Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulie akielekeza jambo kwa viongozi wa wilaya wakati alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa Hospitali mpya ya wilaya ya Bahi mapema leo. |
Baadhi ya majengo ya Hospitali mpya ya Wilaya ya BAHI. |
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Faustine Ndugulile akihesabu mabati ya ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Chonde Wilayani Bahi wakati alipofanya ziara ya kutembelea maendeleo ya ujenzi wa zahanati hiyo leo. |
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile akiongea na wananchi wa kijiji cha Chonde waliofika katika mkutano ambao ulitanguliwa na ziara ya ukaguzi wa zahanati ya kijiji hicho. |
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile ameusifu uongozi wa Wilaya ya Bahi kwa kutekeleza ujenzi wa Hospitali mpya ya Wilaya hiyo ukiwa umekamilika kwa asilimia zaidi ya 90.
Dkt. Ndugulile amesema hayo mapema leo baada ya kutembelea ujenzi wa Hospitali hiyo ambao umefikia hatua za mwisho na kuridhishwa na hatua iliyofikia hadi sasa huku akiusifu uongozi wa Halmashauri chini ya Mkuu wa Wilaya Bi. Mwanahamisi Mkunda kwa kuonesha ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yao.
“Napenda kuwapongeza sana kwa kazi nzuri na ushirikiano mnaoonesha katika kutekeleza mradi huu, ninaamini majengo haya yakikamilika tutaanza kutoa huduma kwa sababu OPD tunayo, jengo la upasuaji, Maabara, jengo la Radiolojia na pia huduma ya Mama na Mtoto tunaweza kuanza nazo”. Amesema Dkt. Ndugulile.
Baada ya kutembelea majengo mbalimbali ya Hospitali hiyo Dkt. Ndugulile ameonesha kuridhishwa na ujenzi huo na kutoa maelekezo kwa uongozi wa Wilaya kuhakikisha huduma zinaanza kutolewa haraka iwezekanavyo ili kusogeza huduma za matibabu karibu na wananchi wa eneo hilo.
Aidha, Dkt. Ndugulile ametembelea ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Chonde Wilayani Bahi na kushangazwa na kasi ndogo ya ujenzi ambao ulianza toka mwaka 2007 lakini haujakamilika mpaka leo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya uhaba wa fedha.
Dkt. Ndugulile ameonyesha kutoridhishwa na gharama za ujenzi ambao unagharimu Shilingi Milioni 90 mpaka kukamilika. Kufuatia hatua hiyo ameagiza ujenzi wa zahanati hiyo kutumia utaratibu wa Force Account na kumuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Dkt. Fatuma Mganga kuleta wataalamu kwa ajili ya kuhakiki gharama za vifaa vinavyohitajika.
Pamoja na hayo Naibu Waziri huyo ameahidi kutoa mifuko 50 ya Saruji ili kuchangia gharama za ujenzi huku akitoa miezi mitatu ya ukamilishaji wa ujenzi huo. Kufuatia hatua hiyo Mkuu wa Wilaya ya Bahi Bi. Mwanahamisi Mkunda amemuahidi Naibu Waziri kukamilika kwa ujenzi wa zahanati ndani ya muda uliowekwa na amechangia mifuko 10 ya saruji huku Mbunge wa Viti Maalum wa Dodoma Bi. Felista Bula akichangia Mifuko 20 ili kuchochea kasi ya ujenzi na huduma zianze kutolewa ifikapo Septemba mwaka 2019.
MWISHO
0 on: "DKT. NDUGULILE AISIFU HALMASHAURI YA WILAYA YA BAHI KWA KUFANIKISHA UJENZI WA HOSPITALI YA WILAYA"