Na.Catherine Sungura,Buchosa
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameahidi kuwapatia mashine ya x-ray ya kisasa ya kidigitali kituo cha afya kome kilichopo halmashauri ya Buchosha wilayani Sengerema.
Waziri Ummy ametoa ahadi hiyo akiwa kwenye ziara ya kikazi kisiwani hapo ya kujionea hali ya utoaji huduma za afya.
“Ninawaahidi wananchi nitaleta x-ray mashine ya kidigitali kwenye kituoa hichi cha afya ili msivuke maji kwenda kupata huduma za vipimo wilayani sengerema".Alisema Waziri Ummy
Aidha, alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Buchosha Crispian Luanda pamoja na Mganga Mkuu wake Dkt. Ernest Chacha kwa jitihada kubwa wanazofanya za kuboresha huduma za afya kwenye halmashauri hiyo"Nimefurahi kumuona daktari wa upasuaji kwenye kituo hiki na hongereni kwa kumpatia mafunzo ya mwaka mzima kwenye eneo hili,sasa mnatakiwa kuweka vifaa na huduma za mtoto njiti ili kusiwepo na vifo vya watoto hao endapo itatokea".
Hata hivyo Waziri Ummy aliwataka akina mama wa kisiwa hicho kuhudhuria kliniki mara nne mara wanapokuwa wajawazito ili kuepukana na vifo vya wajawazito na watoto pamoja na kuepusha kuzaa watoto walemavu.
"Tumeanzisha huduma za upasuaji kwenye kitua hiki cha afya tunataka mama mjamzito wa Kome akipata tatizo la mtoto kukaa vibaya tumboni au mama akipata kifaa cha mimba asaidiwe hapa hapa"Alisisitiza Waziri Ummy.
Naye Mbunge wa Buchosa Dkt. Charles Tizeba ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kuwajengea jengo la upasuaji pamoja na vifaa hivyo kuondoa tatizo kubwa la upasuaji lililokuwa linawakabili wananchi wa Kome na kuomba wizara kuwapatia vifaa vya vipimo katika vituo vya huduma za afya kwenye halmashauri hiyo kwani wananchi wameanzisha ujenzi wa zahanati 30 kwa nguvu zao hivyo wakikamilisha miundombinu huduma za afya zitakuwa zimeboreshwa kwenye jimbo lake.
Kisiwa cha Kome kimeongeza idadi ya akina mama wanaojifungulia kwenye vituo vya huduma za afya kutoka asilimia 42 mwaka 2015 kati ya akina mama 100 hadi kufikia asilimia 80 kwa mwaka ambapo wastani wa akina mama 50 wanajifungua kwa mwezi.
-Mwisho-