Baadhi ya Wabunge wakiwa kwenye magari ya majimbo yao waliyotolewa na Wizara ya Afya na kukabidhiwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa. |
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi funguo za Magari ya kubebea wagonjwa Mbunge wa Urambo Bi. Magreth Sitta kwa niaba ya wabunge wengine. |
Na WAJMW-Dodoma
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ametangaza ongezeko la
wagonjwa wa Corona 196 nchini huku Tanzania Bara ikiwa na Wagonjwa 174 na
Zanzibar wagonjwa 22 ambao walitolewa taarifa na Waziri wa Afya Wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Hamad Rashid na kufanya idadi ya wagonjwa wa Corona
nchini kufikia 480.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema hayo wakati akigawa magari 50 ya
kubebea wagonjwa kwa wabunge wa majimbo mbalimbali tukio lililofanyika leo
katika ofisi ya Waziri Mkuu iliyopo Mlimwa jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema jumla ya wagonjwa waliopona imeongezeka
kutoka 48 hadi kufikia 197, huku Zanzibar waliopona wakiwa 36 na Tanzania bara
83. Pia Waziri Mkuu amesema kumekuwa na ongezeko la vifo vya watu sita (6) na
kufanya kuwa na vifo vilivyotoka na Corona nchini kufikia 16.
Kati ya wenye maambukizi 297 waliobaki, 283 wanaendelea
vizuri na tiba na kusubiri ufuatiliaji wa afya zao na wengine 14 wako chini ya uangalizi
maalumu wa madaktari ambao wanahitaji oksjeni
(Oxygen) ya kuwasaidia kupumua pamoja na wale wenye magonjwa mengine
ambayo yamejitokeza kwenye wodi.
Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuwaondoa washukiwa
waliokua karantini ambao walishatimiza siku 14 baada ya uchunguzi wa kiafya
kuonekana hawana maambukizi na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Hadi kufikia jana tarehe 28 Aprili, watu 644 wameruhusiwa
kutoka karantini katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Zanzibar, Kilimanjaro,
Mwanza, kagera, Songwe, Kigoma na Dodoma.
Hata hivyo Waziri Mkuu amekemea tabia ya upotoshaji na
utoaji wa takwimu ambazo sio rasmi na kuzua taharuki kwa jamii kwamba kila kifo
kimetokana na Corona kuwa sio sahihi na kusisitiza kuwa kuna magonjwa mengine ambayo
yanaua pia.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka wananchi kuendelea kuchukua
tahadhari zote zinazotolewa na wataalamu wa afya huku Serikali ikiendelea kuchukua
hatua mbalimbali za kuweza kupambana na vita hii ya ugonjwa wa Corona.
Katika makabidhiano hayo ya magari, Waziri wa Afya Mhe. Ummy
Mwalimu amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa magari 50 nchiniyenye Tsh. Bilioni 6
ili yaweze kuwezesha rufaa za akinamama Wajawazito na kuepusha vifo vitokanavyo
na uzazi pamoja na kukabiliana na magonjwa ya milipuko kama Corona.
Magari 18 yamepekwa katika Hospitali za Rufaa za Mikoa,
magari 32 yatatumika kwa ajili ya vituo vya afya na Hospitali za Wilaya.
Aidha, Waziri Ummy amemshukuru Waziri Mkuu kwa kutoa
ushirikiano mkubwa unaoutoa kwa Wizara ya Afya kwa kuwezesha mambo mbalimbali lengo
likiwa ni kufikisha huduma bora za afya kwa wananchi wote.
0 on: "WAGONJWA WAPYA WA CORONA 196 WAONGEZEKA NCHINI"