Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumatano, 30 Desemba 2020

ONGEZENI KASI KATIKA HUDUMA ZA MAABARA - DKT. MHAME

 
Mwakilishi wa Katibu Mkuu,Wizara ya Afya na Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Asili/Mbadala Dkt. Paul Mhame akifungua kikao kazi cha usambazaji wa miongozo inayosimamia huduma za tiba kwa Waganga Wakuu wa Mikoa,Wataalamu wa Maabara ngazi ya Mikoa na Wilaya nchini kwenye ukumbi wa Chimwaga jijini Dodoma.

 
Mkuu wa huduma za maabara nchini kutoka Wizara ya Afya Peter Torokaa akiwasilisha miongozo kwa washiriki wa kikao kazi hicho.Jumla ya miongozo 20 imesambazwa.

 
Afisa kutoka Idara ya Huduma za Tiba (Maabara) Bi. Bahati Faki akitoa neno wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha usambazaji wa miongozo inayosimamia huduma za tiba kwa Waganga Wakuu wa Mikoa,Wataalamu wa Maabara ngazi ya Mikoa na Wilaya nchini kwenye ukumbi wa Chimwaga jijini Dodoma. 

 
Washiriki wa kikao kazi hicho ambacho  kimehudhuriwa na watendaji katika ngazi ya Taasisi/Hospitali za Taifa, Mkoa na Halmashauri pamoja na wawakilishi wa Timu za usimamizi huduma ngazi ya Mkoa na Wilaya takriban washiriki 300.

 
Washiriki wa kikao kazi cha usambazaji wa miongozo inayosimamia huduma za tiba wakifuatilia ufunguzi ambapo walisisitizwa kuhakikisha kwamba miongozo hiyo inatumika kwa ufasaha.

 
Kikao kazi cha usambazaji wa miongozo inayosimamia huduma za tiba kwa Waganga Wakuu wa Mikoa,Wataalamu wa Maabara ngazi ya Mikoa na Wilaya nchini kikiendelea kwenye ukumbi wa Chimwaga jijini Dodoma.

 
Picha ya pamoja ikiongozwa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Paul Mhame wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha usambazaji wa miongozo inayosimamia huduma za tiba kwa Waganga Wakuu wa Mikoa,Wataalamu wa Maabara ngazi ya Mikoa na Wilaya nchini kwenye ukumbi wa Chimwaga jijini Dodoma.

 

ONGEZENI KASI KATIKA HUDUMA ZA MAABARA: DKT. MHAME

Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma

Wataalam wa Maabara nchini wametakiwa kuongeza kasi katika kuhakikisha huduma za tiba inayotolewa inafuata miongozi ya wizara na kuhakikisha wanabadili fikra na mitazamo ili kuwafanya wateja wao waweze kuvutiwa na huduma wanazozisimamia.

Hayo yamesemwa leo na Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Asili/Mbadala Dkt. Paul Mhame  wakati wa  kikao kazi cha  usambazaji wa miongozo inayosimamia huduma za tiba katika ukumbi wa Chimwaga jijini Dodoma.

Dkt. Mhame amesema kuwa miongozo hiyo itakayowasilishwa kwa siku mbili imesisitiza kuboresha utoaji wa huduma za tiba pia masuala ya usimamizi wa huduma za damu salama pamoja na sheria, kanuni na miongozo ya kusimamia Tiba Asili nchini.

“Hakikisheni masuala haya ambayo ni mtambuka katika utoaji wa huduma mnayaelewa vyema ili muweze kuisaidia jamii, ikumbuke kuwa yapo maelekezo yaliyotolewa na viongozi wa kitaifa hususan suala la tiba asili na tiba mbadala hivyo muhakikishe mnawawezesha waratibu hao pindi inapotokea changamoto katika kusimamia huduma hizi kwenye ngazi mnazosimamia”.Alisisitiza Dkt. Mhame.

Hata hivyo Dkt. Mhame aliwataka washiriki hao kuhakikisha ujumbe utakaotolewa kwenye kikao kazi hiko kitawafikia walengwa ili pindi ukaguzi na usimamizi shirikishi utakapofanyika uwe na tija katika kuboresha huduma za tiba kwenye maeneo waliyotoka na hivyo itasaidia kuboresha huduma za uchunguzi katika hospitali na ngazi mbalimbali za utoaji huduma za tiba nchini.

Naye Mkuu wa huduma za Maabara nchini kutoka Wizara ya Afya Peter Torokaa amewasisitiza vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini kufanyia tathimini ya ufanisi “Calibration” wa  mashine zote kwa kuwatumia wataalam wa maabara na zile zinazotakiwa kufanywa na Shirika la Viwango (TBS) wanafanyia pia kwani ndio wenye mamlaka.


Aidha, Torokaa amewataka Mameneja na Waratibu wa maabara wa Mikoa na Wilaya kuhakiki uwezo wa mashine “Method Verification” kupima na kutoa majibu yaliyo sahihi hivyo kila kipimo kithibitishwe kama kinatoa majibu ya wagonjwa yaliyo sahihi.

“Jambo la tatu tunalosisitiza ni wataalam wetu kupimwa umahiri kwa kuhakikisha mameneja na waratibu wetu wa Mikoa na wilaya  wanasimamia watoa huduma wetu ambao ni wataalamu wa maabara wanafanyiwa umahiri kama wana uwezo wa kutumia hiyo mashine,kifaa na kutoa majibu ikiwemo uwezo wa tafsiri majibu ambayo yanaenda  kwa Daktari kufanya maamuzi kwa mteja.

Aliongeza kuwa kila kipimo lazima kifanyike kidhibiti ubora kabla maabara haijatoa majibu kwenda kwa daktari kuhakikisha inadhibiti majibu hayo ndani ya maabara kwa kila kipimo pamoja na kuhakikisha maabara inashiriki sampuli zingine  ndani na nje ya nchi ili kuweza kujipima kama wanaweza kutoa majibu yaliyo sawa.

