Wizara Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekuwa ikitoa taarifa kwa wananchi mara kwa mara kuhusiana na mwenendo wa magonjwa ikiwemo magonjwa ya milipuko (epidemic diseases) nchini na hatua zinazochukuliwa kuzuia na kudhibiti magonjwa haya.
Magonjwa yanayofuatiliwa kwa karibu na kutolewa taarifa mara moja pindi yakitokea ni, kumi na nne (14) ambayo ni pamoja na Kipindupindu, Polio, Kimeta, Kuhara Damu, Homa ya Uti wa Mgongo, Mafua makali ya ndege, Surua, Pepopunda ya watoto wachanga, Kichaa cha Mbwa, Ndui, Magonjwa yanayosababishwa na Virusi na Homa yanayosababisha damu kuvuja (Ebola, Marburg, RVF, Homa ya Dengue, Chikungunya), Macho mekundu, Tauni, na Homa ya Virusi ya Manjano.
Utoaji wa taarifa za magonjwa haya zimerahisishwa, ambapo vituo vyote vya kutoa huduma za Afya nchini kuanzia ngazi ya chini hutoa taarifa hizi kwa kupitia mfumo maalum kwa njia ya simu (Integrated Disease Surveillance and Response - IDSR). Hii hupelekea taarifa zote muhimu kuhusu magonjwa kupatikana kwa haraka na hatua kuchukulia mapema na wizara ili kudhibiti magonjwa haya.
Kwa kipindi cha mwezi Septemba 2019, Wizara imeendelea kufuatilia magonjwa haya na matukio hatarishi kwa afya, kutoka kwenye mikoa yote nchini. Katika mwezi Septemba, ugonjwa wa Dengue na Surua tu ndio magonjwa ya milipuko yaliyotokea hapa nchini.
Mwenendo wa Homa ya Dengue nchini.
Kwa Kipindi cha mwezi Septemba 2019, jumla ya wagonjwa 10 walithibishwa kuwa na Homa ya Dengue na hakukuwa na kifo. Wagonjwa hawa walitolewa taarifa kutoka mikoa 2 ambayo ni Dar es salaam – wagonjwa 4 (Hospitali ya Taifa Muhimbili - 4) na Tanga – wagonjwa 6 (Tanga jiji - 6).
Ugonjwa huu umeendelea kudhibitiwa kwa kiasi kikubwa nchini na umeendelea kupungua mwezi hadi mwezi. Takwimu za miezi mitatu (Julai, Agosti na Septemba, 2019) zimeonyesha kupungua kwa ugonjwa huu kwa kiasi kikubwa ambapo mwezi Julai 2019 kulikuwa na wagonjwa waliothibishwa 732, mwezi Agosti wagonjwa 92 na mwezi Septemba wagonjwa - 10.
Aidha tangu mlipuko huu uanze mwezi Januari 2019 hadi kufikia tarehe 30 Septemba, 2019 kumekuwa na jumla ya wagonjwa waliohisiwa kuwa na Dengue 14,369 na kati yao waliothibishwa ni 6,785 na vifo 13 (Dar-6259, Tanga-365, Pwani-115, Morogoro-22, Lindi-8, Arusha-5, Singida-3, Dodoma-3, Ruvuma-2, Kagera-2 na Kilimanjaro-1).
Ili kukabiliana na magonjwa yaenezwayo na wadudu dhurifu wakiwemo mbu, Wizara ilizindua mpango mkakati wa kukabiliana na wadudu dhurifu na mbu (National Vector control strategy 2019 - 2023) tarehe 27 Julai 2019, Dar es Salaam. Uzinduzi huu uliambatana na uzinduzi wa kitaifa wa zoezi la upuliziaji wa dawa kupambana na mbu wapevu na unyunyiziaji wa dawa za kuua viluwiluwi wa mbu waenezao magonjwa kama vile Malaria, Dengue na nk,. Dawa za kuangamiza wadudu zilinunuliwa pamoja na mashine kubwa (4) za kupulizia dawa (Fogging Machine) ambazo zilisambazwa katika mikoa iliyoathirika na ugonjwa wa Dengue yaani Dar es Salaam, Tanga pamoja na Dodoma. Wizara imeshaagiza mashine nyingine 4 ili kuweka mkakati endelevu wa zoezi hili.
Mikoa hii pia (Dar es salaam, Dodoma, Tanga) ilishafanya uzinduzi wa Mkakati wa Kudhibiti Mbu na Wadudu wadhurifu pamoja na kuendesha zoezi la kuangamiza mbu. Hatua hii imesaidia kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa Dengue nchini kama inavyoonyeshwa katika takwimu.
