Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Alhamisi, 13 Desemba 2018

WAZIRI UMMY MWALIMU AHUDHURIA MKUTANO UNAOJADILI AFYA YA MAMA NA MTOTO NCHINI INDIA



Picha mbalimbali zikimuonesha Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akishiriki mkutano maalum wa mawaziri wa afya kuhusu afya ya mama na mtoto unaofanyika jijini New Delhi nchini India ulioanza tarehe 12-14 Desemba 2018. Mkutano huo unajadili afya ya mama na mtoto "4th Partnership for Maternal, Newborn and Child Health 2018".

SERIKALI YATOA RAI KWA WANANCHI KUJITOKEZA KUPATA DAWAKINGA YA MATENDE NA MABUSHA

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Faustine Ndugulile akisisitiza jambo mbele ya waandishi wa Habari (Hawapo kwenye picha) wakati akitoa tamko kuhusu kampeni ya kumeza dawa kingatiba ya magonjwa ya minyoo ya Tumbo, Usubi, Trakoma na Matende na Mabusha katika mikoa saba hapa nchini.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Faustine Ndugulile akitoa tamko kuhusu kampeni ya kumeza dawa kingatiba ya magonjwa ya minyoo ya Tumbo, Usubi, Trakoma na Matende na Mabusha katika mikoa saba hapa nchini, pembeni yake ni mratibu wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Dkt. Upendo Mungila

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Faustine Ndugulile akitoa tamko kuhusu kampeni ya kumeza dawa kingatiba ya magonjwa ya minyoo ya Tumbo, Usubi, Trakoma na Matende na Mabusha katika mikoa saba hapa nchini, pembeni yake ni mratibu wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Dkt. Upendo Mungila


TAMKO LA MHE. DKT. FAUSTINE NDUGULILE (MB.) NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KUHUSU KAMPENI YA KUMEZESHA DAWA  KINGATIBA YA MAGONJWA YA MINYOO YA TUMBO, USUBI, TRAKOMA, MATENDE NA MABUSHA KATIKA MIKOA SABA (7) HAPA NCHINI. 

Ndugu Wananchi
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ikishirikiana na wadau itafanya kampeni ya kugawa dawa za Kingatiba ya magonjwa ya minyoo ya tumbo, usubi, trakoma, matende na mabusha katika mikoa saba (7) hapa nchini, ambayo ni Dar es Salaam katika Manispaa zote, Iringa wilaya ya Mufindi DC, Mtwara wilaya ya Masasi, Pwani wilaya ya Kibaha na Mafia, Rukwa wilaya ya Kalambo, Songwe wilaya ya Songwe na Tanga wilaya ya Mkinga na Korogwe. 
Lengo kuu la kufanya kampeni ni kutibu na kuzuia maambukizi ya magonjwa ya minyoo ya tumbo, Usubi, Trakoma, Matende na mabusha au Ngirimaji. Aidha, dawa hizi au kingatiba hii, zitasaidia kupungua kwa ulemavu na adha za magonjwa haya. Kuna faida kubwa kwa wananchi wakishiriki katika zoezi hili la umezaji kinga tiba hii. Faida hizo ni:
Kukinga upungufu wa damu.
Kumuepusha mtu kupata upofu.
Kupunguza maambukizi kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwingine.
Kuua vimelea vya Magonjwa haya.
Kukinga na kupunguza maumivu na madhara yanayosababishwa na Magonjwa haya.
Kupungua kwa Magonjwa ya ngozi.
Kuongeza virutubisho bora mwilini.
Kuboresha nguvukazi katika jamii.
Kuwezesha watoto kukua vizuri.
Kuongeza uelewa wa watoto wawapo shuleni.

Ugonjwa wa Minyoo ya tumbo huathiri zaidi jamii maskini na husababishwa na mtu kula mayai ya minyoo kutoka katika udongo au minyoo hii kupenya kwenye ngozi. Aidha, Kuna minyoo ya aina tatu ambayo husababisha ugonjwa huu,minyoo mviringo,minyoo mijeledi  na minyoo ya safura. Pamoja na kutoa dawa za kutibu ugonjwa huu lakini pia jambo la msingi ni vyema wananchi mkaweka maeneo yanu katika hali ya usafi na kula vyakula vilivyopikwa vizuri na kuiva. 
Ugonjwa wa Usubi husababishwa na minyoo inayoitwa Onchocerca volvulus, huenezwa na inzi weusi wadogo wanaokaa kandokando ya mito yenye maji yaendayo kasi. Athali za ugonjwa huu ni ngozi kuwasha,  ngozi kuwa na mabakamabaka kama ya chui, ngozi kuwa na muonekano wa kenge, pia uono hafifu na upofu. 

