Pichani ni Kabla ya mapacha hawajafanyiwa upasuaji wakiwa wamebebwa na mama yao Jonesia Jovitus na Kaimu Balozi wa Saudia Arabia nchini Tanzania, Bandar Abdullah Al-Hazzan ,Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru.
Watoto pacha Melness Benatus Benard na Anisia Benatus Benard wakiwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julias Nyerere,wakiwa wamebebwa na Balozi wa Saudi Arabia Mohamed Bin Malik (Kulia) na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bw.Ramadhani Mwinyi (Kushoto).
Bi.Jonesia Jovitus akiwasili MNH pamoja na watoto mapacha kwa ajili ya uangalizi maalumu
Mama mzazi wa watoto mapacha Bi Jonesia Jovitus ,akipokelewa na ndugu yake katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julias Nyerere.
Na Mwandishi Wetu.
Watoto pacha Melness Benard na Anisia Benard waliozaliwa wakiwa wameungana na baadae kufanyiwa upasuaji na kutenganishwa nchini saudi arabia, wamerejea nchini na kukabidhiwa kwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa ajili ya uangalizi maalumu wa afya zao.
Akizungumza leo katika mapokezi ya watoto hao yaliyofanyika kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Elias Kwesi ameishukuru Serikali ya Saudi Arabia kwa kufanikisha upasuaji huo mkubwa wa kutenganisha watoto hao.
“Nawakabidhi watoto hawa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa ajili ya uangalizi maalumu wa afya zao kabla ya kuwaruhusu kwenda nyumbani kwao Wilayani Misenyi, Mkoani Kagera,” amesema Dkt. Kwesi.
Naye Balozi wa Saudi Arabia nchini, Tanzania, Mh. Mohamed Bin Malik amesema kuwa mapacha hao walifanyiwa upasuaji katika hospitali ya King Abdullah Specialist Children’s Hospital ikiwa ni upasuaji wa 47 wa aina hiyo kufanyika kwa mafanikio makubwa nchini Saudi Arabia.
Balozi huyo, ameishukuru Serikali ya Tanzania, Serikali ya Saudi Arabia na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa kuratibu upasuaji huo kwa mafanikio.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji wa watoto wa MNH Dkt. Zaituni Bokhary amesema watoto hao walipokelewa hospitalini hapa mwaka 2018 mapema mwezi wa pili na kufanya vipimo kisha kubaini maeneo walioungana.
“Baada ya kufahamu tatizo lao tuliwasiliana na wenzetu wa Saudi Arabia ambao huwa tunashirikiana kwenye kufanya aina mbalimbali za upasuaji na mara baada ya kuwashirikisha vipimo ilionekana watoto hawa wanatakiwa kusafiri kwenda kufanyiwa upasuaji nchini humo” alisema Dkt Zaituni.
Aliongeza kuwa baada ya taratibu kukamilika yeye pamoja na wataalamu wengine wa MNH waliongozana na mama mzazi wa mapacha hao kwenda nchini Saudi Arabia kushughulikia matababu yao.
Akizungumzia uzoefu wa wake kwa aina ya upasuaji waliofanyiwa mapacha hao Daktari Bingwa Mshauri Mwelekezi wa upasuaji wa watoto kutoka MNH Dkt. Petronila Ngiloi, amesema aina hii ya upasuaji ni wa mfano wa kuigwa kwenye taaluma ya upasuaji.
Pia amewataka wasamaria wema kujitokeza kuwasaidia watoto hao katika malezi ili waweze kupata elimu bora na baadaye waweze kujitegemea.
Kwa upande wake mama mzazi wa watoto hao Bi. Jonesia Jovitus amewashukuru wataalamu wa Saudi Arabia, Serikali ya Tanzania pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa msaada mkubwa waliompa na kufanikisha.
0 on: "MAPACHA WALIOTENGANISHWA SAUDI ARABIA WAKABIDHIWA HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI"