Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndungulile akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi kizimia moto kilichotolewa na kampuni ya SUKOS KOVA Foundation kwa kushirikiana na kampuni ya One Extreme Solution leo katika ukumbi wa taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam. Jumla ya vizimia moto 12 vya kisasa vimefungwa katika maeneo mbalimbali ya taasisi hiyo.
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndungulile akizungumza na mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa ziara yake kutembelea taasisi hiyo pamoja na kupokea vizimia moto vilivyotolewa na kampuni ya SUKOS KOVA Foundation kwa kushirikiana na kampuni ya One Extreme Solution leo Jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndungulile akizungumza na mtoto aliyelazwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya moyo Asha Luhomo wakati wa ziara yake kutembelea taasisi hiyo pamoja na kupokea vizimia moto vilivyotolewa na kampuni ya SUKOS KOVA Foundation kwa kushirikiana na kampuni ya One Extreme Solution leo Jijini Dar es Salaam
Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Polisi na Mkurugenzi wa Kampuni ya SUKOS KOVA Foundation Suleiman Kova akimkabidhi Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndungulile moja kati ya vizimia moto 12 vilivyotolewa na kampuni yake kwa kushirikiana na kampuni ya One Extreme Solution kwa ajili ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo katika ukumbi wa Taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi
Na.WAMJW,Dsm
Asilimia tisini ya wagonjwa wanaokabiliwa na matatizo ya moyo waliokuwa wanatibiwa nje ya nchi, hivi sasa wanatibiwa ndani ya nchi kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya kikwete (JKCI).
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile, alipofanya ziara kwenye hospitali hiyo ambapo alitembelea jengo la watoto lililofanyiwa ukarabati hivi karibuni.
Dkt.Ndugulile alisema Serikali inaendelea kufanya maboresho ya sekta ya afya kuanzia huduma za msingi hadi za kibingwa kwa kuwezesha vituo zaidi ya 352 kutoa huduma za upasuaji wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni.
Alisema hivi sasa ujenzi wa hospitali 67 za wilaya unaendelea katika maeneo mbalimbali nchini na kwamba tangu Uhuru kumekuwako na hospitali 70 za Wilaya pekee, hivyo idadi itaongezeka.
“Nawapongeza sana JKCI kwa maboresho makubwa mliyofanya katika jengo ya watoto ni ya kiwango kikubwa sana, hongereni sana, hivyo hatutarajii hospitali kama hii iwe inatibu magonjwa madogo madogo ambayo yanaweza kutibiwa kwenye hospitali za rufaa za wilaya au mikoa,” alisema.
Aliongeza kusema kuwa, katika miaka minne ya uongozi, serikali imeweza kupiga hatua kubwa kwani ikiwamo kupunguza idadi ya wagonjwa wengi walikua wanatibiwa nje ya nchi.
“Kwa hatua hii, tumeweza kupunguza gharama za matibabu nje ya nchi tulikuwa tunaweza kuhudumia watu wachache lakini kwa kuwa yanapatikana ndani wananufaika watu wengi, kwa gharama ile ile nje ya nchi angetibiwa mtu mmoja, ndani wanatibiwa watu wapatao watatu,” alibainisha.
Alisema mafanikio hayo ni matokeo ya hatua za kuwajengea uwezo kwa kuwapatia mafunzo madaktari wa ndani (wazalendo) ambapo sasa wanaweza kufanya upasuaji mkubwa wao wenyewe.
“Hivyo, Serikali itaendelea kuwapatia mafunzo wataalam wa afya na kuwapatia vibali kwenda kujifunza ama kusoma nje ya nchi ili kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya afya nchini na kuweza kuwatibia wananchi.
Aidha, katika ziara hiyo Dkt. Ndugulile alipokea vifaa vya kuzima moto vipatavyo kumi na mbili vya hospitali hiyo kutoka kampuni ya SUKOS Kova Foundation inayomilikiwa na Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Polisi, Suleiman Kova, kwa kushirikiana na kampuni ya One Extreme Solution ya hapa nchini.
Dkt. Ndugulile alisema Watanzania wengi wanafariki wakati wa uokoaji kwani watu wengi hawana elimu ya uokoaji kwani zipo kanuni zinazotumika wakati wa kumuokoa mtu anayepata ajali.
MWISHO
0 on: "ASILIMIA 90 YA WAGONJWA WA MOYO WANATIBIWA TANZANIA"