Na WAMJW-Dar es Salaam
Serikali
imepokea msaada wa shilingi bilioni 14.9 kutoka Global Fund, Airtel
Tanzania, Rotary Club Tanzania ambazo sehemu kubwa zitatumika kununua vifaa
kinga kwa watumishi wa afya na vifaa tiba kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa
wenye maambukizi ya COVID-19.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameyasema hayo leo wakati akipokea msaada wa
fedha na lita 1,250 za vitakasa mikono ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi
za Serikali za kupambana na maambukizi ya virusi vya Corona.
Waziri Ummy amefafanua kwamba Global Fund
imetoa shilingi bilioni 14, Airtel Tanzania shilingi milioni 700 na Rotary Club
Tanzania shilingi milioni 250.
“Tumepokea shilingi bilioni 14 kutoka
Global Fund, shilingi bilioni 9.6 tumezitoa kwa ajili ya kununua vifaa kinga
kwa ajili ya watumishi wa Afya, lakini pia fedha zilizotolewa na Airtel na
Rotary Club Tanzania tutazielekeza huko. Kipaumbele chetu ni kuwalinda
watumishi wa afya,” amesema Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.
“Natumia fursa hii kuwashukuru watumishi wa
afya ambao wamekuwa wakijitoa usiku na mchana katika kutoa huduma kwa watu
waliopata maambukizi ya virusi vya Corona (Covid-19) pamoja na wale wahisiwa.
"Kipaumbele cha Serikali ni kuwalinda
watumishi wa Afya kwa kununua vifaa kinga kwani fedha tulizozipata hapa
tutazielekeza kwenye ununuzi wa vifaa kinga.
Niendelee kuwaisistiza Watumishi wa Afya wazingatie miongozo ya magonjwa
ya kuambukiza,” Amesema Waziri Ummy .
Amesema watumishi wa afya ambao wamepatiwa
mafunzo katika vituo vya kutoa huduma kwa wenyr maambukizi ya ugonjwa huo,
hakuna aliyepata maambukizi kwa kuwa wanazingatia miongozo ya Serikali
ya kutoa matibabu kwa wagonjwa wa Covid-19 pamoja na miongozo ya magonjwa ya
kuambukiza.
Waziri amesema ushiriki wa kila mdau katika
mapambano dhidi ya maambikizi ya virusi vya Corona ni muhimu na kwamba msaada
uliotolewa na kampuni hizo ni mkubwa katika mapambano ya maambukizi ya ugonjwa
wa Corona.
“Napenda kurudia tena kwa niaba Mhe. Rais
Dkt. John Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, nawashukuru Airtel Tanzania,
Serengenti Breweries na Rotary Club kwa hiki mlichotupatia. Asanteni sana,”
amesema Waziri Ummy.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya
Airtel Tanzania, Bw. Gabriel Malata amesema Airtel Tanzania imetoa shilingi
milioni 700 ikiwa ni sehemu ya kuunga
mkono juhudi za Serikali za kupambana na janga la Corona.
“Sisi bodi ya wakurugenzi wa Airtel na kwa
niaba ya Airtel Tanzania, tunatambua juhudi za Serikali katika kupambana na
ugonjwa wa Corona, lakini pia tumejitathimini na kutambua kuwa sisi kama
Airtel
hatuwezi kuendelea bila kuwepo watu wanaotumia huduma zetu. Watu hawa ndio
mtaji wa Kampuni,” amesema Bw. Gabriel.
Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kampuni ya Bia ya
Serengenti, Bw. John Wanyancha amesema kuwa kampuni hiyo imetoa lita 1,250 ya
vitakasa mikono nyenye thamani ya shilingi milioni 15 kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali
za kupambana na maambukiza ya virusi.
Mwenyekiti wa Rotary Club, Bi. Agnes
Batenga amesema Rotary imetoa shilingi milioni 250 kwa ajili ya kupambana na
ugonjwa wa homa ya mapafu (COVID-19).
“Shilingi milioni 183 zitatumika kutoa
msaada wa vifaa vya kujikinga (PPE), vifaa vya maji safi ambavyo vitasambazwa
katika vituo maalumu vya kuhudumia wagonjwa wa Corona jijini Dar es Salaam,
Hospitali ya Amana, Zanzibar, Hospitali ya Mawenzi na Hospitali ya Mount Meru,”
amesema Bi. Agnes.
Amesema shilingi milioni 67 zitatumika
katika kutekeleza miradi ya kudhibiti ugonjwa wa Corona nchini kupitia Club za
Rotary.
0 on: "SERIKALI YAPOKEA MSAADA WA SHILINGI BILIONI 14.9"