Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee Na Watoto, Mhe. Ummy
Mwalimu akisisitiza jambo mbele ya Watoto wanaoishi katika Mazingira
magumu na Walezi wao (hawapo kwenye picha) wakati wa kukabidhi Bima za
Matibabu kwa Watoto hao wanaoishi katika Mazingira magumu Mkoani Dar es
salaam
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee Na Watoto, Mhe. Ummy
Mwalimu akiteta jambo na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Dkt. Grace
Magembe wakati wa kukabidhi Bima za Matibabu kwa Watoto wanaoishi
katika Mazingira magumu Mkoani Dar es salaam
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee Na Watoto, Mhe. Ummy
Mwalimu akimkabidhi Bima ya Matibabu mmoja kati ya watoto wanaoishi
katika Mazingira magumu wakati wa sherehe za kukabidhi Bima za Matibabu
kwa Watoto wanaoishi katika Mazingira magumu jijini Dar es salaam.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee Na Watoto, Mhe. Ummy
Mwalimu akiwa katika picha ya pamoja na Watoto wanaoishi katika
Mazingira magumu wakati wa saherehe za kukabidhi Bima za Matibabu kwa
Watoto hao leo katika makao ya Watoto UMRA, Magomeni Mikumi jijini Dar
es salaam.
Na WAMJW - DSM
HOTUBA MGENI RASMI WAZIRI WA AFYA,
MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHESHIMIWA UMMY ALLY
MWALIMU (MB) KATIKA SHEREHE YA KUKABIDHI BIMA ZA MATIBABU KWA WATOTO
WANAOISHI KATIKA MAZINGIRA MAGUMU MKOANI DAR ES SALAAM: MAKAO YA WATOTO UMRA, MAGOMENI
TAREHE 17/12/2018
Ndugu Dkt. John Jingu Katibu Mkuu, WAMJW, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii;
Ndugu Ken Cockkerill - Afisa Mtendaji Mkuu wa Stanbic Bank;
Mganga Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam;
Ndugu Bernard Konga Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya;
Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Dar es Salaam;
Ndugu Francisca Makoye Afisa Ustawi wa Jamii Mkuu Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam;
Viongozi wa Siasa na Watendaji Wakuu wa Serikali;
Ndugu Rahma Juma Kishumba Kiongozi Mlezi wa Makoa ya Watoto UMRA;
Ndugu Viongozi na Waratibu wa Huduma za Ustawi wa Jamii kutoka Manispaa za Mkoa wa Dar es Salaam;
Ndugu Viongozi wa Makao na Taasisi za Malezi ya Watoto Wanaishi katika Mazingira Magumu;
Ndugu Wanahabari na Wasanii;
Ndugu Wageni Waalikwa;
Ndugu Wananchi.
Asalaam Aleykum,
Watotoooooo (Wataitikia Kwanzaaaaa!!)
Ndugu Wananchi;
Awali
ya yote, naomba tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa
Makao ya Watoto UMRA Magomeni. Leo ni siku kubwa na muhimu kwa watoto
wote nchini na hususan kwa Watoto Wanaoishi Katika Mazingira Magumu.
Hivyo basi inatupasa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa dhati kwa kutupatia
Fursa hii ambapo LEO kwa Msaada wa Benki ya STANBIC tunawapatia Bima za
Matibabu Jumla ya Watoto 900 nchini. Kati yao, Mkoa wa Dar es Salaam
tunawapatia Bima za Matibabu Jumla ya Watoto 500.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kuchukua nafasi hii kuwashukuru kwa dhati Benki ya Stanbic kwa moyo wao
wa kizalendo wa kuamua kuwalipia Bima za Afya Watoto Wanaoishi Katika
Mazingira Hatarishi. Msaada huu ni muhi sana kwao katika kuhakikisha
kuwa wanapata malezi na makuzi bora, hivyo kujiwekea hazina yenye afya
bora kwa taifa letu miaka inayokuja.
Vile
vile ninawashukuru kwa dhati wenzetu wa Mfuko wa Bima ya Afya kwa
kuchukua hatua za haraka katika kupokea, kuchambua na kuhakiki na
kupitisha orodha ya majina ya watoto ambayo Wizara yangu iliyapendekeza
kupatiwa vitambulisho vya Bima ya Afya. Kasi na umakini mlio onyesha
katika kukamilisha zoezi hili inaakisi sawa sawa kauli Mbiu ya
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli ya Hapa ni Kazi Tu!
Ndugu Wananchi;
Leo
ni siku maalumu kwa watoto wetu wapendwa. Kwa msingi huu sijanuia kutoa
hotuba ndefu za kitaalamu kama ambavyo huwa ninafanya katika hadhira
nyingine za watu wazima. Hata hivyo ngoja nieleze mambo machache ya
msingi hapa chini.
