania bilioni 1.4, zilizozinduliwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu katika Maadhimisho ya Siku ya Wachangia Damu Duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Mwanza, viwanja vya Furahisha.
SERIKALI KUONGEZA IDADI VITUO VYA
UCHANGIAJI DAMU SALAMA
Na.WAMJW - Mwanza
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetenga Sh. bilioni tano katika mwaka wa fedha 2019/20 zitakazotumika kujenga vituo vidogo vya uchangiaji damu salama katika mikoa 12 nchini.
Hayo yameelezwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alipozungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Wachangia Damu Duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Mwanza, viwanja vya Furahisha.
Sambamba na hilo, Waziri Ummy amezindua mashine mpya ‘full automation’ za kupima maambukizi katika damu na za kupima makundi ya damu ambapo mashine 24 zimesimikwa kwenye vituo vya kanda sita ikiwamo Dar es Salaam, Mwanza, Tabora, Kilimanjaro, Mtwara na Mbeya.
Amesema kila kituo kimesimikwa mashine nne ikiwa mbili ni za kupima magonjwa yanayoambukizwa kupitia damu na mbili ni za kupima makundi ya damu.
Amesema hatua hiyo imelenga kuimarisha huduma ya uchangiaji damu salama pamoja na kuwezesha kusogeza karibu zaidi huduma za kuongezewa damu salama wagonjwa wenye uhitaji.
“Hadi sasa kuna vituo vidogo vya damu salama nane ambavyo vimeanzishwa Mkoa wa Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Iringa, Kigoma, Shinyanga, Simiyu, Tabora na Mara.
“Katika mwaka wa fedha 2019/20, tunategemea kujenga vituo vya damu salama katika mikoa 12, imetengwa Sh. bilioni tano, hivi karibuni ujenzi utaanza,” amesema.
Amesema kadri huduma za matibabu ya kibingwa zinavyoboreshwa ikiwamo ya moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, upandikizaji figo na upasuaji mwengine Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Hospitali ya Taifa Muhimbili na Mloganzila, zimepanua wigo wa mahitaji ya upatikanaji wa damu salama.
“Jitihada zinafanyika ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa damu salama, kauli mbiu ya mwaka huu inasema ‘Damu Salama kwa Wote’ ni kwa sababu mkutano mkuu wa WHO mwaka huu ulihusu afya kwa wote.
“Tunataka kumfikia kila mtanzania mwenye mahitaji ya damu salama popote alipo tuhakikishe anapata damu salama bila kikwazo chochote. WHO inakadiria katika kila idadi ya watu 1000 zipatikane chupa 10 za damu, Watanzania tunakadiriwa tupo milioni 55 tunapaswa kupata asilimia moja ya idadi hiyo, hivyo chupa 550,000 zinahitajika kila mwaka kutosheleza mahitaji,” amesema.
Akitoa ulinganisho amesema mwaka 2016 zilikusanywa chupa 196,000, mwaka 2017 chupa 233,000 na 2018 idadi imeongezeka kufikia chupa 307,000.
“Kumekuwa na ongezeko la ukusanyaji damu, katika chupa 10 zinazohitajika kupatikana angalau tunapata chupa sita, hivyo nawasihi watanzania wote kujenga utamaduni wa kuchangia damu mara kwa mara ili tuweze kupata inayotosheleza,” amesema.
Aidha, amewataka waganga wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha wanatekeleza agizo alilowapa la kuandaa kambi za wazi kwa ajili ya uchangiaji damu angalau mara tatu kila mwaka na watenge fedha katika bajeti zao kuwezesha ukusanyaji damu salama.
Awali akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Steven Lalika amesema walipewa lengo la kukusanya chupa 2000, katika wiki ya uhamasishaji wamefanikiwa kukusanya chupa 3705 kufikia Juni 13 na kwamba lengo la mkoa walikusudia kukusanya chupa 4000.
MWISHO
0 on: "SERIKALI KUONGEZA IDADI VITUO VYA UCHANGIAJI DAMU SALAMA"