Naye Meneja wa Maabara wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Tanga-Bombo  Sinde Mtobu amesema maabara yao imekuwa miongozi wa uboreshaji wa huduma nchini na kuwa katika ngazi ya  nyota nne hivyo wanasubiri kupata ithibati ya kimataifa IS0-15-18-9 kwenye huduma za ubora kwa ujumla hivyo wapo miongoni mwa maabara 27 nchini.

Ametaja  moja ya eneo ambalo wamefanya vizuri kwenye maabara ni  kuwawezesha wataalam wa maabara kwenye umahiri kwa kusimamia miongozo yote pamoja na eneo la uhakiki ubora  wa huduma zao kabla ya kwenda kwa daktari.


MWISHO

Jumatano, 23 Desemba 2020

WAFAMASI WAKUMBUSHWA KUHUISHA LESENI ZAO KABLA MWAKA KUISHA

 Msajili wa Baraza la Famasi Bi. Elizabeth Shekalaghe akisisitiza jambo wakati akiongea na afisa habari wa Wizara ya Afya,ofisini kwake jijini Dodoma.

 

 WAFAMASI WAKUMBUSHWA KUHUISHA LESENI ZAO KABLA MWAKA KUISHA

Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma

Wafamasia, fundi dawa sanifu na wasaidizi nchini wamekumbushwa kuhuisha leseni zao kabla ya tarehe 31 Disemba mwaka huu ili waweze kuendelea kufanya kazi za kitaaluma kwa mwaka unaokuja.

Wito huo umetolewa leo na Msajili wa Baraza la Famasi Bi. Elizabeth Shekalaghe wakati akiongea na afisa habari wa Wizara ya Afya,ofisini kwake jijini Dodoma.

Bi. Elizabeth amesema kuwa kwa mujibu wa kifungu Namba 22 cha Sheria ya Famasi, Sura 311 kinawataka wafamasia kuweza kuhuisha majina yao kwenye rejista kwa utaratibu maalamu.

"Pamoja na baraza la famasi kuwasajili wanataaluma kwa mujibu wa kifungu cha sheria ya famasi nchini,kifungu kinatutaka kabla ya tarehe 31 Desemba ya kila mwaka kuhuisha majina ili kuweza kufanya kazi  za kitaalam kwa mwaka unaokuja".Alisisitiza Msajili

Kwa upande wa uuzaji wa dawa Msajili wa Baraza hilo Bi.Shekalaghe amesema  tatizo la uuzaji wa dawa kiholela limekuwa ni tatizo sugu hapa nchini na hivyo mwaka huu Waziri wa Afya ameidhinisha kanuni za udhibiti na usimamizi wa uuzaji wa dawa za cheti na hivyo amewataka wanataaluma wa famasi kuhakikisha wanazisoma na kuzielewa kanuni hizo.

"Kama wafamasia na wataalam tukumbuke tuna watu tunawasimamia na kuhakikisha dawa tunazitoa kwa kuzingatia miongozo iliyopo na Baraza halitosita kumchukulia hatua yeyote atakayeenda kinyume na kanuni hizo".Aliongeza Bi. Shekalaghe.

Mbali na hayo Bi. Shekalaghe amewataka wananchi  kutoa taarifa kwenye Baraza hilo pale wasiporidhika na huduma zitolewazo katika Famasi na maduka ya dawa muhimu kwa kupiga 0736 222 504 au namba bila malipo 0800110015 ili waweze kutatua changamoto wanazozipata wakati wanapatiwa huduma hizo. 


-MWISHO-

Jumamosi, 19 Desemba 2020

SERIKALI KUJA NA MFUMO WA TEHAMA WA UFUATILIAJI DAWA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akisisitiza jambo wakati wa kikao kazi cha kujadili hali ya utoaji huduma za afya nchini ambacho kimewakutanisha Wakurugenzi wa Wizara pamoja na Taasisi zake kilichofanyika kwenye ukumbi wa hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Godwin  Mollel akieleza jambo wakati wa kikao kazi cha kujadili hali ya utoaji huduma za afya nchini ambacho kimewakutanisha Wakurugenzi wa Wizara pamoja na Taasisi zake kilichofanyika kwenye ukumbi wa hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akisisitiza jambo wakati wa kikao kazi cha kujadili hali ya utoaji huduma za afya nchini Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel na kushoto kwake ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw. Edward Mbanga.


Baadhi  ya Wakurugenzi kutoka Taasisi za Wizara  ya Afya wakifuatilia kwa makini neno kutoka kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima (hayupo kwenye picha) wakati wa kikao kazi cha kujadili maendeleo ya Sekta ya Afya, kilichofanyika kwenye ukumbi wa hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.

Wakurugenzi wa Wizara ya Afya pamoja na Wakurugenzi wa Taasisi zake wakiwa katika kikao kazi cha kujadili hali ya utoaji huduma za afya nchini kilichoongozwa na Waziri  wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima, kikao kimefanyika katika ukumbi wa hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.



SERIKALI KUJA NA MFUMO WA TEHAMA WA UFUATILIAJI DAWA

Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma.

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto inatarajia kuanzisha mfumo wa Tehama kufuatilia mnyororo mzima wa utoaji wa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya umma vyote nchini.

Hayo yamesemwa leo na Dkt. Dorothy Gwajima, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto wakati wa kikao kazi cha kujadili hali ya utoaji huduma za afya nchini ambacho kimewakutanisha Wakurugenzi wa Wizara pamoja na Taasisi zake kilichofanyika kwenye ukumbi wa hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.

Dkt. Gwajima amesema kuwa, mfumo huo utasaidia kufuatilia utoaji wa dawa unaofanywa na watoa huduma za afya kwenye vituo vya umma , kwani  Serikali haitaji  upotevu  wa dawa kwenye vituo vyake.

"Tunataka mfumo huu uunganishe vituo vyote pamoja na hospitali zote hadi za Taifa kwani huu ni ulimwengu wa Tehama,hivyo kama kiongozi anatakiwa kuona kila kitu pale alipo ili kuweza kurahisisha kutatua matatizo ya wananchi wetu na hivyo tutadhibiti upotevu wa dawa kwani imekua ni changamoto kubwa na sio kwamba dawa hamna".Alisema Dkt. Gwajima.