Trakoma au vikope ni ugonjwa sugu unaoshambulia macho na kusababisha kope kupinda na kugusa kioo cha jicho ambapo husababisha makovu juu ya kioo cha jicho na hupunguza uwezo wa kuona na kusababisha upofu usiotibika. Ugonjwa huu husababishwa na bakteria aina ya Chlamydia trachomatis. 
Juhudi kubwa za kutokomeza ugonjwa wa Trakoma au Vikope zimefanyika na kuweza kupunguza kiwango cha maambukizi. Kati ya Wilaya 71 zilizokuwa na uambukizo, Wilaya 63 sawa na Asilimia Themanini na Tisa (89%) zimeweza kufikia kiwango cha chini  ya asilimia 5% ambayo inaruhusu kusimamisha zoezi la kingatiba ya Trakoma  katika ngazi ya Jamii. Katika mwaka huu wa 2018 ni Wilaya 8 tu ndio zinaendelea na zoezi la  Kingatiba ya  ugonjwa wa Trakoma kwa kutumia dawa aina ya Zithromax. 
Ugonjwa wa Matende na Mabusha husababishwa  na minyoo midogo midogo ambayo huenezwa na mbu wa aina zote kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. 
Dalili za ugonjwa huu ni homa kali ambayo huchukua siku 3 – na huambatana na baridi kali, Kichefuchefu, kutapika, kuvimba kwa mitoki, kubabuka ngozi, kuvimba kwa miguu, mikono, matiti au sehemu za siri kwa jinsia zote.
Mafanikio katika kutokomeza ugonjwa wa Matende na mabusha yameanza kuonekana, kati ya Wilaya 120 ambazo zilikuwa na uambukizo, Wilaya 98 ambazo ni sawa na asilimia sabini na Saba (77) zimeweza kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo na hivyo kufikia kiwango cha kusimamisha ugawaji wa kingatiba kwa jamii katika Wilaya hizo. 

Hii ina maana kwamba kwa mwaka huu 2018 ni wilaya 28 tu ndizo zitakuwa na zoezi la umezeji kingatiba kwa ajili ya kukinga na kutibu ugonjwa wa Matende na mabusha katika ngazi ya jamii. Magonjwa haya yasipopatiwa tiba haraka mtu anaweza kupata madhara kama:-
Maumivu ya muda mrefu na wakati mwingine ulemavu mkubwa.
Umaskini na kudumaza uchumi wa kaya na hatimaye Taifa.
Kudhoofisha ukuaji hasa kwa watoto wenye umri mdogo kimwili na kiakili.
Utapia mlo kwa watoto
Utumbo kujisokota 
Hatimae kifo kama mgonjwa hakutibiwa.

Ndugu Wananchi
Pamoja na kwamba ugawaji wa dawa utafanyika katika mikoa saba (7) hapa nchini, napenda nijikite sana katika kuelezea umezaji wa dawa katika mkoa wa Dar es Salaam kwa mwaka huu wa 2018. Hii siyo mara ya kwanza kwa mkoa huu kufanya zoezi la umezaji wa dawa Kingatiba ya minyoo ya tumbo, matende na mabusha. Zoezi hili kwa mkoa wa Dar es Salaam lilianza mwaka 2013 na limekuwa likitekezwa kila mwaka. Katika mwaka wa kwanza watu wapatao 3,028,828 walijitokeza na kupatiwa kingatiba hii. Idadi hii imekuwa ikiongezeka kila mwaka zoezi linapotekelezwa na kwa mwaka jana 2017, watu waliojitokeza kupatiwa kingatiba walikuwa 4,914,351 ambayo ni sawa na asilimia 86 (86%) ya lengo lililotarajiwa.  
Ingawa kiwango cha umezaji wa dawa hizi kwa jamii kimeendelea kuwa juu, lakini idadi ya watu wanaojitokeza kwenye zoezi hili bado haijaridhisha sana kutuwezesha kutangaza kwamba tutatokomeza magonjwa haya katika mkoa wa Dar es Salaam, bado maambukizi yapo juu ya kiwango cha asilimia mbili (2%). Lengo la mwaka huu ni kugawa dawa watu wapatao 5,376,207 katika Manispaa zote tano (5) za Mkoa wa Dar es Salaam. 

Kama wizara tumeweza kuwezesha rasilimali za dawa na fedha za utekekelezaji wa kampeni hi muhimu. Aidha tumeweza kusaidiana na wenzetu wa TAMISEMI kufanya uhamasishaji kwa ngazi mbalimbali kwa viongozi wa jamii, kata na mitaa. Kampeni hii itawapa fursa wanajamii kupunguza uambukizo wa magonjwa haya na hatimaye kuwa jamii kuwa huru na vimelea vya magonjwa haya kwa vizazi vijavyo. 
Kampeni hii kwa mwaka huu, itahusisha wakazi wote wa Mkoa wa Dar es Salaam na wageni waliopo katika Jiji hili wenye umri wa kuanzia miaka mitano (5) na kuendelea. Dawa zitakazotolewa ni aina Albendazole kidonge kimoja (kitatafunwa) na Ivermectin (Mectizan)  ambayo itatolewa kulingana kimo chake . 
Ndugu Wananchi
Napenda kuwataarifu kuwa kampeni hii itaendeshwa kuanzia tarehe 15  hadi 20 mwezi Disemba, 2018 kwa watu wenye umri uliotajwa hapo juu. Napenda kusisitiza kuwa viongozi wa ngazi zote ikiwa ni pamoja na ngazi ya jamii wanawajibika kutoa taarifa hii na kuhamasisha wananchi wote washiriki kikamilifu katika kampeni. Aidha, katika kufanikisha zoezi hili nawasishi wananchi na viongoziu wote kutumia njia mbalimbali za mawasiliano kama vile vyombo vya habari, kuhamasisha wananchi makanisani na misikitini  kujitokeza kushiriki zoezi hili.
Aidha, wanachi mtambue kuwa vituo vya kutolea huduma hizi vimesogezwa karibu jamii ili kurahisisha upatikanaji wa huduma. Ambapo Jumla ya vituo mia tisa kumi na tano (915) ambavyo ni pamoja na Zahanati, Vituo vya afya, Hospitali, stendi za mabasi, masoko, ofisi za serikali za mitaa, ofisi za taasisi mbalimbali pamoja na kambi za Majeshi yetu na Magereza vitatoa huduma hiin a takribani wagawa dawa Elfu moja mia nane thelathini (1,830) waliopatiwa mafunzo watahusika katika kutoa huduma hiyo kwenye vituo Mwisho napenda kutoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam na wa mikoa mingine ambayo zoezi hili litafanyika  kushiriki kikamilifu katika umezaji dawa hizi. Zoezi hili ni muhimu kwani magonjwa haya yanaathiri sana jamii yetu. Kwa viongozi wenzangu na wanahabari tunaomba muendelee kuelimisha umma kuhusu magonjwa haya na umuhimu wa umezaji wa kingatiba hii. 

