Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee Na Watoto, Mhe. Ummy
Mwalimu akisisitiza jambo mbele ya Wajumbe na viongozi wa Baraza la
Wafamasia (Hawapo kwenye picha) wakati wa uzinduzi wa Baraza jipya la
Famasia leo katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es salaam
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee Na Watoto, Mhe. Ummy
Mwalimu akimkabidhi zawadi mmoja kati ya Wajumbe wa Baraza la Wafamasia
wakati wa uzinduzi wa Baraza jipya la Famasia leo katika Ofisi ndogo za
Wizara jijini Dar es salaam
Wajumbe wa Baraza la Wafamasia wakiwa katika kikao cha uzinduzi wa
Baraza jipya la Famasia kilichofunguliwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee Na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu leo katika Ofisi
ndogo za Wizara jijini Dar es salaam.
Wajumbe wa Baraza la Wafamasia wakifuatilia kwa makini maelekezo kutoka
kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee Na Watoto, Mhe.
Ummy Mwalimu wakati kikao cha uzinduzi wa Baraza jipya la Famasia, leo
katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es salaam.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee Na Watoto, Mhe. Ummy
katika picha ya pamoja na Sekretarieti ya Baraza la Wafamasia baada ya kikao
cha uzinduzi wa Wajumbe wapya wa Baraza la Famasi katika Ofisi ndogo za Wizara
Jijini Dar es salaam.
Na WAMJW-DSM
HOTUBA YA MHE. UMMY MWALIMU (MB) WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO WAKATI WA UZINDUZI WA BARAZA JIPYA LA FAMASI
KATIKA UKUMBI WA WIZARA TAREHE 17 NOVEMBA, 2018
Mwenyekiti wa Baraza la Famasi uliyemaliza muda na wa sasa;
Wajumbe wa Baraza la Famasi waliomaliza muda na wanaoingia kazini;
Wakurugenzi Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee;
Msajili wa Baraza la Famasi;
Wasajili kutoka Bodi na Mabaraza chini ya Wizara;
Watumishi wa Wizara pamoja na Sekretarieti ya Baraza;
Wageni waalikwa;
Wanahabari;
Mabibi na Mabwana.
Awali
ya yote nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kutukutanisha siku hii ya leo.
Pili nitoe shukrani zangu za dhati kwa kunipa nafasi ya kukutana na
kuzungumza pamoja nanyi na kuzindua Baraza Jipya la Famasi ambalo ni la
awamu ya nne (4) tangu Baraza hili kuanzishwa rasmi mwaka 2003.
Aidha,
nichukue nafasi hii kwa niaba yangu binafsi na ya Wizara kuupongeza
uongozi wa Baraza chini Mwenyekiti Ndugu Legu Mhangwa kwa moyo wa
kujitolea na kufanya kazi nzuri pamoja na changamoto zilizokuwepo. Ni
ukweli usiofichika kwamba mmefanya kazi nzuri katika kulijenga Baraza la
Famasi.
Nimesikiliza kwa
makini mafanikio mbalimbali ambayo Baraza limeyapata kufuatia maelezo
yaliyotolewa na Mwenyekiti aliyemaliza muda wake pamoja na Msajili wa
Baraza na kwamba, pamekuwepo na umuhimu wa kufanya mapitio ya kanuni na
miongozo mbalimbali ambayo imeonekana imepitwa na wakati ili kwenda
sambamba na mabadiliko ya sasa.
Katika
muda wa miaka mitatu (3) mliyotumika, Baraza limeonyesha uwezo mkubwa
wa kudhibiti taaluma na wanataaluma, kusimamia na kudumisha maadili na
miiko ya taaluma ya famasi, pamoja na usimamizi wa utoaji wa huduma za
dawa na hivyo kuendeleza na kuboresha uhai wa fani ya famasi.
