Mkurugenzi wa Huduma za Tiba katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),
Dkt. Hedwiga Swai (wa kati kati) akizungumza na maafisa mawasiliano kutoka Wizara ya
afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na taasisi
zilizo chini ya wizara hiyo kuhusu maboresho yaliofanywa na MNH. Kushoto
ni Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa MNH, Dkt.Sufiani Baruani na uapnde wa kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Shirikishi, Dkt. Praxeda Ogweyo.
Na Mwandishi Wetu - Dar Es Salaam
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeanza kutoa tiba ya awali ya saratani ya damu kwa wagonjwa wenye tatizo hilo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Muhimbili, Dkt.
Hedwiga Swai wakati akizungumza na maafisa mawasiliano kutoka Wizara ya
afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na taasisi
zilizo chini ya wizara hiyo wakati walipoitembelea hospitali kwa lengo
la kujionea maboresho mbalimbali yaliofanywa kwenye kampeni ijulikano kwa jina la Tumeboresha Sekta ya afya.
Katika kuhakikisha huduma hiyo inatekelezwa kwa ufanisi, Serikali
imetoa shilingi bilioni 6.2 kwa ajili ya kuanzisha huduma ya kupandikiza
uloto (Bone Marrow Transplant).
“Ukarabati wa miundombinu tayari umekamilika huko Hospitali ya Taifa
Muhimbili-Mloganzila, ununuzi wa vifaa tiba umekamilika kwa asilimia 90,
huku wataalamu mbalimbali wakiwa wameshasomeshwa nje ya nchi na wako
tayari kuanza kutoa tiba hii,” amesema Dkt. Swai
Dkt. Swai amesema gharama ya mtu mmoja kupandikizwa uloto nje ya nchi
ni kati ya shilingi milioni 150 hadi 200 wakati hapa nchini gharama
itakuwa shilingi milioni 50 tu.
Kuhusu huduma bobezi zinazotolewa MNH, ikiwamo upandikizaji figo,
Dkt. Swai amesema wataalamu wa usingizi, wauguzi, wataalamu wa radioloji
hivi sasa wanaweza kutoa huduma wenyewe kwa asilimia 100 wakati
wataalamu wa upasuaji wanatoa huduma ya upasuaji kwa asilimia 100 kwa
mgonjwa anayechangia figo na kwa anayepandikizwa kwa asilimia 95.
Naye, Mkurugenzi wa huduma za upasuaji MNH, Dkt. Sufiani Baruani
amesema MNH imenunua vifaa mbalimbali vya kisasa kwa ajili ya
kufanikisha upasuaji kwa njia ya tundu dogo yenye dhamani ya shilingi
milioni 800 pamoja na mashine ya kisasa ya ultrasound kwa ajili ya
upimaji wa tezi dume.
Akizungumzia mafanikio ya Idara ya Maabara, Mkurugenzi wa Tiba
Shirikishi Dkt. Praxeda Ogweyo amesema maabara ya Muhimbili imekidhi
viwango vya kimataifa na kupata ithibati ya ISO:15189:2012.
Amesema Huduma zinazotolewa katika maabara hii ni ufanyikaji wa
sampuli zote za magonjwa yanayohusiana himatolojia, kemia uhai,
parasaitolojia, mikrobiolojia, huduma za uchagishaji na upatikanaji wa
damu salama pamoja na histopatholojia.
0 on: "TIBA YA SARATANI YA DAMU YAANZA KUTOLEWA MUHIMBILI"