Waziri Ummy akiwa na baadhi ya akinamama waliopewa vyandarua baada ya kufika kliniki katika kituo cha afya cha Makole Jijini Dodoma wakati Waziri alipofika na kugawa vyandarua hivyo. |
Na WAMJW-Dodoma
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Ummy Mwalimu amelipongeza Jiji la Dodoma kwa jitihada kubwa zilizofanyika kwa
ajili ya kutokomeza ugonjwa wa Malaria.
Waziri Ummy ametoa pongezi hizo wakati alipokua anagawa
vyandarua vyenye dawa kwa akinamama wajawazito na wenye watoto wadogo katika
Kituo cha Afya cha Makole Jijini Dodoma.
Waziri Ummy amesema Jiji la Dodoma limetokomeza Malaria
kutoka Asilimia 1 mpaka asilimia 0.6 ikiwa mafanikio makubwa, ambapo amesema katika
kipindi cha miaka mitatu nchi nzima ugonjwa wa Malaria umeweza kupungua kutoka
asilimia 14 mwaka 2015 mpaka asilimia 7 mwaka 2018.
“Toka Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli
iingie madarakani tumeweza kutekeleza mikakati mbalimbali ya kutokomeza Malaria
nchini, katika kipindi kifupi cha miaka mitatu tumeweza kupunguza Malaria zaidi
ya asilimia 50 kutoka asilimia 14 mwaka mwaka 2015 mpaka asilimia 7 mwaka 2018”.
Amesema Waziri Ummy.
Pamoja na hayo, Waziri Ummy amewataka wananchi kwa ujumla
kutimiza wajibu wao ili kutokomeza Malaria kama kauli mbiu ya mwaka huu
inavyosema “Ziro Malaria inaanza na mimi”,
hivyo amewataka wakina mama wajawazito kuhudhuria kliniki kwa ajili ya
uchunguzi wa afya zao na kufanyiwa vipimo vyote kikiwemo kipimo cha Malaria.
Waziri Ummy amebainisha kuwa Tanzania bado haijafanya vizuri
katika takwimu za akina mama wajawazito kuhudhuria kliniki ambapo katika
akinamama wajawazito 100 ni akinamama 29 ndiyo wanaohudhuria kiliniki mara nne
katika kipindi cha ujauzito.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa ambaye pia ni
Mratibu wa Malaria wa mkoa, Dkt. Francis Bujiku amesema mafanikio ya kutokomeza
Malaria katika jiji la Dodoma yamekuja baada ya utekelezaji wa afua mbalimbali za
Malaria ikiwa ni pamoja na kuhakikisha tiba sahihi za Malaria zinatolewa katika
vituo vyote vya afya, elimu ya kujikinga na ugonjwa huo, pamoja na mkoa
kufanikiwa kuangamiza viluilui wa mbu kwa kunyunyizia dawa kwenye mazalia yao.
Dkt. Bujiku amesema mwaka 2015 mkoa uliendesha zoezi la
ugawaji vyandarua vyenye dawa kwenye ngazi ya kaya, takribani vyandarua milioni
moja na laki tano viligawiwa kwa wananchi, vile vile akina mama wajawazito waliofika
kliniki kwenye hudhurio la kwanza la ujauzito na watoto chini ya mwaka mmoja
waliofika kupata chanjo ya surua walipewa vyandarua hivyo.
MWISHO