Picha ya pamoja ya Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Prof. Abel Makubi akiwa na Maofisa Habari na Mahusiano kutoka Wizara ya Afya na Taasisi zake ambao wapo mkoani Mwanza kujionea hali ya maboresho ya hospitali hiyo.
Na.Catherine Sungura, Mwanza
Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando imefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni tatu kwa mwezi baada ya kuimarisha mfumo wa makusanyo wa kieletroniki katika utoaji huduma.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo Prof. Abel Makubi wakati akielezea mafanikio ya hospitali hiyo kwa maofisa habari wa Wizara ya Afya na Taasisi zake waliotembelea hospitali hiyo kujionea maboresho ya sekta ya afya katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Prof.Makubi alisema kuwa baada ya kuimarisha mfumo huo hospitali hiyo imeweza kukusanya kiasi hicho cha fedha tofauti na awali ambapo walikua wakikusanya shilingi milioni mia nane kwa mwezi.
“Licha ya makusanyo haya mfumo huu pia umesaidia kurahisisha utoaji wa huduma kwa wepesi na kwa haraka kwani zamani kulikuwa na upotevu wa mafaili na hivyo kuleta malalamiko kwa wagonjwa”. Alisema Prof.Makubi.
Kwa upande kwa huduma za kibingwa na bobezi mkurugenzi huyo alisema kuwa baada ya Serikali kushusha huduma za kibingwa kwenye hospitali za rufaa za kanda hospitali hiyo imefanikiwa kununua mashine kadhaa za uchunguzi wa magonjwa ikiwemo CT- SCAN ya kisasa, kwa mapato ya ndani yenye thamani ya shilingi bilioni 1.7 na hivyo kuweza kuwaondolea adha wakazi wa mwanza na majirani zake.
“Pia tumeboresha huduma za maabara kwa kununua vifaa vya kisasa zaidi ya nane kwa ajili ya kupima magonjwa mbalimbali kwa muda wa masaa matatu kutoka masaa 12 yaliyokuwa yakitumika kutokana na vifaa vya zamani na hivyo imeleta faraja kwa wagonjwa kuongezeka kupata huduma hospitalini hapa tofauti na nyuma ambapo vipimo vingi walikua wanavipata nje ya hospitali yetu”. Alisema Mkurugenzi huyo.
Hata hivyo Prof. Makubi alisema katika kuboresha miundombinu wameweza kujenga jengo zuri lenye huduma zote za madaktari bingwa ambapo wanapokea wagonjwa 350 kwa siku wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Taifa (NHIF) ambalo limegharimu shilingi milioni 800 walizowezeshwa na NHIF na tangu mwaka 2017 wamefanikiwa kumaliza kulipa mkopo huo.
Prof.Makubi ameipongeza Wizara ya Afya pamoja na NHIF kuhamasisha wananchi kukata bima ya afya na hivyo kuongeza watumiaji wa bima hiyo kwa asilimia 70 tofauti na awali ambapo walikuwa wakipata wanachama hao kwa asilimia 30 hadi 40.
-Mwisho-
|
0 on: "BUGANDO YAKUSANYA ZAIDI YA BILIONI TATU KWA MWEZI"