Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi akisisitiza jambo kwa wajumbe wa mkutano wa mwaka wa wadau wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma (hawapo pichani) katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Mipango Dodoma.
Meneja wa Mpango wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma nchini Dkt. Beatrice Mutayoba akiongea jambo kwenye mkutano wa mwaka wa wadau wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma
Wajumbe wa mkutano wa mwaka wa wadau wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma wakiwa kwenye mkutano.
Wajumbe wa mkutano wa mwaka wa wadau wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma wakiwa kwenye mkutano.
Picha ya pamoja wajumbe wa mkutano wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma katika ukumbi wa Chuo cha Mipango Dodoma.
Na WAMJW - Dodoma.
Tanzania ni miongoni mwa nchi 30
zenye kiwango kikubwa cha wagonjwa wa kifua kikuu duniani huku takwimu zikionesha
kuwa kati ya watanzania laki moja, 269 wanaugua ugonjwa wa kifua kikuu.
Hiyo ni kauli ya Mkurugenzi wa Huduma
za Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi alipokuwa akifungua kikao cha
mwaka cha cha wadau wa Mpango wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma kilichofanyika
Jijini Dodoma katika Ukumbi Wa Chuo cha Mipango.
Licha ya kupiga hatua katika
uboreshaji wa sekta ya afya ambapo Serikali imekuwa ikitoa huduma za matibabu
bure kwa wagonjwa wa kifua kikuu, bado wananchi hawana elimu ya kutosha
kutambua mapema dalili za ugonjwa huo.
Dkt. Subi anasema kuwa ugunduzi wa
wagonjwa wa kifua kikuu ndani ya jamii upo chini huku asilimia 44 tu ya
wagonjwa wa kifua kikuu hujitokeza kupatiwa matibabu huku asilimia 56 ya
wagonjwa bado wapo mtaani wanaishi na kifua kikuu hivyo kuhatarisha kuongezeka
kwa maambukizi mapya.
“Takwimu hizi si nzuri hivyo kuna
haja ya kuongeza mkakati wa kuwagundua wagonjwa hao kwa wakati na kutoa elimu
kwa wananchi namna ya kutambua na kujinga
na maambukizo ya ugonjwa huo hatari” amesema Dkt. Subi alipokuwa anazungumza na
wataribu wa ugonjwa wa kifua kikuu, waganga wa mikoa, wilaya pamoja na wadau wa
afya katika mkutano huo na kuwataka waganga wakuu wote kuhakikisha dawa za kifua kikuu zinakuwepo
katika vituo vyote vya afya kila wakati bila kupungua na njia pekee ya
kutokomeza ugonjwa huo ni kuahakikisha wagonjwa wote wanagundulika na kupatiwa
matibabu.
Hata hivyo Dkt. Subi amesema kuwa asilimia
40 ya vifo vya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi vilisababishwa na kifua
kikuu, na hiyo inatokana na kupungua kwa kinga na kusababisha mgonjwa kupokea
ugonjwa huo kwa haraka zaidi.
Awali akitoa taarifa yake, Meneja
wa Mpango wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma nchini, Dkt. Beatrice Mutayoba
amesema kuwa Serikali imeendelea kuboresha utoaji wa huduma za matibabu ya
ugonjwa wa kifua kikuu nchini ambapo ugunduzi wa mgonjwa wa kifua kikuu
huchukua muda mfupi tofauti na zamani.
“Serikali imenunua mashine za
ugunduzi wa ugonjwa wa kifua kikuu za vina saba (Genexpert TB Test Mashines)
210 na kuzisambaza Tanzania nzima, mashine hizi zinaweza kumtambua mgonjwa wa
kifua kikuu ndani ya masaa mawili tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo majibu
hutoka baad ya siku tatu” alisema Dkt. Mutayoba.
Dkt Mutayoba anasema kuwa bado wanaendelea
kusambaza mashine za hadubini kwa ajili ya ugunduzi na kuchuguza maendeleo ya
wagonjwa ambao tayari wameanza matibabu.
Aidha Dkt. Mutayoba alisema kuwa
Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea na mpango wa kuwajengea uwezo
wataalamu wa afya katika vituo afya ili waweze kuwagundua wagonjwa wa kifua
kikuu mapema na kupatiwa matibabu.
Inakadiriwa kuwa watu 150,000 huugua ugonjwa wa kifua kikuu nchini kwa mwaka huku wagonjwa wagonjwa 66,000 sawa na asilimia 44 hujitokeza kupata huduma za matibabu hivyo kundi kubwa la wagonjwa bado wapo katika jamii hivyo kuhatarisha kutokea kwa maambukizi mapya.
0 on: "TANZANIA YATAJWA KUWA MIONGONI MWA NCHI 30 ZINAZOONGOZA KUWA NA IDADI KUBWA YA MAAMBUKIZI YA KIFUA KIKUU."