LINDA, OKOA MAISHA, ZUIA ULEMAVU JITOKEZE KUMEZA DAWA-KINGATIBA’


Jumapili, 9 Desemba 2018

HOSPITALI MPYA 67 ZA WILAYA KUJENGWA NCHINI

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile (wakati kati) akishuhudia makabidhiano ya mabenchi yakukalia, wakwanza kulia ni Meneja wa NMB kanda ya Dar es salaam Bw. Badru Idd  akimpa mkono Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. John Rwegasha katika tukio la makabidhiano ya mabenchi yakukalia 52 lililofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es salaam.

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile akiteta jambo na Meneja wa NMB kanda ya Dar es salaam Bw. Badru Idd katika tukio la makabidhiano ya mabenchi yakukalia 52 yenye thamani ya Mikioni 10, lililofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es salaam.

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile akikagua mabenchi hayo baada ya makabidhiano leo, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es salaam.

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile akimuaga Meneja wa NMB kanda ya Dar es salaam Bw. Badru Idd  baada ya tukio la makabidhiano ya mabenchi yakukalia 52 yenye thamani ya shilingi Milion 10, lililofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es salaam.

Jengo la mahala pakupimzikia la Kitengo cha Dharura, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili


HOSPITALI MPYA 67 ZA WILAYA KUJENGWA NCHINI

Na WAMJW - Dar es salaam.

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee ma Watoto inatarajia kujenga Hospitali za Wilaya 67, ikiwa ni mkakati na jitihada za Serikali kuboresha Huduma za Afya na kupunguza adha kwa wananchi kupata huduma za afya.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile leo wakati akipokea viti kwaajili yakupumzikia hospitalini, kutoka benki ya NMB katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es salaam.

Dkt. Ndugulile amesema kuwa kwa sasa zipo Hospitali za Wilaya 80, hivyo Serikali imeamua kuongeza hospitali za Wilaya takribani 67 ikiwa ni mkakati wa kuboresha huduma za Afya hususani huduma za mama na mtoto.

"Mwaka huu tunajenga Hospitali za Rufaa, Mikoa ambayo haina, tunajenga Hospitali za Wilaya 67, na tunahospitali kama 80 za Wilaya," alisema Dkt. Ndugulile.

Dkt. Ndugulile aliendelea kusema kuwa Serikali imeboresha vituo vya Afya takribani 200 ili kusaidia kutoa huduma za upasuaji, hivyo kusaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa kupata huduma katika Hospitali za Wilaya na za Rufaa za Mkoa.

Sambamba na hayo Dkt. Ndugulile ameishukuru Benki ya NMB kwa kutenga Asilimia 1 ya mapato yanayotoka kwenye faida kuelekeza kwenye Jamii ya Watanzania hususani katika huduma za Afya.

"Niwashukuru sana NMB bank, kwa kutenga mapato yenu na faida yenu kuielekeza kwenye jamii, na nimefurahi zaidi, kusikia kwamba mmewekeza zaidi katika huduma za Jamii, Sisi kama Serikali tunawapongeza" alisema Dkt Ndugulile

Dkt. Ndugulile aliendelea kusema kuwa vitawasaidia sana wagonjwa ambao wanatoka sehemu mbali mbali ya nchi kupata maeneo mazuri yakuweza kukaa wakati wagonjwa wao wakipata huduma za Afya, hivyo niwaombe sana msiishie hapo kwani bado kuna maeneo mengi yanahitaji msaada.

Nae Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam Bw. Badru Idd amesema kuwa benki ya NMB huwa inalipa fadhira kwa Jamii baada ya kupata faida, kwa kuleta maendeleo, ikiwemo kujenga miundombinu, na kuboresha huduma za Jamii ili watanzania waweze kunufaika na kutoka Benki yao ya NMB.

"Kwa mujibu wa taratibu za Benki ya NMB huwa tunatoa Asilimia 1% kwenye pato ambalo tumepata kwa mwaka huo, mathalani mwaka Jana tumeingiza milioni 94, hivyo tunatoa Asilimia 1% ya Milioni 94 na kuirudisha kwa Jamii" alisema Bw. Badru Idd.

Bw. Badru Idd aliendelea kusema kuwa hiyo Asilimia 1% ipo kwenye mafungu makubwa 3, kundi la kwanza NMB inapenda sana kutoa huduma kwenye sekta ya Afya, kundi la pili ni Sekta ya Elimu na kundi la tatu ni huduma kwenye majanga yanayotokea.

Mwisho.

Ijumaa, 7 Desemba 2018

WAUGUZI WANAOVUNJA MAADILI YA KAZI KUKIONA CHAMOTO

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akisisitiza jambo mbele ya wananchi wa Nanyumbu (hawapo kwenye picha), wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya utoaji wa huduma za Afya na uhamasishaji kwa wananchi kujiunga na Bima ya Afya Mkoa wa Mtwara.
Waziri wa Afy, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akisoma cheti cha mtoto aliyefikishwa na baba yake Hospitali ya Wilaya Nanyumbu ili kupata huduma za Afya.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akiwasalimia wanafunzi wa shule ya awali pindi tu alipowasili kwaajili ya mkutano wa hadhara na wananchi wa Nanyumbu ili kusikiliza kero zao na kuwaeleza Maendeleo ya Sekta ya Afya kwaujumla.