Pamoja
na maboresho hayo niwapongeze kwa kupandishwa hadhi kwa Baraza na kuwa
taasisi inayojitegemea. Hii inaonesha jinsi mlivyoweza kuweka juhudi
katika kujisimamia na kuongeza ufanisi kiutendaji katika majukumu yenu.
Kwa kuwa baadhi yenu mmemaliza wajibu wenu leo, ninawasihi kutokana na
uzoefu mlioupata katika kipindi cha miaka mitatu, muendelee kutoa
ushauri kwa wajumbe wapya ambao wanakabidhiwa majukumu haya ili
kufanikisha malengo na madhumuni ya kuwepo kwa Baraza hili.
Mabibi na Mabwana,
Kwa
moyo wa dhati nawapongeza wajumbe wapya ambao mnakabidhiwa majukumu
hivi leo, Wizara yangu na Serikali kwa ujumla tuna matarajio makubwa
katika kipindi hiki cha miaka mitatu (3) ambacho mtakuwa na jukumu hili
kubwa la kuishauri Wizara katika mambo kadha wa kadha ya taaluma hii na
hatimaye kuboresha utoaji wa huduma za dawa katika vituo na sehemu
mbalimbali zinazofanya shughuli hizi kwa mujibu wa Sheria.
Mabibi na Mabwana,
Ni
imani yangu kubwa kuwa wengi wenu katika Baraza lililotangulia na hili
la sasa mnafahamu fika majukumu yenu kama yalivyoainishwa katika Sheria
ya Famasi, Sura 311 inayounda Baraza hili. Sitakuwa na sababu ya
kuyataja, ila nashauri muweze kurejea kwenye sheria hiyo ambayo katika
hayo nisisitize kushirikiana na taasisi mbalimbali ambazo kwa namna moja
au nyingine zinagusa masuala ya taaluma hii ikiwa ni pamoja na mafunzo
ya wanataaluma wa fani hii ili kutosababisha migongano ya kiutendaji ya
ndani na nje ya Wizara zinazohusika.
Mabibi na Mabwana,
Pamoja
na kazi nilizozitaja hapo juu, jukumu la Baraza la Famasi ni kuleta
msukumo wa utoaji huduma bora ya afya kwa mtanzania. Hili linawezekana
kwa kuhakikisha kuwa wanataaluma wanazingatia maadili na nidhamu ya
taaluma katika ununuaji, utunzaji na matumizi sahihi ya dawa na vifaa
tiba vilivyo salama na ubora wa hali ya juu.
Vile
vile, napenda nisisitize kuwa Baraza lione umuhimu wa kuweka msukumo wa
pekee kwenye masuala ya kuboresha mafunzo na elimu ili tuwe na
wanataaluma wenye uwezo wa utendaji wa kiwango cha hali ya juu katika
nchi yetu katika maeneo yote ikiwamo uzalishaji wa dawa Viwandani ili
kwenda sambamba na adhima ya Serikali kuelekea uchumi wa Viwanda.
Mabibi na Mabwana,
Napenda
kuwahakikishia kuwa, jamii ya watanzania wanahitaji huduma hii, hali
inaonesha kuwa, kupitia takwimu mbalimbali zaidi ya 40% ya wananchi
wanapopata tatizo la afya huanza kwenda kupata huduma ya awali kwenye
maduka ya dawa (famasi na maduka ya dawa muhimu), hivyo basi kushindwa
kuwa na huduma bora katika maeneo hayo na inahatarisha kwa kiasi
kikubwa maisha ya wananchi.
Wizara
inalitambua hili na umuhimu wa kuwepo kwa fani hii hapa nchini. Kwa
kushirikiana na kada nyingine za afya huduma za afya zitaendelea
kuboreka na kuthaminiwa katika maeneo yetu ya kazi.