Aidha, zoezi hili la uzinduzi linaendelea kufanyika katika Mikoa yote ili kutokomeza magonjwa yaenezwayo na wadudu hao. Elimu endelevu pia inaendelea kutolewa kwa wananchi juu ya namna kujikinga na kudhibiti ugonjwa huu
Mwenendo wa Ugonjwa wa Kipindupindu nchini.
Ugonjwa wa Kipindupindu umedhibitiwa, na kwa sasa HATUNA KABISA mgonjwa wa Kipindupindu nchini. Mara ya mwisho kupata mgonjwa wa Kipindupindu nchini ilikuwa tarehe 14 mwezi Julai 2019.
Kwa kipindi cha kuanzia tarehe 1 Januari hadi Julai 2019, kulikuwa na jumla ya wagonjwa 424 na vifo 8 vya ugonjwa wa Kipindupindu. Wizara inaendelea kuchukua hatua za kudhibiti ugonjwa huu, ikiwa ni pamoja kufuatilia hatua zinazochukuliwa za kuzuia ugonjwa huu na timu ya Mkoa na Halmashauri ambazo ni pamoja na; Kutoa elimu ya afya kwa wananchi ya namna kujikinga kupata ugonjwa huu, Ufuatiliaji wa usafi wa mazingira.
Wizara inakamilisha Mpango Mkakati wa Kipindupindu wa mwaka 2019 hadi 2023 ambao utekelezaji wake utajikita katika maeneo yanayotoa wagonjwa mara kwa mara (Hotspot areas) ambayo ni Dar es Salaam (Halmashauri zote), Ngorongoro (Arusha), Simanjiro (Manyara), Handeni na Mkinga (Tanga), Kilwa (Lindi), Ulanga (Morogoro), Mbarali na Chunya (Mbeya), Songwe, Sumbawanga DC (Rukwa), Mpanda (Katavi), Nyasa (Ruvuma) na Iringa DC (Iringa).
Mpango huu, unalenga kutokomeza Kipindupindu kabisa. Katika mpango huu maeneo yalijikita ni pamoja na: Uratibu na ushirikishwaji wa wadau katika ngazi zote katika kudhibiti ugonjwa, kuimarisha ufuatiliaji na upimaji wa wagonjwa, Kuimarisha utoaji wa matibabu sahihi na mapema kwa wagonjwa, ushirikishwaji wa jamii katika kudhibiti na ugonjwa, kuweka mazingira ya kuwepo kwa maji safi na salama na masuala ya matumizi ya vyoo na vilevile kuimarisha utoaji wa chanjo kwa maeneo sugu na vigezo vitakavyotumika.
Wizara imeendelea pia na utekelezaji wa Kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira yenye kaulimbiu isemayo “USICHUKULIE POA NYUMBA NI CHOO”, ikiwa ni moja ya mikakati ya kutokomeza Kipindupindu na magonjwa ya kuhara. Kampeni hii ambayo ipo katika awamu ya pili, ilizinduliwa rasmi Disemba, 2017 na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Uanzishwaji wa Kampeni hii ni sehemu ya jitihada za serikali kujielekeza katika kutekeleza lengo namba 6.2 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (Sustainable Development Goals) pamoja na lengo namba 3 linahusu kuboresha Afya. Katika kipindi cha miaka mitatu ya utekelezaji (2016-2019), jumla ya kaya 2,464,225 zimejenga au kuboresha vyoo kufikia kiwango cha ubora kati ya lengo la kaya 3,360,000. Hii ni sawa na asilimia 73.3. Kwa upande wa taasisi, shule 1,670 kati ya lengo la shule 2,520 zimejenga vyoo bora kwa kuzingatia uwiano.
Kwa ujumla kaya zenye vyoo bora katika ngazi ya kaya zimeongezeka kutoka asilimia 46 Julai, 2016 hadi asilimia 57.2 Juni, 2019, na kaya zisizokuwa na vyoo zimepungua kutoka asilimia 7.5 hadi asilimia 2.5 katika kipindi hicho.
Mwenendo wa Ugonjwa wa Surua nchni.
Katika kipindi cha mwezi Septemba 2019, mlipuko wa ugonjwa Surua ulitokea katika kitongoji cha Kashasha, Kakoma na kijiji cha Kibare wilayani Kyerwa mkoa wa Kagera. Jumla ya wagonjwa 17 walipatikana na ugonjwa wa surua ambapo kati yao; wagonjwa saba walithibitishwa kwa kipimo cha maabara. Mgonjwa wa mwisho kupatwa na dalili za surua katika eneo la Kibare ilikuwa tarehe 14/09/2019.