Wananchi wa Nanyumbu wakiongozwa na Wazee waliojitokeza kumsikiliza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu pindi alipokuwa katika ziara yake ya kukagua hali ya utoaji wa huduma za Afya na uhamasishaji kwa wananchi kujiunga na Bima ya Afya Mkoa wa Mtwara.

Na WAMJW - Nanyumbu, Mtwara

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu ametoa onyo Kali kwa Wauguzi wote kwenye vituo vya  kutolea huduma za afya nchini wanaovunja maadili na miiko ya kazi za uuguzi ikiwemo matumizi ya lugha chafu kwa wagonjwa na wanaowapiga akina mama wajawazito wakati wakijifungua.

Ameyasema hayo  wakati alipotembelea Hospitali ya Wilaya Nanyumbu, akiwa katika ziara yake Mkoani Mtwara ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya na uhamasishaji kwa wananchi juu ya umuhimu wa kujiunga na Bima ya Afya hasa katika msimu huu wa Biashara ya Korosho.

Waziri Ummy alisema kuwa Serikali kupitia Baraza la Uuguzi litawafutia usajili Muuguzi yeyote atakayegundulika ametenda kosa la kumpiga mama mjamzito au kumtolea lugha chafu wakati wa kujifungua.

"Tunataka kumjua huyo, ambae ni hodari sana wakupiga wanawake wajawazito, makofi wakati wakujifungua, kwa kweli huyo ni wa kumfukuza kazi, Mimi mkiniletea namfutia Leseni yake kabisa, hafanyi kazi Serikalini, hafanyi kazi Sekta Binafsi" alisema Waziri Ummy.

Pia, Waziri Ummy alitoa Maagizo kwa Mganga Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Wilaya ya Nanyumbu Mhe.Hamis Dambaya kuhakikisha  Wauguzi na Watumishi wote wanavaa vitambulisho vya kazi wakati wote wakiwa eneo la kazi ili wananchi wanaokwenda kupata huduma za Afya waweze kuwatambua majina yao.

"Tumewaambia wavae vitambulisho, ili mtusaidie kutaja jina la Wauguzi wanaovunja maadili ya kazi zao, hapa naomba nisiwahukumu wote, Mganga Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi mpo hapa, nikirudi tena nisisikie kuna Muuguzi anapiga makofi wajawazito wanaokuja kujifungua" alisema Waziri Ummy.

Kwa upande mwingine Waziri Ummy amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya italeta mashine mpya ya kisasa ya digitali ya X-Ray ndani ya miezi mitatu itayosaidia wananchi wa Nanyumbu hasa kutokana na Wilaya hiyo kuwa katika Bara bara kuu ya kutoka Masasi hadi Songea.

Aidha, Waziri Ummy ametoa Rai kwa wananchi wa Nanyumbu kuhakikisha kabla ya kufika Disemba 31 mwaka huu, kaya zote katika eneo hilo lazima liwe limejenga na kutumia choo bora ili kupunguza magonjwa ya Bakteria yanayoigharimu Serikali pesa nyingi katika matibabu na Dawa.

"Ndugu zangu nendeni pale Hospitali, katika kila Wagonjwa 100, Wagonjwa 60 wana magonjwa ya kuhara,magonjwa ya tumbo, magonjwa yanayohusiana na kiwango duni cha usafi, nimekuwa nikiimba wimbo huu tangu nikiwa Waziri wa Afya, na hapa tulipofikia ni agizo la Waziri Mkuu pindi alipokutana na maafisa Afya wa Halmashauri na Mkoa jijini Dodoma" alisema Waziri Ummy

Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa akiwa kama Waziri wa Afya kazi kubwa aliyonayo ni kuhakikisha anawakinga watu wasiumwe na pale wanapoumwa waweze kupata Huduma Bora za Afya, lazima niwe mkali kwenye kinga, mimi ni Waziri wa Afya sio Waziri wa Wagonjwa" alisema Waziri Ummy.

Mwisho.

Alhamisi, 6 Desemba 2018

WAZIRI UMMY AAGIZA AFISA AFYA WA WILAYA ACHUNGUZWE KWA TUHUMA YA RUSHWA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akisisitiza jambo kwenye kikao.  
Waziri wa Afya, Mhe.Ummy Mwalimu akikagua wodi ya akina mama na watoto.

Na WAMJW-NEWALA, MTWARA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo, Kumchunguza Afisa Afya wa Wilaya hiyo maarufu kwa jina la Mama Flora kwa tuhuma ya rushwa aliyochukua kutoka kwa Bw.Shaib Mussa kama adhabu  ya kutupa taka  hovyo.

Hayo yamefuatia baada ya Mwananchi aliyejitambulisha kwa jina na Shaibu Musa kutoa malalamiko yake mbele ya Mhe.Waziri ya kilipishwa  shilingi elfu 50,000 na Bibi Afya huyo  mwaka Jana.

Waziri Ummy alisema kuwa Watumishi wa Serikali hasa wa Sekta ya Afya ni lazima wajiepushe na vitendo vya Rushwa na kuacha tamaa zinazopelekea kuminywa kwa haki kwa baadhi Wananchi wanaotaka kupata huduma.