Mabibi na Mabwana,
Wataalam
wa fani ya famasia ndio wahusika wakuu katika masuala yote yanayohusu
dawa katika kuhakikisha kuwa dawa zinapatikana katika hospitali na vituo
vyote vya kutolea huduma za afya nchini. Serikali kwa upande wake
imeongeza bajeti ya Dawa kutoka Shilingi bilioni 30 mwaka 2015/2016 hadi
Tsh 270 Bilioni mwaka 2018/2019, hivyo ni Wataalamu hawa wa Famasi
wanaotakiwa kuhakikisha kuwa ongezeko la bajeti linaenda sambamba na
upatikanaji wa dawa na matumizi sahihi kwa kuzingatia miongozo ya tiba.
Ni dhahiri kuwa utaalamu wa kutengeneza, uagizaji, usafirishaji,
usambazaji, utoaji dawa sahihi kwa wagonjwa, utunzaji na utoaji mafunzo
yahusuyo dawa ndiyo msingi mkubwa wa taaluma hii. Hivyo basi Baraza
ambalo ndilo lililopewa dhamana ya kusimamia kazi za utendaji wa taaluma
hii kuongeza nguvu za usimamizi na udhibiti wa sheria na miongozo na
kuhakikisha kazi za wataalamu hawa zinafuata miiko na taratibu za
kitaaluma zilizowekwa na zinafanyika kwa uangalifu; na kuchukua hatua
zinazostahili pindi inapogundulika kuna ukiukwaji wa Sheria na taratibu
Pia
ni wajibu wa wanataaluma kuwa mfano mzuri kwa jamii wanayoihudumia ili
kujenga imani na kudumisha uhusiano mzuri na jamii wanazozihudumia.
Wageni Waalikwa,
Kuhusu
migogoro ambayo nimekuwa nikiisikia kati ya Baraza na Wafanya biashara
wa Maduka ya Dawa ni vyema tuchukue hatua za haraka ili kuondoa
changmoto hizo na katika hili naelekeza Baraza tufanya yafuatayo:
Maduka
ya Dawa yasiyo na vibali yaliyopo katika maeneo yasiyoruhusiwa
kuendesha maduka ya ADDO, kwa sasa yapewe muda wa mpito wa miaka miwili
(2) kuanzia tarehe ambayo utatoa taarifa hiyo kwa umma;
Katika
kipindi hicho maduka hayo yauze dawa zisizohitaji cheti cha Daktari
(general sales medicines) kwa utaratibu ambao utaandaliwa na Baraza la
Famasi kwa masharti kwamba endapo watakiuka utaratibu huo hatua za
kisheria zitachukuliwa dhidi yao;
Baada ya muda huo
kupita, maduka haya yatatakiwa aidha kufungwa, kupandishwa hadhi kuwa
Famasi au kuhamia maeneo yanyoruhusiwa ADDO na kuendelea kutoa huduma
hiyo; na
Wamiliki wa Maduka ya Dawa ambayo yapo katika maeneo yanayoruhusiwa kuendesha ADDO wayapandishe hadhi maduka yao mara moja.
Mabibi na Mabwana,
Napenda
kuwahakikishia kuwa yote yatawezekana kama sisi sote tutakubaliana
kusimamia na kutekeleza suala la uwazi na ukweli (Transparency &
Good Governance). Nawasihi kuendelea kushirikiana na nchi nyingine ili
kupata uzoefu zaidi wa namna bora ya kusimamia taaluma hii ya Famasia.
Hitimisho,
Mwisho
ningependa kuwahakikishia kwamba Wizara ipo tayari kuwasaidia katika
mipango iliyopo na ile mtakayoipendekeza kwa serikali kulingana na hali
halisi ya uwezo. Niwatakie Baraza jipya linalozinduliwa leo utekelezaji
mzuri wa majukumu yenu.
Baada ya kusema hayo machache, sasa natamka kuwa Baraza la Famasi limezinduliwa rasmi.
Asanteni kwa Kunisikiliza.
0 on: "WAZIRI UMMY AZINDUA BODI MPYA YA WAFAMASIA"