Hata hivyo, Dkt. Gwajima aliwakumbusha watoa huduma kutoa dawa kwa kufuata muongozo wa utoaji wa dawa kwa kuandika jina la dawa na sio jina la kampuni kwani kwa kufanya hivyo inasababisha kukosekana kwa dawa ilhali dawa zipo kwenye stoo.

Kwa upande mwingine, Dkt. Gwajima,  ameagiza kufufuliwa na kukanza vikao mara moja  kwa kamati za dawa kuanzia ngazi ya Taifa hadi Zahanati,  ili kuweza kujadili dawa zote zinazotumika kwenye vituo vyao jambo ambalo litasaidia kugundua upotevu wa dawa  kwenye vituo vya umma.

Naye, Naibu Waziri Dkt. Godwin Mollel amesema  kikao kazi hicho kitasaidia kujua changamoto na kuzijadili kwa pamoja  ili kuweza kuwasaidia wananchi  kupata matibabu bora na huduma zingine  kwenye taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo kwa urahisi.

Amesema kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita  uwajibikaji na uadilifu umefanyika na hivyo nchi kufanya mapinduzi makubwa kwa kutumia mapato ya ndani, Serikali inayo uwezo wa kununua dawa,vifaa na vifaa tiba  na kutoa matibabu kwa wananchi kwa gharama nafuu na hivyo itawaondolea wananchi mzigo mkubwa wa matibabu nchini.

Dkt. Mollel amewataka watumishi kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu ili kuondoa matatizo yalipo, kwani asilimia 75 ya matatizo hayo  yanaweza kutatuliwa na wenyewe bila kutegemea mtu mwingine, hivyo kuwataka kuongeza kasi ya utendaji kazi na kutumia mapato vizuri ili kuweza kuboresha huduma za afya nchini na kuiongezea mapato Serikali na kusiwepo upungufu wa dawa kwa kuweza vipaumbele maeneo muhimu.
-MWISHO-

Ijumaa, 18 Desemba 2020

SERIKALI KUBORESHA MAENEO YA KUTUPA TAKA:DKT. SUBI

 
Mkurugenzi wa huduma za kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi akitoa maelekezo  kwa Maafisa Afya mazingira (hawapo kwenye picha) katika kilele cha wiki ya usafi wa mazingira kitaifa na mkutano wa maafisa afya wa mikoa na halmashauri iliyofanyika jijini Dodoma.

 
Mkurugenzi msaidizi wa Afya mazingira Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Khalid Massa akimkaribisha Mkurugenzi wa huduma za kinga Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi (hayupo kwenye picha) wakati wa kilele cha wiki ya usafi wa mazingira kitaifa na mkutano wa maafisa afya wa mikoa na halmashauri iliyofanyika jijini Dodoma.
 
 
Maafisa Afya  mazingira kutoka ngazi ya Mikoa na Halmashauri wakifuatilia neno kutoka kwa Mgeni rasmi ambae ni Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya Dkt Leonard Subi wakati wa kilele cha wiki ya usafi wa mazingira kitaifa iliyofanyika jijini Dodoma.

Picha ya pamoja ikiongozwa  na Mgeni rasmi ambae ni Mkurugenzi wa huduma za Kinga Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi pamoja na washindi wa tuzo za uandishi wa habari za usafi  wa mazingira, Jijini Dodoma.


SERIKALI KUBORESHA MAENEO YA KUTUPA TAKA:DKT. SUBI

Na.Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma

Serikali ya awamu ya tano ina nia ya dhati ya kuboresha maeneo ya kutupia taka hususani madampo yaliyopo kwenye miji ili yawe ya kisasa.

Hayo yamesemwa leo na Dkt. Leonard Subi  Mkurugenzi wa huduma za kinga kutoka Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto kwenye kilele cha wiki ya usafi wa mazingira kitaifa na mkutano wa maafisa afya wa mikoa na halmashauri iliyofanyika jijini Dodoma.

Dkt.Subi amesema kuwa,uchafuzi wa mazingira utokanao na taka ngumu umeendelea kuwa changamoto katika maeneo ya mijini.

"Ili kukabiliana na tatizo hili,Serikali imepanga kuongeza nguvu kwenye mamlaka za serikali za mitaa ili kuboresga miundombinu katika mitaa iliyopo nchini hasa katika suala la usimamizi wa taka ngumu na majitaka".

Aidha,Dkt. Subi amesema serikali imeandaa mwongozo wa uwekezaji katika taka ngumu ili kuhamasisha uwekezaji na kuongeza jitihada za kuboresha usimamizi wa taka hapa nchini.

Hata hivyo alizitaka halmashauri zipitie sheria ndogo za halmashauri ili kutekeleza vema,Sheria ya Afya ya Jamii ya mwaka 2009 hususani katika maeneo ya utiririshaji maji taka hasa katika maeneo ya mijini na kudhibiti tabia ya kujisaidia porini wakati wa kusafiri maarufu kama ' kuchimba dawa’ ambayo bado imeendelea kuwepo.

Dkt.Subi aliwapongeza maafisa afya hao katika maeneo ya ujenzi wa vyoo bora,unawaji wa mikono ,huduma za afya mipakani,udhibiti wa kipindupindu,Corona,mlipuko wa Dengue pamoja na udhibiti wa taka zitokanazo na huduma za afya na mengine mengi.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Afya Tanzania (CHAMATA) Twaha Mubarak ameishukuru Wizara ya afya kwa kufanya afya mazingira ni kipaumbele katika kuondoa magonjwa,hivyo wataalam wanajivunia na kuweza kupunguza ugonjwa wa Malaria ili kuweza kufanikiwa kutimiza lengo la kutokomeza Malaria ifikapo mwaka 2030.

 

Alhamisi, 17 Desemba 2020

WATAALAM WA TIBA ASILI WATAKIWA KUFANYA UTAFITI WENYE USHAHIDI

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bw. Edward Mbanga akiongea na wataalam wa tiba asili/mbadala kutoka taasisi za serikali na vyuo vikuu mbalimbali vinavyojishughulisha na tafiti za dawa za tiba asili nchini.