"Namtafuta mmoja ili nimtolee mfano kwa Tanzania nzima, bahati nzuri Mimi ni Mwanasheria, Kosa LA jinai halina muda, hata kama ni 2017, tunataka huyu mtu afuatiliwe, achunguzwe kama kweli shilingi 50,000 iliingizwa kwenye Halmashauri au haijaingia, tunataka Mazingira masafi lakini ile hela iende Serikalini" alisema Waziri Ummy.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga amesema kuwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeanza rasmi kampeni ya uandikishaji ya kijiji kwa kijiji katika Mikoa ya Mtwara na Lindi ili kuwawezesha wananchi hao kuwa kwenye utaratibu mzuri wa kupata huduma za matibabu.

Bw. Bernard Konga  aliendelea kusema kuwa, Wananchi wamekuwa wakiingia katika umasikini mkubwa kwa kulazimika kuuza mali za familia kwa lengo la kupata fedha za kugharamia huduma za matibabu.

"Nikuhakikishie Mheshimiwa Waziri na wananchi wote walioko hapa, timu yangu inaanza rasmi kampeni ya kijiji kwa kijini kuanzia wiki ijayo kwa lengo la kumfikia kila mkulima aliyeko katika Mkoa wa Mtwara na Lindi ili wananchi hawa wawe kwenye mfumo bora wa kupata huduma za matibabu wakati wowote, alisema Bw. Konga.

Konga  aliendelea kusema kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wote wako kwenye sekta ya kilimo hususan maeneo ya vijijini na kwa kutambua umuhimu wa kulitunza kiafya kundi hili, Mfuko ulianzisha mpango maalum unaojulikana kwa jina la Ushirika Afya unaowawezesha kujiunga na huduma za NHIF kwa gharama nafuu.

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto yupo Mkoani Mtwara  kwa ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya Pamoja na  uhamasishaji kwa Wananchi kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) na Leo hii yupo Wilayani ya Newala.

Mwisho

OCEAN ROAD KUTUMIA MIONZI YA NYUKLIA KUCHUNGUZA AFYA YA MOYO WAGONJWA WA SARATANI

Mteknolojia Tiba ya Mionzi (Nuclear Medicine) wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk. Faraji Sabaya akimuandaa mgonjwa kwa ajili ya uchunguzi huo.

Daktari Bingwa wa Uchunguzi na Tiba ya magonjwa mbalimbali kwa kutumia Mionzi ya Nyuklia wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Tausi Maftah akiwafafanulia jambo waandishi wa habari (hawapo pichani)

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dk. Julius Mwaiselage akifafanua jambo kuhusu huduma hiyo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani)

Na Mwandishi wetu - Dar Es Salaam.

TAASISI ya Saratani Ocean Road (ORCI) imezidi kuimarisha huduma zake za uchunguzi na tiba kwa wagonjwa wa saratani ambapo awamu hii imeanzisha huduma mpya ya uchunguzi wa afya ya moyo kwa kutumia mionzi ya nyuklia.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk. Julius Mwaiselage amesema huduma hiyo imelenga zaidi kutolewa kwa wagonjwa wa saratani nchini.

Amesema kabla ya kuanzisha huduma hiyo wagonjwa wengi walilazimika kupatiwa rufaa kwenda kuifuata nje ya nchi.

“Serikali ilipoanzisha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ilitusaidia mno, tunashirikiana nao kwa ukaribu lakini kwa upande wa uchunguzi kwa kutumia mionzi bado tulikuwa tunawapa rufaa wagonjwa kwenda nje ya nchi,” amesema.

Ameongeza “Kwa mara ya kwanza nchini ORCI inaanzisha huduma ya uchunguzi wa afya ya moyo kwa kutumia mionzi ya nyuklia, inasaidia kujua afya ya moyo kwa ujumla na iwapo dawa tunazompatia mgonjwa zinamuathiri au la, ili kuboresha zaidi matibabu yake.

“Hivyo, tutatoa huduma hii lakini pia tutaendelea kushirikiana na wenzetu wa JKCI kufanya uchunguzi kwa tiba ya namna hii (ya mionzi),” amebainisha.

Dk. Mwaiselage amesema uchunguzi huo unafanyika kwa kutumia kipimo kiitwacho kitaalamu Myocardiac Perfusion Scan na kingine Multigated Acquisition Scan na mashine maalum ya mionzi iitwayo kitaalamu Gamma Camera.

Dk. Mwaiselage amesisitiza taasisi hiyo inazidi kuboresha huduma zake na kwamba hivi karibuni Rais John Magufuli atakwenda kuzindua rasmi mashine zingine mpya za uchunguzi zilizofungwa.

Awali  Daktari Bingwa wa Uchunguzi na Tiba ya Magonjwa mbalimbali kwa kutumia mionzi ya nyuklia (nuclear medicine physician) ORCI, Tausi Maftah amesema huduma hiyo itasaidia kuimarisha matibabu kwa wagonjwa hao

Naye, Mtaalamu wa Tiba hiyo, Profesa Raphael Giubbini kutoka Italia amesema huduma hiyo ni muhimu mno kwa wagonjwa wa saratani na ndiyo inayotumika katika nchi nchi mbalimbali hivi sasa hasa zile zilizoendelea.

 MWISHO

Jumatano, 5 Desemba 2018

TANZANIA YATAJWA KUWA MIONGONI MWA NCHI 30 ZINAZOONGOZA KUWA NA IDADI KUBWA YA MAAMBUKIZI YA KIFUA KIKUU.

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi akisisitiza jambo kwa wajumbe wa mkutano wa mwaka wa wadau wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma (hawapo pichani) katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Mipango Dodoma.

