Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Ziwa, Bugando Prof. Abel Makubi akifafanua jambo kwa Maofisa Habari wa Wizara ya Afya na Taasisi zake (hawapo pichani) walipotembelea Hospitali hiyo.
Mfamasia Fransisco Chibunda akiweka majitiba kwenye chupa maalum tayari kwa matumizi.
Majitiba ambayo tayari yameshatengenezwa katika Kitengo cha Kuzalisha Majitiba katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa, Bugando tayari kwa matumizi.
Na.Catherine Sungura-Mwanza
Katika kutekeleza kauli mbiu ya Serikali ya awamu ya tano ya Tanzania ya viwanda,hospitali ya rufaa ya kanda Bugando (BMC) imefanikiwa kufufua viwanda viwili kwa ajili ya mahitaji ya hospitali za kanda ya ziwa
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu Prof. Abel Makubi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando(BMC) mwishoni mwa wiki jijini hapa.
Prof. Makubi alisema kuwa katika kutimiza hayo wamefanikiwa kufufua viwanda ambavyo vilikua vinaelekea kufa.
Alitaja viwanda hivyo ni pamoja na kiwanda cha kuzalisha oksijeni na kingine ni cha kuzalisha maji tiba ya wagonjwa katika chupa mchanganyiko.
"Mahitaji ya oksijeni kwa hospitali yetu ni mitungi 4000 ila hivi sasa tunazalisha zaidi ya mitungi 2000 na lengo letu ni kuzalisha mitungi 5100.
Aidha, Prof. Makubi alisema kuwa wamepanga kuzalisha mitungi mingi zaidi ili kuweza kuhudumia hospitali nyingine za kanda ya ziwa kwa bei nafuu na ya nusu bei.
Kwa upande wa kiwanda cha kuzalisha maji tiba ya wagonjwa mkurugenzi huyo alisema "tumefanikiwa kuzalisha maji tiba ya wagonjwa katika chupa mchanganyiko na za kutosha kwa wastani tunazalisha chupa 6000 kwa mwezi na hivyo kuokoa pesa ambazo zingetumika kununua nje".
Hata hivyo Prof. Makubi alisema wanahitaji kiasi cha shilingi bilioni tano ili waweze kuzalisha maji tiba hayo ya kutosheleza kanda yote ya ziwa na hivyo kusaidia hospitali zingine kutonunua maji ya wagonjwa kutoka nchi za jirani.
Naye Mkuu wa kitengo cha kuzalisha maji tiba Mfamasia Fransisco Chibunda alisema kwa sasa upatikanaji wa dawa hospitalini hapo ni asilimia 96 ukilinganisha na asilimia 60 ya nyuma.
"Katika kiwanda cha maji tiba tunazalisha aina 17 za dawa,kati ya hizo aina tisa hazipatikani kabisa kwenye soko letu".Alisema Chibunda
Chibunda alisema katika kuwahudumia wagonjwa kwa wakati wamepanua vituo nane vya kutolea dawa kutoka vituo vinne na kituo kimoja kinahudumia kwa masaa 24.
Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando inayo wafamasia wabobezi katika kuzalisha madawa ya aina mbalimbali.
0 on: "HOSPITALI YA BUGANDO YAFUFUA VIWANDA VYA OKSIJENI NA MAJI TIBA"