 
Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt.Eliud Eliakimu  akizungumza wakati wa kikao hicho

 
Mkemia Mkuu wa Serikali kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt.Fidelice Mafumiko na Msajili wa Baraza la Tiba Asili/Mbadala Dkt. Ruth Suza wakifuatilia ufunguzi wa kikao kazi hicho.
 
Kaimu Katibu Mkuu Edward Mbanga (katikati) na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Eliud Eliakimu(kulia) na Mkurugenzi wa Idara ya Tiba Dkt. Grace Maghembe  wakifuatilia uwasilishaji wa mada kwenye kikao cha kujadili

 
Washiriki wa kikao kazi cha siku mbili  cha kujadili muelekeo wa tiba asili nchini kinachofanyika kwenye ukumbi wa ofisi za wizara zilizopo Area D jijini Dodoma


Picha ya pamoja ya mgeni rasmi na washiriki wa kikao kazi cha kujadili muelekeo wa tiba asili na tiba mbadala nchini.


WATAALAM WA TIBA ASILI WATAKIWA KUFANYA UTAFITI WENYE USHAHIDI

Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma

Wataalam wa tiba asili na tiba mbadala nchi wametakiwa kufanya utafiti ambao utakuwa na  ushahidi wa usalama wa dawa pamoja na ufanisi wa wa dawa hizo kwa watumiaji.

Rai hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Mkuu wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, wazee na watoto-Idara kuu Afya Bw. Edward Mbanga wakati wa kikao cha pamoja cha wizara na  wataalam hao kutoka taasisi za Serikali na Vyuo Vikuu mbalimbali nchini kilichofanyika kwenye ukumbi wa wizara jijini Dodoma.

Mbanga amesema kuwa ushahidi huonekana kwenye utafiti hivyo warudi nyuma na kujiuliza wamekosea wapi na nini kifanyike ili kuwa na uelewa wa pamoja kwani kizazi kijacho kinahitaji kuelezwa na kuelewa tiba asili.

“Lazima tuulizane tunataka kufikia wapi na kuweka mikakati  ya kuyafikia,nashauri tutambue nini kifanyike,tuna changamoto zipi na tunafikaje huko kwa kushirikiana kwa pamoja  ili tutambue kwanini hatufiki hivyo lazima tujikite kwenye utafiti wenye ushahidi”.Alisisitiza.

Aliongeza kuwa katika kikao hicho wataalam hao wanatakiwa kutafuta majibu ambayo tiba asili itaendelea hata baada ya kipindi hiki,na wawe na matamanio kama nchi nyingine ili tiba asili itolewe kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

“Tumekuwa tukifanya utafiti wa masuala ya tiba asili na tiba mbadala  kuanzia miaka ya sitini, sasa tujiulize  tangu tutafiti hadi sasa matokeo yanafanana?,bado kuna changamoto ya watu kushindwa kuthamini vya kwao hasa katika matumizi ya tiba asili kwa kuamini vinavyotoka nje ya nchi vina ubora zaidi kuliko vya kwao.

Hata hivyo Kaimu katibu mkuu huyo aliwataka katika kikao hicho watoke na mkakati wa kuanzisha vituo vya uendelezaji   vya tiba asili kwenye halmashauri zote kwa kuwapatia ujuzi na motisha wataalam wa tiba asili pamoja na kufanyia tafiti dawa zao na mwisho wa utafiti kuwe na haki miliki.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mguu wa Serikali Dkt. Eliud Eliakimu amesema kuwa kama nchi wameamua kuendeleza tiba asili kwa umoja ili kuwe na spidi ambayo italeta mafanikio yenye tija nchini.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Tiba kutoka Wizara ya afya Dkt. Grace Maghembe amesema  tiba asili zipo na zinatumika  kutibu magonjwa mbalimbali  na malighafi ya kutengeneza dawa hizo zipo hapa nchini hivyo uwezo wa kutengeneza katika viwango kama nchini nyingine inawezekana endapo kutawekwa msukumo na hivyo kusaidia kuinua uchumi wa nchi na wa wakulima wa hapa nchini.

Mwisho

Jumatano, 16 Desemba 2020

TIMIZENI WAJIBU WENU KWA WELEDI NA MAADILI.

 
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe akifungua Mkutano wa Maafisa Afya mazingira uliofanyika Jijini Dodoma.

 
Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, ambae pia ni Mkurugenzi wa huduma za Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi akiwasilisha maelekezo ya Mganga Mkuu wa Serikali kwa Maafisa Afya mazingira katika ufunguzi  wa Mkutano wa tathmini wa Maafisa Afya mazingira uliofanyika Jijini Dodoma.
 
 
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe TAMISEMI Dkt. Paul Chawote akitoa neno kwa Maafisa Afya mazingira (hawapo  kwenye picha) walio hudhuria Mkutano wao wa tathmini, uliofanyika Jijini Dodoma.

 
Mwenyekiti wa Maafisa afya mazingira nchini Bw. Evans Simkoko akitoa salam za Maafisa Afya mazingira kwa Mgeni rasmi ambae ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya (hayupo kwenye picha) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa tathmini wa Afya mazingira uliofanyika Jijini Dodoma.
 
 
Maafisa Afya kutoka maeneo ya mipaka wakifuatilia kwa makini neno kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya (hayupo kwenye picha) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa tathmini wa Afya mazingira uliofanyika Jijini Dodoma.
 
Maafisa  Afya mazingira wakifuatilia kwa makini neno kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya (hayupo kwenye picha) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa tathmini wa Afya mazingira uliofanyika Jijini Dodoma.


TIMIZENI WAJIBU WENU KWA WELEDI NA MAADILI.

Na Rayson Mwaisemba, WAMJW- DOM.

KATIBU Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Idara kuu ya Afya Prof. Mabula Mchembe amewataka Maafisa Afya ngazi zote kufanya kazi zao kwa weledi na kufuata maadili wakati watimizapo majukumu yao katika jamii.

Prof. Mchembe ameyasema hayo, wakati akifungua Mkutano wa Maafisa Afya mazingira wenye kauli mbiu ya "Zingatia mahitaji ya Jinsia kwa usafi wa mazingira endelevu " uliofanyika Jijini Dodoma.