Meneja wa Mpango wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma nchini Dkt. Beatrice Mutayoba akiongea jambo kwenye mkutano wa mwaka wa wadau wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma 

Wajumbe wa mkutano wa mwaka wa wadau wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma wakiwa kwenye mkutano.

Wajumbe wa mkutano wa mwaka wa wadau wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma wakiwa kwenye mkutano.

Picha ya pamoja wajumbe wa mkutano wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma katika ukumbi wa Chuo cha Mipango Dodoma.

Na WAMJW - Dodoma.

Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 zenye kiwango kikubwa cha wagonjwa wa kifua kikuu duniani huku takwimu zikionesha kuwa kati ya watanzania laki moja, 269 wanaugua ugonjwa wa kifua kikuu.

Hiyo ni kauli ya Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi alipokuwa akifungua kikao cha mwaka cha cha wadau wa Mpango wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma kilichofanyika Jijini Dodoma katika Ukumbi Wa Chuo cha Mipango.

Licha ya kupiga hatua katika uboreshaji wa sekta ya afya ambapo Serikali imekuwa ikitoa huduma za matibabu bure kwa wagonjwa wa kifua kikuu, bado wananchi hawana elimu ya kutosha kutambua mapema dalili za ugonjwa huo.

Dkt. Subi anasema kuwa ugunduzi wa wagonjwa wa kifua kikuu ndani ya jamii upo chini huku asilimia 44 tu ya wagonjwa wa kifua kikuu hujitokeza kupatiwa matibabu huku asilimia 56 ya wagonjwa bado wapo mtaani wanaishi na kifua kikuu hivyo kuhatarisha kuongezeka kwa maambukizi mapya.

“Takwimu hizi si nzuri hivyo kuna haja ya kuongeza mkakati wa kuwagundua wagonjwa hao kwa wakati na kutoa elimu kwa wananchi namna ya  kutambua na kujinga na maambukizo ya ugonjwa huo hatari” amesema Dkt. Subi alipokuwa anazungumza na wataribu wa ugonjwa wa kifua kikuu, waganga wa mikoa, wilaya pamoja na wadau wa afya katika mkutano huo na kuwataka waganga wakuu wote  kuhakikisha dawa za kifua kikuu zinakuwepo katika vituo vyote vya afya kila wakati bila kupungua na njia pekee ya kutokomeza ugonjwa huo ni kuahakikisha wagonjwa wote wanagundulika na kupatiwa matibabu.

Hata hivyo Dkt. Subi amesema kuwa asilimia 40 ya vifo vya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi vilisababishwa na kifua kikuu, na hiyo inatokana na kupungua kwa kinga na kusababisha mgonjwa kupokea ugonjwa huo kwa haraka zaidi.

Awali akitoa taarifa yake, Meneja wa Mpango wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma nchini, Dkt. Beatrice Mutayoba amesema kuwa Serikali imeendelea kuboresha utoaji wa huduma za matibabu ya ugonjwa wa kifua kikuu nchini ambapo ugunduzi wa mgonjwa wa kifua kikuu huchukua muda mfupi tofauti na zamani.
“Serikali imenunua mashine za ugunduzi wa ugonjwa wa kifua kikuu za vina saba (Genexpert TB Test Mashines) 210 na kuzisambaza Tanzania nzima, mashine hizi zinaweza kumtambua mgonjwa wa kifua kikuu ndani ya masaa mawili tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo majibu hutoka baad ya siku tatu” alisema Dkt. Mutayoba.
Dkt Mutayoba anasema kuwa bado wanaendelea kusambaza mashine za hadubini kwa ajili ya ugunduzi na kuchuguza maendeleo ya wagonjwa ambao tayari wameanza matibabu.

Aidha Dkt. Mutayoba alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea na mpango wa kuwajengea uwezo wataalamu wa afya katika vituo afya ili waweze kuwagundua wagonjwa wa kifua kikuu mapema na kupatiwa matibabu.

Inakadiriwa kuwa watu 150,000 huugua ugonjwa wa kifua kikuu nchini kwa mwaka huku wagonjwa wagonjwa 66,000 sawa na asilimia 44 hujitokeza kupata huduma za matibabu hivyo kundi kubwa la wagonjwa bado wapo katika jamii hivyo kuhatarisha kutokea kwa maambukizi mapya.

Jumamosi, 1 Desemba 2018

MSD YATAKIWA KUKAMILISHA VIFAA VYOTE VINAVYOHITAJIKA KATIKA VITUO VYA AFYA VILIYOBORESHWA


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akiongea na watoto wa kike baada ya kutoa burudani ya ngonjera, wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya Mkoani Mwanza. 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akihutubia wanakijiji wa Koromije (hawapo kwenye picha) pindi alipofanya ziara yake ya kukagua hali ya utoaji wa huduma za Afya Mkoani Mwanza.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akimjulia hali mtoto aliyefika na mama yake katika Hospitali ya Wilaya ya Misungwi ili kupata huduma za Afya.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu (wakatikati) akikagua chumba cha kupima makohozi katika Hospitali ya Wilaya ya Misungwi.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akikagua hali ya Dawa katika stoo yakuhifadhia Dawa katika Hospitali ya Wilaya ya Misungwi.


Na WAMJW – Misungwi, MWANZA.

SERIKALI kupitia Wizara ya  Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeitaka Bohari Kuu  ya Dawa nchini  (MSD) kuhakikisha wanakamilisha kuleta vifaa vyote vinavyohitajika katika vituo vya Afya vinavyoboreshwa nchini kabla ya Januari 15, 2019 ili wananchi waweze kupata huduma.
 Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy wakati akiweka  jiwe la msingi la ukarabati wa kituo cha Afya Koromije na  kukagua hali ya utoaji Huduma za Afya katika Hospitali ya Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza.

