Mkurugenzi wa Tiba, Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akisisitiza jambo katika mkutano na
Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa sheria ya umiliki wa maabara
binafsi za Afya.
Kaimu Msajili wa Bodi ya Maabara Binafsi za Afya akijibu maswali ya
Waandishi wa habari wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari uliohusu
utekelezaji wa sheria ya umiliki wa maabara binafsi za Afya.
Wajumbe wa Sekretariet ya Maabara binafsi pamoja na kamati ya Afya ya
msingi za manispaa za jiji la Dar es salaam wakifuatilia maelekezo
kutoka kwa Mkurugenzi wa Tiba, Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima kuhusu utekelezaji wa
sheria ya umiliki wa maabara binafsi za Afya katika ofisi ndogo za
Wizara ya Afya jijini Dar es salaam
SERIKALI YAAPA KUWACHUKULIA HATUA WAMILIKI WA MAABARA BINAFSI ZOTE ZISIZOKIDHI VIGEZO
Na WAMJW - DSM
SERIKALI
kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
imesema kuwa ifikapo Januari 15 mwaka 2019 Wamiliki wote wa Maabara
binafsi ambao hawajatimiza vigezo vya uendeshaji vya Bodi ya usimamizi
wa Maabara binafsi.
Hayo
yamesemwa na Mkurugenzi wa Tiba Dkt. Dorothy Gwajima leo wakati
akizungumza na Waandishi wa Habari katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya
jijini Dar es salaam.
Dkt.
Gwajima alisema kuwa kipindi cha kuelimishana juu ya umuhimu
wakutimiza sheria na vigezo vya uendeshaji wa Maabara umekwisha hivyo
Wamiliki wa Maabara hizo wanapaswa kufuata vigezo hivyo kabla ya Januari
15 mwaka 2019.
'Wako wamiliki wa maabara binafsi ambao, wameamua
kuamini kwenye kufuatiliwa kila siku, sasa ufuatiliaji na uelimishaji
uliokwisha fanyika awali unatosha, wakati wa kuelewa somo umepita sasa
ni saa ya KAZI TU !. Imefika zamu ya wamiliki wa maabara binafsi kwenda
kutimiza wajibu wao bila shurti tena pasipo kuendelea kuisababishia
Serikali gharama za ziada" alisema Dkt.Gwajima
Aidha,
Dkt. Gwajima amesema kuwa kutimiza wajibu wa matakwa ya kisheria kwa
wamiliki husika wa mabaara binafsi ni pamoja na;-
1. Kila mmiliki
kuhakikisha amekidhi vigezo vyote vya kumiliki maabara binafsi kama
ambavyo amekuwa akielekezwa na wataalamu walioko kila halmashauri na
mikoa husika,
2. Kuhakikisha amelipa ada na tozo stahiki zikiwemo malimbikizo ya nyuma na faini zote stahiki.
3. Amepata risiti halali za malipo hayo
4.
Anaendelea kulipa tozo stahiki kila mwaka ili, kuwezesha bodi husika
kutimiza wajibu wake wa kufanya uhakiki wa ubora wa huduma kwa kila
kituo kila mwaka na kufanya ukaguzi maalumu wa vituo husika kama
vinaendelea kuwa katika viwango stahiki kama siku vilipopewa kibali cha
kutoa huduma husika.
Mbali na hayo Dkt Gwajima amesema kuwa Bodi
imeendelea kuimarisha ushirikiano wake na vyombo vyote vya Serikali
ngazi zote kuanzia OR TAMISEMI na ngazi zake zote za Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa na sasa, huku ikiandaa orodha ya maabara binafsi nchi
nzima na itaweka katika vyombo vya habari na
itasambaza kwa wadau wote.
Dkt Gwajima aliendelea kusema kuwa yeyote ambaye
hayumo katika orodha hiyo asithubutu kutoa huduma hizo maana, mamlaka za
Serikali za mitaa zitambaini na taarifa zitafika mahali sahihi mara
moja na hatua kali zitachukuliwa.
Sambamba na hayo Dkt Gwajima ametoa wito
kwa mamlaka zote za Serikali ngazi zote kuendelea kupeana taarifa kwa
haraka zaidi na kujipanga vema zaidi katika kuhakikisha hakuna mvunja
sheria anathubutu kutoa huduma za kijamii bila kibali.
MWISHO.
0 on: "SERIKALI YAAPA KUWACHUKULIA HATUA WAMILIKI WA MAABARA BINAFSI ZOTE ZISIZOKIDHI VIGEZO"