Na WAMJW – NACHINGWEA,LINDI
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amewaasa Watoa huduma za Afya wote nchini kuzingatia Sheria, Maadili na Weledi wa taaluma yao pindi wanapotoa huduma kwa wagonjwa.
Waziri Ummy ameyasema hayo leo wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya utoaji Ubora wa Huduma za Afya na uhamasishaji kwa Wananchi/Wakulima kutumia Bima ya Afya (UshirikaAfya) katika Mkoa wa Lindi, Wilaya ya Nachingwea.
Waziri Ummy amesema kuwa yeyote katika katika Sekta ya Afya atakaekutwa anajihusisha na vitendo vyovyote vya Rushwa atachukuliwa hatua kali ikiwemo kufutiwa leseni yake ya kutoa huduma za afya popote nchini.
“Masuala yakuchukua Rushwa tuachane nayo, na kama tukikukuta hatutakuwa na msalia mtume na wewe, hatuwezi kukubali, kama umeamua kujitolea kuwahudumia Wagonjwa, wahudumie wagonjwa, suala la rushwa hatutalifumbia macho” Alisema Waziri Ummy
Kwa upande mwingine, Waziri Ummy alikutana na Viongozi wa vikundi muhimu vya Ushirika vya Wakulima (AMCOS) lengo likiwa ni kuwahamasisha ili wajue umuhimu wa kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya kisha wakawahamasishe Wakulima wengine katika maeneo yao.
Waziri Ummy alisema kuwa katika kila Watanzania 100, Watanzania 67 wanapata huduma za afya kwa kulipa papo kwa papo jambo ambalo linawaumiza Wakulima wengi kutokana na matibabu kuwa gharama kubwa bila kutumia Bima ya Afya.
“Wananchi wanatakiwa kuchangia huduma za Afya, kila Watanzania 100, Watanzania 67 wanalipa fedha hapo hapo, maana yake wanaolipa malipo ya papo kwa hapo wanatumia fedha nyingi zaidi kuliko wanaolipa kwa kutumia Bima ya Afya” Alisema Waziri Ummy.
Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa, Serikali kupititia mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, wameanzisha utaratibu mpya wa Bima ya Afya kwaajili ya Wakulima (Ushirika Afya), lengo ni kuona namna ya kuwakwamua Watanzania kupata huduma za matibabu bila ya kikwazo cha fedha
“Katika kuona ni jinsi gani tunaweza kuwakwamua Watanzania kupata huduma za afya bila kikwazo chochote cha fedha, Serikali kupitia mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, tumeanzisha utaratibu mpya wa bima ya afya kwaajili ya wakulima (Ushirika Afya)” alisema Waziri Ummy.
MWISHO.
0 on: "WAZIRI UMMY AWAASA WATOA HUDUMA ZA AFYA KUZINGATIA MAADILI NA WELEDI WA TAALUMA YAO"