"Haina maana ya kuwa na majengo makubwa na mazuri ya Vituo vya Afya kama hakuna vifaa vinavyohitajika, huku Wananchi wanaendelea kupata tabu", alisema Waziri Ummy.


Aidha, Waziri Ummy amewahasa Wazazi na Wananchi wote kwa ujumla kutodharau huduma za Chanjo, hivyo kuwahimiza Wananchi wote kuwapeleka katika vituo vyakutolea chanjo watoto waliofika umri wa kupata chanjo

“Kifafa, Kifaduro,Donda koo, Surua, hayapo siku hizi kwasababu ya Chanjo, kwahiyo tusije tukadharau chanjo, tuhakikishe kila mtoto mwenye umri wakupata chanjo , akapate chanjo” alisema Waziri Ummy Mwalimu.

Aidha, Waziri Ummy amewataka Wananchi wa Misungwi kuhakikisha wanasafisha mazingira,  na kutumia vyandarua vyenye dawa ili kuepuka kupata ugonjwa wa Malaria ambao umeendelea kuwa hatari nchini hasa kwa watoto wenye umri chini ya miaka 5 na Wanawake Wajawazito.

“Ugonjwa wa Malaria umepungua kutoka Asilimia 37 hadi Asilimia 27, kwahiyo niendelee kuwahimiza Wananchi wa Misungwi, kwanza  kuhakikisha wanafukia vidimbwi vya maji, kusafisha mazingira na kulala kwenye vyandarua vyenye dawa” Alisema Waziri Ummy.

Waziri Ummy aliendelea kusisitiza kuwa sio kila homa ni Malaria, hivyo kuwataka Wananchi kutotumia dawa bila kwenda kupata vipimo katika Kituo cha kutolea Huduma za Afya na kuthibitishwa kuwa una Malaria.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Rutha Thomas alisema kuwa Mkoa wa Mwanza unaishukuru Serikali kwa kuwapatia jumla ya shilingi Bilioni 2 zitakazotumika katika ujenzi wa Hospitali 2 za Hamashauri za Ilemela na Bushosa.

Mwisho.

Ijumaa, 30 Novemba 2018

DKT. MPOKI -"MADAKTARI TIMIZENI WAJIBU WENU"

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Utawala wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Beatrice Erasto wakati alipotembelea Taasisi hiyo kujionea hali ya utoaji wa huduma leo jijini Dar Es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Udhibiti wa Ubora wa Huduma kutoka Wizara ya Afya Dkt. Mohamed Mohamed.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya (katikati) akiongea na Mgonjwa wa Saratani (Jina halijafahamika) aliyelazwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road iliyoko Jijini Dar Es Salaam wakati alipofanya ziara kujionea hali ya utoaji wa huduma katika Taasisi hiyo. Kushoto ni Kaimu Meneja wa huduma za tiba Dkt. Sadik Siu na kulia ni Mkurugenzi wa Udhibiti wa Ubora wa Huduma kutoka Wizara ya Afya Dkt. Mohamed Mohamed.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya akiongea na wananchi waliofika kupata huduma za uchunguzi na matibabu katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road wakati alipotembelea Taasisi hiyo leo kujionea hali ya utoaji huduma.


Na.WAMJW, Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya amewataka Madaktari wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road   kutimiza wajibu wao katika kuwahudumia wagonjwa  wanaofika hospitalini hapo kila siku  na kumuagiza Mkurugenzi wa Huduma za  Uhakiki na Ubora kutoka Wizarani kwake kufuatilia.

Dkt.Mpoki ametoa agizo hilo alipotembelea taasisi hiyo ili kujionea hali ya utoaji huduma pamoja na kusikiliza wagonjwa wanaofika kupata huduma kwenye taasisi hiyo kutokana na kulalamikiwa kwa baadhi madaktari na wauguzi “Taasisi hii ni ya faraja lazima mtengeneza mazingira mazuri yakuwahudumia wagonjwa,kwani ndugu wanafuatilia hali za wagonjwa wao hivyo jamii inapolalamika tusiseme moja kwa moja ni waongo bali tushughulikie malalamiko yao ,kama huna jibu muelekeze kwa mtu ambaye anaweza kumpa jibu ili aweze kupata faraja”.Alisisitiza Dkt.Mpoki.

Aidha, aliwataka watumishi wa taasisi hiyo kuvaa vitambulisho ambavyo vinaweka wazi utambulisho wao ili ndugu na wagonjwa waweze kuwatambua na kutaja ni nani ambaye hajatimiza wajibu wake ipasavyo.

“watakaoshindwa kwenda nasi tutawapeleka kwingine,hatutaki maumivu yawe sehemu ya uzoefu wa wagonjwa wanaolazwa Ocean Road,nyinyi kazi yenu ni kuwahudumia wagonjwa”.

Hata hivyo aliwataka madaktari wabobezi (Mabingwa) kutimiza wajibu wao na sio kuwaachia jukumu la kuwahudumia wagonjwa madaktari waliopo mafunzo kwa vitendo”kuanzia sasa tukigundua mgonjwa ameachiwa daktari wa mafunzo kwa vitendo tutawaondoa wasifanye mazoezi hapa lazima tuishi kwa kutii na kufuata miiko ya taaluma zetu”alisema dkt.Mpoki

Aliagiza kufanyika mikutano ya ndani mara kwa mara ya kufuatilia utendaji kazi wa taasisi  na kujibu malalamiko yanayotolewa kwenye mitandao ya kijamii pamoja na masanduku ya maoni ili kupata mrejesho kutoka kwa wananchi ili kuboresha huduma zinazotolewa kwenye taasisi.

