MASHINDANO YA TAIFA YA AFYA NA USAFI WA MAZINGIRA
YAZINDULIWA JIJINI DODOMA
NA WAJMW-DODOMA
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto imezindua mashindano ya taifa ya afya na usafi wa mazingira
yatakayoratibiwa nchi nzima.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari katika ukumbi wa
bunge jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amesema lengo la mashindano hayo ni kuinua hali
ya afya na usafi wa mazingira katika ngazi ya kaya na taasisi ili kulinda na
kuboresha afya ya jamii.
“Mashindano haya yalianza mwaka 1988 ambapo yamekuwa
yakifanyika kila mwaka. Kupitia mashindano haya hali ya usafi wa mazingira
imeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka na kusaidia kupunguza magonjwa ya kuhara
kutoka zaidi ya wagonjwa 1,300,000 mwaka 2014 hadi chini ya wagonjwa 70,000
mwaka 2018”. Amesema Dkt. Ndugulile.
Aidha, Naibu Waziri huyo amesema mashindano hayo yamesaidia
ujenzi wa madampo ya kisasa katika mikoa ya Dodoma, Mbeya, Arusha, Kigoma na
Mtwara. Pia ujenzi wa machinjio ya kisasa katika miji mbalimbali umeweza kutekelezwa na mashindano.
Dkt. Ndugulile ameongeza kuwa mashindano hayo kwa mwaka 2019
yatahusisha Halmashauri zote 184 ambapo Halmashauri zitakazoshinda ngazi ya
mkoa zitashindanishwa kitaifa, pia vipengele viwili vimeongezwa katika
mashindano ya mwaka huu.
“Ili kuongeza chachu katika mashindano haya, Wizara
imeongeza vipengele viwili ambavyo ni ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa na
Taasisi za kibenki. Katika Mkoa Benki itakayoshinda itashindanishwa na mikoa
mingine ili kupata mshindi wa kitaifa”. Amesema Dkt. Ndugulile.
Mashindano hayo yataendeshwa na kamati ya taifa ya
mashindano ya usafi wa mazingira inayojumuisha wajumbe kutoka wizara na taasisi
mbalimbali na pia yatakua na muundo wa
makundi 12 ambapo kila kundi litatoa washindi watatu. Makundi hayo ni Halmashauri
za majiji na manispaa, Halmashauri za Miji, Halmashauri za Wilaya, Kijiji bora
kinachotekeleza kampeni ya usafi wa mazingira, Hospitali za Rufaa za Mikoa,
Hospitali za Rufaa za binafsi, Hoteli, Shule za sekondari na msingi, Shule za serikali
za sekondari za bweni, Shule za binafsi za sekondari za bweni, Ofisi za umma na
Mabenki.
Dkt. Ndugulile amesema Wizara imepanga kutoa zawadi
mbalimbali kwa washindi wa makundi ambapo watapatiwa fedha taslimu, vyeti na
vikombe. Mshindi wa juu atatokana na kundi la Halmashauri za wilaya na atapata
zawadi ya Shilingi Milioni Hamsini.
Hata hivyo, Dkt. Ndugulile ametoa wito kwa Halmashauri zote
nchini kuiga mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ambayo imewezesha kaya
zake zote kuwa na vyoo bora. Naibu Waziri amesema usafi wa mazingira na matumizi
ya vyoo bora unaweza kupunguza magonjwa ya kuambukiza kwa zaidi ya asilimia 80
na hivyo kuipunguzia serikali gharama za kununua madawa na kupambana na
magonjwa ya milipuko.
MWISHO
0 on: "MASHINDANO YA TAIFA YA AFYA NA USAFI WA MAZINGIRA YAZINDULIWA JIJINI DODOMA"