"Tusimamie maadili sana, usitende kitu kwa kufikiria kwamba unamfanyia fulani, natambua changamoto zipo katika baadhi ya sehemu, lakini tunahitaji kutimiza wajibu wetu kwa maadili na uwaminifu wa hali ya juu" alisema Prof. Mchembe.

Pia, Prof. Mchembe amewataka Maafisa Afya mazingira kusimamia usafi katika maeneo ya huduma za vyoo katika jamii, hususan katika ofisi na vituo vya daladala ambavyo huudumia Jamii kwa kiasi kikubwa ili kuikinga Jamii dhidi ya magonjwa ya milipuko.

Aidha, Prof. Mchembe amewaagiza Maafisa Afya mazingira nchini kusimamia usafi na ubora wa vyakula katika maeneo yote yanayotoa huduma za vyakula, yakiwemo maeneo ya migahawa na hoteli ili kuikinga jamii na magonjwa ya tumbo na kuhara.

Mbali na hayo Prof. Mchembe ametoa wito kwa Maafisa afya mazingira kujiepusha na vitendo vya Rushwa wakati wa wakitimiza majukumu yao na kuhakikisha usafi wa mazingira unaendelea kufuatwa katika ngazi zote za Jamii.

"Tuachane na Rushwa, inawezekana baadhi ya sehemu unafika pale, unapewa 10,000 au unapewa bia mbili au tatu unaondoka zako, kitu ambacho hakina maana, sasa kama wewe ni Mtaalamu wa Afya simama kwenye maadili yako" alisema Prof. Mchembe.

Hata hivyo, Prof. Mchembe amewaagiza Maafisa afya mazingira nchini, kusimamia udhibiti wa takataka zinazotokana na utoaji wa huduma za afya ili kuendelea kuikinga jamii dhidi ya maambukizi yatokanayo na taka hizo.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, ambae pia ni Mkurugenzi wa huduma za Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi amewaagiza Waganga wakuu wa mikoa  kutoa elimu mara kwa mara kwa watendaji wao juu ya maadili badala ya kusubiri kuchukua hatua baada ya kosa kujitokeza.

"Kutoa elimu mara kwa mara kuhusu maadili, badala ya kusubiri kuchukua hatua kwa Maafisa Afya au wana taaluma wenu, wanapokiuka au kufanya makosa mbali mbali " alisema Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Subi.

Aliendelea kusema kuwa, baadhi ya maeneo hususan mijini bado kuna hali ya usafi wa mazingira usioridhisha, na kuelekeza kuanza kampeni ya usafi wa mazingira ya muda wa miezi miwili, huku akiwataka kuanza oparesheni hiyo kwa kuzingatia Sheria na kanuni za afya ya mwaka 2009.

Hata hivyo, Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali amewaagiza Maafisa Afya mazingira, kukagua suala la usafi wa mazingira kwenye shule, mabweni, maofisi na maeneo yote yenye mikusanyiko ili kuhakikisha usafi wa mazingira unapewa mkazo ili kuikinga jamii dhidi ya maambukizi ya magonjwa ya mlipuko.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Maafisa afya mazingira nchini Bw. Evans Simkoko ameiomba Serikali kuipa kipaumbele kada ya Maafisa Afya mazingira kwenye ajira mpya, ili kuongeza ufanisi katika utoaji huduma kwa wananchi, kisha kuikinga Jamii dhidi ya maambukizi ya ugonjwa ya milipuko.

Mwisho.

TANZANIA YAVUKA VIWANGO VYA KIMATAIFA VYA UTOAJI WA CHANJO

Prof. Mabula Mchembe, 
Katibu Mkuu 
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Dkt. Leonard Subi
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga
Wizara ya Afya


 Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendheleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe amewapongeza viongozi na watumishi wa huduma za chanjo ngazi zote nchini kwa  utendaji bora wa utoaji wa chanjo kwa bidii na kuhakikisha kuwa malengo yaliyowekwa kitaifa na kimataifa yanafikiwa.

Pongezi hizo zimetolewa leo wakati akifungua mkutano wa mwaka wa tathimini wa huduma za chanjo Tanzania unaofanyika kwenye ukumbi wa Mt. Gasper jijini Dodoma.

"Niwapongeze kwa jitihada zenu na kuifanya nchi kufanikiwa katika utoaji wa huduma za chanjo kwa kuvuka kiwango cha asilimia 90 kilichowekwa kimataifa, hivyo nawataka mkubaliane na kupanga mbinu na mikakati ya kudumisha na kuboresha zaidi viwango vya chanjo nchini".

Hata hivyo katibu Mkuu huyo alisema licha cha kufanikiwa huko Serikali kupitia Wizara yake itaendelea kudumisha  kiwango cha chanjo nchini na ana uhakika takwimu za mwaka 2020  zitakapotolewa na Shirika la Afya Duniani(WHO)  itafikia asilimia 98 au zaidi.

Licha ya pongezi hizo Prof. Mchembe  amewaagiza viongozi wa afya ngazi za Mikoa na wilaya  kuhakikisha kuwa huduma za chanjo zinapewa kipaumbele  ili usitokee tena mkoa utakaoshindwa kudumisha kiwango kilichofikiwa kwani ili watoto waendelee kuwa na afya njema hakuna budi kuwapa chanjo bora za kuwakinga dhidi ya maradhi.

"Nchi yetu imekuwa na utekelezaji wa mkakati wa Fikia kila Wilaya,Fikia kila mtoto apate chanjo,nawasisitiza waratibu wa huduma za chanjo kuhakikisha kuwa mikoa inayofanya vibaya inatumia mkakati huu ili  kuhakikisha kuwa watoto na walengwa wote wanafikiwa katika kupata haki yao ya msingi ya chanjo".