Kuhusu adha ya umbali wa kufuata huduma kwenye taasisi hiyo Dkt. Mpoki aliwathibitishia wagonjwa na ndugu waliopo hospitalini hapo kuwa Serikali kupitia wizara ya afya iko mbioni kupeleka huduma za saratani kanda ya kusini mara tu itakapokamilika hospitali ya Rufaa ya kanda,pia huduma kama hizo zipo mbioni kupelekwa kwenye hospitali ya rufaa ya Tabora pamoja na hospitali maalum ya Benjamin Mkapa iliyopo jijini Dodoma kwani ni wajibu wao kuhakikisha huduma hizo karibu na wananchi.

-Mwisho-

ASILIMIA 85 YA WANAWAKE MKOANI MARA WANAJIFUNGUA KATIKA VITUO VYA AFYA.

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akisikiliza maoni ya mmoja kati ya wagonjwa waliofika kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akihoji juu ya gharama za huduma za Afya zinazotolewa katika Hospitali ya Mkoa wa Mara, pindi alipofanya ziara ya kukagua ubora wa huduma na miundombinu katika Hospitali hiyo.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akisisitiza jambo mbele ya Watumishi wa sekta ya Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara(hawapo kwenye picha)
Watumishi wa Kada mbali mbali za Afya wakimsikiliza mgani rasmi Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu (hayupo kwenye picha) wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya na uboreshaji wa miundombinu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara.


Na WAMJW - MARA.

Asilimia 85 ya Wanawake Mkoani Mara wanajifungua kwenye vituo vya Afya, hali iliyosaidia kupunguza idadi kubwa ya  vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu wakati alipotembelea Hospitali ya Mkoa wa Mara kukagua hali ya utoaji Huduma.

"Mko Asilimia 85, kitaifa tupo Asilimia 51, kwahiyo niwapongeze kwa hilo, lengo letu ilikuwa ifikapo 2020 tunataka angalau Asilimia 80 ya wanawake wajawazito wajifungulie kwenye vituo vya Afya" Alisema Waziri Ummy.

Pia Waziri Ummy ameitaka Mikoa mingine nchini kuiga jitihada zinazofanywa na mkoa wa Mara za kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa kuhakikisha wanawake wajawazito wanajifungulia katika vituo vya kutolea huduma za Afya.

"Sitaielewa mikoa mingine kwa kushindwa kuhamasisha na kuweka Mazingira mazuri kwa wanawake kwenda kujifungulia katika vituo vya kutoa huduma za Afya" alisema Waziri Ummy

Hata hivyo Waziri Ummy Mwalimu amemwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara kuhamasisha jamii hususan wanawake katika maeneo mbali mbali kuhudhuria kliniki angalau Mara 4 katika kipindi cha ujauzito.

"Wanawake ambao wanahudhuria Kliniki angalau mara 4 ni Asilimia 45 hivyo hamjafanya vizuri  kwasababu kitaifa ni Asilimia 51, mjenge tabia ya kuwahamasisha wanawake kuhudhuria kliniki angalau Mara 4, kama watoa huduma za Afya wanavyotushauri" alisema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amemwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Francis Mwanisi Kuhakikisha ifikapo Disemba 30 mwaka huu angalau kaya zote mkoani Mara ziwe na vyoo bora, na kumtaka kutoa elimu na kuhamasisha wananchi juu ya umuhimu wa matumizi ya vyoo bora kiafya na kiuchumi kwa mwanadamu.

"Kaya zilizo na vyoo bora kwa Mkoa wa Mara naona ni Asilimia 40, Kwahiyo tunahitaji kuongeza elimu na kutoa mwamko kwa jamii kuhusu kujenga vyoo bora na kuvitumia" alisema Waziri Ummy

Mbali na hayo Waziri Ummy amesema kuwa Serikali inaendelea kuboresha huduma za Afya Mkoani Mara kupitia kuboresha Vituo vya Afya 14, na kujenga Hospitali 3 za Wilaya ambazo ni Lorya, Musoma DC na Bunda, jambo ambalo litalopunguza mzigo kwa Hospitali ya Mkoa ili iweze kujikita katika kutoa huduma za rufaa.

Sambamba na hilo Waziri Ummy amesema kuwa Serikali itaendelea  kuboresha huduma Bora kwa wananchi kwa  kupeleka jumla ya Watumishi 25 katika Hospitali ya Mkoa wa Mara huku akiwahasa Viongozi mkoani hapo kujenga Mazingira mazuri yakuwavutia Watumishi ili wafanye kazi kwa bidii na wabaki katika vituo vya kazi.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Mara Dkt. Hosea Bisanda alisema kuwa Hospitali ya Mkoa imeweza kupunguza vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 23 mwaka 2015, vifo 14 mwaka 2016, vifo 10 mwaka 2017, na vifo 6 hadi kufikia Oktoba mwaka huu.

Dkt. Bisanda amesema kuwa licha ya Serikali kuwaletea Watumishi 25  Hospitali ya Mkoa wa Mara inatakiwa kuwa na Watumishi 684, lakini Watumishi waliopo sasa ni 305, hivyo kupelekea kuwa na upungufu wa Watumishi 379 sawa na Asilimia 55.

"Hospitali ya Mkoa wa Mara ina uhaba wa Watumishi hasa Madaktari Bingwa, Madaktari wasaidizi, Wauguzi, wateknolojia, Maabara pamoja na wateknolojia madawa" alisema Dkt. Hosea Bisanda

Mwisho.