Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiambatana na Mkuu wa Mkoa wa Njombe
Mhe. Christopher Ole Sendeka wakiongea na Wazee waliofika kupata huduma za Afya
katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe wakati alipofanya uzinduzi wa
huduma za Afya katika Hospitali hiyo.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akitoa maelekezo kwa uongozi wa
Hospitali mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe
wakati alipotenbelea kukagua chumba cha kuhifadhia Dawa katika Hospitali
hiyo, wakatikati (mwenye Koti jeupe) ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo ya
Rufaa ya Mkoa wa Njombe Dkt. Kyambile.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akikagua kadi inayoonesha kiasi cha
dawa kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe pindi alipofanya
ziara ya kuzindua Huduma za Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akieleza juu ya umuhimu wa kuwepo kwa
mabango yanayohamasisha haki ya mgonjwa kupata
huduma za Afya zilozo Bora wakati
wa uzinduzi wa huduma za Afya katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe, kushoto kwake (mwenye Koti jeupe) ni
Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe Dkt. Kyambile.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akimjulia hali moja kati ya wagonjwa
waliofika kupata matibabu kwa mara ya kwanza katika Hospitali mpya ya Rufaa ya
Mkoa wa Njombe, ni baada ya kufanya
uzinduzi wa huduma za Afya katika
Hospitali hiyo, Kulia kwake (mwenye Koti jeupe) ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali
hiyo ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe Dkt. Kyambile.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akipanda mti wa matunda (mpalachichi)
ikiwa ni ishara ya kuhifadhi mazingira, shughuli iliyofanyika baada ya uzinduzi
wa huduma za Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akikabidhi ramani ya ujenzi wa
majengo mengine mapya saba kwa
Mkandarasi, shughuli iliyofuata baada ya uzinduzi wa huduma katika Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.
Moja kati ya vyumba vya Wagonjwa
kilicho na vitanda pamoja na mashine zakutambua hali ya Mgonjwa katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe, iliyoanza kutoa huduma rasmi Julai 10,
baada ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kufanya uzinduzi huo
Wananchi waliojitokeza kushuhudia
uzinduzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe ulioongozwa na Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu aliyeambatana na
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Christopher Ole Sendeka (Hawapo kwenye picha)
Na WAMJW-NJOMBE
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya
imeshusha neema kwa Wananchi wa Mkoa wa Njombe kwa kutoa kiasi cha shilingi
Bilion 7.6 kwaajili ya ujenzi wa awamu ya pili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa
ya Mkoa wa Njombe ili kuboresha huduma kwa Wananchi.
Hayo yamejiri leo wakati wa zoezi la
Uzinduzi wa huduma za Afya na lililoongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu katika Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa wa Njombe iliyofunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. John Pombe Magufuli.
Katika uzinduzi huo, Waziri Ummy
amesema kuwa Serikali inaendelea kuboresha huduma za Afya katika Mkoa wa Njombe
ikiwemo kujenga jengo la wazazi la ghorofa tatu, jengo la maabara, jengo la
wagonjwa mahututi na jengo la upasuaji gorofa mbili, wodi za wagonjwa gorofa
tatu, nyumba za Watumishi tano, pamoja na kichomea taka.
" Tunajenga jengo la wazazi la
ghorofa tatu, tunajenga jengo la jengo la maabara, tunajenga jengo la wagonjwa
mahututi na jengo la upasuaji gorofa mbili, tunajenga wodi za wagonjwa gorofa
tatu, tunajenga jengo la kufulia, tunajenga kichomea taka na tunajenga nyumba
za watumishi tano" alisema Waziri Ummy.
Kwa upande mwingine, Waziri Ummy
amemwagiza Mkandarasi wa Hospitali hiyo kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa
majengo hayo hayo ndani ya miezi kumi ili wananchi wa Mkoa wa Njombe waanze
kufaidika na huduma za Afya katika Hospitali hiyo, huku akiwatoa hofu wananchi
kuwa pesa zote zipo tayari.
Mbali na hayo, Waziri Ummy mewaasa
Wananchi kupambana dhidi ya magonjwa yasiyo yakuambukiza kama Kisukari,
shinikizo la damu, Saratani na magonjwa ya Moyo kwa kubadilisha mtindo wa
maisha ikiwamo ulaji mlo sahihi , kuacha uvutaji wa sigara na tumbaku, kuacha
unywaji wa pombe kupita kiasi pamoja na kutofanya mazoezi mara kwa mara.
Aidha, Waziri Ummy ametoa with kwa
vijana kujiepusha na mambo ambayo yatapelekea kipata maambukizi ya VVU, huku
akiweka wazi kuwa maambukizi mapya ya VVU ni 82,000 kila mwaka nchini Tanzania,
huku katika kila watu 100, watu 40 ni vijana wenye umri kati ya 15 hadi 24 umri
ambao ni nguvu kazi ya taifa.
"Tunatambua kwamba kuna
maambukizi makubwa ya virusi vya Ukimwi Mkoani Njombe,lazima tuzingatie kanuni
za kujikinga na maambukizi ya VVU, kujizuia kufanya mapenzi kwa vijana hasa kwa
wasichana ambao muda wao haijafika, pili kuwa mwaminifu kwa mwenza wako au
mpenzi wako na tatu kutumia kinga" alisema Waziri Ummy
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa
Njombe Christopher Olesendeka amewatoa hofu wananchi wa Mkoa wa Njombe kwa
kuweka wazi kuwa huduma za Afya katika Hospitali mpya ya Rufaa ya Mkoa wa
Njombe haitoathiri utoaji huduma katika Hospitali ya Kibena iliyokuwa Hospitali
ya Mkoa, ambayo kwa sasa imerudishwa chini ya Halmashauri ya Mji wa Njombe.
"Na mimi ntahakikisha wale
Watumishi ambao tilikubaliana waje kwenye Hospitali hii, waje na nguo zao ,
vifaa vyote waviache Kibena na huduma ya Kibena iendelee, na kazi ya Hospitali
hii Mhe. Ummy Mwalimu na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli wataweka vifaa vyote
vitakavyohitajika na huduma zitaendelea" alisema Mhe. Olesendeka
Nae Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji
wa Njombe Mhe. Edwirn Mwanzinga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kupitia Wizara ya Afya kwa kuongeza
bajeti ya dawa na vifaa tiba jambo linalosaidia kuokoa kwa kiasi kikubwa maisha
ya Wananjombe.
Mwisho.
0 on: "SERIKALI YASHUSHA NEEMA KWA WANANJOMBE"