Aidha, Prof. Mchembe aliwashukuru wadau wote wa maendeleo kwa michango yao mbalimbali  katika kuhakikisha kwamba watoto  wanapatiwa chanjo bora  ambayo inaleta kinga dhidi ya maradhi ambayo yanaweza kusababisha ulemevu na vifo kwa watoto.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI  Dkt. Ntuli kapologwe amewapongeza Waganga Wakuu wa Mikoa pamoja na waratibu wa huduma za chanjo nchini kwa kuwa kinara wa utoaji wa chanjo na kuweza kuwafikia walengwa wote nchini na kuongoze kuwa TAMISEMI inaipa uzito mkubwa suala la chanjo kwani kinga ya mtoto inaanza na chanjo.

Kwa upande wake  Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Serikali ambaye pia ni  Mkurugenzi wa Idara ya kinga Kutoka Wizara ya afya, Dkt. leonard Subi amesisitiza kuwa wizara ya afya inasimamia ubora na usalama wa huduma wanazozitoa hasa upande wa chanjo ambao mara kadhaa umekua na mapokeo tofauti,hivyo amesisitiza kuwa wizara ipo makini zaidi na afya za wananchi

Wakati huo huo Mwakilishi wa wadau wa maendeleo ambaye anatoka WHO Nassoro Mohamed  ameipongeza Wizara ya afya pamoja na viongozi wa mikoa kwa kuhakikisha watoto wote nchini wanafikiwa  licha ya changamoto za hapa na pale hivyo kama wadau wanashiriki ili kuhakikisha Serikali inafikia malengo waliyojiwekea katika kutoa huduma za chanjo.

-MWISHO-

Alhamisi, 10 Desemba 2020

DKT. GWAJIMA AWATAKA VIONGOZI WA WIZARA YA AFYA KUSHIRIKIANA ILI KUONGEZA UFANISI KAZINI

 
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akifurahia jambo na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel baada ya kuwasiri katika ofisi za Wizara ya Afya Jijini Dodoma.
 
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akisaini kitabu pindi alipowasiri katika ofisi za Wizara ya Afya Jijini Dodoma.
 
 
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin  Mollel akisaini kitabu baada ya kuwasiri katika ofisi za Wizara ya Afya Jijini Dodoma.
 
Katibu  Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula  Mchembe akisisitiza  jambo mbele ya Watumishi wa Afya wakati  wa mapokezi ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Naibu Waziri wake katika ofisi za Wizara ya Afya Mtumba Jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin  Mollel akisalimiana na Watumishi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pindi alipowasiri katika ofisi za Wizara ya Afya Mtumba Jijini Dodoma.

 

Watumishi wa Wizara ya Afya na Wakurugenzi wake, wakifuatilia kwa makini maelekezo kutoka kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika ofisi za Wizara ya Afya Mtumba Jijini Dodoma.

Picha ya pamoja ikiongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima pamoja na Naibu Waziri wake Dkt. Godwin Mollel, wakiwa na Katibu Mkuu Idara ya Afya, Prof. Mabula Mchembe (wanne kutoka kushoto) na Katibu Mkuu Idara ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu (wakwanza kushoto).

Picha ya pamoja ikiongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima pamoja na Naibu Waziri wake Dkt. Godwin Mollel, wakiwa na Katibu Mkuu Idara ya Afya, Prof. Mabula Mchembe (wanne kutoka kushoto) na Katibu Mkuu Idara ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu (wakwanza kushoto), pamoja na Watumishi na Wakurugenzi kutoka Idara Kuu ya Afya.


 

DKT. GWAJIMA AWATAKA VIONGOZI WA WIZARA YA AFYA KUSHIRIKIANA ILI KUONGEZA UFANISI KAZINI

Na WAJMW-Dodoma

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amewataka Wakurugenzi na watumishi wa Wizara ya Afya kushirikiana ili kuweza kufikia lengo la kuboresha huduma za afya nchini.

Dkt. Dorothy amesema hayo leo wakati akiongea na Wakurugenzi pamoja na viongozi mbalimbali waliompokea mara baada ya kuapishwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Waziri wa Wizara hiyo mapema katika hafla iliyofanyika Ikulu-Chamwino, Jijini Dodoma.

Dkt. Gwajima amesema ili sekta ya afya iweze kusonga mbele na kuwafikia wananchi katika kiwango cha hali ya juu inategemea na ushirikiano utakaokuwepo baina ya viongozi wa Wizara pamoja na watumishi mbalimbali wa sekta ya afya.

“Wapeni ushirikiano makatibu wakuu, mambo mengi yanafanywa na wataalam kwa kushirikiana na makatibu wakuu, tukikubaliana kufanya jambo basi wote tufunge mikanda kuhakikisha tukamalisha kwa wakati lengo likiwa kutimiza dhamira ya Mhe. Rais ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya nchini”. Amesema Dkt. Gwajima.

Aidha, Waziri Gwajima amewataka viongozi wa idara mbalimbali wanapotembelea maeneo mbalimbali ya Sekta kuja na ripoti ya ziara zao na kukabidhi kwa Katibu Mkuu ili ziweze kufanyiwa kazi na kutoa miongozo halikadhalika amewataka makatibu wakuu kutofungia ripoti hizo makabatini bali wazifanyie kazi na kutatua changamoto zinazozikabili sekta ya afya.

“Nawataka Viongozi wa Wizara mnapoenda 'Supervision' mrudi na ripoti na pia nawaomba Makatibu Wakuu msizipuuze ripoti mnazoletewa ili tuone zinaleta faida gani kwenye ofisi zetu na pia katika kuboresha huduma za afya nchini”. Ameongeza Dkt. Gwajima.

Waziri huyo amesema kwa kufanya hivyo itaongeza ufanisi kwa kila kiongozi atakayeenda ili kujua aanzie wapi na siyo kila mmoja kwenda na jambo lake huku akiendelea kusisitiza viongozi hao kushirikiana ili kutatua kero na changamoto zilizopo.

Pamoja na hayo Waziri Dorothy amezitaka Taasisi, Hospitali na vituo vya afya kutoa taarifa za mapato na matumizi na ameagiza kutengenezwa mfumo utakaosaidia kupata taarifa hizo ili ziweze kusaidia kutoa muelekeo wa uboreshaji wa huduma za afya.

