Na WAJMW-MWANZA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula amezidi
kusisitiza mahusiano bora baina ya watumishi walio katika sekta ya afya katika
maeneo yao ya kazi na kuwataka kuongeza mapato ili yaweze kuendesha Hospitali
na vituo vya afya pamoja na kuboresha hali za watumishi kwa ujumla.
Dkt. Chaula amesema hayo wakati akiendelea na ziara yake
katika mikoa ya kanda ya ziwa baada ya leo kutembelea Hospitali ya Wilaya ya
Misungwi Jijini Mwanza na kuona hali ya ujenzi wa jengo la huduma za uzazi na kuonekana
kuridhishwa na ujenzi huo kisha kuongea na watumishi.
Katibu Mkuu huyo amesema lengo la kutembelea maeneo ya utoaji
wa huduma za afya kanda ya ziwa ni pamoja na kuona maendeleo ya utoaji huduma
na kuongea na watumishi ili kubaini maendeleo na kupata changamoto zinazowakabili
na kuona namna gani ya kuzitatua.
Pamoja na yote yaliyozungumzwa Dkt. Chaula amewaomba
watumishi hao kupendana na kufanya kazi kwa moyo ili kuwahudumia wagonjwa
wanaofika kupata huduma huku akiwataka kuongeza mapato na kuweza kujilipa
motisha kutokana na ufanyaji kazi wao.
Kabla ya hapo Dkt.
Chaula alitembelea kituo cha afya cha Buzuruga na kushirikiana na Mkuu wa Mkoa
wa Mwanza John Mongella katika uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya chanjo za
Surua na Ribella kwa watoto wadogo nchini iliyozinduliwa kitaifa Mkoani
Morogoro na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.
Ummy Mwalimu.
Badae Dkt. Chaula akiongozana na Wakurugenzi na viongozi
waandamizi kutoka wizara ya afya na ofisi ya Rais TAMISEMI alitembelea ujenzi
wa Hospitali mpya ya Wilaya ya Ilemela na kituo cha matibabu ya magonjwa ya
hatari na milipuko (Isolation Highly Infectious Unit) cha Buswelu.
MWISHO
0 on: "DKT. CHAULA ATAKA MAHUSIANO BORA KWA WATUMISHI WA SEKTA YA AFYA"