Ndugu Wananchi;
Kupitia
Sera ya Afya 2007, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika huduma
za afya zenye ubora na zinazowafikia wananchi wote ili kuboresha afya
zao. Serikali inatambua umuhimu wa afya bora kwa wananchi wake kwani
afya bora ni raslimali muhimu kwa maendeleo. Kitendo cha kuwapatia Bima
ya Afya Watoto wetu leo hii, ni mojawapo ya jitihada za Serikali kwa
kukushirikiana na Wadau kama STANBIC BANK katika kuhakikisha kuwa
wananchi wote iwemo wale wa makundi maalumu ya uhitaji wanapata Huduma
Bora za Afya.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kuchukua fursa kusisitiza kuwa Maendeleo ya Taifa letu la Tanzania
yataletwa na wananchi wenye afya na wenye uwezo wa kuzalisha mali.
Katika kuhakikisha kuwa wananchi wana afya bora, Serikali imeendelea
kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa huduma za afya kwa kuzingatia
sera na miongozo iliyopo.
Ndugu Wananchi;
Hivyo
basi naomba nitoe Wito kwa wengine wa Maendeleo and Sekta Binafsi hapa
nchini kuiga mfano wa moyo wa kujitolea kwa kuwasaidia Watanzania
wenzetu wasiojiweza kupata mahitaji yao ya msingi ikiwemo uhakika wa
kupata huduma bora za afya.
Ndugu Wananchi;
Kama
Waziri mwenye dhamana wa kusimamia uendeshaji wa Makao ya Kulelea
Watoto Wenye Shida, nachukua fursa hii pia kuueleza Umma wa Watanzania
na Wamiliki wa Makao haya juu umuhimu wa kuzingatia Sheria na Kanuni
husika. Hili likifanyika vyema, litasaidia kuwa na Makao yanayotoa
huduma bora za malezi na makuzi kwa watoto ambao wametoka kwenye shida
nyingi maishani mwao.
Ndugu Wananchi;
Wizara
ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inalojukumu la
uratibu wa uanzishwaji na uendeshaji wa Vituo vya Kulelea Watoto Wadogo
Mchana na Makao ya Watoto walio katika mazingira hatarishi kwa mujibu wa
Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009. Lakini, Pamoja na uwepo wa sheria
hii kumekuwepo na changamoto ya uanzishaji na uendeshaji wa Vituo na
Makao usiozingatia sheria na kanuni za uanzishaji wa huduma hizi.
Ndugu Wananchi;
Katika
kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na Makao Bora ya watoto wenye shida,
yenye uwezo wa kuwapatia mahitaji yao ya msingi kama vile Afya Bora
ninatoa maelekezo yafuatayo;
Natoa tamko kuwa
mamlaka husika katika kila Halmashauri kwa uratibu wa Maafisa Ustawi wa
Jamii, wavifunge mara moja Vituo vyote, Makao yote yanayoendeshwa
kinyume na sheria.
Wamiliki wa Vituo na Makao haya
watii matakwa ya sheria ya kuwasilisha taarifa za utekekezaji za Mwezi,
Robo Mwaka na Mwaka kama ilivyoanishwa katika Kanuni;
Kuanzia
sasa ni marufuku kwa mtu yoyote au Shirika kuanzisha Vituo vya Kulelea
Watoto Wachanga Mchana na Makao ya Watoto bila kibali cha Mamlaka
husika;
Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa na
Halamashauri za Wilaya kupitia kwa Maafisa Ustawi wa Jamii kufanya
Ukaguzi wa Vituo hivi na kuwasilisha taarifa za ukaguzi kila mwezi kwa
Msajili ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa, ikiwemo kufunga Vituo
visivyokidhi vigezo.
Wamiliki wa Vituo hivi kuzingatia Sheria na Kanuni katika utoaji wa huduma na kujiepusha kutumia huduma hii kwa manufaa binafsi;
Jamii
inapaswa kuelewa kuwa familia ndiyo mahala salama kwa malezi ya watoto.
Hivyo baba, mama na walezi wa watoto hawana budi kuwajibika ipasavyo
kulea watoto wao.
Ndugu Wananchi;
Kama
nilivyotangulia kusema awali leo ni siku muhimu wa Watoto Wanaoishi
Katika Mazingira Magumu, na watoto wote kwa ujumla katika nchi yetu.
Maelekezo ya kuzingatia sheria na taratibu husika niliyotoa hapo juu
yanatosha kuwafungua masikio wakorofi wachache wasiopenda kufuata
taratibu.
MWISHO
Ndugu Wananchi;
Narudia tena kuwashukuru kwa dhati Benki ya STANBIC KUWAPATIA ZAWADI BORA YA KRISTMASI WATOTO WETU KWA KUWAPATIA BIMA ZA AFYA.
ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA SASA NIPO TAYARI KUWAKABIDHI KADI ZA BIMA YA AFYA WATOTO WETU WAPENDWA.
0 on: "WAZIRI UMMY AGAWA BIMA ZA MATIBABU KWA WATOTO 900 NCHINI"