Kwa takribani wiki mbili sasa hakuna mgonjwa mwingine aliyepatikana. Wagonjwa wote wamepona na elimu ya jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa surua imetolewa na pia kuhamasisha kuwaleta watoto katika kampeni ya kitaifa shirikishi ya chanjo ya surua na rubella, watoto wote chini ya miaka mitano.
Katika ufuatiliaji wa ugonjwa surua nchini wagonjwa wenye dalili za homa na vipele hufuatiliwa na kuchukuliwa sampuli kupima kubaini kama wana ugonjwa wa surua. Kwa kipindi cha mwezi Septemba 2019, jumla ya sampuli 222 za wagonjwa waliokuwa na dalili ya homa na vipele zilipokelewa na kufangashwa na kuwasishwa maabara ya Taifa kutoka kwenye mikoa 23 ya Tanzania bara.
Mwenendo wa Ugonjwa wa Polio nchini.
Hadi sasa hakuna mgonjwa wa Polio aliyethibika hapa nchini tangu mwaka 1996. Hii inatokana na jitihada kubwa za Serikali katika kutoa chanjo na kufuatilia dalili za wagonjwa wenye ugonjwa huu na pia kwa kununua chanjo za Polio ambazo zimeweza kuwafikia watoto wote chini ya miaka mitano (5) kwa zaidi ya asilimia 90%.
Katika ufuatiliaji wa ugonjwa huu, wagonjwa wote wa dalili za kupooza ghafla (Acute Flaccid Paralysis - AFP) hufuatiliwa na sampuli kuchukuliwa na kupimwa kujua kama wana ugonjwa wa Polio. Kwa mwezi Septemba 2019, jumla ya sampuli 63 za AFP 63 zilifungashwa na kupelekwa maabara kwa ajili ya vipimo. Aidha katika ufuatiliaji wa virusi vya polio katika mazingira, ambapo kirusi hiki pia hukaa kwa muda nao unaendelea na hadi sasa kirusi hiki kimeonekana kuwa hakipo katika mazingira yetu. Ufuatiliaji wa mara kwa mara unaendelea. .
Katika mpango wa kutokomeza vifo na ulemavu kutokana na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo. Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo na kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais - TAMISEMI, itaendesha kampeni ya chanjo dhidi ya Magonjwa ya Surua, Rubella na Polio mnamo tarehe 17 hadi 21 mwezi Octoba 2019. Kampeni hii itafanyika nchi nzima kwa watoto wote lengwa walio na umri wa chini ya miaka mitano. Nawasihi wananchi wote washiriki ili Serikali ifikie lengo la kampeni hii.
Mwenendo wa Ugonjwa wa Ebola unaoendelea kuripotiwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)
Wizara imekuwa ikifuatilia kwa karibu mwenendo wa ugonjwa wa Ebola unaoendelea kuripotiwa nchini DRC na kuchukua hatua za tahadhari za kuzuia na kukabiliana na ugonjwa huu hususani kwa kuwa kwa sasa ugonjwa huu unaendelea kusambaa na kuingia kusini mwa DRC. Takwimu zinaonyesha kuwa hadi kufikia tarehe 30 Septemba 2019, jumla ya wagonjwa 3,194 walithibitishwa kuwa na ugonjwa huu, na vifo 2133 (CFR 66.8%). Kutokana na ukaribu wa nchi hii na Tanzania, Wizara imeendelea kuchukua hatua za utayari kuzuia na kujiandaa kukabiliana na ugonjwa huu
Hatua za utayari na kujiandaa kukabiliana na ugonjwa huu nchini ni pamoja na kuimarisha uchunguzi wa Wasafiri kwenye mipaka yetu yote. Kuimarisha utambuzi katika ngazi ya vituo vya kutolea huduma za Afya; Kuhakikisha uwepo vya Vifaa Kinga hususani kwa watumishi wa Afya; Kuimarisha utambuzi wa Ugonjwa na kuendelea kutoa Elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga ugonjwa huu.
