Mkurugenzi wa tiba toka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Grace Maghembe akiongea wakati wa kilele cha kikao kazi cha Waganga Wafawidhi kilichofanyika Jijini Dodoma. |
Na WAJMW-DOM
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amewataka Waganga wafawidhi kutekeleza maazimio waliyopitisha katika kikao kazi kilichofanyika kwa siku tano Jijini Dodoma.
Dkt. Ndugulile amesema hayo wakati akifunga kikao hicho kilichohusisha Waganga Wafawidhi, Makatibu Tawala wa Halmashauri na Manispaa pamoja na wataalamu mbalimbali wa sekta ya afya nchini waliohudhuria kikao hicho.
“Ninatambua kuwa katika kikao hiki tumepitia mwongozo wa uendeshaji wa Hospitali za Rufaa za Mikoa na kuweka mipango na mikakati endelevu kwa timu za uendeshaji wa Hospitali hizi, ninaomba sana muende mkatekeleze ili kuimarisha Hospitali zetu za Rufaa za Mikoa. Amesema Dkt. Ndugulile.
Katika kikao hicho Waganga Wafawidhi wameweka maazimio ambayo yataratibiwa katika Hospitali zote za Rufaa za Mikoa nchini ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya kukusanya mapato na kuondoa mianya ya upotevu wa mapato, kuimarisha na kuendelea kuzijengea uwezo timu za uendeshaji za Hospitali za rufaa za Mikoa katika kusimamia rasilimali watu, fedha, miundombinu n.k. Kuweka mikakati endelevu ya kupunguza vifo vya mama na mtoto, kila Hospitali kuandaa mkakati wa kununua vifaa na vifaa tiba vitakavyowezesha huduma za kibingwa kutolewa wakati wote, pamoja na kila Hospitali kuja na ubunifu/mikakati ya kukabiliana na upungufu wa watumishi katika maeneo yao kwa kushirikiana na wadau wa mikoa yao.
Aidha, Dkt. Ndugulile ametoa maagizo kwa Waganga Wafawidhi kutekeleza mambo muhimu katika maeneo yao ya kazi ikiwa ni pamoja na kuwa na mfumo wa uongozi na utawala, upatikanaji wa watumishi wenye sifa stahiki katika kada zote, uimarishaji wa miundombinu kwa ajili ya huduma zilizokusudiwa, upatikanaji wa vifaa na vifaa tiba na vitendanishi pamoja na uimarishaji wa matumizi ya teknolojia, taarifa za afya na mawasiliano.
Pamoja na hayo Naibu Waziri amewapongeza Waganga Wafawidhi kwa kushiriki kikao hicho na kuwataka kwenda kutekeleza maazimio waliyopitisha ili kuboresha Hospitali za Rufaa za Mikoa katika maeneo tofauti yaliyokusudiwa ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kabla ya kufunga kikao Dkt. Ndugulile alitoa vyeti vya ubora wa huduma na pongezi, ambapo Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Katavi Dkt. Yustina Tizeba alipata cheti cha pongezi kwa muongozo wa maono, uongozi bora na usimamizi huku Hospitali ya Rufaa ya Amana ikipata vyeti vitatu vya ubora ikiwa ni pamoja na kuongoza katika kupunguza vifo vya mama na mtoto, uongozi bora na mikakati endelevu ya kukusanya mapato na kuwepo kwa vifaa na vifaa tiba vinavyotumika katika huduma za kibingwa.
MWISHO
0 on: "DKT. NDUGULILE ATAKA UONGOZI BORA NA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA ILI KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA NCHINI."