Pia ametaka utengenezwe muongozo wa huduma kwa wateja ili utolewe kwa watumishi wa sekta ya afya ili wabadilike na kuwathamini wagonjwa wanaofika katika maeneo ya kazi ili kupata huduma.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Prof. Mabula Mchembe amewapongeza na kuwashukuru Waziri Dorothy pamoja na Naibu Waziri Dkt. Godwin Mollel kwa kuchaguliwa kuiongoza Wizara hiyo na kuahidi kutoa ushirikiano.

MWISHO

Jumatatu, 7 Desemba 2020

"WATUMISHI WA AFYA MSHIKIRI KATIKA KUCHANGIA MAENDELEO YA SEKTA YA AFYA" - MGANGA MKUU WA SERIKALI

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi

 


Na WAMJW – Mwanza.

 Mganga mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi amewata watumishi wa afya kushiriki kikamilifu katika kuchangia Maendeleo ya sekta ya afya na si kuiachia Serikali na Jamii pekee.

 

Amesema hayo akiwa kwenye kikao kazi na timu ya uongozi wa afya ndani ya Mkoa wa Mwanza kilichofanyika Wilayani Misungwi kujadali mikakati ya uboreshaji wa huduma za afya mkoani humo.

 

“Kwanini tushindwe kuchangia uboreshaji wa huduma za afya, lazima tuwe na moyo wa kujitoa kuchangia, hizi ni mali zetu sote sisi pamoja na watoto wetu sote tutatibiwa huko” Ni lazima sasa Hospitali zetu zianze kuwa na jicho la kutoa huduma huku zilijenga uwezo wa kifedha na kupunguza utegemezi toka serikali, bila kuathiri huduma kwa wananchi wasio na uwezo wa kulipia.. amesema Prof. Makubi.

 

Amesema hatuwezi kuitegemea Serikali na wafadhili pekee kutuletea Maendeleo ya huduma za afya katika maeneo yetu hivyo na watumishi wanapaswa kushiriki katika kuboresha huduma hizo katika maeneo waliyopo.

 

Aidha Prof. Abel Makubi alitumia nafasi hiyo pia kuendesha shughuli ya michango kwa ajili ya uboreshaji wa huduma za afya ndani ya Mkoa huo ambapo juma ya Tsh 6,850,000/= fedha ambayo itaenda kutumika katika ujenzi wa jengo kwa ajili ya huduma kwa watoto waliolazwa mahututi (NICU)

 

Prof. Makubi amesema kuwa Mkoa wa Mwanza una uhitaji mkubwa wa huduma hiyo hivyo ufinyu wa eneo katika Hospitali ya Bugando unasababisha watoto walio wagonjwa kukosa huduma kwa wakati.

 

“Hospitali ya Budango inaendelea kupata wingi wa watoto ambao hawajafikia umri wa kuzaliwa na wengi wakiletwa bugando kunakuwa na shida ya kupata eneo la kuwahudumia, kwa michango hiyo itasaidia kuboresha huduma hizo kwa kuongeza eneo” amesema Prof. Makubi

 

Hata hivyo Prof. Makubi amesisitiza suala la uongozi imara kwa viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia taasisi za afya na kuwasisitiza  kuwajibika ipasavyo katika utumishi wao kwa kuhakikisha watumishi walio chini yao wanatoa huduma bora kwa wananchi.

 

Mwisho

HOSPITALI ZENYE WATAALAM BINGWA ZATAKIWA KUTOA HUDUMA ZA MKOBA KWA WANANCHI WALIO MBALI NA HUDUMA

 

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Makubi akisema jambo kwenye kikao na kamati tendaji ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando



Dkt. Caroline Damian Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tiba anayesimamia Hospitali za Rufaa za Mikoa akisema jambo kwenye kikao na kamati tendaji ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Hosptali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Dkt. Fabian Massaga (aliyesimam) akisema jambo katika kikao kazi cha kamati tendaji ya Hospitali hiyo na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi 


Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akimpima mapigo ya moyo mgonjwa kwa kutumia kipimo cha Echo-Cadiogram katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando

Na Englibert Kayombo, WAMJW - Mwanza

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi ametoa wito kwa Hospitali zenye wataalam wanaotoa huduma za kibingwa kuwa na huduma za mkoa “Outreach Services” endelevu ili wananchi walio mbali na huduma hizo nao waweze kuhudumiwa karibu na maeneo waliyopo.

Prof. Makubi ametoa amesema hayo akiwa katika ziara ya kikazi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando ambapo alikwenda kujionea hali ya utoaji wa huduma na kuzungumza na viongozi na kamati tendaji ya hospitali hiyo.

“Nitoe wito kwa Hospitali zote za Kanda, Maalum na ya Taifa ambazo tunazo nchini, zianze ama kama wameashaanza waendele kushuka chini kwenda kutoa huduma za mkoba kwenye hospitali zetu” amesema Prof. Makubi

Prof. Abel Makubi amesema kuwa Hospitali hizo zina wajibu wa kuwajengea uwezo wataalam waliopo kwenye Hospitali ngazi ya chini yao kuanzia Hospitali za Rufaa za Mikoa, Wilaya hadi ngazi ya chini ili waweze kutoa huduma kwenye maeneo yao na kuwapunguzia gharama wananchi kwenda umbali mrefu kwa ajili ya kupata huduma za matibabu.

Amesema kuwa wananchi wengi hawapati huduma za kibingwa katika maeneo yao kutokana na kukosokana kwa wataalam hao na pamoja na miundombinu ya vifaa wezeshi vya huduma hizo katika Hospitali za Wilaya hivyo ni vyema wakawa na mipango ya huduma hizo kwenye maeneo ya karibu na wananchi.

Prof. Makubi amesema kuwa huduma za mkoa zinawasaidia pia wataalam waliopo kwenye Hospitali za Wilaya kuongeza ujuzi wa kazi hasa kwenye kuwahudumia wananchi wenye uhitaji wa huduma za kibingwa ambazo hazipatikani kwenye maeneo yao.

Aidha Prof. Makubi ameipongeza Hospitali ya Kanda ya Bugando kwa kuwa na program endelevu ya huduma za mkoa na kuwahimiza wasiache kutoa huduma hizo kwa wananchi huku akizitaka Hospitali nyingine kuiga kutoka hospitali hiyo.