Wizara inayo namba ambayo hutumika bila malipo na wananchi kutoa taarifa za kuwepo kwa tetesi za ugonjwa huu ambazo ni 0800110124 au 0800110125. Kuanzia 2018 hadi sasa, tetesi 28 za wagonjwa wanaohisiwa kuwa na Ebola (washukiwa 2 kwa mwezi Septemba), zimekwisha kutolewa taarifa na uchunguzi kufanyika kwa ukamilifu na kuthibitisha wagonjwa hawa hawakuwa na Ebola, na taarifa zake kupelekwa pia katika Shirika la Afya Duniani. Aidha Wizara imeendelea kufanya pia mazoezi ya kujinoa na kijipima utayari wa kukabiliana na ugonjwa huu (Simulation Exercises) katika mikoa ya Dar es Salaam, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro na Arusha.
NAPENDA KUSISITIZA KUWA HADI SASA HAKUNA MGONJWA ALIYETHIBITISHWA KUWA NA UGONJWA WA EBOLA HAPA NCHINI. WIZARA INAWASIHI WANANCHI KUTOKUWA NA HOFU NA KUPUUZA TAARIFA ZINAZOTOLEWA KILA KUKICHA NA BAADHI YA VYOMBO VYA HABARI NA MITANDAO YA KIJAMII.
Katika kudhibiti ugonjwa wa Ebola na magonjwa mengine ya milipuko yenye madhara makubwa duniani, nchi yetu kila wakati imekuwa mstari wa mbele ikiwa ni pamoja na kusimamia kwa ukamilifu na kutekeleza Kanuni za Kimataifa za Afya (International Health Regulation - IHR 2005). Mnamo mwaka 2016, Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza duniani kuweza kukubali bila kipingamizi kuleta wataalam duniani kuja kupima utayari wa nchi yetu katika kukabiliana na magonjwa haya hatarishi (Joint external evaluation). Hatua hii kubwa na ya uwazi ilifanywa kwa mara ya kwanza Duniani, kama moja ya njia ya kuhakikisha nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani, wanatekeleza Kanuni hizi za Kimataifa (IHR 2005). Aidha nchi nyingine zenye uwezo mkubwa duniani zilisita kufanyiwa tathmini hadi miaka miwili baadae, na nyingine hadi sasa hazijafanya zoezi hili. Hivyo basi, taarifa zinazoenea kuelezea kuhusu Tanzania kutokuweka wazi taarifa za magonjwa hususan uwepo wa ugonjwa wa Ebola nchini, si za kweli na hivyo ziendelee kupuuzwa. Taratibu za utoaji wa taarifa za magonjwa ya milipuko zinajulikana na ninatoa rai kwa sote tuzingatie sheria na taratibu za nchi husika na za kimataifa.
Ikumbukwe kuwa, ugonjwa wa Ebola ambao unaweza kusambaa kwa haraka, na ambao madhara yake ni makubwa na yanajulikana duniani kote, kamwe hauwezi kufichwa na nchi yetu. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua madhara makubwa ya kuficha ugonjwa kama huu kwa wananchi. Narudia tena na kuwataka wananchi kutulia na kupuuza taarifa zisizo rasmi kutoka kwenye baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, maana HAKUNA UGONJWA WA EBOLA NCHINI TANZANIA. Inaonekana kuna njama ovu za kueneza taarifa hasi dhidi ya nchi yetu. Ninaendelea kuwasihi Wananchi kuwa watulivu na kushikamana kwa pamoja katika kuzuia ugonjwa huu usiiingie nchini.
Aidha, Serikali inapenda kuwahakikishia Mataifa yote kuwa nchi yetu ni SALAMA na HATUNA UGONJWA WA EBOLA. Nirudie tena kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na nchi na mashirika mbalimbali ya kimataifa ikiwemo Shirika la Afya Duniani katika kujenga utayari wa kukabiliana na tishio la ugonjwa wa Ebola. Na endapo kutatokea mtu atakaethibishwa kuwa na ugonjwa wa Ebola nchini tutaendelea kuzingatia miongozo na taratibu za kimataifa ikiwemo kutoa Taarifa WHO kwa mujibu wa Kanuni za Kimataifa za udhibiti wa magonjwa hatari ya kuambukiza (IHR 2005).
Kipaumbele cha Wizara kwa sasa ni kuendelea kuimarisha utayari wa kukabiliana na ugonjwa huu usiingie nchini na endapo kutatokea kisa cha ugonjwa huu nchini tuweze kukabiliana nao na kuudhibiti mara moja.
Asanteni sana
0 on: "TAARIFA KUHUSU MWENENDO WA MAGONJWA YA MILIPUKO NCHINI KWA MWEZI SEPTEMBA NA HATUA ZINAZOCHUKULIWA NA SERIKALI KUZUIA NA KUDHIBITI MAGONJWA"