“Watu wanaona umuhimu wa Bugando kwamba ipo pamoja na wao, kwa hiyo ni vizuri na nyie mkatimiza huo wajibu wa kuendelea kushikamana na viongozi kuanzia ngazi ya Mikoa, Wilaya, Vituo vya afya mpaka kwenye zahanati”Amesema Prof. Makubi

Amemtaka Mkurugenzi pamoja na kamati tendaji ya hospitali hiyo na hospitali nyingine za Kanda na Taifa kukaa pamoja kwa muda wa miezi 3 ijayo kuona ni jinsi gani kuziendeleza huduma hizo za mkoba katika Mikoa 8” Amesisitiza Prof. Makubi

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Dkt. Fabian Massaga amesema hospitali hiyo inaendela kutoa na kuboresha huduma zaidi ili wananchi wengi waweze kupata huduma bora katika kanda ya ziwa.

Amesema Hospitali hiyo imekuwa ikitoa huduma za mkoba pamoja na ‘camp’ za huduma za kibingwa kwa wananchi hivyo kuwapunguzia gharama ya kwenda umbali mrefu kufuata matibabu bugando.

Amebainisha kuwa hospitali hiyo katika mwezi huu wa desemba kuazia tarehe 18 itaendesha ‘camp’ ya huduma za upasuaji wa moyo pamoja na upasuaji kwa watoto ambapo wataalam bigwa wa huduma hizo kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Bugando na Daktari kutoka nchi ya Uganda.

Ijumaa, 4 Desemba 2020

“VITA YA MAGONJWA YASIYO YA KUAMBUKIZA INAHITAJI JUHUZI ZA KILA MMOJA WETU” – MGANGA MKUU WA SERIKALI

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akisema jambo kwa viongozi wa Mkoa wa Geita katika kikao cha kujadili miundombinu ya Sekta ya Afya

Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Robert Gabriel akisema jambo kwenye kikao cha mkoa kujadili miundombinu ya sekta ya afya


Na Englibert Kayombo WAMJW - GEITA


Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi amesema juhudi za kila mwananchi mmoja mmoja zinahitajika ili kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa kubadili mtindo bora wa maisha, ulaji wa chakula bora pamoja na kufanya mazoezi.


Prof. Makubi amesema hayo akiwa kwenye kikao cha viongozi ndani ya Mkoa wa Geita kilichofanyika mkoani huyo kujadili miundombinu ya sekta ya afya na elimu.


“Sasa tumeingia katika vita nyingine ya kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, magonjwa haya hayana dalili ya kukushtua kwenda Hospitali, haya ni hatari zaidi kuliko yale magonjwa ya kuambukiza” amesema Prof Makubi.


Amesema dalili magonjwa yasiyo ya kuambukiza huwa hazijitokezi kwa haraka zaidi hivyo mtu huwa anajiona kuwa yuko salama ili hali akiwa mgonjwa ambapo dalili huja baadae kwa uzito mkubwa na mtu huwa amechelewa kuanza kupata matibabu.


“Magonjwa ambayo ni ya kuambuzika yana dalili, utajisikia homa au uchovu, magonjwa yasoyo ya kuambukiza hayana hizo dalili za kukushtua kwenda hospitali, utaanza kuona matatizo baadae na kugundua moyo au figo imefeli, hizo ndo dalili za kwanza” amefafanua Prof. Makubi


Prof. Makubi amesema ni lazima tuelewe magonjwa hayo kama vile presha, moyo, kisukari, kufeli kwa figo na kifua ni hatari kuliko hata yale ya kuambuza yakiwemo Malaria, Ukimwi na Kifua Kikuu ambapo mtu asipojitambua mapema kufanya vipimo, kubadilisha tabia, mwenendo wa chakula huishia kuathirika kiuchumi yeye na familia yake kwa kuwa magonjwahayo yana gharama kubwa za matibabu.


“Usijitambua mapema kufanya vipimo, kubadilisha tabia na mwenendo wa chakula utajikuta uko kijana wa umri wa miaka 30 hadi 50 unapata matatizo ambayo yatakufanya ushindwe kushikiri katika majukumu yako ya uzalishaji na kuiingiza serikali katika gharama kubwa ya kukuhudumia” amesema Prof. Makubi


Amesisitiza wananchi kubadili mtindo wa maisha, mwenendo wa chakula na kuzingatia kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kupambana na magonjwa hayo ambayo yameshika kasi hasa kwa vijana na watu wazima.


“Zamani tulikuwa tunafanya mazoezi, tunalima, tunaendesha baiskeli, kutembea sasa hivi hatufanyi hivyo na ndio maana tumejikuta tunapata haya matatizo ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa haraka sana, tufanye mazoezi na kubadilisha mtindo wa maisha yetu tunayoishi sasa na kuzingatia mwenendo bora wa vyakula vyetu” amesisitiza Prof. Makubi


Aidha amewataka viongozi hao kuendelea kutoa elimu ya afya kwa wananchi ili kuweza kubadilisha mtindo wa maisha na wananchi hao waanze kwenda hospitalini kufanya vipimo ili kutambua dalili za haraka za magonjwa hayo.


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi. Robert Gabriel amewataka wananchi kuzingatia mtindo bora wa maisha na kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kuepukana na magonjwa hayo


“Tumeambiwa maisha yamebadilika, mazoezi ndio mpango mzima wa afya, tumekuwa ‘busy’ mno kila siku kwenye magari maisha yamebadilika na magonjwa haya yasiyo ya kuambukiza huja na mtetemo mkubwa na kupona huwa ni shida, tukumbushane na kubadilika ili tuweze kupambana na magonjwa hayo” Amesisitiza Mkuu wa Mkoa wa Geita.


Mhe. Robert Gabriel ametoa wito kwa wananchi kufanya mazoezi ya mara kwa mara na kubadili mtindo wa maisha kuepukana na magonjwa hayo ambayo amesema huathiri uchumi wa familia na nchi kuingia gharama kubwa ya matibabu.

Mwisho